Ffu wafyatua risasi, wanafunzi 18 wazirai

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,900
21,989
Vurugu zatanda, wanafunzi Kibasila walala barabarani

FFU WAFYATUA RISASI, WANAFUNZI 18 WAZIRAI


Waandishi Wetu


WANAFUNZI 18 wa kike wa Shule ya Sekondari ya Kibasila jana walizirai na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Temeke wakati askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walipopambana na wanafunzi wa shule hiyo waliofunga Barabara ya Mandela na Chang’ombe.


Takriban wanafunzi 1,000 wa shule hiyo, ambao mwaka jana walifunga barabara hizo kwa saa kadhaa kupinga vifo mfululizo vya wenzao kutokana na kugongwa na magari, jana walichukua tena sheria mkononi baada ya mwanafunzi mwenzao aliye kidato cha sita, Emmanuel Mapande kugongwa na daladala linalotoa huduma kati ya Tandika na Kariakoo.


Uamuzi wao wa kufunga barabara hizo ulisababisha msongamano mkubwa wa magari yanayotumia barabara hizo, yakiwemo malori ambayo hubeba mizigo kwenda na kutoka Bandari ya Dar es salaam.


Wanafunzi hao walikaa kwenye makutano ya barabara hizo mbili kufuatia mwenzao wa kidato cha sita, Emmanuel Mapande kugongwa na daladala aina ya Isuzu Journey linalofanya safari kati ya Karikoo na Tandika. Mapande, ambaye alikuwa katika hali mbaya, alikimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.


Jana wanafunzi hao walifunga barabara hiyo kuanzia saa 4:00 asubuhi na magari ambayo yalijaribu kupita kwa nguvu yalirushiwa mawe na vioo vya baadhi ya magari hayo vilivunjwa.


Kutokana na hali hiyo, FFU waliitwa na walipofika eneo hilo, walilazimika kufyatua risasi za mpira hewani na kusababisha wanafunzi 18 wa kike kuzirai na kukimbizwa katika Hospitali ya Temeke.


Kamanda wa polisi mkoa wa Temeke, Liberatus Sabas alisema wanafunzi walitoka nje ya shule hiyo baada ya mwenzao kugongwa na kwenda kuifunga barabara hiyo kwa saa tatu.Alisema awali mwanafunzi aliyegongwa alikimbizwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu ya haraka.


"Baada ya kuona hali hiyo inaendelea kukithiri ndipo tukatoa taarifa watawanyike, lakini wanafunzi hao waligoma ndipo tukaamua kurusha bomu la kishindo ambalo halina madhara yoyote kwa binadamu licha ya wanafunzi zaidi ya 20 walipatwa na mshtuko na kukimbizwa hospitali," alisema Sabas.


"Tulitaka wanafunzi hao watawanyike na magari yaendelee na safari zao kama kawaida, lakini wanafunzi hao walidhihaki na ndipo tukafanya maamuzi hayo."


Naye Mratibu wa tiba wa Hospitali ya Temeke, Dk Gilbert Bubelwa alithibitisha kupokewa kwa wanafunzi hao na kusema hali zao zinaendelea vizuri.

"Ni kweli majira ya saa 6:00 mchana tumepokea wanafunzi wa kike 18 kutoka Sekondari ya Kibasila na hadi sasa hali zao zinaendelea vizuri, wote hawa walipatwa na mshituko," alisema Buberwa.


"Lakini yule mmoja aliyegongwa tulimpokea, alikuwa ameumia kwa ndani na sehemu ya nyuma ya kichwa alikuwa na uvimbe uliosababishwa na damu kuvilia."

Dk huyo alisema Mapunda alifanyiwa uchunguzi wa awali na kisha akapelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.


Makutano ya barabara hizo mbili hayana taa za kuongozea magari, hali ambayo hufanya madereva wa magari kupita kwa kutegeana. Baada ya wanafunzi kufunga njia hiyo mwaka jana, sehemu hiyo iliwekwa matuta ya kufanya magari yapunguze mwendo, lakini hakuna matuta kwenye inayotoka Temeke kuelekea Changombe.


Akizungumza na gazeti hili jana kiongozi wa nidhamu shuleni hapo, Faida Mshamu alisema waliamua kutoka darasani na kufunga barabara hiyo ili kuishinikiza serikali iondoe kero ya wanafunzi kugongwa pamoja na vifo vya wanafunzi katika eneo hilo.


"Naishauri serikali kujenga matuta, kuweka taa za barabarani na kuweka alama za kutaka magari yasipite eneo hili kwa mwendo wa kasi," alisema.

Kutokana tukio hilo, uongozi wa shule hiyo ulilazimika kusitisha ratiba za masomo na kuwarudisha wanafunzi nyumbani hadi Jumatatu ijayo.
 
Back
Top Bottom