Epuka makosa haya kwenye usaili wa ajira

Feb 19, 2013
26
11
Kwa ufupi
Mahojiano haya maarufu kwa jina la usaili wa ajira, yanaweza kufanywa kwa mazungumzo ya ana kwa ana au hata kwa maandishi kupitia taratibu kama mitihani.

By Elizabeth Edward, Mwananchi
Taratibu za utoaji ajira katika ofisi nyingi zinajumuisha mambo kadhaa ikiwamo kuwafanyia mahojiano waombaji wa ajira.

Mahojiano haya maarufu kwa jina la usaili wa ajira, yanaweza kufanywa kwa mazungumzo ya ana kwa ana au hata kwa maandishi kupitia taratibu kama mitihani.

Kwa kawaida, usaili unafanywa kama njia muhimu ya mwajiri kung’amua sifa za mtu anayetaka kumpa majukumu ya kikazi.

Ili ushinde usaili kuna mbinu unazoweza kutumia kuwashawishi watu wanaokuhoji, wakupe wewe majukumu hayo na siyo wengine ambao ni washindani wako.

Kwa mujibu wa kitabu kiitwacho UK’s Leading Interview Expert , utulivu ni moja ya silaha kubwa anazotakiwa kuwa nazo muomba ajira anapokuwa mbele ya jopo la watu wanaomuuliza maswali.

Maelezo yanasema; ‘’Unapoingia kwenye chumba cha usaili, jenga utulivu wa akili, mwili kwa kufuata maelekezo kutoka kwa wanaokufanyia usaili. Jenga uso wa tabasamu huku ukijiweka tayari kujibu swali kwa ufasaha na kuzingatia mipaka ya swali lako.’’

Kitabu kinaongeza kusema: ‘’Wazoee kwa haraka watu wanaokusaili kuwa sehemu yao na wao wawe sehemu yako. Hili utalifanya kwa kuondoa hofu. Wachukulie kama rafiki zako wa karibu ambao mnaweza kuzungumza na kujadili jambo lolote kwa uhuru.’’

Mdau wa masuala ya ajira, Cheryle Palmer anasema ukweli ni jambo la muhimu, siku zote sema ukweli katika usaili kwa kuwa utakusaidia kukuongoza.

“Epuka kuweka maelezo kwa lengo la kupata sifa zinazoweza kukugharimu itakapobainika kwamba kuna taarifa hazioani na siyo za kweli,”anaeleza.

Usifanye makosa haya kwenye usaili

Mwandishi Susan Joyce wa Uingereza anayataja makosa 10 ambayo unapaswa kuyaepuka unapokuwa kwenye usaili.

Moja: Epuka kuvaa mavazi yasiyo na staha au muonekano usio na staha wala unadhifu. Kumbuka kwamba usaili huhusisha watu wengi. Katika usaili epuka mavazi yasiyoruhusika katika maadili au sehemu za kazi..

Mbili: Jiandae, usipojiandaa kwa ajili ya usaili unaweza kupoteza ya nafasi kuchaguliwa. Kutojiandaa kutakufanya kujibu maswali kinyume na matarajio ya unachooulizwa.

Tatu: Epuka hasira. Usithubutu kuingia chumba cha usaili ukiwa na hasira. Wakati mwingine unaweza kuulizwa maswali ya uchokozi. Dhibiti hisia zako na jibu maswali husika bila kukasirika.

Nne; Epuka kutoa maelezo mengi yasiyohitajika. Kueleza mambo mengi, kunaweza kukutoa nje ya mada.

Tano; Kuwa makini na matumizi ya lugha za mwili au ishara. Kwa mfano, unapojibu kwa kutumia kichwa au kutoa miguno, hautawezesha wanaokuhoji kupata kile walichotarajia.

Sita; Ukipewa nafasi ya kuuliza maswali, usiulize mambo yasiyohusiana na ajira unayoomba. Aidha epuka maswali yanayoweza kuwapa wasiwasi waajiri wako.

Swali kama je, mkiniajiri mtanipatia usafiri, ni aina ya maswali yanayoweza kumpa mwajiri wako nafasi ya kubaini udhaifu wako tangu mapema. Unaweza kuuliza swali kama; nini siri ya wateja wenu kusifu huduma mnazotoa?

Swali hili linakujenga kwa kuwa mwajiri anaweza kukutazama kama mtu unayefuatilia kwa karibu masuala ya ofisi yake. Pia swali hili ni ishara kuwa umefanya utafiti kuhusu ofisi husika.

Aidha, unaweza kuuliza matarajio yako kuhusu usaili huo kwa kuuliza swali kama, lini nitarajie majibu ya usaili?

Saba; Epuka matumizi ya simu ukiwa kwenye usaili.

Nane; Achana na majibu mafupi hasa ya ndiyo na hapana. Ukilazimika kujibu hivyo, hakikisha unatoa na mifano kadhaa ili kufanya jibu lako liwe na mawanda mapana zaidi.

Tisa: Jibu maswali ukilenga maeneo ambayo unayafahamu vyema. Jibu swali ukioanisha na uzoefu ulionao kwa kufanya kazi katika ofisi ulizowahi kufanya kazi kabla.

Kumi; Usionyeshe udhaifu wako. Jikite katika kuelezea mafanikio hasa kama umewahi kufanya kazi maeneo mengine. Kama ni mhitimu, mweleko uwe ni kuonyesha namna utakavyotekeleza majukumu yako kwa ufanisi, hasa ukioanisha elimu uliyonayo na majukumu unayaomba.

Ukilazmika kuelezea kuhusu udhaifu wako, tumia udhaifu huo kama nguvu ya kukujenga. Kwa mfano, unaweza kutaja udhaifu wa kuwa na pupa ya kufanya kazi, ukijenga hoja kuwa hali hiyo inakuwezesha kupenda kufanya kila kazi kwa haraka na kwa muda.
 
Mwongozo mzuri sana! Naomba mnisaidie hili mfano Mimi Nina matatizo ya kusikia na ulimi ni mzito wa kuongea, namaanisha sio kwamba sisikii kabisa. Na hii nimehitimu cert, diploma na bachelor ya IT, ila hali hali hii nimekuwa Nayo kabla sijaanza shule ya primary. Je walemavu kama wasioweza kuzungumza vizuri na kusikia kwenye usaili wa oral wanapewa vipaumbile?
 
Mwongozo mzuri sana! Naomba mnisaidie hili mfano Mimi Nina matatizo ya kusikia na ulimi ni mzito wa kuongea, namaanisha sio kwamba sisikii kabisa. Na hii nimehitimu cert, diploma na bachelor ya IT, ila hali hali hii nimekuwa Nayo kabla sijaanza shule ya primary. Je walemavu kama wasioweza kuzungumza vizuri na kusikia kwenye usaili wa oral wanapewa vipaumbile?
Unatakiwa kutoa taarifa zako za kwa wahusika wa usaili kabla ya kuhudhuria kwenye usaili wa oral ukijua tu umchaguliwa kuhudhuria usaili. Hii itapelekea wahusika kukuandalia mazingira mazuri kutoka na hali uliyonayo.
Natumai kuwa umenielewa
 
Back
Top Bottom