Fahamu hatari za watumishi wa Umma kukimbilia Ubunge

kali KENYATTA

JF-Expert Member
Mar 4, 2015
288
166
Na Markus Mpangala,

Kuporomoka hadhi ya utumishi wa umma, kazi za kitaaluma kutothaminiwa, maslahi hafifu, hofu ya kutumbuliwa, usalama mdogo wa kazi, mazingira magumu ya siasa na kuwa njia rahisi ya kupata mafanikio, kutoa michango kupitia siasa, uhaba wa mifumo ya taasisi huru, kutafuta fursa za kuteuliwa ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchochea wimbi la watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta binafsi kukimbilia ubunge mbali ya ile ya kutanuka demokrasia kuelekea uchaguzi mkuu wa urais, ubunge na madiwani mwezi Oktoba mwaka huu 2020.

Idadi kubwa ya watumishi wa umma na wafanyakazi sekta binafsi wametia nia ya ubunge kupitia chama tawala CCM kuliko vyama vya upinzani ambavyo vimekuwa na idadi ndogo hali ambayo imeibua mjadala juu ya taswira ya chama tawala na vile vya upinzani mbele ya wapiga kura.

Dalili za kuibuka wimbi la watia nia lilianza kuonekana wakati wa uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015, ambapo makada 42 walijitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa CCM ili kuwania nafasi za urais, ikiwa ni idadi kubwa inayotajwa kufungua njia ya joto kali miongoni mwa watu kushiriki siasa kutoka utumishi wa umma na sekta binafsi.

Aidha, kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 watia nia ya urais visiwani Zanzibar walikuwa 32, ikiwa ni idadi kubwa kuliko vipindi vingine, hali ambayo nayo inatafsiriwa kuwa sababu nyingine ya kuibuka wimbi la watu kutia nia za ubunge hadi nafasi ya chini ya udiwani baada ya kujipima.

Je, nini chanzo cha watu kukimbilia siasa hasa nafasi ya ubunge?

Kimsingi zipo sababu kubwa na ndogo. Yapo mambo matatu ya msingi katika hoja hii; Kwanza ni suala la maslahi yatokanayo na ubunge linavutia watu wengi, hivyo siasa imekuwa sehemu inayolipa zaidi. Takwimu zinaonesha kuwa mbunge analipwa mshahara wa shilingi milioni 3.8 kwa mwezi, posho ya mwezi shilingi milioni 8, posho ya kikao kimoja ni shilingi 240,000 kwa siku, posho ya kujikimu shilingi 120,000 kwa siku.

Baada ya miaka mitano ya ubunge wake anapokea pensheni ya shilingi milioni 240. Endapo mtu akichaguliwa kuwa mbunge anapata bima ya afya daraja la kwanza na familia yake, safari za nje ya nchi, pamoja na mishahara ya mbunge kutokuwa na makato ya mifuko ya jamii.

Mtumishi mmoja wa umma ambaye kwa sasa yuko masomoni barani Ulaya amemwambia mwandishi wa makala haya, "Mifano ni mingi, hebu tulitazame suala la pesheni ya mbunge just in five years (kwa miaka mitano). Tukiwaangalia Maprofesa nchini Tanzania wanalipwa mshahara takribani milioni 6 kwa mwezi lakini hawawezi kufikia pensheni hiyo asilani.

Uprofesa wao watafanyia kazi miaka 30 hivi na hawatoweza kuambulia hata robo ya pensheni wanayopata wabunge. Wafanyakazi nchi hii hawapati maslahi makubwa kama wanayopata wabunge katika kipindi chao. Wafanyakazi na sekta nyingine hawana makazi ya kudumu, bima za afya za uhakika, mazingira ya kazi ni magumu."

Sababu nyingine ni suala la demokrasia ambapo watia nia wote wana haki sawa kushiriki michakato ya kidemokrasia wakilindwa na Katiba ya Tanzania ambayo inasisitiza kila mwananchi anayo haki ya kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa Ibara ya 21 (1) na (2).

Duru za kisiasa zinaonesha kuwa baadhi ya watia nia wanapenda kuona mabadiliko ya kweli yanatokea nchini, ikitafsiriwa kukata tamaa pamoja na kuamua kushughulikia matatizo ya nchi kwa vitendo badala ya kusubiri wanasiasa pekee kila awamu.

Je, sababu ipi huwafanya watu wengi kukimbilia ubunge kupitia CCM kuliko vyama vya upinzani?

Akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi wapya jijini Dodoma, rais John Magufuli alisema kwa taarifa alizonazo kutoka CCM hadi tarehe 16 Julai mwaka huu 2020 kulikuwa na jumla ya watia nia ya ubunge 8205, huku mkoa wa Dar es salaam ukiongoza ukiwa na 829, Arusha (320), Kagera (328), Kusini Unguja (53), Kilimanjaro (82). Kwenye majimbo ya uchaguzi kuna jumla ya watia nia 6533, Viti Maalum (1539), wawakilishi (133).

Duru za kisiasa zinaonesha kuwa wengi waliokimbilia kutia nia kupitia CCM wamejenga dhana kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa sawa ule wa wenyeviti wa serikali za mitaa wa mwaka 2019, kwamba kugombea kupitia CCM unakuwa na uhakika wa kutangazwa mshindi.

Hayo ni mazingira ya sasa yanavyoonekana katika siasa ambazo zinatajwa kutokuwa na uwanja sawa, huku taifa hilo likiwa na kumbukumbu ya maonyo yaliyowahi kutolewa na wenye mamlaka dhidi ya wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali ambao wana jukumu la kusimamia uchaguzi huo wakiwakilisha Tume.

Aidha, matokeo ya hatua hii yataonekana baada ya miaka kadhaa ijayo. Hasara ni kuwa inaonekana kunatengenezwa kama mfumo wa chama kimoja bila kushurutishwa, huku vyama vya upinzani kama vile CHADEMA, CUF, ACT Wazalendo na kadhalika vikiachwa vipauke kutokana na mbinyo wanaokutana katika shughuli za siasa kwa kipindi cha miaka mitano sasa.

Vilevile ni matokeo ya kushindwa kuwa na mifumo ya taasisi huru na imara za kuongoza na kusimamia nchi. Ni rahisi kubashiri kinachoweza kutokea baadaye kutokana na wimbi hili, ikiwa na maana idadi ya makada wa CCM itakuwa kubwa zaidi, na tayari tumeona hata wastaafu wa majeshi wamechukua fomu za kuomba kuteuliwa.

Tumeona wakuu wa tume za uchaguzi nao wakitia nia ya kuteuliwa ndani ya CCM. Hivyo watia nia wanahofu kujiunga na vyama vya upinzani ambavyo wanavitazama kama vile havina fursa ya kuibuka na ushindi.

Je, kuna hatari gani watumishi wa umma kukimbilia ubunge?

"Utitiri wa watia nia wengi kutoka utumishi wa umma si ishara nzuri hata kama watu wengi wanachukulia kama hali ya kawaida na haki za watia nia kulindwa kikatiba. Ni tishio kwenye amani ya nchi kuliko matisho mengine. Utumishi wa umma umedharauliwa na hivyo watu hawana uadilifu kufanya kazi za taaluma.

Wanatamani walau wateuliwe na kwa hilo wako tayari kufuata masharti yoyote watakayopewa ili waweze kuteuliwa maana wanafanya mbinu za kuvaa sare za CCM hata kama ndani wana mapenzi na vyama vingine tofauti ili waonekane na wateuzi hao hapo baadaye," Anasema Richard Ngaya, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine na mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania.

Ameongeza kuwa, "Kutia nia na kuchukua fomu wala si ajenda yao, wengi wao wanataka kuonekana na hilo wameamua kutumia kidogo walichonacho ama ni sawa na kuvaa jezi ya Simba nje huku ndani wakiwa wamevaa jezi ya Yanga kwa kuhofia tu kuwa Yanga haiwezi kuchukua kombe, hivyo wanajifanya nao ni mashabiki wa Simba ili waishi kwa amani mitaani huku wakifaidi keki ya wana Simba kutokana na kelele na ubabe. Watu wa aina hiyo ni hatari kwa amani ya nchi siku ikitokea mtu wa kuwashawishi kupindua sahani, wakipata hamasa kidogo hao wanaweza kuwa mstari wa mbele kuchochea maasi."

Ni ishara ya kukosekana ajira au biashara zinazolipa vizuri sekta binafsi?

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Edinburg nchini Scotland amemwambia mwandishi, "Suala la wimbi la watia ni ya ubunge lina tafsiri mchanganyiko. Tuanze hapa kwenye fursa. Fursa nyingine hasa za kwenye sekta binafsi zimeonekana kupugua. Uhakika wa maisha unaonekana upo zaidi kwenye siasa kuliko kipindi kingine chochote. Kwamba kuwa nje ya mfumo wa siasa kunatiliwa mashaka. Nje ya siasa hakulipi. Hivyo ili uwe salama na ufanikiwe ni vizuri ujulikane na uwe na madaraka,

"Pili, kuwa mbunge kumeonekana kuwa jambo rahisi ambalo kila mtu analiweza. Hakuna haja ya kuwa makini au kujua mengi ili kujenga hoja ngumu. Kila kitu kinaamuliwa na wachache hivyo hakuna haja ya kusoma makabrasha ili kujenga hoja yoyote. Unaweza kusema chochote au ukakaa kimya tu, hakuna shida. Zamani watu waliogopa sana kusoma makabrasha na kujenga hoja. Sasa siyo lazima kwani hoja ikiletrwa haipingwi. Jambo la tatu, sasa tunaweza kusema CCM imeimarika imekuwa na mvuto hivyo watu wanaipenda na kujisikia fahari kujibainisha nayo,"

Ni tumbua tumbua na ukosefu wa usalama wa ajira vimeathiri utumishi wa umma?

"Ubunge ni ajira ya uhakika. Taasisi nyingi za serikali kwa sasa zimekuwa zikikumbwa na mabadiliko ya hapa na pale kwamba mtumishi anaweza kulala akijua kesho yake atakwenda kazini, lakini akiamka anakutana na barua ya kusitisha kibarua chake. Utumishi wa umma umekuwa mgumu kwa kuwa watumshi wamechanganyikiwa, hawana uhakika na usalama wa ajira za," Anasema Happy Joseph, mwalimu na mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha NorthEast Normal University nchini China na raia wa Tanzania.

Anaongeza, "Changamoto nyingine ya utumishi wa umma ni kuondolewa kazini bila mjadala, yaani zile taratibu za kisheria hazipo. Akija kiongozi yeyote anaweza kuamua kazi iishe au uendelee. Lakini mbunge hawajibishwi kabisa iwe amekaa kimya ama kuzungumza bungeni, haiwezekani mbunge kutumbuliwa. Hebu fikiria mwalimu mkuu shule yake inapoboronga matokeo ya mitihani miaka miwili, anajikuta amepewa uhamisho wa adhabu kwenda vijijini. Hakuna atakayemjali mwalimu akihamishiwa mazingira mabaya,

"Chukulia mfano halmashauri imeboronga kwenye mapato, huyo mhasibu au mkurugenzi anajikuta ameshushwa cheo na kuhamishwa au kufutwa kazi. Mtu kama huyu atachagua nini kati ya utumishi wa umma na ubunge? Suala jingine mtumishi unafuata sheria lakini ukiwa mbunge unatunga sheria inayokufaidisha. Jamii yetu ifikirie ingekuwaje kama wabunge wangekuwa wanatumbuliwa au kazi hiyo isingekwua na maslahi mazito kama posho, usafiri na ulinzi? Naamini wengi wasingekimbilia ubunge,"

Je, watu wengi wanakimbilia ubunge wa CCM ili kuvizia teuzi za kisiasa?

Uzoefu unaonesha kuwa wengi waliopata uteuzi wa nafasi za makatibu tawala wilaya, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala mikoa, wakuu wa mikoa na nafasi nyingine za umma ni wale makada ambao walionekana kugombea ubunge 2015 au ujumbe wa NEC kupitia CCM.

Teuzi hizo pia zinakwenda kinyume cha utaratibu na sheria ambapo watumishi wa umma wanapaswa kuteuliwa nafasi mfano za makatibu tawala hali ambayo inachangia baadhi kujitosa kwenye ubunge.

Mbali ya mazingira rafiki yaliyowekwa kipindi hiki hususani matumizi makubwa ya fedha, lakini ni ushindani na kuongeza wasifu kulenga kuteuliwa baada ya uchaguzi mkuu ni jambo kubwa linalozingatiwa na watia nia wengi. Wengi wanaamini wakikosa kupenya kwenye kura za maoni, na wakionekana kwa wenye mamlaka yaani mwenyekiti wa CCM, iwapo atashinda urais huwa anakuwa na turufu iliyo kibindoni hata kupata teuzi za nafasi zilizotajwa hapo juu.

Je watumishi wa umma wanaruhusiwa kujiunga na vyama vya siasa?

Wakili Stanislaus Kigosi ameeleza kuwa, "Ninaona kuna mtego watumishi wa umma wamejitega wenyewe. Kwanza sheria inakataza watumishi wa umma kujiunga na vyama vya siasa. Lakini walio wengi wameingia kwenye mtego wa kuamini kuwa hata wasipopenya kwenye kupitishwa kugombea basi wanajua kwamba kuna nafasi nono za kuteuliwa watakuja kuzipata, kwahiyo wanauza wasifu wao kwenye mamlaka za uteuzi.

"Mwenyekiti wa CCM, Dkt John Magufuli ambaye anagombea kipindi cha pili na endapo akishinda bila shaka huu mchezo ameshausoma. Mtumishi wa umma akitaka kujiunga na chama cha siasa anatakiwa kufuata taratibu. Kiutaratibu anatakiwa kujiuzulu nafasi yake ya utumishi kwanza ndipo aingie chama cha siasa au anatakiwa kuomba ruhusa ya kuwa nje ya ajira yake kwa sababu zenye zinazoeleweka,"
 
Back
Top Bottom