Fahamu haya kabla ya kutuma picha yako ya faragha mtandaoni

Status
Not open for further replies.

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
624
934
Sext.jpg
Umeshawahi kukutana na picha za ngono mtandaoni? Bila shaka jibu ni ndiyo. Ipo mitandao (porn sites) iliyojikita mahususi kwa ajili ya kutengeneza na kuonesha picha ama video za ngono. Mara nyingi, picha au video zinazopatikana katika mitandao hiyo huwekwa kwa makubaliano baina ya mitandao hiyo na wahusika wanaoonekana katika picha au video hizo.

Tuache mitandao hiyo kwa sasa, tuzungumzie zile picha za faragha zinazoweza kusambaa mitandaoni bila ridhaa ya mhusika.

Tunaishi katika ulimwengu wa kidigitali, na hali hii hutufanya sote, kwa wakati fulani, kuwa katika uwezekano wa kuwa wahanga wa matukio ya picha au video zetu kusambaa mitandaoni bila ridhaa yetu, ikiwa hatutakuwa makini. Fikiri, utakuwa katika hali gani pale utakapokutana na picha yako ya faragha mitandaoni?

Neno 'connection' limejipatia umaarufu katika siku za hivi karibuni hasa kila mara inapotokea picha au video za uchi zimesambaa mitandaoni. Unaweza kutamani kupata 'connection' au hata kuisambaza kwa watu watakaokuomba uwatumie, bila kufikiri madhara unayoendelea kumsababishia mhusika mwenye picha au video hiyo, mbali na makosa ya kisheria unayoyatenda kwa kusambaza picha au video hizo.

Wengi hupenda kuwatuhumu wahusika wanaoonekana katika video hizo kuwa wanaotakiwa kuwajibishwa kwa kusambaa kwa picha au video hizo. Inaweza kuwa kweli; lakini si mara zote, kama ilivyokuwa kwa Nandi na Billnass.

"Bado siko sawa," aliandika Nandy katika mtandao wake ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Instagram baada ya video yake ya faragha na msanii mwenzake, Billnass, kusambaa katika mitandao ya kijamii, huku Billnass akikiri kuwa alikuwa 'analia tu' baada ya kuona video hiyo ikisambaa mitandaoni!

Utafiti uliofanywa hivi karibuni kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini Marekani unaonesha kuwa asilimia 20 ya wanafunzi wamekwisha wahi kutuma picha au video za faragha mtandaoni, huku asilimia 25 wamewahi kusambaza picha au video za faragha walizotumiwa. Si vijana tu wanaohusika kutuma au kupokea picha au video za faragha, utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Pew unaonesha kuwa asilimia 22 ya watu wenye umri kati ya miaka 35 na 44 wanapokea picha au video hizo.

Ni dhahiri kuwa kwa sehemu kubwa picha au video hizo husambaa baada ya penzi 'kuchacha.' Zaidi ya visa 6 kati ya 10 vya kuvuja na kusambaa kwa picha au video za faragha hutokana na wapenzi walioachana kuvujisha picha hizo. Hii inamaanisha kuwa wapenzi hutumiana picha hizo wakiwa katika kipindi cha mapenzi, kitendo kinachojulikana kwa Kiingereza kama 'sexting.'

Usalama kwanza
Licha ya madhara ya kisaikolojia au kisheria yanayotokana na kutuma au kusambaza picha au video hizo za faragha, mambo mawili yanaweza kuwa dhahiri zaidi:-
Kwanza, tofauti na picha ngumu, picha za kidigitali huweza kunakiliwa kwa wingi na kuwa urahisi mkubwa.

Pili, picha za kidigitali ni rahisi kuhusishwa na mhusika moja kwa moja, hata kama sura yake haitaonekana katika picha hiyo.

Picha yako ya faragha kuwepo mtandaoni ni ishara tosha kuwa faragha yako ipo mashakani hata kama ipo mikononi mwa mtu unayemwamini. Kama hautaweza kumzuia mtu mwingine kusambaza picha au video hiyo, jambo utakaloweza kulifanya ni kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeweza kupata picha au video hiyo.

Lakini wakati mwingine unaweza kujikuta katika hali ya ushawishi wa kutuma picha au video ya faragha kwa mtu 'unayemwamini.'
Utakapofikia hatua hiyo, ni lazima kuhakikisha usalama wako kwanza: hakikisha sura yako haionekani kwenye picha au video hiyo; hakikisha mazingira ya nyuma ya video hayawezi kulinganishwa na uhalisia wa mazingira yako; ficha vitu vinavyoweza kukutambulisha moja kwa moja kama vile alama zilizopo kwenye mwili wako au tattoo.

Taarifa zinazoambatana na picha
Picha zote za kidigitali zinaambatanishwa na tarifa inayoonesha kifaa cha kidigitali (simu, tablet au kamera) kilichotumika kupiga picha, jinsi picha ilivyopigwa, mahali picha ilipopigwa, nk. Taarifa hizi hujulikana kama EXIF.

Ili kuwa salama kidigitali, picha unayoituma haitakiwi kuwa na nyayo za kidigitali zinazoweza kufanya picha hiyo kutambuliwa kutokana na kifaa unachomiliki.

Ili kuondoa taarifa hizo, utapaswa kufuata hatua kadha, rahisi. Kama unatumia kompyuta ya Windows, unaweza kufungua 'properties' za picha, kisha chagua kiunganishi kilichoandikwa 'remove properties and personal information.' Kama wewe ni mtumiaji wa Mac, unaweza kutoa EXIF kwa kutumia programu inayoitwa ImageOptim. Unaweza kutumia simu yako ya mkononi kuondoa EXIF kwa kutumia programu nukushi (app) inayoitwa Photo Exif Editor. Kufahamu zaidi kuhusu jinsi ya kuondoa EXIF bonyeza hapa.

Tuma kwa njia salama
Kuondoa taarifa za kidigitali za picha ni hatua ya mwanzo tu katika kuhakikisha kuwa picha hiyo haiwezi kuunganishwa kwako.
Njia nyingine inayoweza kuacha nyayo za kidigitali ni jinsi unavyotuma picha hiyo. Kifaa au akaunti zetu za kidigitali (Twitter, instagram, WhatsApp, nk.) zinaweza kutumika kumtambua mhusika wa picha hizo. Zipo njia kadhaa zinazoweza kutumika kutuma picha 'bila kujulikana.'

Zipo programu nukushi (apps) zinazoweza kutumika kutuma picha bila kuonesha inakotokea. CoverMe ni mfano wa programu hizo. Unaweza kumwambia mwenzi wako kwa njia ya mdomo kuwa ajiandae kupokea picha kutoka kwako, kisha unaweza kumtumia picha ukijiamini kuwa uwezekano wa picha hizo kuunganishwa na wewe ni mdogo.

Subiri kwanza!
Kabla ya kufikia uamuzi wa kutuma, jikumbushe haya:

Kwanza, hakuna ulazima wa kutuma picha au video hizo. Kama unahisi, kwa namna yoyote, kuwa hautakiwi kutuma, ni vyema kuchagua kuacha kutuma.

Pili, jiulize kama unamwamini mtu unayemtumia picha au video hizo. Unaweza kuwa makini kuhifadhi picha au video zako zitakapokuwa kwako, lakini hali huweza kuwa tofauti zitakapokuwa kwa mtu mwingine. Kama kweli unamwamini mwenza wako unayemwamini, ni muhimu kukumbuka kuwa anaweza kuhifadhi picha au video ulizomtumia katika kifaa chake, kisha picha hizo zinaweza kusambazwa kutoka kwake.

Tatu, kutuma picha za faragha inaweza kuwa jambo la kufurahisha hadi pale utakapogundua kuwa maisha yako ya baadaye yameharibiwa! Hivyo, kabla ya kutuma hiyo picha au video kwa mwenza wako, kumbuka madhara ya muda mrefu yanayoweza kutokana na kitendo hicho.

Nne, fahamu sheria za nchi yako. Ni muhimu kuelewa sheria za nchi yako zinasema nini kuhusu kutuma au kusambaza picha za uchi.
Nchini Tanzania, kwa mfano, kifungu cha 14 cha sheria ya makosa ya mtandao kinasema kuwa ni marufuku kwa mtu yoyote kuchapisha au kuweka picha za ngono mitandaoni au kwa mfumo wa kompyuta. Kwa lugha nyepesi, uchapishaji wa picha za ngono mtandaoni ni kosa la jinai. Endapo mtu atapatikana na hatia ya kuchapisha picha za ngono mtandaoni adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni 21 au kifungo cha miaka 7 gerezani au vyote kwa pamoja.

Upo tayari?
Baada ya kuainisha mambo yote, jiulize kama bado unataka kutuma picha au video hiyo. Mchakato wa kusafisha picha kuondoa mlingano na uhalisia wako tayari ni kazi kubwa, na mara zote kuna mbinu mbadala: kutopiga na kutuma picha au video za faragha mtandaoni.​
 
Nadhani usalama zaidi ni kutopiga kabisa picha za faragha. Lengo la kupiga picha ni kuweka kumbukumbu, sasa ni kweli kwamba unahitaji kuweka kumbukumbu ya mambo yako ya faragha? Weka kumbukumbu zako za faragha kichwani na sio kwenye vifaa hivi vya kielektroniki.
 
Status
Not open for further replies.
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom