Falsafa ya elimu yetu ni sahihi kwa maendeleo ya watanzania na taifa

mwengeso

JF-Expert Member
Nov 27, 2014
9,219
6,650
Nimeipata habari hii ya Prof Kamuzora, RAS Kagera, kutoka mitandao ya kijamii. Naamini hoja zilizomo humu ni hoja changamshi kuhusu falsafa (aina na mfumo) ya elimu yetu, tangu uhuru, kama inasaidia kutengeneza jamii ya kujitegemea au kutegemea ajira.

Tujadili

"Tatizo lile lile nililolisema awali. Falsafa ya Elimu yetu ni kuwa watu wanasomea taifa na si kusomea maisha yao. Hivyo, wote mnaingizwa kwenye behewa kuelekea kwenye combinations ambazo Taifa limechagua yaani PCM, PCB, PGM, CBG, CBN, ECA, EGM, HGL, HGE, HGK. Ukikosa nafasi kwenye behewa sasa ndio ukatafute hizo fursa zingine za NACTE na VETA.

Falsafa hii na mfumo huu una athari za kisaikolojia. Kwanza unafanywa watu wakikosa nafasi kwenye behewa la form five wajione kuwa ni watu waliofeli na waliopoteza ndoto za maisha. Pili, inafanya elimu ya NACTE na VETA kuonekana kama ni sitara na hifadhi kwa waliokosa nafasi behewani. Matokeo yake, tunapeleka huko kwenye NACTE na VETA waliopoteza matumaini. Yaani tumegeuza NACTE na VETA kuwa ni elimu mbadala na si chaguo tu kama kwenda form 5.

Katika hili nitapenda kutoa mfano wa jamii ya watanzania wenye asili ya asia. Hivi hawa wanaishiaga wapi? Mbona wengi hawaendi form 5 na hata wanaoenda hawasomi HGL, HGK na HGE bali utawakuta aidha kwenye PCB, PCM na ECA na EGM? Na je mbona huko chuo hawaonekani kwenye vitivo vya Sheria, Sayansi ya Siasa, Sociolojia na Historia na Archaeology? Mbona ni kama hawapo kabisa kwenye Masters degree zinazotolewa na Chuo Kikuu kipendwa cha UDSM na pia hawapatikani kule kwenye Masters za jioni za Mzumbe wala zile za Open University? Lakini mbona pamoja na kutowaona huko kote hatuwaoni mtaani wakipita na bahasha za khaki zenye photocopy za vyeti na barua za kuomba ajira?

Wenzetu hawa walishajinasua siku nyingi katika mtego wa fikra tuliouingia wa kusomeshea watoto kwenda kujaza nafasi za wanaostaafu na kufa katika sekta ya umma. Wenzetu wanajifunza stadi zaidi. Anayetaka uhasibu, akifika form four anajisajili kwenye mitihani ya Bodi za Uhasibu (NBAA na ACCA) anaendelea huko. Wengine watakwenda kujifunza masuala ya kukatisha tiketi za ndege IATA system, wengine watakwenda kujifunza stadi za Hardware na Software Engineering na stadi nyingine nyingine. Wengine watasomea u-pilot, wengine insurances nk. Leo nenda kwenye nursery schools walimu wengi ni watanzania waasia kwa kuwa wanakwenda kusomea fani hiyo. Kwao behewa la form 5 ni moja tu kati ya mabehewa mengine na si behewa takatifu au la wateule.

Wenzangu na sisi tunakwenda na behewa, tunaingia chuo tunapigwa sumu ya DS 101 tunakuwa wanamapinduzi na wachukia mabeberu huku tukisoma archaeology, Sociology, Political Science na Kiswahili mwisho wa siku tunasubiri Sekretariati ya Ajira itangaze kazi tunajikuta inaajiri asilimia 10 tu ya waliomaliza chuo. Mwishowe hao hao wasomi wanarudi kuajriwa na mabepari waliokuwa wanawachukia wakiwa chuo"

Je, kuna kitu tunakosea mahala kuhusu mwelekeo wa mfumo wa elimu yetu?
 
Back
Top Bottom