Elimu yetu ifundishwe kufuatana na mazingira yetu

Lascodaily

New Member
Jul 15, 2021
1
1
Elimu ni msingi wa maisha ya mwanadamu hapa duniani katika nyanja za kijamii, kifikra, kiuchumi na kiutamaduni.

Elimu ya nchi haitakiwi iwe ya mzahamzaha kwa kila mtu kuweza kubadilisha mfumo kutokana na atakavyoamka au atakavyojisikia kufanya.

Ni vizuri sana elimu yetu ifundishwe kwa kufuata mazingira ya jamii husika kama vile jamii za wafugaji, wavuvi, wakulima, wafua vyuma na wengineo na hili litasaidia :-

1. Kutatua changamoto za ajira; kutokana na elimu kutolewa kutokana na mazingira yao wanayoyaishi itawasaidia kupata ujuzi wa ziada wa juu ya kile wanachokifanya kila siku, kwamfano wananchi wanaoishi pembezoni mwa maziwa na bahari wangepata elimu zaidi ya uvuvi kuliko ilivyo sasa.

2. Kuwa na wataalamu wa kutosha wa kada fulani; Elimu inayotolewa kwa kufuata mazingira ya jamii fulani ni lazima itazalisha wataalamu wengi sana wa kada husika ambao wanaweza kusambazwa katika mazingira tofautitofauti kutokana na uhitaji wa jamii ile, ilivyo sasa mtu amezaliwa Dar es Salaam na kukulia palepale Dar es Salaam anaenda kusomea kazi ya Bwana shamba ambapo yeye mwenyewe tangu azaliwe hajawahi hata kushika jembe ndio maana tunakuwa na wataalamu wa ofisini na siyo kazini.

3. Kuongeza uzalishaji; Elimu itakapotolewa kwa kufuata mazingira ya jamii itasaidia sana kuongeza uzalishaji katika jamii kwa sababu wananchi wengi watafanya shughuli zao kisasa zaidi kutokana na kuwa elimu juu ya mazingira yao yanayowazunguka na siyo kusomea kitu ambacho kujiajiri inakuwa ni changamoto.

4. Kuongeza mapato ya serikali; kitendo cha kuwepo kwa uzalishaji mkubwa kwenye jamii itasaidia serikali kupata mapato makubwa yanayotokana na kodi mbalimbali ambazo itachukua kwenye ushuru wa mazao au bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini mfano ikiwa jamii ya wakulima watalima mazao mengi na kuuza nje ya nchi serikali itapata mapato kutokana na ushuru wa mazao.

5. Kupunguza utegemezi mkubwa wa ajira za serikali; kutokana na watu kupata elimu kutokana na mazingira yao itapunguza utegemezi wa ajira za serikalini kwa sababu kila mmoja atakuwa na uwezo wa kujiajiri kutokana na mazingira yake yanayo mzunguka tofauti na sasa elimu yetu inaijenga jamii zaidi kwenye kutegemea zaidi ajira za ofisini kuliko zile za kwenda kufanya kazi nje ya ofisini.

Mwisho; Ili jamii iweze kupata elimu kutokana na mazingira yao kunahitajika uwekezaji mkubwa sana kuanzia kwenye muda, fedha, wataalamu na maeneo kwa ajili ya kufanyia hiyo elimu.

Ni vyema serikali ikafanya jambo hilo mapema kabla tatizo la ajira halijawa tatizo kubwa la kitaifa kwa wananchi wa Tanzania japo mpaka sasa tayari ni Changamoto.
 
Back
Top Bottom