FANYA HAYA KUZUIA WATU WASIINGILIE MAPENZI YENU

Joseverest

JF-Expert Member
Sep 25, 2013
51,742
68,596
Wasalaam wana MMU... Naomba niende moja kwa moja kwenye mada.

Sio mbaya kwa marafiki wa karibu au ndugu na jamaa kufahamu kushirikiana nanyi katika mapenzi yenu kama vile wakati wa sherehe au msiba. Pia sio mbaya kujuliana hali na kutambulisha mambo ya msingi yanayoendelea katika mahusiano yako wewe na mpenzi wako.
Hata hivyo kuna wakati watu wengine wa pembeni, wawe majirani, ndugu, wazazi au marafiki wanaweza kuwa ‘sumu’ ya mahusiano yako, hasa pale unapowategemea sana kutoa msaada, maoni au maelekezo katika maisha yako ya mapenzi. Makala hii inaeleza mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kupunguza uwezekano wa rafiki, ndugu, jamaa, au wazazi kuwa ‘sumu’ ya mapenzi yako.


1. Udhibiti wa taarifa kwa wengine:

Kadri unavyoelezea mahusiano yako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi watu kutoa maoni, na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako. Hivyo basi, chukua muda wa kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu maswala yako ya mahusiano kabla haujaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine. Ni bora ukasoma vitabu, na makala mbalimbali, hususani zihusuzo tabia na maisha ya mahusiano, zitafakari vema ili kuona zinahusiana vipi na unayokumbana nayo katika mahusianao yako.


2. Upekee wa mambo:

Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako. Ukitambua hili, utafanya bidii ya kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo katika mahusiano na kutafuta suluhisho kabla ya kutegemea watu wengine.


3. Mwenye maamuzi ni wewe:

Ni kweli kuwa kuna nyakati ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa watu wengine, na zaidi sana watu wenye uelewa sahihi na unaowaamini, hakikisha kuwa unatambua kuwa wewe mwenyewe ndio mwenye kubeba lawama ya maamuzi utakayochukua.


4. Kuwa na subira:

Usichukue maamuziya haraka katika mahusiano hususani uamuzi wa kuamua kuwashirikisha watu wengine habari ya mambo yahusuyo uhusiano wako. Unapofanya uamuzi wa kuwashirikisha wengine kwa haraka unajinyima nafasi ya kulichunguza jambo kwa ufasaha hususani madhara yanayoweza kutokea kwa kuwaeleza wengine, au kama ni tatizo, basi kufikiria njia sahihi ambazo ungeweza kuzitumia kupata suluhu ya tatizo.


5. Fungua njia za mawasiliano kati yenu:

Pengine chanzo cha wewe kutaka kuzungumza mambo ya ndani yanayohusu mahusiano yenu kwa watu wengine ni kwakuwa umekosa nafasi ya kuzungumza kwa ufasaha na mwenzi wako. Tafuteni nafasi za kutosha, jengeni mazingira ya kuzungumzia mambo yenu kabla ya kutaka kuwashirikisha watu wengine.


6. Kuweni peke yenu:

Hata kama hautaki kueleza watu kuhusu mambo yanayoendana na maisha yenu, mazingira unamoishi yanaweza kuchangia watu kutaka kuingilia mahusiano yenu –kwa kutoa maelekezo, ushauri au maoni kuhusu muishivyo wewe na mpenzi wako. Inapobidi hakikisha hamuishi karibu na wazazi wenu, ndugu au rafiki wa karibu. Au haufanyi kazi na mwenzi wako sehemu moja, kwani hiyo itakuwa njia rahisi sana ya watu kuona mnavyoishi. Inapobidi kuwa karibu na watu wengine , hakikisha mnakubaliana wewe na mwenza wako namna bora ya kuendesha mawasiliano kati yenu mbele za watu, ili msiwape nafasi ya wao kuwa‘soma’ na kisha kuanza waje waanze kutoa ‘maelekezo’ ya vile wanavyoona mnapaswa kuishi.


7. Nenda ‘darasani’ :

Kumbuka mahusiano yanahitaji sana uelewa mkubwa wa jinsi ya kufanya mawasiliano fasaha, kuelewa hisia za mwenzi wako, kutambua mbinu za kusuluhisha migogoro, na zaidi sana kufanya mipango ya muda mrefu ya uhusiano wenu. Jizoeshe kusoma makala na vitabu mbalimbali vyenye kuboresha ufahamu wa mambo ya msingi kama hayo tuliyoeleza hapo juu.


Karibuni wana MMU, kama kuna nyongeza unaweza kuongezea twende sawa.....!

f22fe18935b5f9a9bdeceb7aafd397ff.jpg
 
Umpate wa hivyo.... ukimpata asiye wa hivyo, mpango mzima utaharibika.
 
8 Reactions
Reply
Back
Top Bottom