EWURA yasitisha bei mpya za maji ili kufanya uchunguzi wa kina kutokana na kukithiri kwa malalamiko ya kubambikiziwa ankara za maji wateja

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,498
9,279
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza kufuta bei mpya za maji zilizopaswa kutozwa kuanzia Januari, mwaka huu, ili kufanya uchunguzi wa kina kutokana na kukithiri malalamiko ya kubambikiziwa ankra za maji wateja.

Bei hizo zilizofutwa ni ambazo zilikuwa zimeidhinishwa na mamlaka hiyo kwa mwaka 2020/21 na kwa sasa zitaendelea kutozwa zilizokuwapo za mwaka 2018/19.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Godfrey Chibulunje, alisema hivi karibuni kumekuwapo na malalamiko makubwa ambapo kati ya malalamiko yote yanayopokelewa na EWURA katika sekta ya umeme, mafuta, gesi asilia, asilimia 60 ni ya maji.

“Kilio kikubwa kutoka kwa wateja wa huduma za maji kipo kwenye ankara za maji ambapo asilimia 75 ya malalamiko yote ni kutokubaliana na ankra zinazotolewa na mamlaka mbalimbali nchini,” alisema.

Alieleza kuwa malalamiko mengine ambayo ni makubwa na migogoro ya uunganishaji huduma za maji ambapo ni asilimia 13.

“EWURA huidhinisha bei kwa mamlaka za maji kwa miaka mitatu ambapo bei hizo ziliidhinishwa kwa mwaka 2018/19, 2019/20 na 2020/21 na kwa utaratibu wetu kuanzia Januari 2021 mamlaka nyingi zilikuwa zinatarajia kuanza kutumia bei za mwaka 2020/21,” alisema.

Alisema kutokana na malalamiko hayo imefuta bei zote ambazo zilitakiwa kuanza kutumika mwezi huu na kuelekeza zitumike bei za mwaka 2018/19.

“Hatua hii inachukuliwa ili kuipa uwezo EWURA kufanya uchunguzi wa kina juu ya malalamiko haya ya maji ili kubaini ukweli wa malalamiko hayo, ambapo baada ya kumaliza shughuli ya uchunguzi wa kiufundi, EWURA itatoa maelekezo mengine ya matumizi ya bei ambazo zilitakiwa kuanza Januari, 2021,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema jumla ya mamlaka za maji za mikoa, wilaya, mji midogo na miradi mikubwa ya kitaifa 117 iliomba kuidhinishiwa kupandisha ankra za maji, lakini zimesitishiwa na kwa sasa ankra zitakazotumika ni za 2018/19.

Awali, akifafanua mchakato wa uidhinishaji ankra hizo, Chibulunje, alisema EWURA ina jukumu la kupitia gharama kama zina uhalali kwa kulinganisha na gharama za kipindi cha nyuma za mamlaka husika pamoja na mahesabu ya fedha yaliyokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

“Tunazingatia kulinda maslahi ya wateja, huduma kwa wasio na uwezo pamoja na uendelevu wa huduma husika, na pia tathmini ya mapendekezo ya bei huzingatia mlingano wa gharama za uendeshaji za mamlaka nyingine za maji nchini,” alisema.

Kadhalika, alisema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza agizo la Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, la kutaka wananchi washirikishwe katika kusoma ankra za maji ambapo wanatarajia kuja na mfumo wa kielektroniki ambao utashirikisha wasomaji wa ankra za maji na wateja.

Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa mamlaka hiyo, Exaud Maro, alisema bei za maji zinatofautiana kwa mamlaka za maji huku akisema inatokana na gharama za usafirishaji wa maji kutoka kwenye vyanzo vya maji hadi kuwafikia wateja.
 
Hizi ni mamlaka zilizoanzishwa kisiasa tu, futa mamlaka hii na huduma hii weka chini ya local governments na hii ni moja ya chanzo cha mapato na wanawajibika kuona kuwa wananchi wanapata huduma hii kwa standard inayokubalika.
 
Mashirika yetu huwa kama mfugaji mwenye ng'ombe mmoja wa maziwa anaetaka faida kubwa kwa kumkamua hata kama hana maziwa!

Badala ya kufikilia kusambaza na kuboresha huduma, wao wanataka kukamua tu!

Ukitembelea maeneo kitunda haina maji, mbagala haina maji.

Ukienda kule KIGAMBONI pamoja na ukaribu wa maji DAWASCO wameshindwa kusambaza maji manispaa ya kigamboni kavu wilaya ambayo iko umbali wa mita 500 kutoka IKULU YA DAR lakini HAINA MAJI!

Dawasco wameshindwa hata kusubcontract wawekezaji binafsi?
 
Hizi ni mamlaka zilizoanzishwa kisiasa tu,futa mamlaka hii na huduma hii weka chini ya local governments na hii ni moja ya chanzo cha mapato na wanawajibika kuona kuwa wananchi wanapata huduma hii kwa standard inayokubalika.
Hizi mamlaka za maji ni majini nyonya damu hatari sana
 
Back
Top Bottom