Fahamu kosa la “defamation” kama lilivyoainishwa kwenye Sheria ya Huduma za Habari namba 12

tabibumtaratibu

JF-Expert Member
May 29, 2011
2,405
1,181
FAHAMU KOSA LA “DEFAMATION” KAMA LILIVYO AINISHWA KWENYE SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI NAMBA 12 YA MWAKA 2016 (The Media Services Act, 2016)

Ndugu msomaji, yamkini si mara yako ya kwanza kusikia neno “Defamation” ambalo kwa tafsiri ambayo sio rasmi linajulikana kama “Kudhalilisha”. Sheria mpya inayojulikana kama sheria ya huduma za habari,2016 (The media services Act, 2016) ambayo imefuta sheria ya Magazeti (The Newspapers Act, No.3 of 1976) imeainisha kosa hili katika SURA YA TANO kama ifuatavyo.

“Defamation” ni nini?

Kwa mujibu wa kifungu cha 35 kifungu kidogo cha 1 sheria ya Huduma za habari imefafanua kuwa “jambo lolote ambalo likichapishwa na kusambazwa linaweza kuharibu hadhi ya mtu, au utu wake au kuibua chuki dhidi yake au kuharibu kazi au fani ya mtu huyo, ni jambo la kudhalilisha”

Nanukuu: Section 35(1) “any matter which, if published, is likely to injure the reputation of any person by exposing him to hatred, contempt or ridicule, or likely to damage any person in his profession or trade by an injury to his reputation, is defamatory matter”.

Hivyo basi kudhalilishwa ‘Defamation’ ni hali inayojitokeza kwa mtu yoyote pale ambapo jambo la kudhalilisha limechapwa na kusambazwa dhidi yake na kupelekea kuharibu hadhi ya mtu huyo, utu wake au kuibua chuki dhidi yake au hata kuharibu kazi au fani ya mtu huyo. Kwa mujibu wa kifungu tajwa hapo juu mtu yeyote anaelalamika kuwa amedhalilishwa ni lazima ithibitike/athibitishe mbele ya mahakama kuwa:-

a) Jambo lililochapishwa ni la kudhalilisha.

Kujua kama jambo lililochapishwa ni la kudhalilisha au la ni lazima mkazo utiiwe kwenye jambo lenyewe, pia inategemea na mazingira sababu inawezekana jambo likawa la kudhalilisha kwenye jamii moja lakini lisiwe la kudhalilisha kwenye jamii nyingine.

b) Jambo la kudhalilisha lililochapishwa ni lazima liwe limeelekezwa kwa mtu anaelalamika

Hii inamaana kuwa endapo jambo la kudhalilisha limechapishwa na kuelekezwa kwa kikundi cha watu wengi au jamii nzima basi mtu mmoja kutoka kwenye kikundi au jamii hiyo hawezi kwenda na kulalamika kuwa amedhalilishwa.

c) Jambo la kudhalilisha lililochapwa limesambazwa

Hii inamaana kuwa jambo la kudhalilishwa ni lazima liwe limefichuliwa kwenye jamii ya watu wengi. Tambua kua kama usambazaji wa jambo hilo umefanywa na mtu aliedhalilishwa mwenyewe basi mtu hawezi kulalamika kuwa amedhalilishwa bali kwa mazingira hayo itasemwa kuwa mtu huyo amejidhalilisha mwenyewe hivyo kosa la defamation haliwezi kuwepo.

d) Jambo lakudhalilisha lililosambazwa ni lazima liwe limesababisha madhara(damage) kwa mtu aliedhalilishwa.

Hiki ni kipedhele muhimu sana kuthibitika mbele ya mahakama. Madhara yanaweza yakawa ni kufukuzwa kazi,Kuharibu biashara, msongo wa mawazo, kukosa kuaminiwa, kushuka hadhi katika jamii n.k.

KUMBUKA: Vipengele vyote hapo juu (a-d) vinakwenda sambamba, hivyo basi mlalamikaji akishindwa kuthibitisha mbele ya mahakama vipengele hivyo anaweza akashidwa kabisa au akashinda nusu kesi ya defamation.

Je marehemu anaweza kudhalilishwa?

Kwa mujibu wa kifungu cha 35 (2) cha sheria ya huduma za habari, kama jambo la kudhalilisha kama lilivyo elezwa kwenye kifungu kidogo cha kwanza hapo juu litabaki kuwa jambo la kudhalilisha hata kama jambo hilo litachapwa na kusambazwa dhidi ya marehemu.

Nanukuu Section 35(2) “The matter referred to under subsection one (1) shall qualify to be a defamatory matter even when it is published against a deceased person.”

Hivyo basi, ndugu msomaji tambua kwamba marehemu pia anaweza kudhalilishwa. Lakini kwa mujibu wa kifungu cha 35 (3) cha sheria ya huduma za habari, kesi ambayo marehemu amedhalilishwa haiwezi kupelekwa mahakamani mpaka pale mkurugenzi wa kuendesha mashtaka ya uma (Deirector of public prosecutor) atakapoidhinisha.

Nanukuu Section 35 (3) ‘the prosecution for the publication of defamatory matter concerning a person who is dead shall not be instituted without the written consent of the Director of Public prosecution.’

Aina za defamation

Kimsingi zipo aina kuu mbili za defamation

i. Defamation ya kudumu (libel-Defamation in permanent form) kwa kutumia Michoro, picha,maandishi, nembo n.k

ii. Defamation ya muda (slander-Defamation in temporary form) kwa kutumia maneno au vitendo vya kudhalilisha.

Ndgu Msomaji, sheria ya huduma za habari inatambua aina ya kwanza ya defamation ambayo ni Defamation ya kudumu chini ya kifungu cha 36 (1) ambacho kinasema kwamba ‘mtu atakua amefanya defamation ya kudumu kama akichapisha, akiandika, akichora au kwa vyovote vile akitoa jambo la kudhalilisha kwa njia ya kudumu aidha kwa njia ya maonyesho, kwa kusoma, kurejea, kuelezea au kutoa au vinginevyo kwa njia ambayo inajulikana au inaweza kujulikana na mtu aliedhalilishwa au mtu mwingine yeyote.’

Nanukuu: Section 36 (1) A person shall be deemed to make publication of a libel if that person causes the print, writing, painting, effigy or other means by which the defamatory matter is conveyed, to be dealt with, either by exhibition, reading, recitation, description, delivery or otherwise, in a way that the defamatory meaning thereof becomes known or is likely to be known to either the person defamed or any other person.

Kwa mujibu wa kifungu cha 36 (2) haijalishi defamation hiyo ya kudumu imefanyika kwa mafumbo au imetaja dhahiri muhusika. Hii inamaana kwamba hata kama mtoa habari akitoa jambo la kudhalilisha kwa njia tajwa hapo juu kwa mafumbo lakini watu wakaelewa au wakamtambua mlengwa wa jambo hilo bado anaweza kushtakiwa kwa kosa la defamation.

Ndugu msomaji, Ni muhimu kutambua kua defamation ya kudumu pia ni kosa la jinai. Hivyo Mtu atakaetenda kinyume na vifungu tajwa vya sheria ya huduma za habari hapo juu anaweza akashtakiwa kwa mujibu wa sheria hii na sheria nyingine zinzoshughulikia makosa ya jinai.

Je ni wakati gani ambapo sheria inaruhusu usambazaji wa jambo la kudhalilisha? (Exceptions for publications of defamatory matter)

Msomaji unaweza kujiuliza “Je sheria ya huduma za habari inakataza kabisa usambazaji wa jambo la kudhalilisha?” jibu ni HAPANA. Kwa mujibu wa sheria hii chini ya kifungu cha 37 (1) inaruhusiwa mtu kusambaza jambo lakudhalilisha kama:-

a) Jambo hilo ni la kweli na unalisambaza kwa manufaa ya jamii (hapa kunahitaji umakini zaidi kwa sababu jambo linaweza kuwa la kweli lakini Je unalisambaza kwa manufaa ya jamii?)

b) Jambo hilo limesambazwa na mtu mwnye kinga ya kisheria.

Vyombo/taasisi /Watu wenye Kinga ya kisheria juu ya usambazaji wa jambo lakudhalilisha

Kinga juu ya usambazaji wa jambo lakudhalilisha imegawanyika katika makundi makuu mawili

1) Kinga kabisa (absolute privilege)

Kinga hii ni ya moja kwa moja.Inatumika kumtoa mtu kwenye kosa la defamation bila masharti yoyote.

2) Kinga ya masharti (conditional privilege)

Kinga hii inatumika tu endapo mashrti husika yamekidhiwa.

Ifahamike kuwa kifungu cha 38 (1) cha sheria ya huduma za habari inatoa kinga kabisa (absolute privilege) kwa Vyombo/taasisi/watu/ wafuatao kutoshitakiwa kwa kosa la defamation kama watatoa au kusambaza jambo la kudhalilisha katika mazingira yafuatayo.

a) Kama Raisi,serikali, au bunge litasambaza jambo la kudhalilisha kwenye nyaraka zozote za ofisi au mahakamni (legal proceedings)

b) Kama Raisi, serikali, au mbunge au speaker wa bunge atasambaza jambo la kudhalilisha akiwa Bungeni.

c) Kama jambo la kudhalilishwa limesambazwa kwa amri ya Raisi au serikali.

d) Kama jambo la kudhalilisha lililosambazwa linamuhusu mwanajeshi ambae ana kosa la kinidhamu na aliesambaza jambo hilo lazima awe na mamlaka ya kusambaza.

e) Kama jambo la kudhalilisha limetolea wakati kesi inaendelewa mahakama ni (Legal proceeding) na hakimu, wakili, shahidi au mzee wa baraza (assessor).

f) Kama jambo la kudhalilisha limesambazwa na mtu ambae analazimika kisheria kulitoa jambo hilo.

Lakini pia hata kama jambo la kudhalilishwa limekingwa na sheria ya huduma za habari kama nilivyobainisha hapo juu haizuii msambazaji wa jambo hilo kushitakiwa aidha kwa kosa la jinai au madai kama jambo alilosambaza linakatazwa na sheria nyingine au na katiba ya nchi. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 38(3) cha sheria ya huduma za habari.

Nanukuu: Section 38(3) “Nothing in this section shall exempt any person from any liability of a civil or criminal nature under any other Part of this Act or under any other written law if the publication of a matter alleged to be absolutely privileged is prohibited or the relief to a person injured is available under the Constitution of the United Republic.”

Kinga ya masharti dhidi ya usambazaji wa jambo linalidhalilisha inatolewa chini ya kifungu cha 39 cha sheria ya huduma za habari . Kwa mujibu wa kufungu hicho usambazaji wa jambo lakudhalilisha utakua na kinga ya masharti endapo msambazaji amesambaza jambo la kudhalilisha kwa nia njema si nia ya kumdhalilisha mtu au Kama mlalamikaji na mlalamikiwa walikua kwenye uhusiano ambayo mlalamikiwa alilazimika kisheria, kimaadili au kijamii kusambaza jambo hilo dhidi ya mlalamikaji na nilazima usambazaji huo uwe umefanyika kwenye mazingira yafuatayo.

a) Kama jambo lakudhalilishwa limesambazwa Kwenye uchambuzi wa makala inayochambua mwenendo wa kesi lakini itakua ni kosa la defamation kama mahakama ilipiga marufuku kwa case husika kuchambuliwa.

b) Kama jambo la kudhalilishwa limechapishwa na kusasambazwa na mtu ambae anatoa maoni yake kwa nia njema juu ya utendaji kazi wa mfanyaakazi wa uma..

Nafuu anazoweza kupata mtu ambae anashutumiwa kusambaza jambo la kudhalilisha.

· Nafasi ya kubadilisha/kureebisha jambo hilo (offer to amend)

Nafuu hii inatolewa chini ya kifungu cha 40 (1) cha sheria ya huduma za habari. Kwa mujibu wa kifungu hicho mtu aliesambaza jambo la kudhalilisha ataomba nafasi ya kubadilisha au kurekebisha jambo hilo kwa mtu aliemdhalilisha endapo tu atasema kwamba alisambaza jambo hilo akiwa hajui kuwa lilikua ni jambo la kudhalilisha

Endapo ombi hili likikubaliwa na mtu aliedhalilishwa basi hakuna kesi yoyote ya defamation( aidha ya defamation ya kudumu au ya muda) itakayofunguliwa au kama ilishafunguliwa basi kesi hiyo haitaendelea dhidi ya mlalamikiwa.

Nini Kitatokea endapo ombi la nafasi ya kubadilisha litakataliwa?

Kama mlalamikaji(mtu aliedhalilishwa) atakataa ombi la nafasi ya kubadilisha jambo la kudhalilisha aliloletewa na mlalamikiwa (mtu aliedhalilisha) basi itakua ni utetezi (defence) wa mlalamikiwa katika kesi ya defamation itakayo funguliwa na mlalamikaji kuwa:

i. Alisambaza jambo hilo akiwa hajui kuwa lilikua ni jambo la kudhalilisha

ii. Na aliomba nafasi ya kubadilisha jambo hilo haraka sana baada tu ya kujua kuwa jambo hilo lilikua linamdhalilisha mlalamikaji.

Je mtu aliedhalilishwa anatakiwa afanye nini?

Kwa mujibu wa kifungu cha 41 cha sheria ya huduma za habari mtu yeyote atakaeona kuwa machapisho au vyombo vya habari vimotoa jambo la kumdhalilisha kwa njia za kieletronic mtu huyo anaweza kufungua kesi mahakamani kwa ajili ya kudai fidia.

Sababu za kujitetea(possible defense) kwa mtu anaeshtakiwa kwa kosa la defamation

Mshatakiwa wa kosa la defamation anaweza akaachwa huru au akapunguziwa adhabu endapo mshtakiwa/mlalamikiwa ataiambia mahakama kati ya sababu zifuatazo.

1) Jambo la kudhalilisha alilolisambaza haliku mlenga mlalamkaji.

2) Mlalamikaji ndie aliesambaza jambo hilo.

3) Jambo hilo ni la kweli na alilisambaza kwa manufaa ya jamii.

4) Kama ana kinga kabisa au kinga ya masharti juu ya usambazaji wa jambo la kudhalilisha.

5) Nakadhalika



Hitimisho

Ndugu msomaji mpaka kufikia hapa natumaini kuwa umeelewa vizuri kosa la udhalilishaji, yaani “defamation”. Ni rai yangu kwa waandishi wa habari na jamii kwa ujumla kutambua uwepo wa sheria hii na kufanya kazi kwa weledi ili kuepuka kuingia mkononi mwa sheria pindi wanapotoa machapisho yenye maudhui ambayo kisheria yatahesabika kua ni ya kidhalilishaji.

Imeandaliawa na;

Isack Kimaro (Mwanasheria)

+255 (0) 656673686
 
Na kesi zake zinaweza kuchukua muda gani hadi kwenye hukumu?

Sent from my SM-G610F using JamiiForums mobile app
 
Nashukuru mleta mada. na Kuanzia leo nitakuwa rafiki wa hili jukwaa la sheria.

Sent from my E6883 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom