Fahamu PANOPTICONISM na jinsi inavyoweza kusigina haki na uhuru wa raia

Mtafiti77

JF-Expert Member
Oct 31, 2011
1,842
2,272
Kwa mujibu wa kamusi ya mtandaoni ya Cambridge, “panopticon” ni gereza ambalo vyumba vyake vimejipanga kimzunguko kiasi cha wakazi wake kuweza kuonekana kutokea katikati. Kwa kawaida katikati ya jengo hili kunakuwa na jengo mithili ya mnara kama ule wanaoutumia waongoza ndege. Ndani ya jengo hili kunakuwa na askari anaepiga doria (tazama hapa panopticon. Aidha, japo wafungwa hufahamu uwepo wa ulinzi huu, mara nyingi hawana uwezo wa kuthibitisha uwepo wa mlinzi katika mnara huo. Kwahiyo, wafungwa hudhibitiwa kifikra na hivyo kuwa watiifu ndani ya gereza bila ya kutumia nguvu kubwa.

Dhana ya “Panopticon” inahusishwa na mwanafalsafa wa Kiingereza, Jeremy Bentham. Hata hivyo, kwa mujibu wa Thomas McMullan kwenye makala yake aliyoyaita “The power of privacy Technology” na kuchapishwa kwenye jarida la The Guardian mnamo tarehe 23 Julai, 2015, Bentham alipata wazo la kubuni aina hii jengo kutoka kwa kaka yake aliyeishi na kufanya kazi huko Krichev, Belarus mwishoni mwa miaka ya 1780. Huko alimuona kaka yake akiwa anasimamia vibarua akiwa amekaa kwenye dawati lililokuwa katikati yao. Hapo Bentham akaona inawezekana kuja na aina hii ya jengo ambapo si tu gereza, bali viwanda, mahospitali, mashule n.k., vinaweza kutumia ubunifu huu kudhibiti watu wanaoishi kwenye majengo hayo.

Katika kukosoa dhana hii na utendaji wa dola, mwaka 1975 mwanafalsafa Michel Foucault kutoka Ufaransa alionesha kuvutiwa na nadharia ya Bentham. Katika kitabu chake maarufu, “Discipline and Punish: The birth of prison,”Foucault anakosoa vikali dhana ya “panopticon.” Kwake anaona hii ni namna ya tabaka tawala au mamlaka fulani kuwadhibiti na kuwakandamiza watu wake,yani, “panopticonism”. Kwa maana nyingine Foucault alijiongeza, hakubaki gerezani pekee. Kwahiyo,vile namna dola ama mamlaka fulani zinavyodhibiti taarifa; vile namna dola au mamlaka fulani hunyamazisha watu wake kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama; vile namna vyombo hivi vinapeleleza na kuweka sheria kali dhidi ya raia na vyombo vya habari ni mifano ya “panopticonism.” Hali hii ikikomaa, raia huwa sawa na mnyama aliyefugwa, ni sawa na mfungwa aliye kwenye gereza la “panopticon.” Hapa wakati wote anakuwa mtiifu kwa dola ama taasisi bila ya kujali aliyepo madarakani ni nani au anafanya nini kuhusu maslahi ya nchi, taasisi, raia au wafanyakazi. Maisha ya “panapticonism” wakati wote huelemea upande mmoja.

Kwa mujibu wa Thomas, dhana ya “panopticonism” ni pana na tata hasa katika kipindi hiki cha teknolojia. Wakati katika “panopticon” ya Bentham na kwa kiasi fulani matumizi ya kamera za CCTV watumiaji wa maeneo hayo wanaweza kufahamu uwepo wa ulinzi, kwenye mtandao “panopticonism” hufanyika kimyakimya. Si rahisi kujua mpelelezi yupo wapi. Unaweza kudhibitiwa kutoka upande wowote ulimwenguni.

Kwa kifupi, tumeweza kuona namna ambavyo Benthan alibuni dhana ya “panopticon.” Kisha baadae Foucault akaitumia dhana hii kama sitiari(metaphor) kuonyesha vile mamlaka zinaweza kuwadhibiti raia katika namna isiyo sahihi. Baadhi ya viongozi hutumia sana mfumo huu kuwajaza watu hofu kwa vitisho na ikibidi kuwafunga ama kuwaua, mradi tu baada ya muda fulani, raia wajikute ni mazezeta wasioweza kuhoji haki na uhuru wao. Hali hii hubinya maendeleo ya kweli.

Je, kwa kiasi gani nchi yako inatumia panopticonism?

Mtafiti77
 
Back
Top Bottom