ElimuTiba: Jinsi ya kujieleza kwa Daktari

meningitis

JF-Expert Member
Nov 17, 2010
8,349
4,674
Kwa heshima na taadhima napenda kuelezea utaratibu muhimu wa kujieleza kwa daktari ili kurahisisha upatikanaji wa tiba kwa usahihi.

UTANGULIZI

Ni ukweli usiopingika kuwa wengi wetu hatujui ni jinsi gani tujieleze kwa daktari ili tuweze kupata tiba sahihi na kwa wakati.

Pia kuna wakati tunashangazwa na baadhi ya maswali tunayoulizwa na daktari ambayo kuna muda yanaonekana kuwa hayana uhusiano na tatizo linalotusumbua.

Nimeona ni vyema nikaelezea ni taarifa zipi muhimu za kumuelezea daktari ili aweze kufikia hitimisho la kubashiri tatizo lako.

1: Tatizo Kuu(main complaint)

Hapa unatakiwa kumueleza daktari ni kipi kinakusumbua mpaka ukaamua kumuona.ni muhimu sana kueleza tatizo hili limechukua muda gani.

Mfano miaka kadhaa, miezi kadhaa, wiki kadhaa au siku kadhaa au limekuwa likijirudia mara kwa mara kwa muda flani.

Kwa mfano, kukohoa kwa zaidi ya wiki mbili kunaweza kusababishwa na kifua kikuu,kansa au ugonjwa wa moyo, kukohoa kwa wiki moja yaweza kuashiria ni homa ya mapafu, kukohoa kwa masaa kadhaa yaweza kuwa umepaliwa na chakula, kukohoa mara kwa mara yaweza kuwa ni pumu n.k

2: Historia ya tatizo

Hapa unatakiwa kueleza tatizo lako limeanza vipi, linatokea wakati gani(usiku, mchana au muda wote), linahusiana na nini mfano kukohoa na kutapika au tumbo kuuma na kuharisha.

Pia eleza kama tatizo lako linaongezeka au kupunguzwa na kitu flani, mfano unakohoa sana unapolala chali au moyo unakwenda mbio unaposimama lakini unapata afadhali unapochuchumaa au kiungulia kinapungua unapomeza vidonge vya magnesium n.k.

Kwa lugha fupi ya kitabibu maelezo ya ugonjwa wako yatafuata acronym ya DOPARA(Duration, Onset, Periodicity, Associating factors, Relieving or Aggreviating factors).

3: Historia ya afya yako kwa ujumla

Hapa unatakiwa kujieleza kwa ujumla kuhusu afya yako toka uzaliwe. Je umewahi kutibiwa kwa tatizo hilo hilo? Umewahi kulazwa hospitali kwa tatizo lolote, umewahi kufanyiwa upasuaji? Usiogope kutaja hata kama ulitibiwa kwa dawa za kienyeji.

Pia ni muhimu kueleza dawa au tiba zozote ulizowahi kupata miaka kadhaa nyuma au siku chache kabla ya kufika kwa daktari anayekuona mda huo.

Mfano tatizo lako kwa sasa ni mimba kutoka na hapo hapo ukawa na historia ya kutoa mimba kadhaa hapo ulipokuwa kigoli yaweza kuelezea kuwa shingo ya uzazi imelegea. N.k

Pia ni muhimu kumueleza daktari kuwa kuna baadhi ya dawa zinakuletea mzio(allergy)

4: Historia ya kifamilia

Kuna baadhi ya magonjwa yanasababishwa na lifestyle zetu na pia kuna baadhi ya magonjwa ni ya kurithi hivyo ni muhimu kueleza masuala ya kifamilia kwa ujumla.

Mfano babu, baba, mama au bibi walikuwa na tatizo flani kuna uwezekano na wewe ukawa nalo.

Mtoto anaweza kuwa na tatizo la utapiamlo kisa mama ni mfanyakazi wa TBC na hivyo hapati muda wa kumnyonyesha au mume ni dereva wa magari ya mizigo ya kwenda zambia na hivyo kamuambukiza mke wake UKIMWI n.k.

Haya ni baadhi ya maelezo muhimu yanayotakiwa kutolewa kwa daktari ili kufanikisha ugunduzi wa ugonjwa wa mteja
aliyefika kupata huduma.

Yanaweza kubadilika kidogo kulingana na mazingira ya mgonjwa au tatizo lakini huu ndio msingi wa kujieleza kwa daktari.


Baada ya kutoa maelezo haya daktari anatakiwa kukufanyia uchunguzi wa mwili(physical examnation) ili aweze kylinganisha na maelezo yako na baada ya hapo atakuandikia vipimo(investigations) ili kupata ugonjwa halisi unaokusumbua.

Kwa leo niishie hapa...

Aksanteni!

=============
Feb 2016: Nyongeza toka kwa mdau mwingine
Leo naandika kuhusu jinsi ya kujieleza vizuri kwa daktari. Jinsi mgonjwa anavyojieleza kwa daktari ni muhimu sana, kwa sababu inaathiri moja kwa moja ubora wa tiba atakayopatiwa mgonjwa.

Ni muhimu tukafahamu kuwa, maelezo yako kwa daktari yanachangia mpaka asilimia 75 ya daktari kuweza kugundua tatizo linalokukabili! (asilimia 25 iliyobaki ni ya daktari kukufanyia uchunguzi wa mwili kwa mikono yake, na vipimo vya maabara).

Hii ina maana ya kwamba, historia anayoipata daktari kutoka kwako, ina mchango mkubwa sana katika kumuelekeza daktari kwenye tatizo sahihi linalokusumbua; ama kumpelekea daktari kukosea kabisa aina ya tatizo ulilonalo, ama hata kushindwa kabisa kufahamu ugonjwa unaokusumbua hasa ni nini. Mambo yafuatayo yatakusaidia kuweza kujieleza vizuri kwa daktari

1. Usimwambie daktari ugonjwa wako (diagnosis), bali mueleze daktari dalili ulizonazo:

Hapa ninawazungumzia wale ambao wanaingia chumba cha daktari na kuanza kujieleza "daktari nina malaria" au "nina typhoid". Hii sio njia sahihi kabisa ya kuanza kujieleza kwa daktari!

Kufahamu aina ya ugonjwa unaoumwa (diagnosis) ni kazi ya daktari, unachotakiwa kufanya ni kuelezea dalili zako, kwa mfano "kichwa kinaniuma na ninaharisha tangu juzi". Hii ndiyo namna bora kabisa ya kuanza kujieleza mbele ya daktari!

Hakuna kitu ambacho kinamfanya daktari aghafilike kama mgonjwa kuanza kusema diagnosis yake badala ya kuelezea dalili zake.

2. Epuka kutumia maneno ambayo yanaweza kuwa na maana zaidi ya moja kwa watu tofauti

"Daktari nina homa tangu juzi" siku zote mgonjwa akianza kujieleza kwa kauli hii kwangu, swali linalofuata ambalo huwa nauliza ni "unamaanisha nini unaposema homa"?

Na huwa napata maana tofauti kwa watu tofauti. Wengine husema wanamaanisha mafua na kukohoa, wengine wanamaanisha kuwa joto la mwili liko juu, wengine husema wanamaanisha kuwa wanaharisha, na kadhalika.

Hivyo basi, badala ya kuanza kujieleza kuwa una "homa" (ambayo kiukweli,kwa daktari asiekuwa makini, na akachukulia homa kwa maana ya kidaktari, anaweza kukupa ugonjwa ambao wala hauna kabisa), ni vyema ukajieleza kwa kutumia maneno ya moja kwa moja na kwa kutaja dalili zote ulizonazo, moja baada ya nyingine.

3. Usiseme uongo wala kuficha kitu chochote kwa daktari kuhusu afya yako:

Hakuna kosa kubwa (mimi huita suicidal mistake) kwa mgonjwa kufanya, kama kumdanganya kwa makusudi daktari, au kuficha kitu fulani kuhusu afya yake au kuhusu ugonjwa wake. Huna sababu yoyote ya kumdanganya daktari au kumficha kitu daktari kwa sababu zifuatazo;

- Kwanza, kumdanganya daktari kutapelekea daktari kushindwa kubaini tatizo lako, au hata kumpelekea kukosea ugonjwa unaokusumbua; kwa sababu kama tulivyoona awali, daktari anatagemea maelezo yako kwa asilimia 75 kuweza kugundua tatizo lako.

- Pili, hicho unachoogopa kumwambia, kuna uwezekano mkubwa kabisa ya kuwa ameshawahi kukisikia/kukiona na haitakuwa mara ya kwanza yeye kusikia/kuona hicho kitu, hivyo huna sababu ya kuogopa.

- Tatu, nakuhakikishia kuwa kuna uwezekano mkubwa sana (asilimia 99.9) kuwa, daktari atasahau hata sura yako mara baada tu ya wewe kutoka nje ya chumba chake, achilia mbali tatizo lako ulilomwambia!! Kwa mfano, kwa wastani siku ambayo naona wagonjwa naweza kuona wagonjwa zaidi ya 50; na nara zote mwisho wa siku huwa sikumbuki sura za wagonjwa niliowaona, achilia mbali matatizo yao.

4. Unapoenda hospitali, nenda na dawa zako zote unazotumia au uliwahi kutumia kwa tatizo ulilo nalo:

"Nilikuwa natumia vidonge fulani hivi vyeupe vikubwa vya duara" usitegemee kabisa daktari aweze kugundua kuwa ni aina gani ya dawa uliyokuwa unatumia kwa maelezo ya aina hii!

Maana, rangi ya dawa haina umuhimu wowote katika kile ambacho kipo ndani ya dawa. Na kimsingi, kuna dawa ambazo zinapatikana katika rangi tofauti kutegemea na kiwanda zilipotengenezwa, lakini zina kitu kile kile ndani yake!!

Hivyo basi, kama tatizo ulilo nalo ni la muda mrefu, na uliwahi kwenda hospitali na ukapewa dawa ni vyema ukaenda na dawa hizo pale unapokwenda tena hospitali kwa tatizo hilo; au angalau ukabeba kikopo ambacho kilikuwa na dawa hizo.

5. Kwa watoto, aende mtu ambae anakaa na mtoto na/au anafahamu vizuri historia ya ugonjwa wa mtoto:

Huwa napata tabu sana pale ninapomuona mtoto anaesumbuliwa na dalili fulani, halafu namuuliza aliemleta, "amekuwa na dalili hizo kwa muda gani" halafu jibu ninalopata linakuwa "sijui".

Jibu la aina hii linakuwa halina msaada wowote ule kwa daktari, bali huleta usumbufu usio wa lazima kwa daktari; Hivyo basi ni muhimu aende mtu ambae anafahamu vizuri historia ya tatizo la mtoto.

6. Uliza maswali kuhusu ugonjwa wako, vipimo na matibabu:

Mara nyingi madaktari huwa tunajisahau kuwaelezea wateja wetu kwamba ni nini tumegundua anaumwa, na ni vipimo gani anatakiwa kufanya (na majibu ya vipimo hivyo), na matibabu ni yapi.

Hivyo basi, daktari akimaliza kukuhudumia na kukwambia "nenda maabara" kwa mfano, unatakiwa umuulize kwa utaratibu, kuwa je, daktari anadhani una ugonjwa upi? na amekuandikia vipimo gani?

Na pia, hata ukirudi kwa daktari na majibu ya vipimo vyako, ni vyema ukamuuliza majibu yanasemaje, na yanamaanisha nini; Vile vile kwa dawa atakazokuandikia.

Daktari ambae anajua anachokifanya hatapata shida kabisa kukuelezea yote hayo (labda kama umeuliza kwa ukali au kwa kutumia lugha isiyo ya kistaarabu).
 
wanasema 70% ya diagnosis hutegemea maelezo ya mgonjwa.kabla ya vipimo ni lazima ujieleze au kuchukuliwa maelezo ya daktari ili kupata the right diagnosis.
 
wanasema 70% ya diagnosis hutegemea maelezo ya mgonjwa.kabla ya vipimo ni lazima ujieleze au kuchukuliwa maelezo ya daktari ili kupata the right diagnosis.

ni muhimu kwa mgonjwa kutambua haya niliyoeleza ili aweze kunga'amua kama huduma aliyopewa ni sahihi au la
 
Somo zuri sana. Asante kwa kutukumbusha. Kuna wamama wanapelekewa watoto clinic na mahausigelo. Msome hapa!
hapo kwenye bold umegusia jambo zuri sana.kuna wakati daktari anashindwa kupata taarifa muhimu kutokana na ukosefu wa muhusika sahihi.ingawa tiba yaweza kupatikana lakini tiba sahihi na endelevu inahitaji taarifa kamilifu.
 
Thanks for the lesson maana huwa mswahili kujieleza ni ishu bora utusaidie..
 
kuna baadhi yetu tunaogopa kujieleza kwa daktari kwa kuona kuwa siri zako zitajulikana.ukweli ni kwamba daktari au mtumishi wa afya hana ruhusa ya kutoa siri zako kwa mtu yoyote bila idhini yako.
Ni mazingira adimu sana yanamruhusu kufanya hivyo mfano pale vyombo vya sheria kama mahakama vikimtaka kufanya hivyo !

Pindi unapogundua siri zako zimepelekwa kwa asiyehusika bila ridhaa yako basi una haki ya kumshitaki daktari.
 
maelezo haya niliyoyatoa yanatumika duniani kote.uwe unatibiwa Tanzania au India!
 
Kuna watu ukiwauliza unafanya kazi gani wanadhani unataka kuwakamua/kuwafuatilia. Lengo ni kujua occupation ya mtu kwani kuna occupationa diseases. Pia strategy za matibabu hazilingani kulingana na uwezo wa mtu. Kuna mtu unatamani umwandikie dawa effective ila unaona hatamudu gharama zake hivyo inabidi umwandikie dawa zetu za siku zote.
 
Kuna watu ukiwauliza unafanya kazi gani wanadhani unataka kuwakamua/kuwafuatilia. Lengo ni kujua occupation ya mtu kwani kuna occupationa diseases. Pia strategy za matibabu hazilingani kulingana na uwezo wa mtu. Kuna mtu unatamani umwandikie dawa effective ila unaona hatamudu gharama zake hivyo inabidi umwandikie dawa zetu za siku zote.

nashukuru sana mdau kwa kuendelea kutoa elimu.there are so many misconception huko kwa wanajamii wa kawaida na kwa bahati mbaya hakuna wafafanuzi wa mambo na hatimaye watu hupotoshwa mno.
 
Naomba na mimi nichangie hii mada nzuri, mimi ninasema tatizo la kujieleza pia huwa linatokana na baadhi ya madaktari sio wote, kuwa harsh kwa mgonjwa inawezekana kutokana na muonekano wa mgonjwa au tabia ya kuzaliwa ya daktari.

Pili kuna baadhi ya wagonjwa huwaogopa madaktari (sijui sababu ni nini) na hivyo hushindwa kujieleza kwa ufasaha/usahihi.
 
Na madaktari wengine ukianza tu kuwaambia kichwa kinaniuma kabla hujamaliza hata kusema kichwa kinaniuma keshakuandikia ukapime choo, mkojo, marelia (a.k.a. damu) kha! utajieleza saa ngapi yaani unakuwa kama unampotezea muda? hii sijui imekaaje wallah!
 
Nashukuru sana kwa elimu hii. Naomba nichangie hapa kidogo. Unajua asilimia kubwa ya watanzania hawana elimu na walio na elimu hawatoi elimu yao waliyopata kwa jamii kwa mfano somo kama hili wanaofaidika ni wachache tu (wasomi). Naomba tutumie fursa hii kama wasomi kuwapa/kupeleka elimu hii tunayoipata kwa watu wengine(jamii). Asante sana
 
Na madaktari wengine ukianza tu kuwaambia kichwa kinaniuma kabla hujamaliza hata kusema kichwa kinaniuma keshakuandikia ukapime choo, mkojo, marelia (a.k.a. damu) kha! utajieleza saa ngapi yaani unakuwa kama unampotezea muda? hii sijui imekaaje wallah!

chezea governmet hospital, dokta anakimbizana na mda aende kwenye private yake, tuwe waungwana jamani
 
Nashukuru sana kwa elimu hii. Naomba nichangie hapa kidogo. Unajua asilimia kubwa ya watanzania hawana elimu na walio na elimu hawatoi elimu yao waliyopata kwa jamii kwa mfano somo kama hili wanaofaidika ni wachache tu (wasomi). Naomba tutumie fursa hii kama wasomi kuwapa/kupeleka elimu hii tunayoipata kwa watu wengine(jamii). Asante sana

ni kweli mkuu!ni muhimu kufanya jambo au mambo kwa manufaa ya watu wa kawaida.
 
ushaur wako ni mzur mi mwenyewe nasumbuliwa na tatizo la kusikia miungurumo ndan ya masikio lakin cjapata tiba stahiki labada sababu ni kutojieleza vizur kwa daktar
 
Back
Top Bottom