Elimu ni funguo ya uzima na pia funguo ya mauti

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,884
MSHIKE SANA ELIMU USIMUACHE; ELIMU IPI ILIKUWA INAZUNGUMZIWA?

Na, Robert Heriel


Miaka ya 2000 katika nchi yetu kulikuwa na muako mkubwa sana wa elimu. Serikali, taasisi na mashirika mbalimbali yalianzisha programu za kuhamasisha jamii ipeleke watu shule. Ni kutokana na umuhimu wa elimu ndio maana serikali ikaondoa ada ya shule ya msingi ili kutoa nafasi kwa kaya masikini kupeleka watoto wao shule. Serikali pia ilianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi
kwa Walioikosa (MEMKWA) na, Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), lengo kuu ni kuongeza idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika na kuongeza elimu kwa Watanzania.

Pia Kutokana na ongezeko la idadi ya watu nchini, ilikuwa lazima kujengwe shule na vituo vya elimu kusudi pawe na uwiano baina ya madarasa na idadi ya watu, hivyo serikali ilianzisha programu ya ujenzi wa shule za kata, jambo ambalo liliongeza kiwango cha idadi ya wanafunzi waliosajiliwa na waliofika kiwango cha sekondari.

Ni kipindi hicho hicho ziliundwa washaa, matamasha, propaganda za kuhamasisha jamii iipende elimu, na kwa asilimia kubwa muako ulikuwa ni mkubwa mpaka serikali ikaelemewa.

Propaganda na matamasha mengi ya kipindi kile yalilenga zaidi kuitukuza elimu, kueleza matokeo chanya ya mtu kupata elimu ikiwa ni pamoja na kuwa na maisha mazuri kwa kupata kazi zenye vipato vikubwa mbali na kuheshimika ndani ya jamii. Hali hiyo ikapelekea watu kupeleka watoto shule kwa wingi, na vijana na mabinti wengi kusajiliwa kwa ndoto za kuwa na maisha mazuri.

Huko shuleni waalimu na wadau wa elimu waliwaasa wanafunzi na kuwapa sumu kuwa bila elimu hakuna maisha mazuri, waliwaambia elimu ndio ufunguo wa maisha. Hii ikawajengea watoto dhana kuwa bila elimu hakuna mafanikio jambo ambalo ni ukweli mkubwa.

Pia, serikali, taasisi na mashirika yalipambania kombe, yalipigana kufa kupona kuinua elimu kwa jinsia ya kike na kuondoa dhana potofu yakuwa mwanamke ni wanyumbani tuu, ambaye anasubiri kuolewa, hivyo miaka ya 1990 - 2005 kazi kubwa ilifanyika kuielimisha jamii kwa habari za kumkomboa mwanamke kielimu. Kwa sasa mafanikio yanaonekana mbali na athari hasi zilizopo lakini athari chanya ni nyingi zaidi.

Kwa sasa wasomi wameongezeka kwa kiasi, sio wengi sana lakini pia sio wachache sana. Kwa ngazi ya shahada mpaka diploma ni asimilia ndogo sana, lakini angalau kidato cha nne ni karibu nusu ya wananchi wa Tanzania kwa wale waliozaliwa kuanzia miaka ya 1990, hii ni kutokana na sababu kuwa kuanzia miaka ya 2005, ilikuwa kawaida kwa nusu ya darasa la saba katika shule kwenda sekondari. Huku Darasa la saba wakiwa bado wapo wengi kuliko makundi mengine.

Viongozi wa dini nao hawakuwa nyuma kuhamasisha waumini kwa habari ya kusoma, kila dhehebu lilihangaika kwa namna yake kuhamasisha waumini wake kwenda shule kusoma, Aya na Sura za maandiko matakatifu yanayohamasisha elimu zilifanywa mahubiri na mawaidha.

Kwenye Biblia baadhi ya aya zilipata umaarufu mkubwa mathalani, kitabu cha Mithali 4:13 ;
MIT. 4:13 SUV

"Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako."

Kwa Waislamu walipewa mawaidha yasemayo; "TAFUTA ELIMU HATA KAMA NI CHINA" Somo hilo likiwa kama hadithi za maswahaba wa Mtume (s.a.w.w).

Tukaona dini na madhehebu ndani ya nchi hii yakianzisha na kujenga shule na Vyuo vikuu hapa nchini. Na hakika vimetoa mchango mkubwa ndani ya nchi yetu.

Ni kutokana na umuhimu wa elimu ndio maana baadhi ya Watanzania wenye fedha wanasomesha watoto wao katika shule zenye gharama kubwa sana, wengine wakiamua kuwasomesha nje kabisa ya nchi.

Sasa vijana wamesoma na wengine wanaendelea kusoma. Waliosoma kwa sasa wanalalamika hawana ajira, wengine wamefikia hatua ya kuona elimu haina umuhimu wowote. Wanajuta na kuona kama wametapeliwa na kuingizwa mjini na ndevu. Wanaona wamepoteza miaka mingi kwenye jambo lisilo na manufaa yoyote.

Hata wale waliobahatika kusoma na kupata mafanikio bado jamii inawaona kama hawana msaada ndani ya jamii zao. Imekuwa ni kawaida kwa watu kusema, wasomi hawana faida kwa nchi yetu, pengine ni kutokana na tabia ya ubinafsi miongoni mwetu ndani ya taifa hili; kwamba mtu akishapata mahali pa ulaji anajitumikia mwenyewe yeye na tumbo lake na watoto wake badala ya kuitumikia jamii.

Kauli ya Mshike sana Elimu usiiache iende zake, kwa maana huo ndio uzima wako, ni kauli ya jumla, ni kauli ambayo inaweza kuwa na manufaa au laa.

Sio kila elimu ni yakuishika, elimu zipo nyingi, zipo elimu ambazo ni uzima wako na uzima wa taifa; na zipo elimu ambazo ni mauti kwako na mauti kwa taifa. Ni lazima tutumie kauli mahususi katika kuelezea suala la elimu,

Elimu inaweza kuwa uzima lakini wafundishaji wakawa wauaji, ni sawa na, tiba inaweza kukuponyesha lakini Tabibu anaweza akawa muuaji. Sasa endapo Tabibu ni muuaji na ndiye anayekupa dawa ya kukuponyesha sioni namna ya wewe kuwa mzima.

Elimu inaweza kuwa uzima wako lakini watoaji wakawa wauaji. Hivyo wanaweza wakaku-overdoze au wakakupa pungufu hivyo ukadhurika.

Elimu waliyopewa vijana katika nchi yetu kwa kiasi kikubwa wamepewa na wauaji licha ya kuwa elimu yenyewe ni Uzima. Waalimu wetu wengi walitupa elimu kwa namna isiyofaa, Elimu hutolewa kwa upendo, kwa Ukweli na uhalisia, kwa vitendo na nadharia, kwa umoja na ushirikiano, kwa nidhamu na maadili, kwa ujasiri na ushujaa.

Lakini elimu tuliyopewa wengi wetu haikuwa upendo, walimu wengi sio wote walieneza chuki baina ya wanafunzi, walikuza matabaka ndani ya darasa kati ya wenye uwezo darasani na wasio kuwa na uwezo darasani, adhabu nyingi zilitolewa kwa chuki, walimu walikuwa wakichapa watoto kuwakomoa na sio kuwafundisha, Walimu walifundisha uongo uongo bila uhalisia wakiwaambia watoto kuwa wakisoma wakifika kiwango fulani na hapa ni chuo kikuu watakuwa wamefanikiwa na maisha mazuri, hatimaye watoto waliojitahidi walifika huko chuo kikuu na kuona kumbe walidanganywa, hapakuwa na ukweli wowote zaidi ya uongo.

Waalimu hawakuwafundisha watoto umoja na ushirikiano hasa katika mambo makubwa, na hapa ni kwenye kazi za darasani, watoto wakafundishwa ubinafsi kwamba hakuna kusaidiana wakati wa mitihani,hivyo mwenye kujua hamsaidii asiyejua. Hii imepelekea watoto walipokuwa watu wazima waliofanikiwa kwenye maisha hawawasaidii wale walioshindwa, elimu imeongeza ubinafsi ndani ya jamii maradufu.

Kabla ya elimu hii ya kikoloni, watu kusaidiana ilikuwa ni jambo la kawaida sana na lazima, lilikuwa jambo la kimila, na wasiopenda ushirikiano na umoja walitengwa na kupewa adhabu kama sio kufukuzwa kabisa. Elimu ya kikoloni imeleta utengano ndani ya koo, jamii na taifa.

Walimu wamekuwa watu wa kwanza kuiharibu jamii kwa kufundisha mambo yasiyofaa. Kwenye maisha hakuna kuibia, kushirikiana sio kuibia. Kitendo cha kukataa ushirikiano kwenye mitihani kuna lenga zaidi kukuza uchoyo wa watoto na kutoa elimu ya ubinafsi.

Mtu yeyote aliyehitimu shahada au elimu ya kikoloni basi lazima awe amehitimu pia suala zima la ubinafsi, uchoyo, uongo na kutokuwa na uhalisia, kozi ya porojo kuliko vitendo. Wenye elimu karibu wote wana sifa hizo.

Ndio maana ni rahisi kwa msomi wa zama hizi akifanikiwa tuu utashangaa ndugu zake hawaendi kumtembelea katika jumba lake la kifahari, wanajifanya wanasheria nyingi zinazohamasisha ubinafsi kuliko umoja.

Waalimu walijigeuza miungu watu, wao hawakosea wala hawakosolewi. Waliwafundisha wanafunzi hofu na mashaka. Waalimu walitoa elimu ya mauti ya kuwafanya watoto wasiwe na uwezo wa kukemea maovu na uhalifu. Na wale wanafunzi walioonekana wapenda haki waliionja joto ya jiwe. Waalimu badala ya kuwafundisha wanafunzi nidhamu waliwafundisha nidhamu ya woga.

Hii ikapelekea wanafunzi walipohitimu wakawa wamebobea katika kozi ya nidhamu ya woga. Woga wa mtu kwa hapa nchini unalandana kiwango chake cha elimu. Kwa kadiri mtu anavyopata elimu ndivyo kiwango cha woga kinavyoongezeka.

Hivyo ukimuona mtu ana degree ya fani fulani basi jua kuwa pia ana degree ya woga, Diploma ya woga na Astashahada ya woga, na hapa nazungumzia elimu ya nchi zetu za Afrika.

Waalimu walifundisha wanafunzi kunyamaza na kutokutetea haki zao, na ndio maana kwa sasa ni rahisi kwa msomi kuonewa na kunyamaza kimya kuliko kwa mtu ambaye hajasoma.

Maprofesa wanaofundisha katika vyuo vyetu karibia wote wamefuzu shahada ya uzamivu wa uoga, sio watu wa kujaribu, ni watu wa ndio mzee wakiwatetemekea wakubwa zao hata kama wanakosea..

Waalimu wamewafundisha watoto kutumia zaidi mawazo ya wengine na kuyaamini kuliko kutumia mawazo yao na kuamini katika fikra zao. Huko chuo wengi wao hukaririshwa habari za kizamani za wahenga na wanafalsafa, hauruhusiwi kufikiri kwa akili zako bali lazima umsome Noam Chomsky, Sijui Fayor, sijui Freud Segmund, wakina Karl Marx, Kina Isack Newton, Nicola Tesla, Kina Faraday, Kina Da Vinci'. n.k Sio kosa kuwasoma watu hao lakini kulazimisha watu wafikiri kama wao ndio kosa.

Kulazimisha mtu afikiri kama alivyofikiri Nicola Tesla, au Niccolo macheavelle, kama sio Galilei Galileo ni dalili ya wendawazimu. Ni kuua ubunifu wa watoto, kuua fikra za watoto na kuzifanya ziwe tegemezi kwa watu wengine, hii itafanya watoto wasijiamini wao wenyewe.

Huwezi ukawa msomi wa kukariri mawazo ya watu wengine, usomi sio ukasuku yaani kurudia alichosema mwingine. Sishangai kuona wasomi wengi wakijitambulisha usomi wao kwa ku-state laws na principles za watu wengine.

Matokeo ya waalimu kuua ubunifu wa watoto tunayaona hivi leo, watu wanasoma mpaka PhD lakini bado wanaakili kama hawajasoma, hakuna ubunifu, hakuna mambo mapya kutoka kwao, lakini tunauona ubunifu kwa watu ambao hawajasoma licha ya kuwa ni ubunifu usio na ufanisi mzuri.

Elimu iliyouzima wako na ambayo unapaswa uishike ni elimu itakayokufunsihsa upendo, ubunifu, uthubutu, vitendo, umoja na ushirikiano.

Elimu itakayokufanya uipende jamii yako, elimu itakayokufanya ubuni mambo yatakayosaidia jamii yako. Elimu ambayo itakufanya uwe na uthubutu wa kujaribu mambo mbalimbali.
Elimu itakayokufanya ulete umoja na ushirikiano ndani ya jamii.

Waalimu wamefundisha watoto kudharau kazi zingine yaani mtu aliyesoma mpaka degree ya jambo fulani tuchukulie Udaktari, basi hawezi kufanya kazi nyingine kwani anazidharau.

Elimu ya dizaini hii sio uzima bali ni mauti kwani kama furasa ya udaktari haitapatikana basi mtu huyu atabaki anashangaa shangaa tuu akilaumu watu na kujilaumu yeye mwenyewe.

Elimu inapaswa kutolewa na kusisitiza kuwa kazi zote ni sawa. Waalimu wanapaswa wawafundishe watoto kuwa kazi zote na fani zote ni sawa na ni bora. Waalimu wawafundishe watoto kuheshimu kazi zote, kuheshimu fani zote bila kujali zinalipa au laa.

Tunaona zama hizi kuwa wasomi wa fani fulani wakizubaa zubaa kama kondoo wakati wa mvua kutokana na kuhitimu degree ya dharau na kejeli. Mtu kasomea shahada ya elimu, ni mwalimu kakosa kazi lakini zipo kazi zingine anakataa kufanya anasubiri kazi ile ile, wewe ni mpumbavu na mpuuzi.

Nitakupa mifano,

Yesu wa Nazareth kitaaluma alikuwa ni Fundi seremala, lakini akabadili kazi akawa mhubiri wa habari njema, Daudi mwana wa Yese alikuwa Mchungaji wa ng'ombe, mbuzi na kondoo huko porini, hivyo kitaaluma alikuwa mfugaji lakini alibadilisha upepo akaingia kwenye siasa na kuwa mfalme.

Petro alikuwa mvuvi lakinia akabalisha upepo akawa mhubiri habari njema, Mtume Muhamadi alikuwa mfanyabiashara yeye na Babaake mdogo aitwaye Abu Twalib ambaye alikuwa akimsaidia katika misafara yake. Baadaye mtume akabadili upepo akawa mtume kwa kuhubiri habari za ALLAH.

Viongozi wakubwa nchini kwetu, kama Hayyati Mwl Nyerere, Mkapa wote walibadili fani zao.

Mwalimu bora ni yule anayemfundisha mtoto kuwa Flexible, kwamba awe mwepesi kubadilika na kukubali mabadiliko. Sasa waalimu wengi huwakaririsha watoto mifano ile ile hata darasani na kwenye mitihani huwapa sehmu ya mifano ile kama sehemu ya maswali, sasa ikifika siku ya mtihani wa NECTA ambapo mtungaji wa mtihani ni mwingine inakuwa changamoto kwa mtoto, na wengi husindwa.

Kusoma sio kudharau kazi za wengine bali kuzipa heshima.

Usomi ni kuifanya kazi iliyokuwa haiheshimiki kuifanya iheshimike.

Kwa mfano, kazi ya muziki, ngumi, upiga debe katika stendi, uuzaji wa mkaa, kuuza karanga, vitumbua, hizo ni kazi ambazo ndani ya jamii zetu zinachukuliwa poah, hivyo hiyo ni fursa kwa wasomi kuzifanya kazi hizo ziheshimike.

Wajiajiri kupitia kazi hizo ili kuziinua, sio utafute kazi zilizoheshimishwa na watu wengine na wewe kudandia dandia.

Wasomi wamegeuzwa ngedere kudandai dandia matawi ya watu wengine. Wakisikia jambo fulani linalipa anaenda tena shule anasomea jambo hilo, msomi anakuwa na degree kumi kidogo kisa upumbavu wake.

Sasa si imeandikwa kuwa mshike sana elimu usiiache kwa maana huo ndio uzima wako, nami nakuambia, angalia aina ya hiyo elimu ya kuishika na mchunguze sana mwalimu atakayekupa hiyo elimu.

Elimu inaweza kuwa nzuri ila anayekupa elimu akawa mbaya.

Mwisho; Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa.

Taikon nimemaliza, hongera nawe kwa kumaliza kusoma mpaka hapa, najua wengi ni wavivu.
Tupendane, tuijenge nchi.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa, Morogoro
 
Back
Top Bottom