Facebook kuanzisha mradi wa kufundisha mfumo wake wa ufahamu bandia kwa kutumia video

Sam Gidori

Verified Member
Sep 7, 2020
94
150
Kampuni ya Facebook imesema inaanzisha mradi wa kuifundisha mifumo yake kujifunza picha, video na sauti kutoka katika maudhui yaliyopo katika jukwaa lake.

Mradi huo unaoitwa "Kujifunza Kutokana na Video" una lengo la kuufundisha mfumo wa Facebook wa ufahamu bandia (artificial intelligence system) ili uweze kuboresha mapendekezo ya maudhui kwa watumiaji wake na kusimamia sera za kampuni hiyo.

Chapisho la blogu la Facebook linaeleza kuwa matumizi ya video katika mradi huo utasaidia kuboresha ufanisi wa mfumo wa ufahamu bandia na kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia, ukisaidia pia kutambua tofauti ya tamaduni zilizopo duniani.

Facebook inasema kuwa kwa kutumia mfumo unaojiendesha wenyewe wa ufahamu bandia, ni rahisi kwa mfumo huo kuelewa mahitaji ya watumiaji.
Mfano, mtumiaji anapoandika "Nioneshe mara zote tulipomwimbia Bibi wimbo wa heri ya siku ya kuzaliwa," mfumo huo unaweza kuhusianisha 'siku ya kuzaliwa' na vitu kama keki, mishumaa na nyimbo za siku ya kuzaliwa kwa kutumia video.

Mfumo huo unatajwa pia kusaidia kutambua sauti na kusaidia kutengeneza maelezo ya video (caption) bila msaada wa mtu na kusaidia kutambua video zenye maudhui ya chuki.

Facebook imekuwa ikiboresha mfumo wake wa ufahamu bandia katika siku za hivi karibuni. Mapema mwezi huu kampuni hiyo ilisema mfumo wake kompyuta wa uoni uliopewa jina Seer uliweza kujifunza kutoka picha bilioni moja katika mtandao wa Instagram na umefanikiwa kutambua vitu vinavyoonekana zaidi kwenye picha kwa ufanisi wa asilimia 84.2. Kampuni hiyo pia imesifu mfumo wake wa ufahamu bandia ikisema umefanikiwa kutambua maudhui yenye chuki kabla hayajaripotiwa na watumiaji.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom