#COVID19 Elimu zaidi itolewe kuondoa dhana potofu juu ya chanjo ya Covid 19

Chu joe

Member
Jul 15, 2021
7
3
Na Chu Joe

Dunia ina mengi nayo mengi hayana maana, ni msemo ambao unatumika kwa muda mrefu hapa nchini kwetu, lakini kwasasa jambo linalosemwa kwa maneno mengi yasiyo na maana ni chanjo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona.

Kila mtu amekuwa na lake la kusema iwe ni mtaani au katika mitandao ya kijamii lakini kwa asilimia kubwa wanaozungumza mawazo mgando kuhusu chanjo ya covid 19 ni watu ambao hawana uelewa wowote juu ya faida ya chanjo hiyo.

Nadhani umefika wakati sasa kwa wizara ya afya na viongozi mbalimbali kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili kuwaondoa hofu waliyojiwekea mioyoni mwao kuhusu chanjo hii.

Katika hili wizara ya afya kupitia waziri wake Dkt Doroth Gwajima, wana kazi kubwa ya kuifanya kwasababu bado kuna watu wengi wenye uelewa mdogo kuhusu chanjo hii hali inayosababisha kuwaongopea na wengine kuwa chanjo hiyo ni sumu na ina madhara kwa binadamu.

Kwa upande wangu nimefarijika sana kumuona Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa mstari wa mbele kuchanjwa ili kuwadhihirishia wananchi kuwa chanjo hiyo ni salama na ina faida ya kumkinga mtu atakayekuwa ameipata.

Mbali na kujitokeza kuchanjwa Rais Samia pia alisema anatambua kuwa yeye ni amiri jeshi mkuu na mama wa familia hivyo asingejitoa na kujipeleka kwenye kifo kwasababu anamajukumu, kwahiyo amekubali kuchanjwa kwasababu chanjo imethibitishwa na wataalamu.

Waziri mkuu Kassim Majaliwa naye ni miongoni mwa watu waliozungumza katika uzinduzi wa chanjo hiyo na akasema amekubali kuungana na rais kuchanjwa ili kuonyesha Serikali haina nia mbaya kwa wananchi wake, na wameileta kwasababu imetokana na utafiti.

Kwa upande wake waziri wa afya Dkt Doroth Gwajima, naye alikuwa mstari wa mbele katika kupata chanjo hiyo na akasema watanzania hawapaswi kuwa na hofu kuhusu chanjo ya Covid 19 kwani iko salama.

Ukiachana na kauli hizo walizotoa viongozi wa kisiasa wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo bado elimu zaidi inahitajika ili kuwaweka sawa wananchi ambao wana mashaka na kupata kinga hiyo.

Mitaani na katika mitandao ya kijamii kuna maneno mengi ambayo ni upotoshaji wa hali ya juu kuhusu chanjo ya Corona kwahiyo elimu inapaswa kutolewa kuanzia katika ngazi ya mtaa, wilaya, na mkoa ili kila mwananchi aelewe umihimu wa chanjo hiyo.

Nafikiri kwasababu chanjo imeishafika nchini serikali haina budi kuendelea kuitoa huku upande mwingine ikizidi kutoa elimu wa wananchi ili wajitokeze kupata chanjo hiyo inayotolewa bure bila malipo na kwa hiari.

Ikiwa serikali kupitia wizara ya afya itaendelea kutoa chanjo bila kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi natarajia kuona watu wengi wakishindwa kujitokeza kuchanjwa kwasababu wana hofu mioyoni mwao.

Natumaini wizara ya afya pamoja na serikali kwa ujumla ni sikivu na wamesikia malalamiko ya wananchi kuhusu chanjo baadhi wakidai ina madhara na inaweza kupelekea kifo, kwahiyo natumaini watatoa elimu zaidi ili kuondoa dhana potofu kwa wananchi.
 
Back
Top Bottom