Fahamu kuhusu tatizo la homa kwa watoto wadogo na tiba yake

Dr. Wansegamila

JF-Expert Member
Feb 3, 2012
2,954
8,093
Awali ya yote, ningependa kuelezea maana ya neno “homa” kitaalamu, maana naelewa kuwa, kuna maana nyingi sana za neno hili ki-mtaani mtaani. Kitaalamu, maana ya homa ni hali ya mwili kuwa na joto kuliko kawaida. Kwa wastani, joto la mwili huwa sentigredi 37. Pia, ningependa kushauri kuwa, kama wewe ni mzazi mwenye mtoto wa chini ya miaka mitano, basi ni muhimu sana wewe kuweza kumiliki kipima joto (theremometer) hapo nyumbani, na kuifahamu jinsi ya kuitumia (nashauri umiliki thermometer ya digitali,kwani ni rahisi sana kuitumia). Nimeamua kuandika makala hii baada ya kuona kuna ongezeko kubwa sana la matumizi ya dawa za kupunguza homa kwa watoto katika jamii yetu, hata pale ambapo mimi kama mtaalamu unaona kabisa hakuna umuhimu wowote wa mtot kupewa dawa ya kutuliza homa.

Kwa watoto chini ya miaka mitano, joto la kawaida la mwili huwa kati ya 36 sentigredi hadi 37.4. Hivyo basi, kitaalamu, joto likizidi sentigredi 37.4 (kuanzia sentigredi 37.5), basi hapo tunasema kuwa mtoto ana homa.

Je, unapaswa kuwa na wasiwasi kila mara mtoto wako anapopata homa? Na ni zipi njia bora za kuitibu?

Kitaalamu, homa ambayo joto la mwili ni kati ya sentigredi 37.5 na 38.4 huitwa “low grade fever” (homa ya kiwango cha chini), na ile ambayo ni zaidi ya sentigredi 38.5 huitwa “high grade fever (homa ya kiwango cha juu).Homa ya kiwango cha chini, mara nyingi husababishwa na vijidudu aina ya virusi (kama vile virusi vya mafua), ambavyo mara nyingi hupona tuu yenyewe bila kuhitaji msaada wa dawa ya aina yoyote. Lakini, homa ya kiwango cha juu mara nyingi husababishwa na vijidudu aina ya bakteria ambao mara nyingi itahitajika msaada wa dawa kupambana na vijidudu hivi, hivyo ni busara kumpeleka hospitali mtoto kwa ushauri wa kitabibu.

Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Watoto cha Johns Hopkins huko Baltimore, Maryland, Marekani, asilimia 91 ya wazazi waliamini kwamba “hata homa kidogo tu inaweza kusababisha angalau tatizo moja kama vile mshtuko wa moyo au kuharibu ubongo.” Uchunguzi huo unaonyesha kwamba “asilimia 89 ya wazazi waliwapa watoto wao dawa za kupunguza homa kabla ya joto la mwili wa mtoto kufikia nyuzi 102 za Fahrenhaiti (nyuzi 38.5 za Sentigredi).”

Umuhimu wa Homa

Homa husababishwa na nini? Ingawa kwa kawaida joto la mwili huwa nyuzi sentigredi 37 (linapopimwa kwenye mdomo), linabadilika-badilika kwa nyuzi moja au zaidi siku inapoendelea.* Kwa hiyo joto la mwili wako linaweza kuwa chini asubuhi na kuwa juu jioni. Sehemu fulani inayoitwa hypothalamus, iliyoko chini ya ubongo, hudhibiti joto la mwili. Homa hutokea wakati mfumo wa kinga unapotokeza vitu fulani katika damu vinavyoitwa pyrogen, labda unaposhambuliwa na bakteria au virusi. Hiyo hufanya hypothalamus iongeze joto la mwili.

Ingawa homa inaweza kusababisha maumivu na kupunguza maji mwilini, si kwamba ni mbaya. Kulingana na Taasisi ya Mayo ya Elimu na Utafiti wa Kitiba, homa husaidia mwili sana kuondoa bakteria na virusi. “Virusi vinavyosababisha mafua na magonjwa mengine ya kupumua husitawi wakati wa baridi. Homa kidogo inaweza kusaidia mwili kuondoa virusi hivyo.” Taasisi hiyo inasema kwamba “haifai kutibu homa kidogo kwani inaweza kudhoofisha kinga ya mtoto.” Hospitali moja nchini Mexico hata hutibu magonjwa fulani kwa kuongeza joto la mgonjwa.

Dakt. Al Sacchetti wa Chuo cha Marekani cha Madaktari wa Dharura anasema: “Mara nyingi homa si ugonjwa lakini inaweza kuwa dalili ya ugonjwa. Hivyo mtoto anapokuwa na homa, unapaswa kuzingatia afya yake badala ya kuwa na wasiwasi kuhusu joto lake.” Chuo cha Marekani cha Tiba ya Watoto kinasema: “Hupaswi kumpa mtoto wako dawa akiwa na kiwango cha joto chini ya nyuzi za sentigredi 38.5 ila tu ikiwa anaumwa au hupatwa na degedege mara kwa mara. Hata joto la mwili wake likiwa juu zaidi hilo si hatari, isipokuwa awe na degedege au ugonjwa mwingine hatari. Ni vizuri kumfahamu. Ikiwa anakula na kulala vizuri, anacheza vizuri, basi hahitaji matibabu yoyote.”

Kutibu Homa Isiyo Kali

Haimaanishi kwamba huwezi kufanya lolote kumsaidia mtoto wako. Madaktari fulani hutoa madokezo yafuatayo ya kutibu homa isiyo kali: Hakikisha chumba cha mtoto hakina joto sana. Mvishe mavazi mepesi. (Mavazi mazito yanaweza kuongeza homa.) Mpe mtoto vinywaji kama vile maji, maji ya matunda yenye maji mengi, na supu, kwa sababu homa inaweza kumfanya aishiwe na maji.* (Vinywaji vyenye kafeini kama vile kola au chai isiyo na maziwa, vinaweza kumfanya apoteze maji zaidi.) Watoto wachanga wanapaswa kuendelea kunyonyeshwa. Epuka vyakula ambavyo havisagiki kwa urahisi kwani homa hupunguza utendaji tumboni.

Mara nyingi mtoto hupewa dawa za dukani za kutuliza maumivu kama vile acetaminophen (panadol) au ibuprofen joto lake linapopita nyuzi za sentigredi 38.5(hakikisha unafuiata maelekezo ya mfamasia). Dawa za kupunguza homa haziui virusi hivyo, hazitibu mtoto mafua au magonjwa mengine kama hayo, ingawa zinaweza kupunguza maumivu. Ni muhimu kutambua kuwa dawa hizi zina madhara makubwa iwapo zitatumiwa kila mara, bila kufuata ushauri wa kitaalamu. Siku zote kumbuka kuwa “SI KILA MARA MTOTO ANAPOPATA HOMA, BASI APEWE PARACETAMOL/PANADOL” unaumiza ini la mtoto wako bila sababu ya msingi.

Homa inaweza kutulizwa pia kwa kumwosha mtoto. Mweke ndani ya beseni yenye maji kidogo yaliyo vuguvugu na umwoshe kwa sifongo. (Usitie dawa yenye alkoholi kwenye maji hayo kwani inaweza kumdhuru.)

Kwa vyovyote vile, jambo unalopaswa kuzingatia ni kumpunguzia mtoto wako maumivu. Kumbuka, haielekei kwamba homa itasababisha ugonjwa wa mfumo wa neva au kifo. Ingawa homa inatisha wakati inaposababisha degedege, mara nyingi inafifia baadaye.

Bila shaka kuzuia ni bora kuliko kuponya, hivyo njia bora zaidi ya kumkinga mtoto wako na magonjwa ni kumfundisha kuhusu usafi. Watoto wanapaswa kufundishwa kunawa mikono mara kwa mara, hasa kabla ya kula, baada ya kwenda kujisaidia, baada ya kuwa mahali penye watu wengi, au baada ya kumshika mnyama. Mtoto wako anapopata homa hata baada ya jitihada hizo zote, usiwe na wasiwasi. Kama tulivyoona, unaweza kumsaidia mtoto wako apate nafuu.
 
Dr asante kwa ushauri! Nimetafuta huu uzi baada ya kuona mwanangu joto limepanda sana usiku! Je huduma gani ya kwanza anapaswa kupatiwa mara hali hii inapojitokeza? Pia anakohoa mara kwa mara! Hii ni dalili ya nin?
 
Back
Top Bottom