Elimu ya Uwekezaji wa Hisa

Jan 3, 2017
11
38
Hisa Ni Nini, Nafaidikaje Na Uwekezaji huo?
___________________________________________



Na #Mwenda ND,

Nimekuwa nikipata maswali mengi juu nini maana ya hisa na nini faida na changamoto za kumiliki hisa na uwekezaji wa dhamana za fedha (Hisa, Hatifungani pamoja na Vipande) kwa ujumla, nimekuwa nikipata maswali hayo kutoka kwa watu mbalimbali, lakini itoshe tu kusema siwezi kumjibu kila mmoja kwa wakati wake na ndiyo maana mwaka huu nikaamua kuwa nitaandika kitabu ambacho bado siku 39 kiweze kuwa mikononi mwa watu!

Kitabu hiki naamini kitaweza kujibu maswali mengi ambayo watu hujiuliza. Imeelezwa nini maana ya Hisa, Hatifungani, Vipande, Historia ya biashara hii, historia ya baadhi ya masoko ya hisa duniani, mbinu na vigezo vitumikavyo kuwekeza katika hisa na namna ya kuorodhesha kampuni soko la hisa!

Tukirejea kwenye maada ya msingi juu ya hisa (stocks/equities/shares), Kwa kifupi, Hisa ni sehemu ya umiliki halali katika kampuni husika. Hisa moja huwakilisha masilahi madogo ya mwekezaji/mtu katika kampuni husika kwani mwekezaji anayemiliki hisa nyingi huwa na masilahi makubwa na nguvu kubwa ya maamuzi ndani ya kampuni husika. Kwa mfano, kama kampuni ina fulani ina hisa zipatazo 1,000,000 hivyo basi kama mtu/mwekezaji anamiliki hisa zipatazo 100,000 maana yake anamiliki 10% ya kampuni.

Haki na stahiki za mwekezaji huyo katika kampuni husika hazitazidi 10%, yaani kama kampuni imefanya biashara na kupata faida TZS 100,000 baada ya kodi basi yeye atapata gawio la TZS 10,000 kama faida kutokana na alichowekeza kwenye kampuni hiyo.

Pia mwanahisa/mwekezaji ana haki ya kuhudhuria Mkutano Mkuu wa mwaka wa Wanahisa (Annual General Meeting) AGM wa kampuni husika ambapo katika mkutano huo ndipo maamuzi yote juu ya kampuni husika hufanyika maamuzi, maamuzi hupitishwa kwa kupiga kura kwa wanahisa wote.

Kwa kifupi hisa ni biashara, hisa ni mali fedha (yaani unaweza ibadili muda wowote), hisa ni kitegauchumi. Kuna aina mbili (2) za hisa, kuna hisa za makampuni binafsi (Private Limited Companies), Kwa mfano, familia ya Gulambass Dewji ni wamiliki wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL Group) ambapo kila mwanafamilia ana hisa zake pale, pia familia ya Said Salim Bakhresa ambao ni wamiliki wa kampuni ya Bhakresa Group of Companies/Azam kila mwanafamilia ana hisa zake katika kampuni

Lakini pia kuna hisa za makampuni ya Umma (Public Limited Companies) kama vile Vodacom Tanzania PLC, TBL PLC, Tanzania Cigarettes Company PLC, NMB Bank PLC, Acacia PLC na zinginezo. Tanzania hadi sasa ina idadi ya makampuni 28 ya Umma yalioorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar Es Salaam (DSE), makampuni 21 miongoni mwao ni makampuni yaliopo hapa Tanzania (local companies),na makampuni 7 miongoni mwao ni makampuni kutoka nje ya Tanzania (cross-listed companies). Hivyo hisa tunazokwenda kuzijadili hapa ni hizo za makampuni ya Umma.

Kwanini tunayaita makampuni ya Umma? Ni kwasababu yanauza hisa kwa wananchi wa kawaida (Umma) tofauti na yale makampuni binafsi ambayo wanahisa ni wanafamilia pekee. Mahesabu ya makampuni ya Umma huwekwa wazi kwa Umma tofauti na makampuni binafsi kama niliyoyataja hapo juu.

Hata hivyo hisa za makampuni ya Umma zimeagwanyika, zipo aina nne za hisa za makampuni ya Umma, (1.) Hisa za kawaida (ordinary shares), (2.) Hisa za waanzilishi (preferred shares), (3.) Hisa za kampuni (corporate shares) pamoja na hisa za wamiliki (lion shares), maelezo ya kiundani zaidi juu ya aina hizi za hisa yapo kwenye kitabu.

Lakini hisa ambazo huuzwa katika soko la hisa mara nyingi ni zile hisa za kawaida (ordinary shares) ziliitwa hisa za kawaida kwasababu zinaweza kununuliwa/kumilikiwa na mtu hata wa hali ya kawaida (mwenye kipato kidogo ama cha kati) na mtu au taasisi yeyote inaweza kuwekeza (companies, institutions, pension funds, high networth individuals, small investors etc) katika hisa hizi.

Mwanahisa wa kampuni husika ana haki za mbalimbali, mojawapo ni;-

(a) Haki ya kuhudhuria mkutano mkuu wa wanahisa unaoitishwa kila mwaka.

(b) Haki ya kuchagua wakurugenzi kwenye mkutano mkuu (AGM) kupitia upigaji kura.

(c.) Haki ya kupitia taarifa na mahesabu ya kifedha ya kampuni husika (Financial Statements) nakutoa maoni yake.

(d) Haki ya kupata upendeleo (mfano kampuni ikitoa hisa za kuuza (rights issue) inampa kipaumbele mwanahisa kununua hisa kwa bei ndogo ukilinganisha na bei itakayo kuwa sokoni.

NB: Zipo haki nyingi na wajibu wa mwanahisa katika kampuni husika, maelezo zaidi yapo kwenye kitabu cha "HISA NA HATIFUNGANI: Mwongozo wa Uwekezaji Kwenye Masoko ya Hisa" kitakachozinduliwa 20 Oktoba 2019.

Kuna faida nyingi za kuwekeza kwenye hisa, zipo faida nyingi sana lakini hapa nitaeleza kubwa tatu pekee, ambazo ni;-

1. Gawio (Dividend), haya ni malipo yanayofanywa na kampuni baada ya kutengeneza faida katika biashara, na hiyo hutolewa kulingana na sera ya kampuni husika, inaweza kutoa asilimia kadhaa kama gawio kwa wanahisa wake.

Katika utoaji wa gawio (faida) makampuni yanatofautiana kwa kiasi na muda wa kutoa gawio, mfano, Tanzania sekta ya benki ambapo benki kama CRDB, DCB na NMB) pamoja na sekta ya mawasiliano (Vodacom Tanzania PLC) hutoa gawio kwa awamu moja kwa mwaka wakati makampuni mengine kama vile kampuni ya DSE,TBL,TCC,SWISS, Twiga hutoa gawio mara mbili kwa mwaka.

NB: Gawio siyo lazima kutolewa kwa wanahisa, hivyo kampuni yaweza kupata faida na ikaamua isitoe gawio bali ipanue biashara zake kwa kuwekeza tena hiyo faida. LAKINI, kampuni nyingi hutoa gawio kama njia ya kushawishi wawekezaji.

2.Kukua kwa mtaji, yaani (Capital gain) - hii ni pale bei ya hisa inapopanda ukilinganisha na bei uliyonunulia, mfano hisa za TCC zilikwenda sokoni kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 kwa bei ya TZS 410/- kwa hisa moja lakini sasa hivi 2019 bei ya hisa moja ni TZS 14,500/- kwa hiyo mtu/mwekezaji aliyenunua hisa hizo mwaka 2000 kwa sasa atakuwa na ongezeko la mtaji wa TZS 14,090/- kwa kila hisa (hii ina maanisha kuwa, kama alinunua hisa 1,000×410 mwaka 2000 alitoa jumla ya TZS 410,000/- lakini kwa sasa thamani ya hisa hizo 1,000 imeongezeka yaani 1,000× 14,500=14,500,000/- Hilo ni ongezeko la asilimia ngapi? Wataalam mtanisaidia!

3.Dhaman/Amana, pia unaweza kutumia hisa kama dhamana (Collateral) unapotaka kuchukua mkopo kwenye mabenki ya kibiashara mfano una hisa 1,000 za TCC ambazo zina thamani ya TZS 14,500,000/- ukienda benki na shida ya TZS 7, 100, 000/- Benki husika 'inaweza' kukukopesha na kuchukua cheti chako cha umiliki wa hisa na kuweka kama dhamana mpaka pale utakapomaliza kulipa mkopo wako, ikitokea umeshindwa kulipa basi benki itakuja kuuza hisa zako na kujilipa hela uliyokopa. Kipindi chote wakati umeweka dhamana haki yako ya kupata gawio bado utaipata, isipokuwa hutoweza kuuza hisa zako mpaka umalize mkopo.

NB: Kuna faida nyingi sana katika Uwekezaji wa hisa, maelezo zaidi yapo kwenye kitabu.

Pia za kuwekeza kwenye hisa hasara na changamoto nyingi, hapa nitaeleza kwa ufupi. Hasara na changamoto ambazo unaweza kuzipata ni pamoja na;-

1. Kushuka kwa mtaji (capital loss), Hiyo hutokea pale bei ya hisa inaposhuka, kama bei ya hisa ikishukaikawa ndogo tofauti na ulivyonunua utakuwa mtaji wako umepungua, hivyo ukitaka kuuza utapata hasara. Mfano, mwaka 2017, Hisa moja ya Vodacom Tanzania PLC iliuzwa kwa TZS 850/- lakini kwasasa inaizwa kwa TZS 760/- maana yake kwa kila hisa moja iliyonunuliwa mwaka 2017, imeshuka bei kwa TZS 90/-

Hivyo kama mtu alinunua hisa 1,000 za Vodacom mwaka 2017 alitumia TZS 850,000/- leo hii akitaka kuuza atauza kwa TZS 760,000/- hivyo atakuwa amepata hasara ya TZS 90,000/-

Kuna njia mbili tu za kuepuka hasara hii, (i) Kuendelea kuzimiliki hisa mpaka zitakapopanda bei (ii) Kununua zaidi zinapokuwa zimeshuka bei ili siku zikiongezeka bei upate faida mara dufu.

2.Kutopata gawio, hii inategemea na kampuni ilivyofanya kazi zake kwa mwaka mzima wa fedha, kama kampuni inaishia kupata hasara (loss) basi itakuwa ni ngumu kwa kampuni kutoa gawio. Kwa mfano, hisa za kampuni ya TOL Gas tangu ziorodheshwe DSE mwaka 1998 haijawahi kutoa gawio mpaka mwaka jana kampuni hiyo ilipotangaza kuwa itatoa gawio. Gawio hilo linalipwa mwaka huu.

Pia kampuni ya saruji ya Twiga yaani Twiga Cement PLC kwa mwaka huu imetangaza kuwa haitatoa gawio kwa wanahisa wake licha ya kupata faida, kwani faida ya mwaka huu itatumika kulipa mkopo wa $ 150m (Zaidi ya TZS 300 ilizokopa kununua mitambo mipya mwaka jana) hivyo mwaka huu hakuna gawio kwa wanahisa wa Twiga Cement.

3. Kufilisika kwa kampuni au kampuni kufuata masharti ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana 'Capital Markets and Securities Authorities (CMSA ), Kwa mfano----kampuni ya NICOL iliondolewa kwenye orodha ya makampuni yaliyomo DSE (delisted) mwaka 2011 kwa sababu ya kukiuka baadhi ya kanuni za CMSA na DSE na ilirejeshwa sokoni (DSE) mwaka 2018 baada ya kutimiza vigezo vya CMSA na DSE .Kwa hiyo mwanahisa kwa kipindi chote hiko wakati kampuni imetolewa sokoni anakuwa hapati gawio wala hawezi kuuza hisa zake.

NB: Zipo changamoto na hasara mbalimbali ambazo mwekezaji anaweza kupata kutokana na uwekezaji wake katika hisa kupitia soko la hisa lolote lile duniani, liwe katika nchi zilozoendelea ama zile zinazoendelea.

PICHA: Kitingoji cha Lower Manhattan katika Jiji la New York, nchini Marekani zilipo Ofisi za Soko la Hisa New York (NYSE), Soko la hisa kubwa zaidi duniani kimtaji.
 
Naomba kujuzwa kwa wale wazoefu wa masuala ya hisa ni kampuni zipi ambazo ni nzuri kwasasa nikinunua hisa zake, baada ya miaka kumi mpka kumi na tano angalua faida na matumaini yatakuwepo bila kuwa na hofu ya kampuni husika kufilisika. Natanguliza shukrani.
 
Mada ni nzuri sana.
Utakapo rejea ni vizuri zaidi ungezungumzia changamoto la solo letu LA DSE naamini hii italeta mwamko Wa uwekezaji katika hisa nchini .
Kwani elimu ni ndogo sana inayotolewa kuhusu DSE hususan sheria mbali mbali kuhusu uwekezaji Wa mashirika ya umma nk
 
mkuu swala la hisa ni swala ambalo elimu yake yafaa itolewe kwa kina ili elimu ifike kwa watu waamuwe kuwekeza ila mkuu binafsi sipendi sana kuwekeza katika hisa kutokana na uhalisia wa biashara ya hisa bora bonds na bills kidogo nafuu kule
 
8 Reactions
Reply
Back
Top Bottom