Faini ya bil. 185/- yawashitua Watanzania

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,072
1,250
WAKATI wananchi wakishitushwa na hatua ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), kutoa uamuzi kuwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) liilipe Kampuni ya Dowans Sh bilioni 185, shirika hilo linatafakari hukumu hiyo.

Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud akizungumza na gazeti hili jana kuhusu hukumu hiyo, alisema shirika hilo limepata uamuzi huo na linaufanyia kazi kabla ya kutoa taarifa kwa Watanzania.

Hata hivyo, baadaye Idara ya Mawasiliano Tanesco ilieleza kuwa inaleta taarifa kuhusu suala hilo, lakini baadaye ilitangaza kuwa imesitisha kutoa taarifa hiyo na kueleza kuwa wataitoa leo.

Tanesco imeamriwa kuilipa kampuni ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Limited zinazofanya kampuni ya pamoja ya Dowans iliyoanza rasmi kuzalisha umeme kwa ajili ya Tanesco mwaka 2007 baada ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond kushindwa kufikia lengo.

Katika uamuzi huo ambao nakala yake gazeti hili linao, jopo la wasuluhishi limeamuru Tanesco kuilipa Dowans zaidi ya Sh bilioni 36 (dola za Marekani 24,168,343) na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 25 (dola za Marekani 19,955,626) kuanzia Juni 15, mwaka huu mpaka muda utakapofanyika malipo ya fidia hiyo.

Pia katika uamuzi huo uliofanywa na mahakama hiyo yenye makao yake makuu nchini Ufaransa, liliamuru Sh bilioni 60 sawa na dola za Marekani 39,935,765 na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 54 sawa na Dola za Marekani 36,705,031.94 kuanzia Juni 15, mwaka huu mpaka siku ya malipo ya fidia.

Aidha pia katika uamuzi huo, jopo lilipitisha fidia ya zaidi ya Sh bilioni moja (Dola za Marekani 750,000) kwa ajili ya gharama za uendeshaji wa shauri na waamuzi ambazo zinapaswa kulipwa na pande zote mbili pamoja na Tanesco kumlipa mdai Sh bilioni tatu (USD 1,708,521) kama gharama za uendeshaji kesi. Madai mengine ya pande hizo mbili (Tanesco na Dowans) yalielezwa kuwa yametupiliwa mbali.

Katika usuluhishi huo, Dowans ndiyo iliyokimbilia katika mahakama hiyo baada ya serikali kuweka pingamizi baada ya kampuni hiyo kutangaza kuuza mitambo yao, lakini uamuzi huo wa ICC Court umepokewa kwa mtizamo tofauti na wananchi hao huku wakihoji na kutaka kujua msimamo wa serikali kuhusu suala hilo.

Mahakama hiyo ya ICC Court iliwahi kuipa ushindi Serikali ya Tanzania dhidi ya iliyokuwa Kampuni ya City Water baada ya kukimbilia mahakamani kutokana na serikali kuvunja mkataba wake wa usambazaji wa maji jijini Dar es Salaam, kutokana na kutokidhi matakwa ya mkataba.

Lakini baadhi ya wananchi wamesema hukumu hiyo katika kesi ya Dowans ambayo ni fidia kubwa kuwahi kuamuriwa serikali kulipa ni mzigo wa Watanzania wasio na hatia.

Kwa nyakati tofauti jana, wananchi wa kada mbalimbali, walisema suala hilo limeiingiza nchi katika hali ngumu hasa kwa wafanyakazi na wafanyabiashara ndio watapaswa kulipia fidia hiyo kwa kupitia kodi zao.

Wakati wananchi wakitoa kilio hicho, awali Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, Kabwe Zitto ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, aliwahi kushauri Tanesco kununua mitambo hiyo, lakini ulikataliwa kwa sababu zilizoonekana kuwa za kisiasa zaidi.

Hata aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco wakati huo, Dk. Idris Rashid aliunga mkono kuuzwa kwa mitambo hiyo, lakini wote wakakumbana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wanasiasa ikiwemo kamati nyingine ya Bunge ya Nishati na Madini chini ya uenyekiti wa aliyekuwa Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo na Makamu wake, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Kamati ya Shelukindo ilikuwa ikigoma kununuliwa kwa mitambo hiyo kwa madai kuwa ni chakavu na kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004 yenye kipengele kinachokataa serikali kujiingiza katika ununuzi wa bidhaa zilizotumika.

Aidha, kutokana na mvutano huo, serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilifuta mpango wa kununua mitambo hiyo, jambo lililosababisha Dowans kutangaza kuiuza na ndipo serikali ilipoweka pingamizi katika Mahakama ya Biashara kuhusu hatua hiyo, ikidai kumalizika kwanza kwa suala la mkataba.

Jana, Zitto alipoulizwa kuhusu matokeo ya uamuzi huo uliofanywa na jopo la wasuluhishi watatu, Swithin Munyantwali, Jonathan Parker na Mwenyekiti wa jopo Gerald Aksen, alisema hana maoni yoyote kwa kuwa akizungumza ataonekana kuwa anaingiza siasa, wakati alishalizungumzia hilo kabla ya uamuzi wa serikali wa kutonunua mitambo kupitishwa.

Miongoni mwa wananchi walioonesha kushtushwa na uamuzi huo uliotolewa na Mahakama ya ICC Novemba 15 mwaka huu, ni wafanyabiashara wa maduka ya nguo eneo la Posta jijini Dar es Salaam, waliosema mzigo huo sasa utawaelemea wananchi wa kawaida ambao tayari wanaelemewa na kodi wanazotozwa katika bidhaa na mishahara.

“Watakaoumia katika hili ni sisi, hakuna wengine, nakumbuka hili suala lilileta mgogoro mkubwa baina ya wabunge na serikali, nakumbuka Zitto aliwahi kutaka mitambo hiyo iuzwe kuepusha hili, lakini wakamuona anakula na mafisadi, sasa cha moto tutakiona,” alisema Steven Joseph, mfanyabiashara wa nguo.

Aidha wafanyakazi wa Benki ya Posta ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao gazetini, kwa nyakati tofauti jana walisema pia kuwa hayo ni matokeo ya serikali kutokuwa makini katika kusaini mikataba ambayo inalipa hasara taifa na kuwataka mawaziri wakati huu kuwa macho na suala hilo.

“Masuala ya mikataba inayohusu maslahi ya umma yanapaswa kuangaliwa, la sivyo tunaliingiza taifa pabaya, sasa uamuzi ndiyo umetoka, iwe iwavyo lazima Tanesco watalipa tu, pesa hizo watatoa wapi ikiwa za kuzuia mgawo tu sasa wanazikosa, hela yote ya walipa kodi badala ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo, italipa deni hili, hili ni doa kubwa,” alisema mkazi mmoja wa Mbezi Beach, Dar es Salaam.

Katika kufafanua hilo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana alisema bado Tanesco hawajampelekea taarifa ya uamuzi huo wa mahakama na kuwataka wananchi na vyombo vya habari kutulia, kwani serikali itatoa ufafanuzi muda mfupi ujao kuhusu suala hilo.

“Nataka kusema tu kwamba bado sijaletewa taarifa na Tanesco, lakini najua wanaiandaa, muwatafute mjue, lakini nataka kusema tu kwamba wananchi watulie na vyombo vya habari vitulie, tutachambua uamuzi huo kwa kina na kisha serikali itatoa taarifa kwa umma kuwa ni nini hatua itakayochukuliwa,” alisema Ngeleja.

Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans, Stanley Munai simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokewa jana wakati alipotafutwa kufafanua suala hilo, ingawa kampuni hiyo ilikuwa imetoa matangazo katika magazeti jana ikieleza kuhusu mgogoro wake na Tanesco umemalizika baada ya uamuzi wa ICC Court.
 

Msanii

Platinum Member
Jul 4, 2007
9,241
2,000
Ni kweli wananchi tutaumia zaidi.
Ila napenda kuweka wazi maoni yangu kuhusu hili swala kuwa. watawala wetu hawana uchungu na nchi hii na wamejiunga na mafisadi kuitafuna.
tukikumbuka suala la IPTL ambapo serikali ilipeleka wanasheria dhaifu kuitetea, napata taswira kwamba hata suala hili ni mwendelezo wa kosa la kiufundi. iweje mitambo iliyoingizwa nchini kwa kashfa kubwa ihaulishwe na kuwekwa chini ya msimamizi mwingine??? je DOWANS walikuwa na uhalali wa kurithi deal ya RICHMOND ambayo haiexist???
kama kuna mwenye data atuletee majina na wasifu wa wanasheria waliokuwa wanaitetea Tanesco kule barazani.

Tumefungiwa jiwe shingoni na tupo kwenye kina na msaada hakuna
 

Mkora

JF-Expert Member
Apr 11, 2008
370
225
Kuanzia leo nakuwa mkwepa kodi nambali one Tanzania,
yaani kodi yangu ilipie umeme ambao sijawahi kutumia pamoja na kununulia mashangingi
 

Shamu

JF-Expert Member
Dec 29, 2008
510
0
Hizo ni hela nyingi sana, kwa nchi kama TZ. Serikali inabidi iapeal haraka iwezekanavyo.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom