Fahamu Kuhusu Ruzuku (Grant)

Jun 21, 2021
5
10
1625420281905.png


Ruzuku ni kiasi cha fedha kinachotolewa na mashirika binafsi ya hisani (charitable giving foundation), mashirika ya ya umma ya hisani (public charity) au wakala/Taasisi za serikali (government agencies/insitutions) kwa asasi za kiraia (Civil Society Organizations) ili kuziwezesha kutekeleza shughuli mbalimbali kwa lengo la kuleta maendeleo katika jamii. Taasisi/kampuni za kibiashara pia huweza kuwa chanzo cha upatikanaji wa fedha hizi kupitia kwenye program zao za kusaidia jamii (corporate funding programs).

Pendekezo la Ruzuku (Grant Proposal)
Hili ni andiko linaloandaliwa na muombaji wa ruzuku lenye kuonyesha mtiririko wa shughuli ambazo muombaji atazifanya, muda atakaotumia kuzikamilisha na kiasi cha fedha atakachohitaji ili aweze kutatua tatizo linaloikumba jamii fulani na hatimae kufikia lengo lake yeye kama Taasisi na lengo la mfadhili. Andiko hili linapaswa kuonyesha vitu vifuatavyo;
  • Tatizo linaloenda kutatuliwa, ni lazima tatizo lielezwe kimamilifu na kinaga ubaga
  • Gharama zitakazotumika kutatua tatizo hilo
  • Matokeo yanayotarajiwa (expected results) baada ya tatizo husika kutatuliwa
Baada ya pendekezo la ruzuku kukubaliwa na mfadhili, hufanyika makubaliano kwa kuandaa mkataba baina ya muombaji wa ruzuku na mfadhili. Mkataba ukishasainiwa muombaji wa ruzuku hutambulika kama "grantee" hivyo atapaswa kuutekeleza mradi kama ambavyo ameaininsha katika pendekezo lake, kinyume cha hapo atakuwa amekiuka mkataba.

Taasisi zinazostahili kupata RUZUKU?
Mara nyingi ruzuku zinazotolewa hulenga Asasi za Kiraia zenye usajili (registered civil society organizations) ambazo huweza hujumuisha NGOs, Taasisi za kidini (faith-based organizations), Makundi ya kijamii (community-based organizations), jumuiya za makundi mbalimbali kama 'Professionals' Societies' n.k. Wakati mwingine ruzuku huweza kutolewa kwa makundi ya kijamii yasiyo na usajili (unregistered community-based organizations), ili kupata ruzuku, kundi husika hupaswa kutafuta Taasisi yenye usajili na kuifanya kuwa mdhamini wake.

Ruzuku pia huweza kutolewa kwa kampuni za kibiashara au mawazo ya kibiashara. ili kampuni au wazo husika liweze kupata fedha, muombaji anapaswa kuwasilisha pendekezo la ruzuku lenye sifa zifuatazo;
  • Mradi wa kibiashara unaoombewa ruzuku uwe na uwezo wa kusaidia jamii kwa kiasi kikubwa
  • Uandaaji wake uwe na ubunifu
Mtu mmoja mmoja pia huweza kulengwa na mfadhili kwa ajili ya kupata ruzuku, mara nyingi ruzuku zinazoelekezwa kwa mtu mmoja mmoja huusiana na masomo (scholarship) au utafiti (research grant)

Aina na Matumizi ya Ruzuku/Msaada kutoka kwa Mfadhili
  • Ruzuku Mtaji (Capital Grant): Hii ni ruzuku ambayo hutumiwa kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya Taasisi, kwa mfano ujenzi wa jengo la Taasisi, Ukarabati n.k
  • Ruzuku kwa ajili ya kuendesha shughuli za kila siku za Taasisi (General Operating Grant) ruzuku hii hutumika kwa ajili ya kulipa posho watendaji wa Taasisi, kulipia "bills" za umeme, maji n.k
  • Msaada wa Kiufundi (Technical Assistance): Aina hii ya msaada huusiana na Mfadhili kuijengea uwezo Taasisi husika katika maeneo mbalimbali kama Usimamizi wa Fedha, Usimamiaji wa Miradi, Usimamizi wa Mifumo ya Mawasiliano n.k
  • Challenge Grant (nashindwa kuweka kiswahili chake hapa)., hii maaana yake ni kwamba, kuna kipindi mfadhili anaweza kukutaka kwamba ili akupatie kiasi cha fedha unachohitaji kwake, ni lazima wewe kama Taasisi utafute kiasi kidogo kwanza kutoka kwenye vyanzo vingine.
  • Ruzuku kwa ajili ya jaribio/mfano (Demonstration Grant) hii ni ruzuku ambayo hutolewa na Mfadhili kwa aina ya miradi ambayo haikuwahi kufanyika hapo kabla, ikiwa utekelezaji wa miradi hii utafanikiwa, basi itakuwa ni "model" au mfano wa kuigwa kwa sehemu zingine.
  • Ruzuku za Uanzilishi (Start-Up Grant) Hii ni aina ya ruzuku ambayo hutolewa kwa lengo la kuanzisha Mradi mpya au kuanzisha Taasisi, kwa kitaalamu tunaita "seed grant"
Mafanikio ya Taasisi yoyote hutegemea uwepo wa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ambayo itapelekea malengo ya Taasisi husika kufikiwa. Hivyo Uongozi wa Taasisi kwa kushirikiana na Afisa Rasilimali (Resource Mobilization/Acquisataion Officer) unapaswa kuangalia aina ya ruzuku inayowafaa/wanayohitaji na kufuata hatua zinazopaswa kutumika ili kuomba aina hiyo ya ruzuku/msaada. KUMBUKA; kila aina ya ruzuku/msaada ina utaratibu wake wa kuomba.

Ahsante
 
Nakushukuru kwa hii elimu, ingependeza pia kuwepo na muendelezo au ufafanuzi zaidi hizo hatua za kupitia ili kupata, na watoaji ni kina nani, mfano mimi au kikundi chetu tukiwa na hilo andiko tunapitia taratibu zipi na hao watoa ruzuku ni wepi!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom