Elimu kwa wananchi juu ya katiba mpya ni muhimu

Mahesabu

JF-Expert Member
Jan 27, 2008
5,971
3,827
NA STEPHEN BALIGEYA
“FUNGENI milango tupigane, tuone mbabe ni nani kati yetu na nyinyi,” hayo ni baadhi ya maneno yaliyotolewa na wabunge, wakati wa mabishano juu ya kanuni za Bunge, Dodoma, juzi. Wabunge hao walikuwa wakibishana juu ya utaratibu uliotumika kuteua majina matatu ya wabunge watakaowania nafasi ya Wenyeviti wa Bunge badala ya majina sita kama kanuni zinavyoeleza. Spika alieleza kuwa, kwa mujibu wa Kamati ya Bunge, majina mengine hayakuwa na sifa, hivyo kukubaliana kuyaengua kwa ushirikiano wa kambi ya upinzani. Hoja ya kutaka kufunga milango ili ‘watwangane makonde’ ilitokana na baadhi ya wabunge wa CCM kumtaka Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje (Chadema), kusema kuwa, uamuzi wa Kamati ya Bunge, ulifanywa katika ‘Dark Market’.
Kimsingi, ‘neno’ hilo lilionekana kuwakera baadhi ya wabunge na kutaka Wenje aondoe kauli hiyo, na hapo ndipo, kutunishiana msuli kupoanza na wengine kwa busara zao, wakaomba milango ifungwe, ‘watwangane’ makonde ili kumaliza ubishi.
Kauli ya wabunge hao haitofautiani sana na kinachoendelea katika mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mapitio ya Katiba, ambayo tayari imesomwa kwa mara ya kwanza bungeni.
Muswada huo wa sheria unalenga kutoa utaratibu wa namna ya kuandaa mchakato wa kuelekea kwenye upatikanaji wa muswada wa katiba mpya, katiba ambayo wengi wanadhani itakidhi matakwa ya wananchi.
Lakini pamoja na kuwepo kwa rasimu hiyo, kinachoendelea kutokea hakina tofauti na kutunishiana msuli baina ya makundi yanayohasimiliana, na kutaka kila kundi lionekane lenya kuteka mjadala huo kuliko lingine.
Kitendo cha kuchana muswada huo mbele ya watu ambao ni viongozi wa serikali sio tu kinaonyesha kwamba muswada huoni mbovu kama inavyoelezwa bali ni utovu wa nidhamu uliokubuhu, kwani ukitaka kujua upeo wa mtu kifikra tazama matendo yake.
Kwa kuwa rasimu hiyo imetolewa, Watanzania wanatakiwa kuitumia kama njia ya kuelekea kule wanakotaka kwenda kwa kujadili kwa kina na kuelezea uzuri na ubaya wake, na siyo kuonyeshana ubabe mbele ya uso wa umma.
Kwa sababu wale ambao wanajadili kwa kuipinga na bila kuichana sio kwamba ni wapumbavu kiasi hicho, bali kwa kuwa jambo limetolewa kujadiliwa, watu wajadili kwa hoja na siyo ‘matusi’.
Wala Watanzania wasije wakadanganyika kwamba, kuna watu wana hatimiliki ya kujadili muswada huo wa sheria na kuuteka mjadala unaoendelea, bali hata asiyejua maana ya katiba anatakiwa kuzungumza anachofikiri.
Tena watu wasiendelee kupotosha umma kuwa, kilichopelekwa bungeni ni muswada wa katiba, bali wananchi wanatakiwa kuelezwa ukweli kwamba hiyo ni sheria ambayo inalenga kutoa utaratibu wa kupata katiba mpya.
Ndiyo maana Profesa Issa Shivji anasema kuwa, hata kama mtu atatoa mawazo ambayo yako kinzani na mtazamo wako, mwache aseme, kwani yakichambuliwa vizuri mawazo yake, inawezekana yakawa na maana ndani ya katiba.
Kwa mfano, kama mtu anasema hajui maana ya katiba, mtu huyo anamaanisha kwamba amekosa kitu muhimu katika maisha yake, kwa maana ya elimu, hivyo katiba inatakiwa kutoa elimu ya kina juu ya dhana ya katiba kwa kila raia.
Hivyo hivyo, kama watu wanafariki dunia kwa sababu ya kukosa huduma ya afya au kwa njaa wakati katiba inasema kila mtu ana haki ya kuishi, maana yake lazima kiwepo kifungu cha kuwalinda wananchi wasife kwa njaa kwa mujibu wa katiba.
Kwa kuzingatia mtazamo huo, bila shaka hatuwezi kusimama na kueleza kuwa fulani ana mawazo thabiti na ambayo hayatakiwi kuhojiwa na watu wengine.
Bali kinachoweza kutokea ni kwamba, kila mmoja ana nafasi yake katika kujadili na kuzungumzia katiba, na viwango vya mawazo vitatokana na elimu, mazingira, makundi ya kijamii, hali ya kipato na hulka ya mtu na mtu.
Kwa maana kuwa, wakulima wanapojadili katiba wataijadili kwa kulilia soko la mazao yao na namna athari za mvua za msimu zinavyokwamisha uzalishaji wao.
Aidha, wafugaji wataeleza namna wanavyoathirika pindi mifugo yao inapokufa kwa njaa na magonjwa, mambo hayo yakijadiliwa kwa kina, yatawekwa katika katiba kwa namna ambayo yatawalinda watu hao.
Kwa hiyo, kisiwepo kikundi cha watu ambao kwa hulka na mazoea yao wanadhani wanaweza kufikiri zaidi kwa niaba ya Watanzania, kila Mtanzania ana haki ya kuzungumza na kusikilizwa, hata kama mawazo yake yanaenda kinyume na matakwa ya wengi.
Kwa mfano, mjadala wa katiba uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mwanzoni mwa mwezi huu, alitokea kijana mmoja ambaye aliwalaumu sana watu waliokuwa kwenye mjadala, kuwa walijadili katiba badala ya kujadili mambo ya msingi.
Kijana huyo alieleza kuwa badala ya watu kujadili kupanda kwa bei za vyakula na maisha kwa jumla, watu wanapoteza muda wa kujadili katiba, kitu ambacho kwa mtazamo wake hakikuwa na maana.
Jaji Mkuu Mstaafu Barnabasi Samatta, alijaribu kumwelisha kwamba, kama baraza la mawaziri likipungua na matumizi makubwa kwa serikali yatapungua pia, na je, haoni kwamba huduma zingine za kijamii kama afya, na elimu zitaboreshwa?.
Kwa mujibu wa Jaji Samatta, baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuwa na gharama kubwa kwa serikali yatatakiwa yaainishwe kwenye katiba, ili kila serikali itakayoingia madarakani, ifuate mkondo huo.
Kwa kufanya hivyo, itakuwa njia mojawapo ya kubana matumizi na hivyo, kusaidia kuboresha huduma zingine za kijamii, na kuinua hali ya maisha kwa wananchi masikini.
Hiyo ni njia moja tu ya umuhimu wa katiba, lakini pia, haikupaswa kumlaumu kijana huyo na kuonekana kama ‘mpumbavu’ mbele ya umma wa watu waliohudhuria, mwenye kumdharau hajui muhimu wa katiba.
Kwani, katiba inatoa fursa kwa watu kujieleza na kutoa maoni yao kwa uhuru na bila kuingiliwa ilimradi tu havunji taratibu, hivyo kumshangaa mtu wa mawazo tofauti ni ‘ujinga’ kikatiba.
Kwa maana hiyo, kila mwananchi anatakiwa kuwa na ujasiri wa kujadili kwa uhuru juu ya mchakato huo unaondelea bila kurubuniwa na mtu au kushawishiwa na mtu.
Mjadala huo sio wa kuonyeshana itikadi za kisiasa za kutaka chama fulani kionekane shujaa dhidi ya vyama vingine, bali uwe mjadala wa kuwaunganisha Watanzania.
Lazima ieleweke kuwa kama kutatokea majadiliano ya kujengeana chuki kwa sababu ya utofauti wa mawazo wakati bado serikali haijasema kama imekubali maoni au imekataa, utakuwa uchizi kifikra.

Kwani, kuna watu wanafikiri kuwa kwenda kinyume na watu wengine, ni njia ya kuonyesha umaarufu kuliko kwenda pamoja na msingi wa taifa, mawazo ya kudumisha umoja na kuondokana na vurugu na chuki.
Mfumo huo ambao unataka kuonekana kukua nchini, umechangiwa na siasa za ‘maji taka’, siasa za watu kujiona miungu watu kwenye jukwaa la siasa na kuwaona wengine, ‘mazimwi’.
Mazimwi wanaonekana wale wenye mawazo kinzani, na matokeo yake, kila anayeonekana kwenda kinyume na matakwa ya itikadi fulani, anapewa jina la ‘fisadi’.
Kama mawazo hayo mfu yataendelezwa na kutukuzwa katika mjadala huo wa muswada wa sheria na hatimaye mchakato wa muswada wa katiba, hakuna shaka kuna uwezekano wa wananchi wa kada ya chini, kusemewa badala ya kusema wao.
Kwa maana hiyo, mawazo au masuala ambayo yanawagusa moja kwa moja wananchi wa Vijiji vya Butiriti, Hamkoko, Nantare na Nebuye kule Ukerewe, wanakuwa hajaeleza kero zao za kilimo cha mhogo.
Kwa hiyo, kushindwa kwa wananchi hao kueleza kero hiyo, maana yake, maisha yao ndani ya katiba yanakuwa yametengwa na kutegemea kudra za mwenyezi mungu kuishi kwa uhakika.
Kwa mantiki hiyo, ni wajibu wa wananchi kuelezwa umuhimu wao kujieleza na kutoa maoni yao juu ya rasimu ya sheria hiyo na kujiengua kutumiwa kwa namna yoyote ili kukuza umaarufu wa watu au kikundi fulani.
Na wala hakuna kiongozi wa serikali, taasisi au chama cha siasa anaweza kusimama na kuwauliza wananchi kama wanaitaka rasimu hiyo au hawaitaki, huo ni wizi na ufinyaji wa mawazo ya watu wengine.
Kiongozi au mtu wa namna hiyo ni mchochezi kwa sababu yeye kama mwananchi, anatakiwa kutoa msimamo wake na siyo msimamo wa watu wote, kutaka kuungwa mkono kwa kuuliza watu wengine, ni uchakachuaji wa fikra za watu wengine.
Hakuna haja ya Watanzania kutwangana makonde wakati fursa ya kujadiliana bado ipo, kukimbilia vita badala ya majadiliano sio muafaka mzuri kimaisha
 
Back
Top Bottom