Nimejongea JamiiCheck kwa mara nyingine, tafadhali naomba kupata uhalisi wa barua hii kama ni ya kweli kwamba Fei Toto amevunja mkataba na Azam FC
- Tunachokijua
- Feisal Salum ni mchezaji wa timu ya Azam FC yenye makazi yake Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es salaam, Feisal alisajiliwa na Azam akitokea Yanga kwa makubaliano ya pande mbili kati ya timu hizo, alisaini mkataba wa miaka miwili utaokoma mwaka 2026 kuitumikia timu hiyo. Feisal amekuwa na mchango mkubwa katika timu yake na hata timu ya taifa kutokana na umahiri wake wa kufunga na kutengeneza pasi za magoli.
Feisal amekuwa akihusishwa na na timu mbalimbali nchini na nje ya nchi licha ya kuwa na mkataba na Azam FC. Katika mitandao ya kijamii kumeibuka barua ambayo inaeleza kuwa Azam FC imeridhia kuvunja mkataba na Feisal Salum baada ya mchezaji huyo kutekeleza matakwa ya kimkataba.
Je kuna uhalisia gani dhidi ya barua hiyo?
Ufuatiliaji wa kimtandao uliofanywa na JamiiCheck umebaini kuwa barua hiyo si ya kweli na haijatolewa na Azam Football Club, aidha imebainika kuwa na mapungufu kadhaa yanayoitofautisha barua hiyo na barua rasmi zinazotolewa na timu ya Azam FC, sehemu ya mapungufu hayo ni pamoja na kutumiwa kwa zaidi ya aina moja ya mwandiko (fonts), kukosewa kwa mwezi badala ya ‘Nov’ imetumika ‘Dov’ ukirejewa mwezi wa 11, mpangilio wa tarehe ambayo haijafuata mpangilio wa maneno yaliyo juu ya tarehe.
Katika kutafuta uhalisia zaidi JamiiCheck ilimtafuta afisa habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe ambaye amekanusha juu ya uwepo wa barua hiyo na kwamba haina ukweli wowote na haijatolewa na ukurasa wowote rasmi wa Azam FC
“JamiiForums ni taasisi ambayo ninaiheshimu sana kwa uhakika wa taarifa zake, nadhani hata hiyo barua mkiangalia vizuri mtabaini kuwa ni fake, kutokana na aina ya uandishi wake pia haipo kwenye ukurasa wetu wowote wa Azam FC. Barua hizo ni fake, wanazisambaza, tunachotaka kuwaambia ni kuwa waache waendelee kujiandikisha barua za uongo, sisi tukiandika ya kwetu itakuwa ni barua ya ukweli na hatuchagui nyumba ya kubisha hodi.”