Ewe Mtanzania, utasimama upande gani ifikapo Oktoba 31, 2010? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ewe Mtanzania, utasimama upande gani ifikapo Oktoba 31, 2010?

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MwanaHaki, Aug 28, 2010.

 1. MwanaHaki

  MwanaHaki R I P

  #1
  Aug 28, 2010
  Joined: Oct 17, 2006
  Messages: 2,403
  Likes Received: 122
  Trophy Points: 145
  Ndugu yangu Mtanzania

  Nimeandika makala, ambayo ni wosia wangu kwako. Tafadhali usome, nimeyaambatanisha kwenye waraka huu.

  Utakapotafakari na kuelewa nilichokuasa, tafadhali fikisha ujumbe kwa wengine.

  Shukrani,

  -> Mwana wa Haki


  ----------------------------------

  Ewe Mtanzania, ifikapo Oktoba 31, 2010, utasimama upande gani?

  Na MwanaHaki

  TANZANIA ni nchi iliyosheheni kila aina ya utajiri. Ina maeneo mengi ya ardhi nzuri, yenye rutuba na inayofaa kwa kilimo, kuliko hata nchi jirani kama vile Kenya, ambayo ina sehemu ndogo inayofaa kwa kilimo ikilinganishwa na Tanzania. Vile vile, Tanzania ina mbuga nyingi zenye wanyama-pori ambao ni kivutio kikubwa cha watalii. Isitoshe, kuna vivutio vingi tofauti vya utalii, kama vile makumbusho ya kihistoria, yaliyoko Tanga, Iringa, Manyara, Arusha, Lindi na kwingineko. Kana kwamba Mwenyezi Mungu aliona haya yote hayatoshi, ametujaalia urithi mkubwa wa madini mengi na yenye aina tofauti. Mikoa ya Kanda ya Kusini imesheheni dhahabu, makaa ya mawe na platinum – madini yenye thamani kubwa kuliko hata almasi! Kanda ya Ziwa ni maarufu kwa madini ya almasi na dhahabu, lakini pia madini ya uranio yanapatikana huko pia. Kanda ya Kaskazini ni maarufu kwa madini ya Tanzanite, ambayo yanapatikana Tanzania pekee! Na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni maarufu kwa madini ya dhahabu. Lakini kuna madini mengi zaidi ambayo hayana thamani kubwa, kama vile Zinc, Manganese, Copper, na kadhalika. TANZANIA NI NCHI TAJIRI!

  Licha ya utajiri wake huu, sehemu kubwa ya wananchi wake ni maskini, tena maskini wa kutupwa. Mpaka leo – takriban miaka 49 baada ya kupata uhuru – wananchi hawa wanaishi kwenye nyumba zilizojengwa kwa matope ya kukandika kwenye miti na kuezekwa kwa nyasi; nyumba za msonge. Wananchi hawa hawana uhakika wa kupata mlo mmoja kwa siku, na kwao, kilimo ni cha 'kujishikiza'. Kwa wale wakulima ambao wanapata mazao mengi, tatizo lao kuu ni masoko; barabara za kwenda kwenye maeneo yao ya mashamba na makazi ni duni, wakati wa masika hupitika kwa shida sana, na pale ambapo wachuuzi wanapofanikiwa kupeleka magari ya kuchukua mazao yao, huwa wanafika wakati ambapo wakulima hao huwa na hali mbaya ya kifedha, kiasi kwamba wanaridhika na bei yoyote ile wanayopewa na wachuuzi hao. Badala ya wakulima – kama ilivyo kwa nchi nyingine – kuwa na nguvu ya bei, wachuuzi ndio wanaokuwa na nguvu hiyo. Hali si tofauti kwa wafugaji, ambao kutwa huwa kwenye 'mikong'oto' wanayopata kutoka kwa watendaji wa serikali za mitaa na tawala za mikoa, ambao ni kama wamepewa ruksa ya kufanya wanayotaka, hata kama wanavunja sheria. Ubabe wao umesababisha wafugaji wengi kupoteza mifugo yao, ambayo hukamatwa na watendaji hao kwa visingizio kedekede, wanapowabambikia makosa ambayo mengi huwa ni ya kubuni, yaani, hakuna sheria inayoyataja.


  Vijana wengi – takriban asilimia 60 – waliokuwa wakiishi vijijini wamehamia kwenye miji mikuu, kwa kufuata dhana kwamba maisha ya mjini ni nafuu kuliko vijijini. Dhana hii haiko mbali na ukweli, lakini kama ni kweli, basi maisha yao ni magumu sana. Nimeshuhudia – hapa jijini Dar es Salaam – wahamiaji hao, ambao ninawaita wakimbizi wa kiuchumi, wakiishi katika mazingira magumu kiasi kwamba nimeyaona maisha yangu ni kama peponi. Ukipita maeneo ambayo yanatambulika kama Uswahilini – Manzese, Tandale, Mburahati, Kigogo, Tandika, Buza, Yombo, na kwingineko – utakuta mambo ya kusikitisha. Wakati wa usiku, wahamiaji hawa hulazimika kulala chini – sakafuni – kwenye 'corridor' na barazani, kwenye nyumba ambazo wamefikia baada ya kuhamia mjini, kwa ndugu au jamaa zao. Wengi wa wahamiaji hawa huwa wanafika mjini bila kutoa taarifa, na hufanya hivi kwa makusudi; wakitoa taarifa hawatapokelewa, na hili wanalijua vema.


  Wote tunaifahamu vema historia ya utendaji wa chama cha TANU; ni historia isiyokuwa na dosari kubwa. Binafsi, siwezi kusema kwamba utawala wa TANU, chini ya Hayati Mwalimu Nyerere, ulikuwa kamilifu, kwani hata siku hizo umaskini ulikuwapo, nyumba za msonge zilikuwapo pia. Wakati huo, kaulimbiu ya TANU ilikuwa kupambana na maadui wakubwa watatu – ujinga, maradhi na umaskini. TANU ilijitahidi kadri ya uwezo wake, mpaka pale ilipokabidhi mzigo huo kwa CCM.


  Kilichotarajiwa ni kwamba CCM ingeendeleza kwa juhudi na uadilifu vita hiyo takatifu ya kupambana na maadui hao – ujinga, maradhi na umaskini – lakini, kinyume na matarajio hayo, ameongezeka adui mmoja – ufisadi!


  Ufisadi ni dhana pana sana ambayo wengi wamejaribu kuifafanua, bila mafanikio. Lazima ufisadi uangaliwe kwa mapana yake, si mafupi yake. Kwa mfano, ufisadi – ambao ni mfumo wa kupanga mipango ya kuvunja sheria, taratibu na kanuni, kwa lengo la kujipatia maslahi, haswa kwa matumizi mabaya ya madaraka – umejikita zaidi kwenye asasi za kiserikali, ambapo licha ya kuwapo kwa sheria zinazodhibiti matumizi ya rasilmali za umma, watendaji wamediriki – bila chembe ya soni – kupanga hujuma za kukiuka na kupindisha sheria hizi, kuanzia uongozi hadi ngazi ya chini kabisa. Zipo asasi ambazo kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act) inayosimamiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (Public Procurement Regulatory Authority – PPRA) ni jambo la kawaida kabisa, kwani, wamegundua namna ambavyo nyaraka zinaweza kuandaliwa wakati wa 'uchakachuaji' wa zabuni na kufanikiwa kuonesha kwamba hakukuwa na ukiukwaji wowote wa sheria. Kwa mfano, kiongozi mkuu wa asasi anaweza kuwa na maswahiba zake ambao anataka kuwapa zabuni, kwa minajili ya yeye kunufaika na mgao wake binafsi, baada ya fedha kulipwa kwa kampuni 'inayoshinda' zabuni hiyo. Kwa hiyo, wakati wa uendeshaji wa zabuni, kampuni hiyo inayopendelewa 'kushinda' zabuni ndiyo inayoandaa michanganuo yote ya zabuni. Mchanganuo wenye jina la kampuni ndio unaokuwa umekamilika – kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa ndani wa asasi hiyo, ambao ndio wanaoipa kampuni hiyo 'siri' za kushinda zabuni – na michanganuo mingine mitatu inayoandaliwa na kampuni hiyo, kwa kutumia majina ya kampuni nyingine zilizopo au za kubuni, inaandaliwa ili kuhakikisha kwamba inakuwa na mapungufu kiasi cha kukosa alama zinazotakiwa ili kuweza kushinda. Mambo haya hufanyika kwa ushirikiano wa karibu, kati ya watendaji wa kampuni inayokusudiwa kushinda zabuni hiyo, na watendaji wa asasi hiyo ya kiserikali, kupitia mwongozo na maelezo kutoka kwa uongozi wa juu. Yeyote anayediriki kukiuka amri hiyo ya 'wakubwa' anaweza kujikuta, ama ameshushwa cheo chake au amestaafishwa mapema kabla ya kufikia muda wake wa kustaafu kazi kwa mujibu wa sheria, au kufukuzwa kazi kabisa, kadri kiwango chake cha 'ukaidi' huo wa kukiuka amri za wakubwa kitakavyokuwa. Huu ni mfano wa ufisadi, ambao tunauita 'ufisadi mkubwa' kwa kuwa kiwango cha fedha kinachohusika hufikia mamia ya mamilioni ya shilingi au hata bilioni kadhaa!


  Lakini pia upo ufisadi mdogo, ambao ni ule wa watendaji wa serikalini kukwapua mali za asasi hizo na kwenda kuziuza mitaani, ama kwa ushirikiano na uongozi wa juu au bila ushirikiano huo. Kwenye baadhi ya asasi hizo, viongozi wa juu huwa na kampuni zao zenye kuendesha biashara zao binafsi, kwa hiyo huwatuma watendaji waliopo chini yao kupeleka vifaa mbali mbali kutoka kwenye asasi hizo, kama vile vifaa vinavyopatikana kwenye maduka ya 'stationery', kwa hiyo kuhakikisha kwamba wanapunguza gharama zao na kupata faida kubwa. Tembea mitaani, utayakuta magari ya serikali yakiwa kwenye harakati ya kusambaza bidhaa hizo kwenye maduka binafsi ya 'stationery'. Lakini pia kwenye ufisadi mdogo, wako viongozi wenye kampuni zao ambao nao hujihakikishia upendeleo wa kampuni zao, ili ziweze kupewa hizo zabuni ndogo ndogo, lakini kibaya zaidi, upo ushirikiano kati ya watendaji wa ngazi za chini na wazabuni, kuhakikisha kwamba, kwa masharti ya zabuni zao kupita, wao ni lazima wapewe 'chochote' ili wapitishe maombi yao ya zabuni, hata kama hawana sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa masharti ya zabuni hizo.


  Yote haya yamekuwa yakifanyika huku uongozi wa CCM ukiyatambua na kuyaona, bila kuyachukulia hatua yoyote, kiasi kwamba haya yamekuwa 'utamaduni' ambao, kwa sasa, bila ya kubadilisha mfumo wa utawala – kwa kuweka chama kingine madarakani – haitawezekana. Ufisadi umekuwa jadi, si desturi tena.


  Lakini wananchi waliopo vijijini hawayaelewi mazingira haya ya mjini. Hawaujui ufisadi huu. Wao wanaujua ufisadi wa 'kuvuna mapesa' kutoka kwa wagombea wa ubunge, udiwani na urais. Yapo maeneo kadhaa ambayo, kama wewe ni mgombea na hutatoa rushwa kuwapa watu wakuchague, basi moja kwa moja unakuwa umepoteza sifa ya kuteuliwa kugombea. Umejengeka utamaduni mbaya wa rushwa, ambao uliasisiwa na CCM, ambapo wananchi, wapigakura, tena wale maskini fukara waliofukarika, husema: Waliokuja kabla yako walitupa pesa, khanga, vitenge, kofia, fulana na pilau. Wewe mbona hutoi? Tutakuamini vipi kama wewe hutujali kwa haya?


  Huu ni utamaduni mbaya kuliko wote, ni mbaya kuliko hata utumwa, kwani kwenye utumwa kila kitu kilikuwa wazi – minyororo, mijeledi, kamba, silaha, vilitumika kuwakamata watu na kuwapeleka utumwani. Utamaduni huu wa rushwa wakati wa uchaguzi unawapeleka watu utumwani bila kuwakamata na kuwatia nguvuni, ila wanakamatwa akilini. Wamefundishwa utamaduni ambao umeteka fikra zao, wakiamini kwamba mgombea mwenye sifa ya kuchaguliwa si mwingine ila yule atakayewakirimu kwa khanga, kofia, vitenge, sukari, nyama, pesa, na hata pombe! Bila ya kutoa yote hayo, mgombea – hata kama ni msomi mwenye stashahada ya udakrati wa falsafa (PhD) – hatakuwa na sifa ya kuchaguliwa. Na Watanzania hawa – wale maskini kabisa – watatoa fadhila kwa wagombea wenye kutoa rushwa kwa kuwapigia kura. Ni utamaduni wa 'kuwanunua' Watanzania, kama nyanya sokoni, na baada ya kuwanunua na kutumia kura zao, papo hapo thamani yao hutoweka, wagombea wanaoshinda kuwa wabunge kwa njia ya rushwa hupotea kabisa jimboni hapo na huonekana tena baada ya miaka tano, wakija kujinadi kwa ahadi zisizotekelezeka, wakisindikizwa na 'zawadi' za kuwadanganya wapigakura ili wawanunue na kuhakikisha wanapigiwa kura.


  Ndugu yangu Mtanzania, mimi sikuelewi – baada ya kukueleza yote haya – unaponiambia kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinastahili kuendelewa kupewa ridhaa ya kuitawala nchi hii! Sikuelewi kabisa. Ninakuona kama msaliti. Ndio! Msaliti!


  Kabla ya kuandika makala haya nilifikiria kwa muda mrefu, na kila nilipojitahidi, sikupata jibu lingine zaidi ya ukweli, ambao ni kwamba, kwa sasa, Watanzania tumegawanyika kwenye kambi mbili kuu: Wazalendo na Mafisadi.


  Mzalendo ni yule ambaye anatambua madhara ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi; hata kwenye CCM wapo wazalendo kadhaa, ninawafahamu wengi tu. Lakini, kibaya ni kwamba ufisadi ndio umewekwa kuwa sera rasmi ya CCM, kwani, kinyume na matarajio ya Watanzania wengi – wazalendo – Kamati Kuu imeamua kupitisha wagombea wote 'walioteuliwa' kwenye kura za maoni, HATA KAMA WALIPITA KWA NJIA YA RUSHWA! Makada wengi wa CCM wamelalamika kuhusu hili, lakini uongozi mkuu wa CCM umeamua kufumbia macho malalamiko yote, tena yakiwa yameambatana na ushahidi usiopingika. Zoezi la kura za maoni ndani ya CCM liligubikwa na kila aina ya hila – hujuma, rushwa, ukiukwaji wa Sheria ya Uchaguzi (kwenye sehemu nyingi watoto wadogo, chini ya umri wa miaka 18 wamepiga kura za maoni, na hata wasiokuwa wananchama wa CCM, na wale ambao hawakujiandikisha kupiga kura, nao wamepiga kura za maoni), na pia kwenye mchakato wa kura za maoni kwa upande wa viti maalum, wanawake wengi wamekubali kudhalilishwa kwa kufanya ngono na wanaume (ama wakiwa waume au maswahiba wa viongozi wa UWT au viongozi wanaume wa CCM) ili tu majina yao yaweze kupita. Rushwa ya ngono imetumika hata kwa baadhi ya wagombea wa ubunge wanawake, ambao baadhi yao wamesadikiwa kutoa hongo hiyo ya ngono kwa viongozi wa wilaya na kata ili waweze kupita. Jumapili, Agosti 1, 2010 ni siku ambayo watu wengi hawataisahau kwenye historia ya CCM – kila aina ya ufedhuli ulifanyika siku hiyo! HUU SI UZALENDO!


  Ninapowaona Watanzania wenzangu wakivalia sare za CCM na kuipigia debe, huku wakiimba na kucheza kwa furaha, ninajiuliza: Wana akili timamu?


  Haiyumkini ukamwona mtu anakupeleka mtoni kwenye maji yenye kina kirefu, tena yenye mkondo wa kasi, ambapo ni dhahiri utazama na kufariki, na wewe ukamshika mkono, ukitabasamu na kucheza kwa furaha, na kumwambia: Fanya haraka tufike upesi! HAIYUMKINI!


  Ndugu yangu Mtanzania, nimeamua kuandika waraka huu kwako, ili nikupe wosia huu, kwani huu ni wosia wangu kwako.


  Sisi wote ni Watanzania, achilia mbali itikadi zetu za kisiasa, bado tu Watanzania. Tumepewa ardhi hii na Mwenyezi Mungu, tuitunze, pamoja na kila kilichomo ndani yake. Lakini leo tumekubali mabaya yote haya yatokee. Tumekubali kuwapa nafasi ya kututawala – kadri watakavyo – baadhi ya watu, ambao wamejipachika tabaka la WATAWALA, na sisi tumejipachika tabaka la WATAWALIWA! Tumeyakubali. Lakini hatujui nini kitakuja kutokea baadaye. Hatujui tutakuja kuadhibiwa kwa namna gani, na vizazi vijavyo au hata na Mwenyezi Mungu.


  Wale wanaotoa na kupokea rushwa – wakati wowote ule – watambue kwamba watakuja kuwajibishwa Siku ya Hukumu, kwani vitabu vyote takatifu vimeandika kwamba rushwa ni DHAMBI! Haki hainunuliwi hata kwa dau kubwa namna gani! Haki hupatikana kwa anayestahili haki hiyo! Kama wewe huna sifa za kuchaguliwa kuwa kiongozi, basi, usinunue haki hiyo!


  Ndugu yangu Mtanzania, jichunguze nafsi yako. Oktoba 31, 2010, utasimama upande gani? Upande wa Wazalendo au upande wa Mafisadi? Watu wengi wamesema mwaka huu hawatachagua viongozi kwa kuangalia vyama vyao, bali sifa zao na matendo yao. Huu ni mwanzo wa mwamko wa mapinduzi ya kifirkra, lakini mapinduzi haya bado hayajawafikia watanzania walio wengi – WATAWALIWA – ambao bado wanaamini kwamba CCM ndio chama pekee chenye sifa ya kuwatawala. Je, CCM bado inastahili kuitawala Tanzania huku watu wengi wakiishi kwenye mazingira duni, tena yasiyostahili kwa mwanadamu, tena wakiwa hawana uhakika wa mlo mmoja kwa siku?


  Kama umesafiri kwa basi, kuelekea mikoa ya kusini au kaskazini, umejionea jinsi ndugu zako Watanzania wanavyoishi maisha duni; nyumba za msonge ni nyingi barabarani, tena zimejengwa kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara kuu, kwa hiyo, ifikapo wakati wa kupanua barabara ni dhahiri kwamba nyumba hizo zitabomolewa! Lakini Serikali inawatazama wakati wanapojenga – Wapiga kura wetu hawa! Waacheni, msiwasumbue! – lakini wakati wa kupanua barabara Serikali inageuza kichwa upande mwingine na kusema: Mmekiuka sheria! Hamkuona alama zinazoweka mipaka kwenye eneo la hifadhi ya barabara?


  Lakini jiulize; ni jambo gani linalowafukuza Watanzania hawa kutoka vijijini kwenye makazi yao asilia, hadi kuja kuishi pembezoni mwa barabara kuu?


  Mimi najua nitasimama upande wa Wazalendo, ifikapo Oktoba 31, 2010. Wewe Mtanzania, utasimama upande gani?


  Asante kwa kunisikiliza.  --> Mwana wa Haki
   
 2. Domhome

  Domhome JF-Expert Member

  #2
  Aug 28, 2010
  Joined: Jun 28, 2010
  Messages: 2,004
  Likes Received: 1,054
  Trophy Points: 280
  Kama kweli watz hawa wataipa tena kura CCM basi mateso na taabu wanayoendelea kupata ni halali yao kabisaa na kwahili Mwenyezi Mungu, hahusiki kwani jukumu la kufanya mabadiliko liko ndani yetu na wahusika ni sisi. Chukueni hatua watanzania wenzangu nchi inazidi kuuzwa!!!

  Iwapo CCM itachaguliwa tena basi naomba taabu na mateso yazidi mno kwa watanzania na hasa wale wa vijijini ili 2015, wabadilike.
   
 3. Kaa la Moto

  Kaa la Moto JF-Expert Member

  #3
  Aug 28, 2010
  Joined: Apr 24, 2008
  Messages: 7,668
  Likes Received: 166
  Trophy Points: 160
  Nasimama upande wa mabadiliko na namchagua Dr Slaa kuwa rais wangu.
   
Loading...