FIDIA DOWANS: Wizi uleule, wezi walewale katika suti mpya

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
125,012
2,000
FIDIA DOWANS: Wizi uleule, wezi walewale katika suti mpya


picture-4.jpg

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 December 2010


Gumzo la Wiki


dowans_218.jpgWATUHUMIWA wakuu wa ufisadi nchini wanashangilia. Waliojiita wapambanaji, wanazomewa. Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO), linajikuta lipo katikati na sasa linalazimika kutii agizo la mahakama.

Tarehe 15 Novemba 2010, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), ilitoa amri kwa uongozi wa TANESCO kulipa fidia ya Sh.185 bilioni kwa kampuni ya ufuaji umeme ya Dowans Tanzania Limited.
Kampuni ya Dowans ilipata kazi hiyo baada ya kurithi mkataba wa kufua umeme kutoka kwa dada yake – Richmond Development Company (RDC), ambayo ilibainika baadaye kuwa haikuwa na hadhi, sifa wala uwezo wa kupewa kazi iliyoomba.

Hatua ya mahakama kuamuru TANESCO kulipa Dowans imefuatia uamuzi wa uongozi wa TANESCO kuvunja mkataba wake na Dowans.
Tangazo la kuvunja mkataba lilitolewa 30 Juni 2008 na aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashid.

Taarifa zinasema, wakati Dk. Rashid anaamuru TANESCO kujiondoa katika mkataba wake na Dowans, mkataba huo ulibakisha siku 90 kumalizika.
Hivyo basi, wakati TANESCO ikikandamizwa na zigo la fidia; huku watuhumiwa wa ufisadi wakiendelea kupeta; na wapambanaji wakizibwa midomo; serikali inapaswa kueleza wananchi mambo mawili:

Kwanza, nani anayelipwa mabilioni yote haya ya shilingi za wananchi?
Anayetajwa kuwa "mmiliki" wa kampuni ya Dowans Holding Tanzania Limited, Jenerali Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), amewahi kukana kumiliki kampuni hiyo.

Katika mahojiano yake na shirika moja la habari nchini Marekani, KLHN International, Machi mwaka jana, Bregedia Jenerali Al Adawi alisema, makampuni anayomiliki hayajishughulishi na mambo ya nishati bali ujenzi na kwamba Dowans siyo kampuni ya ujenzi.

Alisema iwapo kuna kampuni inatajwa kuwa yake wakati hajawekeza humo hata shilingi, basi angefurahi sana kupewa "kwa dezo" kampuni ya namna hiyo.
Mahojiano na Bregedia Jenerali Al Adawi yalifanywa na M.M. Mwanakijiji – mwandishi wa habari Mtanzania – anayeishi Detroit, Marekani.
Yalifuatia jina la Jenerali huyo kutajwa katika jarida la Africa, toleo la 7 Machi 2009.

Hii ilikuwa na maana kuwa Jenerali Al Adawi haifahamu Dowans na wala hajawekeza katika kampuni hiyo.
Lakini nyaraka mbalimbali za kampuni ya Dowans zilizopo kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), zinaonyesha Bregedia Jenerali Al Adawi kuwa mmoja wa wakurugenzi.
Anuani iliyotumika katika fomu hiyo ni P.O.Box 823, PC 112, Sultanate of Oman. Anuani hiyo ndiyo inayotumiwa na kampuni ya Services and Trade ya Oman ambayo Bregedia Jenerali Al Adawi alianzisha na mshirika wake mwingine mwaka 1977.

Sasa kama anayetajwa kuwa mmiliki wa Dowans anakana kampuni yake, nani anayelipwa fedha hizi?

Je, Bregedia Jenerali Al Adawi anaogopa nini kujitambulisha kuwa mmiliki wa kampuni hiyo?
Jibu ni moja: Kwamba kampuni ya Dowans Tanzania Limited, tayari waliudanganya ulimwengu wakati wa kuhuisha mkataba wa Richmond kwenda kwa Dowans.

Kwa muda mrefu wanaoitwa wamiliki wa kampuni hiyo wamekuwa wakitaja karibu makampuni manne ya Dowans ambayo walidai kuwa yanahusiana na Dowans Tanzania Limited.
Awali ilitajwa Dowans Holdings ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu. Lakini ghafla wahusika walibadilisha maelezo.

Hiyo ilikuwa baada ya taasisi ya Uwekezaji ya Dubai, Wizara ya Uchumi na Biashara ya Falme za Kiarabu ambayo hutoa leseni za biashara na Idara ya Kanda Huru za Falme za Kiarabu inayohusika na uwekezaji, kuthibitisha kuwa hakuna kampuni yenye jina hilo nchini humo.

Vilevile wamekuwa wakitaja kampuni ya Dowans Holdings ya Afrika Kusini. Lakini haikuchukua muda ilikuja kubainika, kwamba nchini Afrika Kusini hakuna kampuni yenye jina kama hilo ambayo inahusiana na Dowans Tanzania Limited.

Ilielezwa na wachunguzi wa habari kuwa herufi "SA" ambazo zinapatikana kwenye majina ya Dowans, zinasimama badala ya maneno ya Kiihispania "Sociedad Anónima" ambayo ni sawa na hadhi ya "shirika" katika Tanzania na siyo South Africa (Afrika Kusini).
Kampuni pekee ya Dowans ambayo ilionekana kuhusiana na Dowans Tanzania Limited ni ile ya Costa Rica.
Hata hati za madai zinathibitisha hili: Kwamba mbia mkuu wa Dowans Tanzania Limited, ni kampuni ya Dowans Holdings SA kutoka nchini Costa Rica.

Lakini ni katika nchi hii ambako sheria za uwekezaji zinaruhusu watu kufungua makampuni feki na zinalinda wawekezaji hao kutokujulikana.
Kwenye orodha ya wanaohusishwa na Dowans ni Kampuni ya Portek International ya Indonesia, kupitia kampuni yake tanzu ya Portek Systems and Equipment Ltd., inayodaiwa kuwa na hisa ya asilimia 39.

Sasa tatizo linaanzia hapa. Kwanza, kwa mwaka 2007 na 2008 kampuni hiyo ya Indonesia haikuwa na hisa yoyote kwenye Dowans Tanzania Limited wala haikuonesha kuwa wanaitambua kwa namna yoyote ile.

Pili, kwa upande wa Afrika, kampuni hiyo ya Portek Systems and Equipment ilikuwa inafanya kazi nchini Algeria kupitia kampuni ya Bejaia Mediterranean Terminals S.p.a. Portek, na kwamba ina asilimia 15 ya hisa kwenye kampuni moja tu ya kigeni nayo iko visiwa vya Philippines.

Sasa swali la kujiuliza ni hili: Kama haya ndiyo yaliyojificha nyuma ya pazia la Dowans, serikali inapata wapi mamlaka ya kulipa kampuni hiyo fedha za wananchi?

Kama anayejiita mmiliki wa Dowans Tanzania Limited na ambaye nyaraka za BRELA zinamtaja, Bregedia Jenerali Al Adawi kuwa ndiyo mwanzilishi, lakini mwenyewe anakana kumiliki kampuni hiyo, kwa nini TANESCO walazimishwe kulipa kampuni isiyofahamika wamiliki wake?


Kinachofahamika kwa wengi, ni kwamba Bregedia Jenerali Al Adawi ana sura nyingi: Anajitambulisha kama Mtanzania anayeishi katika nchi za Falme za Kiarabu.
Vilevile, Bregedia anajitambulisha kuwa mmiliki wa Dowans; huku anakana kuifahamu Dowans na kusema hajawahi kuwekeza katika kampuni yenye jina hilo.

Hapa ndipo inaibuka sura na tabia yenye utata. Hakuna hata anayejishughulisha kumhoji mfanyabiashara Rostam Aziz, ambaye aliruhusu anuani ya posta na barua pepe za kampuni yake ya Caspian Tanzania Limited, kutumiwa na Dowans.

Lakini kuna hili pia: Hatua ya serikali kunyamazia mkataba wenye utata na hata umiliki wa kampuni ya Dowans inafanana, kwa kiwango kikubwa, na umiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.

Kwa zaidi ya miaka sita sasa, serikali imeshikwa na kigugumizi cha kutaja mmiliki wa Kagoda. Wala haijasema sababu za kushindwa kumchukulia hatua mmiliki au kampuni yenyewe kwa kuchota zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Serikali inajua kuwa kati ya makampuni yote yaliyochota mabilioni ya shilingi kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya BoT, Kagoda ndiyo ilikuwa kinara wa ukwapuaji huo.
Serikali inajua pia kwamba hata kabla Kagoda haijasiliwa, tayari ilishakwapua mabilioni hayo na kuyatawanya katika matawi saba tofauti ya benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.

Hivyo basi, ni muhimu kabla ya serikali kuamuru TANESCO kulipa "fidia"hiyo, kwanza itaje nani mmiliki wa Dowans, anaishi wapi na ameletwa na nani nchini.

Vinginevyo wananchi wataamini kuwa fedha zao zinakwenda kwa watu walewale walioshindwa kukamwatwa kwa zaidi ya miaka sita sasa tangu kutendwa kwa jinai.

Tatu, kabla ya serikali kuruhusu fedha kutoka kwa mlango wa nyuma, waliohusika kuingiza serikali katika mkataba huu wa kinyonyaji waonekane wakichukuliwa hatua.

Ni lazima serikali iseme, tena bila kutafuna maneno, kwamba wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria; na ionekane ikifanya hivyo.
Hatua ambazo zinasemwa, zisiishie kwenye majukwaa ya kisiasa na vyombo vya habari. Ziwe hatua zinazoambatana vitendo.

Nne, kabla ya serikali kukamua TANESCO, ambayo iko hoi kiuchumi, ieleze hatua ambazo itachukulia wanasheria wake waliokubali kuingizwa kwa kifungu cha kuruhusu mkataba kuhamishiwa kwa kampuni nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa, kuwapo kwa kifungu hicho ndiko kulikotoa mwanya kwa wamiliki wa kampuni ya Richmond kuhamishia mkataba wao kwa Dowans na hivyo kuifanya kampuni hiyo kuwa na kiburi hadi sasa.
Hivyo, kuwapo kwa kifungu hicho kuliipa haki Richmond kuhamisha mkataba wake na kufanya mkataba mzima kukosa maana, kwani dharula inafahamika kuwa ni muda maalum. Basi!
Wala wanasheria wa serikali hawawezi kujitetea kuwa hawakufahamu mkataba uliofungwa ulihusu uzalishaji umeme wa dharula. Walijua na wanajua mpaka sasa.
Kifungu hicho ndicho kinachodaiwa na baadhi ya wanasheria kuwa kilitumika kuingandamiza serikali katika shauri lililoamriwa katika mahakama ya kimataifa.
Tano, kabla ya serikali kulipa mabilioni haya ya shilingi, lazima iseme kipi kilimchochea Dk. Rashid kuamuru TANESCO kuvunja mkataba wakati uhai wa mkataba ulikuwa unaelekea ukingoni.
Je, nani alimsukuma Dk. Rashid kuchukua uamuzi huo unaoligharimu taifa hivi sasa? Wataalam wa sheria TANESCO hawakujua madhara? Je, wale wa serikali? Mwanasheria Mkuu wa serikali hakuwepo kutoa maoni yake katika mikataba mikubwa ya aina hii? Je, wote walijua na kukaa kimya?

Kabla ya kuwa mtendaji mkuu wa TANESCO, Dk. Rashid alikuwa mtendaji mkuu wa kampuni ya Vodacom ambayo inajihusisha na biashara ya simu za mkononi.
Miongoni mwa wamiliki wa Vodacom alikuwa Rostam Aziz ambaye, amedaiwa kuwa mmiliki wa Dowans (ingawa amekana); swahiba wa Bregedia Jenerali Al Adawi na mfadhili wa Dowans kwa kuwaruhusu kutumia anwani za kampuni yake.

Sita, kabla ya kuamuru kulipwa fedha hizo, serikali inapaswa kuweka wazi ni hatua zipi itakazochukua dhidi ya Nazir Karamagi, ambaye wakati huo alikuwa waziri wa nishati na madini.

Ni Karamagi aliyekubalia Richmond kuhuisha mkataba wake kwa Dowans. Kosa la Karamagi hapa ni kukubali kuhuisha mkataba wa kampuni ambayo "haikuwapo kwa mujibu wa sheria."

Huku akijua kwamba mkataba kati ya serikali na Richmond ulikuwa wa mwaka mmoja, Karamagi aliubadilisha na kuufanya kuwa wa miaka miwili.
Si hivyo tu; wakati Karamagi anasaini mkataba mpya, tayari janga kuu lililokuwa limesababisha serikali kuhaha kutafuta umeme wa dharula, lilikuwa limemalizika.

Saba, serikali iseme itamchukulia hatua gani aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Dk. Ibrahim Msabaha anayedaiwa "kushinikizwa" kuipa mkataba Richmond.
Hata kama Dk. Msabaha alishinikizwa, lakini ni wazi kuwa alishindwa kusimamia kazi za serikali kwa uaminifu alioapa kutunza; badala yake akaruhusu kampuni isiyo na hadhi kupewa mkataba.

Nane, kabla ya TANESCO kulipa mabilioni hayo ya shilingi, lazima serikali; na hapa Rais Jakaya Kikwete, aeleze atamchukulia hatua gani za kisheria, aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa kwa kuingiza taifa katika hasara hii ya mabilioni ya shilingi?

Kosa la Lowassa linafahamika. Anadaiwa kushikiza watendaji serikalini kuipa kazi kampuni isiyokuwa na sifa.
Kwa hiyo basi, hatua yoyote ya kulipa fedha bila kujulikana mmiliki halali, kutafanya wananchi waamini fedha zinalipwa kwa Kagoda yuleyule, lakini aliyekuja kupitia mgongo wa Dowans. Tusifike huko.

Katika jina la demokrasia na uwazi, serikali haina budi kutaja mmiliki wa Dowans Tanzania Limited na anakoishi wapi.
Ifahamike pia kampuni ilisajiliwa wapi na lini; nani wamiliki wake ndani na nje ya nchi; wabia wake ndani na nje; na hatua ambazo zitachukuliwa kwa watendaji wake.

Hadi hapa na sasa, hakuna uhalali wowote wa kulipa mabilioni ya shilingi za walipakodi wa Tanzania kwa vivuli vinavyoletwa kwa jina la Dowans. .
Tunaibiwa!
 

Interested Observer

JF-Expert Member
Mar 27, 2006
2,147
2,000
Very strange case! Hivi nani Alishitaki? Maana mshitakiwa anajulikana; sasa mshitaki ni nani? Hata kama represented na lawyers; a company has shareholders, Directors, Certificate of Incorporation, Business license etc etc For sure this is looting. Je hii ICC panel iliyotoa huo uamuzi haikufanya uchunguzi wa kina kujua hii kampuni na uhalali wake? Looks as if this panel parted with something maana wanajua hili ni shamba la bibi. There are many arbitration hearings but this is very strange, I have to question the legality of this panel of judges.
 

pmwasyoke

JF-Expert Member
May 27, 2010
4,122
2,000
Inatisha - inamaanisha hata hizi mahakama za majuu zinakuwa manipulated na mafisadi!
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom