FIKIRISHI: Mkenge wa mfotoa picha na kamera ya nyumbani

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
386
FIKIRISHI ZA NGUMBALU 02:


Baada ya kukupa kisa cha mkulima na sekeseke la Magugu Shambani, leo nakulete kisa kiitwacho Mkenge wa mfotoa picha na Kamera ya Nyumbani.

SASA ENDELEA....

Yule kibarua wa nne aliyeajiriwa na mkulima, mbali na kuwa na sifa ya kutembelea mashamba ya jirani kuomba virutubisho ama kukopa mbegu, alikuwa pia na sifa kuu ya mfotoa picha hodari sana. Picha alikuwa na macho makali sana ya kujua Kamera ipi ni Nzuri , mbovu ama mbaya, japo kipaji hiki alikitumia mara chache sana. Katika pitapita zake mashamba ya jirani, siku moja akajikuta kafika kwenye shamba la majirani wa Magharibi. Haya ni mashamba ambayo wale mababu wa kufikia waliomrithisha mkulima shamba la nyumbani walikuwa wakiishi kabla. Na hata hivyo, nimesikia wakulima wengi wa nyumbani wameendelea sana kuwalaumu mababu wa kufikia kwa kuwa si tu kwamba waligema virutubisho kwenye shamba la nyumbani, bali pia mazao yote waliyovuna baada ya mkulima kuwalimia, walisafirisha wakapeleka kwenye mashamba yao.Kwamba hali hiyo imefanya mashamba ya Magharibi kuwa na sifa za kutoa mazao mengi sana kuliko mashamba ya nyumbani.

Pia nilikusimulia kuwa Kibarua wa Kwanza aliweka utaratibu wa ama yeye mwenyewe kumpeleka Mkulima na majirani zake huko kwenye mashamba ya majirani wa Magahribi ama kujifunza mbinu za kulima ama kutembea kushangaa ubora wa mazao yao lakini pia aliyapeleka yale niliyoita 'magugu dhibiti' ili kuwekewa kemikai za kuwezesha kuyadhibiti Magugu fyonza. Utaratibu huu ulionekana unafaa sana maana hata baada ya mababu wa kufikia kurejea kwao, waliuendeleza kama njia ya ama ya ‘kulipa’ fadhila kwa kuhifadhiwa kwa muda mrefu na kuchuma kwa kufanyiwa kazi bure ama ulikuwa ni utaratibu ama mbinu yao ya kuendelea ‘kulima’ Mashamba waliyomrithisha mkulima kwa njia ya ‘kilimo masafa’. Hili tuachane nalo kwa leo.

Tukirejea kwenye simulizi yangu ya leo. Kibarua wa nne alikuwa mtaalamu sana wa kufotoa picha na kuchagua Kamera nzuri. Hakuwa tu mtaalamu wa kufotoa wengine bali pia alikuwa ni mjuzi wa ama kujifotoa kwa ile ambayo watoto wake huita 'Selifie' ama kupozi kwenye picha ili afotelewe na wengine. Alikuwa na tabasamu na haiba nzuri na hata mkulima aliyemuajiri na majirani zake hawakusita kuweka picha yake kwenye malango yao kama njia ya kumtukuza kibarua huyu aliyetukuka. Kuna wakati kibarua alitengeneza mashati, akayaweka picha zake mbele na nyuma kisha akampa Mkulima aliyemwajiri na majirani zake wavae. Mkulima na majirani walifurahi na kumsifu bila kujua kuwa fedha alizotumia Kibarua zimetokana na mazao ya shambani mwao. Hata ule mti wanaokaa ndege weusi na weupe nilioueleza katika simuizi lililopita nao ulining’iniza picha ya kibarua wa nne katika shina lililo kubwa kabisa, kabla ya kuibadili baada ya kuhamishiwa kwenye shimo lenye giza wakati wa Kibarua wa Tano.

Kama nilivyosema, sifa za Kibarua za ufotoaji picha ziliambatana na kujua kuchagua Kamera iliyo bora hasa alipoenda mashamba ya jirani. Wapo waliomsemasema kuwa alikuwa hodari kuwany'ang'anya watu Kamera zao na wengine walisema akipenda Kamera yoyote Shambani mwake anaweza kwenda kuificha mashamba ya jirani ili siku akitembelea huko zimfotoe picha hasa zile za faragha. Sina uhakika na hili jambo nami nilisimuliwa kama ninavyosimulia.

Kuna kipindi alietembelea shamba la majirani wa Kusini. Huko akaona Kamera nzuri sana iliyokuwa inaweza kupiga picha hata urefu mrefu. Kamera hii ilikuwa na uwezo wa kupiga picha mashamba ya mbali hasa yenye mbegu na virutubisho vingi. Basi kibarua huyu mfotoa picha akavutiwa nayo sana. “Hii inaweza kunisaidia siyo tu kupiga picha mahali zilipo mbegu bali 'kuzizuumu' na kisha kuziprinti pale shambani mwangu”. Bahati alivyoulizauliza, akaambiwa ile Kamera, japokuwa Lenzi yake imetengenezwa huko Kusini, Kava yake imetokana na madini ya Plastiki ya kung’aa yaliyoochimbwa Shambani mwake upande wa Kaskazini Magharibi mahali ambapo kulikuwa kuna dimbwi kubwa lililosababisha sehemu hiyo ya Shamba kuitwa ukanda wa dimbwi hilo. Madini hayo yalichimbwa ama wakati shamba likisimamiwa na Kibarua wa Pili ama wa Tatu. Basi mfotoa picha akainunua Kamera hiyo kwamba anairejesha nyumbani kwao ambapo aliahidi kuishonea mfuko mzuri wa kuiihifadhi. Kweli wamiliki wa muda wa Kamera ile wakampa Kibarua na akaileta kimya kimya biala mkulima kujua. Nitakusimulia siku nyingine kuhusu Kamera hii maana siyo ile niliyotaka kukusimulia.


Kibarua aona Kamera ya Nyumbani shamba la Magharibi

Kamera ninayongelea ni ile ambayo, Kibarua aipoenda kutembea mashamba ya majirani wa Magaharibi, kule ambako mababu wa kufikia walirejea walipomrithisha mkulima Shamba, maana palikua ndiko kwao walipotokea awali. Katika pita pita zake kwenye harakati za Kukopa mbegu akaona Kamera mahali Fulani. Kamera hii ilikuwa na sifa kadhaa. Kwanza, kama ile ya majirani wa Kusini, hii pia ilikuwa na Kava jeusi. Pia, Kamera hii siyo tu kwamba Kava lake lilitengenezwa kwa matirio yaliyotoka Shambani mwa Kibarua, hasa wakati likisimamiwa na vibarua waliomtangulia, bali Matirio hayo yalisafishwa na kusindikwa humo humo Shambani. Wakati huo Kibarua wa nne ama alikuwa mdogo au alikuwa na ndoto za kuomba ajira kwa mkulima ila hakuwa na nguvu sana. Pia, toleo la Kwanza la Kamera hiyo lilitengenezwa Shambani mwa Kibarua huyo na alikuwa analijua vema. Ila safari hii alivyoikuta kwa majirani hawa wa Magharibi, alishangaa kuona Kamera hii haikuwa na mwonekano wake wa awali. Kwanza ilikuwa imeongezeka ukubwa na Sifa. Ukubwa wake uliboreshwa sana kwa kuwekewa Matirio mapya na bora zaidi. Hii ilifanya sifa zake zivume karibu na mbali. Ilikuwa na mlio mzito sana, unaoliwaza ama kuchukiza masikioni pale inapopiga picha. Iliweza kupiga picha mashamba yote ya Kusini, Magharibi, Mashariki, Kaskazini na Kati, tena picha zenye ubora wa hali ya juu. Kuikodi kwa siku moja pekee ulitakiwa uwe na fedha nyingi sana. Sifa yake kuu ni kuwa ilikuwa inatoa picha ya uhalisia halisi mfano, iliweza hata kufotoa vipele vilivyoanza kuota chini ya Ngozi hata kabla mhusika hajaviona au havijaanza kumuwasha. Pia, ilikuwa na uwezo wa kuonyesha kilichomo ndani ya Nguo badala tu ya kuonyesha Nguo alizovaa mfotolewaji. Kamera hii ilikuwa pia ni automatiki. Yaani ukishaiseti mahali pake tu basi mambo mwake mwake. Pia pale ilipokuwa kwenye Shamba la majirani wa Magharibi, tayari ilikuwa imepewa ukuu wa kitengo cha Kamera zinazopiga picha upande liliko Shamba la Kibarua.

Basi Kibarua alipoiona siyo tu kwamba alifarijika bali aiingiwa na tamaa. Usiku huo hakupata usingizi na alisonona sana. Kwamba iweje kamera iliyotengenezwa Nyumbani ije kutumiwa huku wa majirani wa Magharibi? Hata kama wameiboresha si imetengenezwa Shambani mwake?Yaani ati kwa kuwa mababu wa kufikia wameiwekea 'urembo' basi ndiyo wawe na haki zote za kuimiliki na kuitumia? ‘Haiwezekani” alijiapiza. Kwa vile Kibarua alikuwa mtaalamu wa kuongea na kujenga hoja, akawashawishi wamili wakakubali kumpa Kamera. Naamini Kamera pia ilifurahi kurejeshwa nyumbani na maana ilifanyiwa tafrija kubwa ‘kuagwa’ na kamera nyenzake huko kwa mababu wa kufikia.

Kamera ya ‘Nyumbani’ yapewa ukuu wa Kamera

Kamera ilipofika nchini Mkulima akafurahi sana na kummwagia sifa kedekede Kibarua wake kwa kuirejesha nyumbani. Ikawa asubuhi ikawa jioni. Mwezi huohuo Kibarua akaiteua Kamera ya “Nyumbani” kuwa Kamera kuu kuliko zoote za Kibarua. Nilisahau kukwambia kuwa Kamera za Kibarua zote zilikaa pamoja ili kuziongezea nguvu kupiga Picha shamba zima na zilikuwa na umaarufu kiasi. Baaba ya Kamera ya Nyumbani kuizoea kitengo , vile ilikuwa na nguvu ya kuvaibreti, basi ikazisukumasukuma Kamera ndogo ndogo kuzipanga kulingana na sifa za Lenzi zake. Yenye Lenzi kubwa ilisogezwa karibu na yenyewe, sehemu ambayo inaweza kuisaidia kufotoa Picha shamba zima la Kibarua na zenye lenzi ndogo zilisogezwa hadi mahali ambapo ama zingepiga picha kivuli cha jembe ama kivuli cha miti ya shambani. Zile zenye lenzi kubwa zilipangwa pamoja na kwa kushirikia na Kamera iliyoletwa nyumbani zilitoa flashi kali sana na picha safi na zenye ustadi sana haza zilipobonyezwa kwa pamoja. Hali hii ilifanya zipige picha shamba zima. Picha zake zilikuwa bora sana na zinavutia machoni. Mkulima na majirani zake walifurahi sana. Utendaji kazi wa Kamera hii iliyorejeshwa nyumbani hasa uwezo na ustadi wa kuzipanga nyenzake na kutoa picha zenye ubora wa hali ya juu zilifanya Mkulima na majirani zake kuacha kupiga picha kwa vikamera uchwara vingine.

Kibarua na Picha ya tathmini ya utendaji

Nilisahau kukwambia kuwa mkulima na Kibarua walisaini mkataba wa nusu muongo na Kibarua alikuwa na uwezo wa kuongeza mkataba hasa mkulima akiridhika na utendaji. Utaratibu huu wa mkataba wa nusu muongo ulianza kipindi kile cha Kibarua wa kwanza, kimsingi yeye ndiye aiyeupendekeza na mkulima aliona unafaa.

Basi muda wa tathmini ya kuongeza mkataba ulifika, Kibarua akaiendea Kamera na kujisemea maneno kimiyomoyo, “nina ushindani mkubwa sana wakati huu maana nimesikia kuwa kuna watu wengine wamejitokeza kuomba nafasi ya ukibarua, laiti kama ungekuwa na uwezo wa kunifanyia upendeleo maalumu ukanifotoa picha nzuri sana ili Mkulima akiiona nifaulu hii tathmini, nitafurahi sana”. Sina uhakika kama Kamera iliyasikia maneno haya. Kwa kujiamnini kabisa kuwa Kamera itakuwa imeyasikia maombi yake ya kimoyomoyo, Kibarua akapanga tarehe ya kujifotoa picha. Safari hii alitaka atumie Kamera hii pekee kujifotoa picha atakayoipeleka kwa mkulima wakati wa tathmini na si vinginevyo.

Basi akatuma wawakilishi wake wakaileta Kamera kwenye Ukumbi wa wazi. Yeye mwenyewe akavalia Suti ya chini kabisa mwa Sanduku, ambayo ingekuwa kwa mkulima ingekuwa inanukia vile ambavyo watoto wa mkulima tunaita "Viuamende". Viuamende vilikuwa vinatufaa sana sisi watoto wa mkulima, tuliokuwa na matumbo makubwa sana kuliko vyakula tunavyokula. Tusimamapo pamoja na watoto wa Kibarua, Viuamende vilituepusha tusipate aibu ya kutokwa na Mende aliyejificha kwenye Pindo la Bukta ama kupitia matundu yaliyopo matakoni. Ilikuwa ni kawaida sana kuona Kaptula ya mtoto wa mkulima ikiwa na mashimo ya mviringo matakoni na miguu yenye mipasuko mikubwa iliyokuwa na sifa kuu ya kuhifadhi Funza. Hali ilikuwa tofauti kwa watoto wa Kibarua tuliobahatika kukutana nao maana wao waliishia kutucheka. Najua unashangaa kwa nini watoto wa Kibarua walikuwa na Maisha mazuri kuliko wa Mkulima ambaye ni Bosi wake. Tuyaache haya ni ya siku nyingine.Nilikujulisha awali kuwa sifa kuu ya kibarua wa nne ilikuwa ni kujua kutokelezea vizuri. Usihoji hili kwa sasa. Mwili wake ulikuwa na uwezo mkubwa wa kuyatendea haki mavazi yoyote iwe na mabuti ya kulimia au Kaoshi za mazoezi.

Basi siku ya ujifotoa Picha, yeye mwenyewe akaiseti Kamera na vile ilikuwa na vaibresheni ikajisogeza vizuri juu ya meza mkabala na Kibarua. Siku hiyo hadi mkulima na majirani zake walialikwa kuona Kibarua alivyo stadi wa kupozi kwenye kamera.Muda wa kufotoa picha ulivyowadia, Kamera ikavaibreti kimadoido na kuanza kutoa Mwanga Mwekundu na Mweusi kuashiria Kibarua akae vizuri kwenye Kiti na washuhudiaji wakae mkao wa kushuhudia. ‘Chwaa, Chwaa, Chwaa” Kamera ikafotoa picha. Picha ya Kwanza Kibarua akatoka amefumba Macho. Akalalamika kuwa Kamera haijamtendea haki maana imemuwahi akiwa anafumbua Macho , basi akaseti tena na kuipa fursa ifotoe nyingine. Akarekebisha Tai na kukaa vyema tena Kitini. “Chwaa, Chwaa, Chwaa” tayari! Safari hii akatoka Mdomo umefunga, akalalamika kuwa Kamera imemuwahi wakati anajiandaa kutabasamu. "Mbona nilikuwa najiandaa kutabasamu lakini Kamera inanitoa nimefunga mdomo?" Hii siyo haki, akalalama. Basi Kamera ikarudia ya picha ya Tatu, ikatoka Jicho moja limefunga. Kibarua akalalama na akaanza kushikwa na hasira na kutokwa Jasho japo alijitahidi asionekane.Alilalama kuwa Kamera ilimemuwahi akiwa anafunga jicho kuzuia Nzi aliyekuwepo mahali pali asiingie jichoni. Picha ya nne, ikatoka Mweusi ti, akalamika kuwa Kamera itakuwa imemfotoa wakati kivuli cha msaidizi wake kimemueelekea maana yeye ni maji ya kunde. Ya Tano ikatoka ameinamisha kichwa akiwa ameshika tama. Hii kwa kweli hata waangaliaji waliona kabisa Kibarua ameshika tama lakini yeye alichukia kimoyomoyo maana aliamini kamera ilimuwahi wakati anajikuna kipele Shavuni.

Kibarua aichukia Kamera

Japo mwisho wa siku alifaulu tathmini ya mkulima na akaongezea muda mwingine wa kuwa Kibarua, kwa kweli alighafirika sana kutokana na Kamera ile kumuaibisha mbele ya bosi wake mkulima. Haikuchukua muda sana Kamera ilikiona cha mtema kuni. Kwanza ikaondolewa ukuu wa Kamera zote kwa visingizio kadhaa na baadae ikafutwa kazi ya kumfotoa picha Kibarua. Ilikaripiwa sana na wapambe wa Kibarua. Kimsingi Kamera ya ‘nyumbani’ ilikuwa imeingizwa Mkenge ama kwa Kiswahili cha watoto wa Kibarua , “Kamera iliingizwa Mujini”.

Kosa kubwa la Kibarua ni kwamba alisahau kuwa sifa kuu ya Kamera hii ilikuwa ni kumfotoa picha mtu jinsi alivyo ,uwe umefumba mdomo, jicho ama kushika tama, ili mradi ni picha yako, ni yako tu.Baada ya kufutwa kazi,Kamera ikajiondokea kwa kavaibresheni kake kwa unyonge sana.Mkulima alijaribu kulalamika lakini wa kuwa mkataba wake ni kusubiria mazao tu na kubadili mkataba muda ukifika hakuwa na namna. Kimsingi ilipoteza hata mng'aro wake wa asili. Kwanza ilikumbuka jinsi ilivyokuwa na fursa kubwa sana kule kwenye mashamba ya majirani wa Magharibi na ilikuwa na bei ghali sana huko kabla ya kurejeshwa nyumbani.. Sasa baada ya kufutwa kazi, hata bei yake sokoni iliporomoka sana. Ikajiapiza kuwa ikipata tenda ya kufotoa picha, itachagua ile ambayo inafotoa kimya kimya bila kutoa mlio.

Maswali kwa msomaji

1) Ilikuwa haki Kibarua kuikataa picha yake na kuweka visingizio?
2) Kwa kuwa kuna Kamera nyingine nyingi sana huko kwenye mashamba ya majirani wa Magharibi, je Kibarua wa sasa zirejeshe nyumbani? Je unadhani zitashawishika tena kujirejesha ama kurejeshwa nyumbani?
3) Je ubora wa zile kamera zilizokuwa zimepangwa pamoja kumlika shamba zima umeimarika baada ya Kamera ya Nyumbani kuondolewa, ama umerejea ilivyokuwa kabla?
4) Kwa kuwa Shamba lina Kibarua wa Tano sasa, atakuwa tofauti na yule wa Nne?
5) Ni busara kuchukua Kamera walizo boresha watu wa Mashamba ya Magharibi baada ya wewe kushindwa kuziboresha? Ipi njia sahihi?
Tuendelee kusubiri
 
Back
Top Bottom