The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 617
- 1,799
(Picha: The Sheriff)
Umewahi kupata dalili ya afya ambayo haijawahi kutokea hapo awali na ukaanza kujiuliza ni nini kinachoweza kuwa tatizo? Of course, huenda jibu lako ni kama langu pia, "Kabisa!"
Sasa basi, inapotokea hivi hatua ya kwanza inayopaswa kufanyika ni kuwasiliana na mtoa huduma wa afya ili kupata ushauri au/na matibabu. Lakini mara nyingi hatupendi kufanya hivyo na badala yake tunaishia kujaribu kufumbua wenyewe kuhusu kinachotutatiza.
Mfano, jambo la kwanza tunalofanya, hususan katika enzi hizi za teknolojia, ni kutoa simu zetu na kuandika dalili zetu mtandaoni na kisha kujiridhisha na majibu tunayokutana nayo huko na dawa zinazopendekezwa kisha tunaanza kujitibu.
Wakati mwingine tunamtafuta Dkt. Google ili tu kupata faraja kwamba chochote kinachoendelea si tatizo kubwa.
Hii si sahihi kwani maelezo ya matibabu ya mtandaoni si sahihi kila wakati. Kuna sababu muhimu za kuonana na madaktari kwa huduma za afya: wao ni wataalam, na sisi sio.
Haya yanaweza kuwa madhara ya kutegemea mtandao kupata utatuzi wa changamoto za kiafya:
Wasiwasi wa kuwa na tatizo kubwa kuliko uhalisia
Vyanzo vya mtandaoni vinaweza kuleta magonjwa yoyote ambayo yana dalili zinazofanana. Hii ina maana kwamba, hata kama hali si ya kutisha sana, tunaweza kuishia kupata matokeo kuwa ni suala zito linalohatarisha maisha. Lakini pia, hakuna njia ya kujua kabisa kila kitu kinachoendelea bila kuonana daktari. Yeye anaweza kuona dalili tofauti au zaidi ya unazopata mtandaoni.
Majibu ya mtandaoni yanaweza kukupa mfadhaiko ambao utakusababishia madhara zaidi ya kiafya.
Wasiwasi wa kiafya (health enxiety) ni hali ambayo huathiri watu wengi. Wale walio na wasiwasi huu huhangaika kufikiria kwamba wana tatizo kubwa la kiafya ambalo halijatambuliwa. Wanaamini kwamba wao ni wagonjwa sana, hata kama wanaonyesha dalili ndogo tu. Ikiwa wana afya bila matatizo yoyote, wanaweza kusisitiza kwamba kuna kitu kibaya kinaendelea katika miili yao.
Kuchukua dawa zisizo na ufanisi au kuchanganya
Baada ya wagonjwa kuangalia dalili zao au kudhani kuwa wana hali fulani, wanaweza kuchukua hatua zaidi kwa kujaribu kujitibu wao wenyewe. Njia moja wanayoweza kufanya hivyo ni kwa kuchukua dawa za dukani au kujaribu matibabu ya nyumbani ili kusaidia suala lolote wanalofikiri kuwa wanasumbuliwa nalo.
Lakini dawa zina madhara, hivyo ikiwa hatuhitaji kutumia basi hatupaswi. Kutumia dawa isiyofaa kwa ugonjwa husika haitatui chochote kwani utaendelea kuugua maradhi yaleyale. Pia kunaweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi au kusababisha matatizo makubwa zaidi.
Kupuuza dalili na kudhani tatizo ni dogo kuliko uhalisia
Jambo la kwanza nililosema ni kwamba kutegemea taarifa za mtandaoni ni hatari kwa sababu husababisha msongo wa mawazo na hofu; na kwamba watu wanaweza kuchukua hatua ambazo badala yake zitazidisha shida zao. Lakini wakati mwingine, ni kinyume chake. Wengine wanaweza kudhani ni jambo dogo tu na hivyo kutoona umuhimu wa kumuona daktari.
Pia, wanaweza kuona ni tatizo dogo tu linaloweza kutibiwa nyumbani bila maelezo ya daktari kumbe ni jambo zito ambalo linahitaji matibabu ya haraka. Kupuuza kabisa kunaweza kuifanya hali kuwa mbaya zaidi. Hii ndiyo sababu watu wanapaswa kuwasiliana na madaktari wao ikiwa wanakumbana na hali za kiafya zisizo za kawaida.
Ufafanuzi mbaya na mkanganyiko
Kwa sisi ambao si madaktari, inaweza kuwa vigumu kuelewa masharti ya matibabu ya matatizo tuliyo nayo. Tunaweza kutafsiri vibaya dalili, tatizo, na jinsi linavyoathiri afya zetu. Au tunaweza kutoelewa matibabu, taratibu, na chaguzi za dawa tunapojaribu kujitibu wenyewe.
Ni vyema kuzungumza na daktari kuhusu matatizo yoyote ili aeleze kwa njia ambayo unaweza kuelewa.
Kila mgonjwa ni tofauti na mwingine
Kunaweza pia kuwa na taarifa mtandaoni ambao ni ya kupotosha kwa sababu ya muktadha au ukosefu wa maelezo mengine. Afya ya kila mtu ni tofauti. Kila familia ina historia tofauti ya matibabu, na afya ya mtu binafsi hutofautiana na wengine.
Ndiyo maana ni muhimu sana kwa wagonjwa kuzungumza na madaktari ambao wana historia yao ya matibabu. Madaktari wanaweza kuamua jinsi afya ya jumla ya mtu binafsi inavyohusiana na dalili anazopata. Hii inatoa ufahamu bora juu ya hali ambayo mtu anayo.
Hitimisho
Katika ulimwengu mkamilifu, maelezo ya afya ni ya kweli, sahihi na yanaweza kutoa majibu sahihi kwa kila mtu. Lakini sivyo ilivyo. Hatuishi katika ulimwengu mkamilifu. Taarifa za kupotosha zinajitokeza kila wakati katika utafutaji wetu mtandaoni, na inaweza kuwa vigumu kutambua tofauti ya ukweli na uongo.
Hii inafanya kuwa hatari kwa wale wanaojaribu kushughulikia afya zao peke yao bila kuwashirikisha wataalamu wa afya. Wanaweza kupata msongo wakijaribu kutatua matatizo yao wenyewe, au kupuuza kwamba wanahitaji huduma kabisa. Hii inafanya kuwa vigumu kwa madaktari kutoa huduma muhimu.
Ahsanteni!