Faida kumi (10) za kujua kusoma namba za biashara na taarifa tatu za kifedha unazopaswa kujua kuzisoma ili kufanikiwa

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,781
3,070
Wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa wanafanya biashara zao kwa kubahatisha. Wamekuwa hawana uelewa wa namna ambavyo fedha zinazunguka kwenye biashara zao. Wanachojua ni kununua na kuuza, kitu ambacho ni hatari kwao na kinachozuia biashara zao zisikue zaidi.

Wale ambao wanafanya kazi kwenye makampuni na taasisi kubwa, wamekuwa wanajihusisha na majukumu waliyoajiriwa kuyatekeleza tu. Huwa hawajisumbui kujua mwenendo wa kifedha wa kampuni au taasisi wanayofanya kazi, kwa sababu wanachukulia hilo ni jukumu la wahasibu.

Ukweli ni kwamba, kila mtu anayejihusisha na biashara ya aina yoyote ile, iwe una biashara ndogo au umeajiriwa kwenye biashara au taasisi kubwa, unapaswa kujua jinsi ya kusoma namba za kibiashara na taarifa za kifedha. Namba na taarifa hizi za kifedha ndizo zinazopima uhai wa biashara na kukuwezesha kufanya makadirio kwa siku zijazo.

Karen Berman, Joe Knight na John Case ambao ni waandishi na washauri wa mambo ya fedha kwenye biashara, kupitia kitabu chao kinachoitwa Financial Intelligence; A Manager’s Guide to Knowing What the Numbers Really Mean wametushirikisha namba muhimu za kibiashara ambazo kila mtu anapaswa kuzijua. Na pia wameeleza kwa lugha rahisi sana na kwa mifano inayoeleweka kuhusu taarifa tatu za kifedha ambazo kila mtu anapaswa kujua kuzisoma.

Kwenye makala hii ya leo nakwenda kukushirikisha faida kumi za kujua kusoma namba za kibiashara na taarifa tatu za kifedha unazopaswa kujua kuzisoma. Kwa uchambuzi zaidi wa kitabu hiki na jinsi ya kuandaa na kusoma namba zako mwenyewe, utapatikana kwenye TANO ZA JUMA.

Faida kumi za kujua kusoma namba za kibiashara.

Zifuatazo ni faida kumi za kujua kusoma namba za kibiashara.

1. Kujua mwenendo wa biashara yako. Kama unamiliki biashara, njia pekee ya kujua mwenendo wa biashara hiyo na kujua kila senti ya biashara hiyo iko wapi ni kupitia namba za biashara. Kama huna namba za kibiashara, huwezi kujua biashara inaendaje, utakuwa unafanya biashara kwa kubahatisha na mwishoni biashara hiyo itakufa. Kujua namba za biashara kunakuonesha wazi kama biashara inatengeneza faida au inapata hasara, kama inakua au inakufa.

2. Kukabiliana na ‘chuma ulete’. Kuna imani kali sana kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo kwamba kuna watu wana njia za kishirikina za kuweza kuondoa fedha kwenye biashara. Hivyo huwa wanabagua ni watu gani wa kuwahudumia na kwa wakati gani. Imani hii ni potofu, hakuna kitu kinachoitwa chuma ulete kwenye uhalisia, bali kinachosababisha biashara inapoteza fedha ni kutokuwepo kwa mfumo sahihi za kudhibiti fedha hizo. Unapojua kuziandaa na kuzifuatilia namba za kifedha kwenye biashara yako, utaona wazi fedha zinapotelea wapi, na hapo utagundua chuma ulete ni uzembe wako mwenyewe.

3. Kufanya maamuzi sahihi kiuwekezaji. Kuna wakati utapewa taarifa kuhusu fursa ya uwekezaji kwenye biashara nyingine, ambapo watu wanakuambia biashara hiyo inafanya vizuri sana. Wanakushawishi kwamba ukiweka fedha zako basi utapata faida kubwa. Kama utasikiliza maneno ya watu na kuweka fedha zako, umechagua kuzipoteza. Njia pekee unayoweza kujua kama kweli biashara inaendeshwa vizuri na inapata faida ni kupitia namba zake za kibiashara na taarifa za kifedha. Hivyo kama unataka kuwa mwekezaji mzuri, jua kusoma namba za kifedha kwenye biashara.

4. Kujua udanganyifu unaoweza kuwa umefanyika kwenye hesabu za kibiashara. Kama tulivyoona namba tatu hapo juu, utatumia namba za kibiashara na taarifa za kifedha kuchagua kama unaweza kuwekeza kwenye kampuni au la. Lakini siyo kwamba kila taarifa inayoandaliwa ni sahihi, hivyo ukiwa hujui kusoma kwa usahihi na vitu vya kuangalia, unaweza kuambiwa biashara inatengeneza faida kumbe ni faida ya kwenye vitabu, kiuhalisia hakuna faida. Na njia nzuri ya kupima afya ya biashara siyo kwenye hesabu za faida na hasara, bali kwenye hesabu za mizania. Kama biashara ina madeni mengi kuliko mali, ipo kwenye hali mbaya kifedha.

5. Kufanya maamuzi ya kuajiriwa na kampuni au taasisi kubwa. Watu wengi wanapoomba kazi kwenye kampuni na taasisi kubwa, huwa wanaamini taasisi hizo zinaendeshwa vizuri na hivyo watakuwa na usalama wa kipato. Ni mpaka pale wanapoajiriwa ndiyo wanakuja kugundua mambo siyo mazuri kama yanavyoonekana kwa nje. Pale anapoambiwa inabidi subiri, mshahara hautatoka kwa wakati kwa sababu kampuni haina fedha kwa wakati huo. Unaweza kuliona hili mapema kama unajua kuzisoma namba za kibiashara na kusoma taarifa za fedha za kampuni husika kabla hujaamua kuajiriwa nayo. Namba huwa zinaonesha wazi mwenendo wa kampuni au taasisi.

6. Kuchagua biashara sahihi ya kushirikiana nayo. Kama unafanya biashara na unataka kufanya maamuzi ya biashara itakayokuwa inakuuzia wewe malighafi au bidhaa muhimu, au unataka kuchagua biashara ambayo utakuwa unaiuzia bidhaa au huduma zako, ni muhimu kujua hali ya kifedha ya biashara unazotaka kushirikiana nazo. Kwa sababu unataka ushirikiano uwe wa muda mrefu na wenye manufaa kwa pande zote. Hivyo kujua kusoma taarifa za kifedha na kuzisoma kabla ya kuingia makubaliano na biashara nyingine, kunakuwezesha kufanya maamuzi sahihi na yenye manufaa.

7. Kuweza kujenga hoja za kutetea kile unachopendekeza. Kama umeajiriwa kwenye kampuni au taasisi kubwa, na una nafasi kama meneja, kuna wakati utahitaji kupata fedha zaidi au rasilimali zaidi kwenye kitengo chako. Sasa fedha na rasilimali muhimu huwa ni haba kwenye kampuni na taasisi nyingi, hivyo huwa zinatolewa kwa vipaumbele. Unapotaka kupata fedha au rasilimali kwa ajili ya kitengo chako, kama unajua kuzisoma taarifa za kifedha, utaweza kujenga hoja ya kutetea kwa nini ni muhimu kitengo chako kipewe fedha au rasilimali zinazohitajika, kwa sababu huenda sehemu kubwa ya faida inatengenezwa na kitengo hicho.

8. Kuweza kuthaminisha biashara. Kujua kuzisoma namba za kibiashara pamoja na taarifa za kifedha, kunakuwezesha kufanya tathmini kuhusu biashara husika na kujua thamani yake halisi. Hiki ni kitu muhimu unachopaswa kukijua kama unataka kununua au kuuza biashara. Thamani halisi ya biashara utaweza kuiona kupitia taarifa za kifedha na namba zilizopo, kuanzia mauzo, faida na mali pamoja na madeni ya biashara hiyo.

9. Kujua makisio na upendeleo uliotumika. Kwenye kila taarifa ya kifedha inayoandaliwa, huwa kuna makisio yanayofanyika. Kwa taratibu za kihasibu, makisio hayo yanapaswa kuelezwa kwenye taarifa hiyo ya kifedha. Hivyo unapojua kusoma taarifa hizi za kifedha, utaweza kujua makisio yaliyotumika kwenye kuiandaa. Wakati mwingine makisio hayo huwa siyo sahihi na hivyo kuathiri matokeo ya mbeleni. Lakini pia kila taarifa ya kifedha huwa ina upendeleo fulani (bias), kuna baadhi ya vitu vinaweza kuripotiwa au kutokuripotiwa sehemu sahihi na hivyo kuleta matokeo tofauti kwenye taarifa hiyo. Kwa kujua kusoma taarifa hizi, utaweza kuona wazi upendeleo uliofanyika na kutokustushwa na madhara yake ya baadaye.

10. Kuielewa lugha ngumu ya wahasibu kwa urahisi na kuweza kufanya maamuzi sahihi. Kila taaluma huwa ina lugha yake ngumu ambayo mtu wa nje siyo rahisi kuielewa. Madaktari wakiongea mbele yako, kama wewe siyo daktari unaweza usiambulie chochote, kadhalika kwa wanasheria. Wahasibu nao wana lugha yao ambayo kama wewe siyo mhasibu ni vigumu kuelewa. Wanaweza wakawa wanasema kitu cha kawaida kabisa, mfano faida, lakini wakatumia maneno mengi kiasi cha mtu wa kawaida kuvurugwa. Kwa Kiingereza faida ni profit, lakini wahasibu wanaweza kutumia maneno kama earnings, income au margin, yote hayo yana maana moja, lakini kama huelewi, utavurugwa. Kwa kuelewa kusoma taarifa za kifedha, utaweza kuelewa lugha hizo za kihasibu na kuzitumia kufana maamuzi sahihi.

Hizi ni faida kumi, kati ya nyingi utakazozipata kwa kujua kusoma namba za kibiashara na taarifa za kifedha.

Taarifa tatu za kifedha unazopaswa kujua kuzisoma.

Kuna taarifa tatu muhimu za kifedha unazopaswa kujua kuzisoma na kuzielewa kama unataka kufanikiwa kwenye biashara au chochote unachofanya.

Hapa nakwenda kukushirikisha taarifa hizo kwa ufupi na kwenye makala ya TANO ZA JUMA tutajifunza kwa kina jinsi ya kuandaa na kusoma taarifa hizi tatu na kuzitumia kufanya maamuzi muhimu.

MOJA; TAARIFA YA FAIDA NA HASARA (PROFIT AND LOSS STATEMENT)

Taarifa ya faida na hasara inaonesha kama biashara imepata faida au hasara kwa kipindi husika. Taarifa hii inajumuisha mapato ambayo biashara imeingiza na kuondoa matumizi ambayo biashara imegharamia. Kama mapato ni makubwa kuliko matumizi basi biashara inakuwa imepata faida. Na kama matumizi ni makubwa kuliko mapato biashara inakuwa imepata hasara.

Taarifa hii inaweza kuandaliwa kwa kipindi cha mwezi mmoja, kipindi cha miezi mitatu na kipindi cha mwaka mmoja. Muhimu ni yale yote yaliyofanyika kwenye kipindi husika yaweze kuingizwa kwenye hesabu hizi za biashara.

MBILI; TAARIFA YA MALI NA MADENI (BALANCE SHEET)

Taarifa ya mali na madeni au kama inavyojulikana kama mizania ni taarifa inayoonesha afya ya biashara kwa kipindi husika. Taarifa hii itaonesha kama biashara ina mali za kutosha kujiendesha kwa faida au ina madeni mengi na hivyo kuwa upande wa kufilisika.

Kwa kuangalia taarifa ya mizania, utaona kama biashara inajiendesha kwa faida au hasara, yaani kama ina mali nyingi au madeni mengi.

Taarifa hii huandaliwa kwa kipindi cha mwaka, lakini pia unaweza kuandaa kwa mwezi na kwa miezi mitatu kwa matumizi yako binafsi.

Hesabu hizi zikiandaliwa vizuri, lazima jumla ya mali na madeni ilingane. Lakini kwa kupitia kipengele kimoja kimoja utaweza kuona kama biashara ipo kwenye hali nzuri au mbaya. Mfano kama mtaji ni mkubwa kuliko mikopo, biashara inakwenda vizuri.

TATU; TAARIFA YA MZUNGUKO WA FEDHA (CASHFLOW STATEMENT)

Kwa lugha rahisi, mzunguko wa fedha ni kitendo cha fedha kuingia na kutoka kwenye biashara. Fedha zinaingia kupitia mauzo na fedha zitatoka kwa kupitia matumizi. Huu ndiyo mzunguko wa fedha, namna ambavyo biashara inatoa na kupokea fedha.

Mzunguko wa fedha unaweza kuwa chanya au ukawa hasi.

Mzunguko chanya wa fedha kwenye biashara ni pale fedha inayoingia kwenye biashara ni nyingi kuliko inayotoka. Hii ina maana kwamba mapato ni makubwa kuliko matumizi. Hapa biashara inabaki na fedha na ndiyo maana tunaita ni mzunguko chanya.

Mzunguko hasi wa fedha kwenye biashara ni pale ambapo fedha inayotoka kwenye biashara ni nyingi kuliko inayoingia. Hii ina maana kwamba matumizi ni makubwa kuliko mapato na hivyo biashara inapoteza fedha na kupata hasara. Hapa biashara inahitaji fedha zaidi ziingie kutoka vyanzo vingine ili kuinusuru.

Upo usemi maarufu kwenye biashara unaokwenda hivi; turnover is vanity, profit is sanity and cash flow is reality. Ukimaanisha; mauzo ni ubatili, faida ni usafi, mzunguko wa fedha ndiyo uhalisia.

Mzunguko wa fedha ndiyo unatuonesha kwa uhalisia biashara ipo kwenye hali gani. Mauzo na faida siyo vipimo vya uhakika kwenye kujua ufanisi wa biashara.

Rafiki, kwenye uchambuzi wa kitabu hiki cha Financial Intelligence nitakushirikisha kwa kina na kwa mifano kuhusu taarifa hizo tatu ni jinsi unavyoweza kuzisoma na kuzifanyia kazi kwenye biashara yako.

ZAWADI; Siku siyo nyingi nilitoa zawadi ya chati yenye namba za biashara ambayo unaweza kuitumia kudhibiti mzunguko wa biashara yako. Watu wengi wamejipatia chati hiyo na mafunzo mengine muhimu kuhusu namba za biashara. Kama wewe bado hujapata zawadi hii niliyoitoa bure kabisa, ipate sasa kuwa kuandika email kwenda maarifa@kisimachamaarifa.co.tz kwenye email andika NAOMBA ZAWADI YA NAMBA ZA BIASHARA. Utatumiwa zawadi hiyo bure kabisa kwenye email yako.

Karibu kwenye channel ya TANO ZA JUMA ili kupata uchambuzi kamili wa kitabu Financial Intelligence na vitabu vingine vingi. Kwa sasa makala ya TANO ZA JUMA itakuwa haipatikani tena kwenye AMKA MTANZANIA kama awali, bali itapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA pekee. Soma hapo chini kupata maelezo ya kujiunga na channel hiyo muhimu sana kwako kujifunza zaidi.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpendwa, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
 
Wafanyabiashara wadogo na wakati (SME) wamekuwa wakiendesha biashara zao kwa mazoea badala ya kuongozwa kwa namba muhimu zinazoweza kuwasaidia kupima ukuaji wa namba zao.

Kwa wale ambao wanataka kutoka kwenye mazoea hayo na kuweza kupima ukuaji halisi wa biashara zao, ipo zawadi ya chati muhimu za kupima namba hizo.
Karibu sana ujipatie chati hiyo, maelekezo ya kuipata yapo kwenye makala hapo juu.
 
Huu uzi mzuri ila hauna wachangiaji ungekuwapo uzi wa link za kunua m*lay* telegram ungukwa na page 100+ saizi
 
9 Reactions
Reply
Back
Top Bottom