Fedha za kuhudumia ofisi za wabunge Mbeya zaleta mzozo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Utata kuhusu matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kuhudumia ofisi za wabunge umepamba moto ambapo Mbunge wa Mbozi Mashariki, (CCM), Godfrey Zambi,ametoboa siri kuwa katika mwaka wa fedha wa 2009/2010 serikali ilitoa kiasi cha Sh.milioni 14 ili zitumike kuhudumia ofisi za wabunge wa mkoa wa Mbeya.
Zambi ametoboa siri hiyo jana wakati wa mkutano wa kamati ya ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC),kwa kueleza kuwa pamoja na kutolewa kwa fedha hizo katika hali ya kushangaza ofisi za wabunge ikiwemo ya kwake hazihudumiwi vizuri ambapo nyingine zipo katika hali mbaya kiasi cha kutokuwa na samani.
Alisema kwa fedha hizo zilizotolewa na serikali kwa Mkoa wa Mbeya, zingeweza kutolewa shilingi milioni moja kwa kila ofisi ya mbunge zisaidie kununua samani na vinywaji laini lakini cha kushangaza hakuna hata shilingi moja iliyotolewa kuzihudumia ofisi hizo.
Kufuatia madai hayo ya mbunge huyo,Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile alisitisha hoja hiyo isijadiliwe kwenye kikao kwa kumweleza Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Moses Chitama alitafutie ufumbuzi suala hilo.
Kumekuwa na malalamiko ya wabunge wapya waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu ambao kila wanapokwenda kwenye ofisi wanakuta hakuna samani .
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa ofisi za wabunge nyingi hazina samani hali ambayo imepelekea wabunge wapya waliochaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu kukuta ofisi hizo hazina kitu chochote.
Akizungumza na NIPASHE kwa simu, Katibu wa Bunge, Dk David Kashilila, alisema Bunge halishughuliki na masuala ya ofisi za wabunge.
Dk.Kashilila alisema ofisi za wabunge ni mali ya serikali kwa hiyo wenye mamlaka ya kuzihudimia ni makatibu tawala wa mikoa na Wilaya ambao hata mafungu ya fedha yanayotolewa na serikali kuu kwa ajili ya matumizi ya ofisi za wakuu wa mikoa na Wilaya zikiwemo ofisi za wabunge yanapitia kwao.
Alipozungumzia suala hilo, Katibu Tawala Msaidi Mkoa wa Mbeya, Moses Chitama, alisema hakuna fedha maalum zinazotengwa kwa ajili ya kuhudumia ofisi za wabunge isipokuwa zinahudumiwa kwa fedha za matumizi ya kawaida kama ilivyo kwa ofisi za Wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya.
 
Back
Top Bottom