EPA: Twasubiri hatua za kisheria, si ripoti

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,720
21,779
EPA: Twasubiri hatua za kisheria, si ripoti

John Bwire Julai 31, 2008



MWISHONI mwa wiki iliyopita magazeti kadhaa nchini yaliripoti kwamba Timu ya Rais ya kuchunguza wizi wa Sh. bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu, imemaliza kazi yake baada ya kujifungia kwa siku kadhaa huko Bagamoyo kuandaa ripoti yake.

Kwa mujibu wa ripoti hizo za vyombo vya habari, muda wowote kuanzia sasa ripoti hiyo itakabidhiwa kwa Rais, na kwamba timu hiyo, inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, imependekeza watuhumiwa wa wizi huo wafikishwe mahakamani.

Kama ripoti hizo ni sahihi, basi, kuna maswali chungu nzima ya kujiuliza; lakini kubwa likiwa ni kwa nini kina Mwanyika na wenzake hawaendi mbali zaidi na kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, na badala yake wanazungumzia suala la kuwasilisha ripoti kwa Rais.

Ni muhimu Watanzania kupata jibu la swali hili kwa sababu wakati Rais anaituma timu hiyo kazi, Januari 9, mwaka huu, aliipa mamlaka (mandate) ya kuchukua hatua za kisheria na kiutawala dhidi ya makampuni na watu binafsi waliohusika na ufisadi huo katika Benki Kuu.

Katika taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kwa waandishi wa habari, Januari 9, kuhusu hatua ya Rais kuunda timu hiyo, hakuna popote ilipoelezwa kwamba timu hiyo itaandika ripoti na kuiwasilisha kwa Rais au kwamba itawasilisha mapendekezo yake kwa Rais kuhusu nini cha kuwafanyia watuhumiwa wa wizi huo.

Kwa hakika kilichowekwa wazi na Rais (kupitia taarifa hiyo ya Luhanjo), ni kusikitishwa na kukasirishwa kwake na taarifa ya kuwepo kwa vitendo hivyo vya wizi katika asasi hiyo nyeti ya umma, na hivyo kuiagiza timu hiyo ichukue hatua za kisheria kwa wote waliohusika na wizi huo.

Sasa inakuaje leo, miezi sita baadaye, Mwanyika na jopo lake wanazungumzia ‘lugha ya kuandaa ripoti na kuiwasilisha kwa Rais’ na pia kusubiri kibali chake cha kuwakamata watuhumiwa wakati tayari alishawapa mandate hiyo Januari 9 wakati akiwatuma kazi?

Kama ni kweli timu hiyo imekamilisha uchunguzi wake, basi, kitu ambacho wananchi wanatarajia kukiona ni kukamatwa, mara moja, kwa watuhumiwa wa kweli kweli wa wizi huo na kufikishwa mahakamani.

Kama hilo halitatokea hivi karibuni, basi, wananchi wana kila sababu ya kuamini kwamba yalikuwepo makubaliano mengine ya siri kati ya Rais na timu hiyo kuhusu nini kifanyike baada ya uchunguzi kukamilika.

Na wananchi wana kila sababu ya kuamini hivyo, kwa sababu, kwa mujibu wa taarifa ya Luhanjo ya Januari 9, mandate ya kuwafungulia mashitaka watuhumiwa ilishatolewa, na wala hapakuwepo na suala la kuandaa kwanza ripoti na kuiwasilisha kwake.

Ni matumaini yetu, hivyo basi, kwamba Mwanyika na wenzake watawachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wote haraka iwezekanavyo, kwa sababu walishapewa nguvu hiyo na Rais tangu Januari 9 mwaka huu.

Vinginevyo, watwambie basi ni maelekezo gani mengine walipewa na Rais mbali ya hayo ya Januari 9 ambayo Luhanjo aliutangazia umma.
 
Back
Top Bottom