Elimu bure/elimu pasipo malipo inatekelezeka au ni mzigo kwa walimu ?

BUMIJA MOSES

Member
Aug 27, 2020
75
85
Serikali ya Tanzania kupitia Dira ya maendeleo ya Taifa imelenga kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, miaka minne ijayo. Lengo hilo lilitazamiwa kufanikiwa kupitia sekta ya elimu na mafunzo ambapo ilitarajiwa kuleta maendeleo ya haraka kwa kutumia rasilimali watu iliyoelimika. Serikali ilikusudia kuhakikisha uwepo wa fursa ya elimu bora kwa wote.

Mwaka 2016, Serikali ilitangaza kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidatu cha nne, katika kufanikisha hilo Serikali iliendelea kutumia ruzuku ya uendeshaji wa shule (Capitation Grants), ambayo ilianza kutolewa na Benki ya Dunia kuanzia mwaka 2002 hadi 2006 (Dola 10 kwa kila mwanafunzi kwa mwaka). Benki ya Dunia ilisitisha utoaji wa ruzuku hiyo mwaka 2006, baada ya kutoridhishwa na matumizi yake. Kuanzia mwaka 2007, Serikali iliazimia kutoa Tshs 10,000/= kwa kila mwanafunzi. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, Serikali ikaja na kauli kuwa sasa elimu ni bure.

Ninalenga kuangalia fedha zinazotolewa na Serikali zinatosheleza kuendesha elimu bure.
kwenye hiyo ya Ruzuku ya Tshs 10,000/=, inayotolewa kwa kila mwanafunzi. Mchanganua wa matumizi yake ni kama ifuatavyo:-

1. Tshs 4,000/=, zinabaki Wizarani kwa ajili ya kununua vitabu vya pamoja. Kwa maana nyingine fedha zinazotakiwa kufika shuleni ni Tshs 6,000/=, kwa kila mwanafunzi. Twende pamoja katika matumizi ya fedha hizo.

(a) Ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia visivyo vitabu (Non Textual material), 30% ya Tshs 6,000/=, ambazo ni sawa na Tshs 1,800/=. Fedha hizo zinatakiwa kununua tufe, vivunge vya sayansi, vivunge vya mwili wa binadamu, manila, madaftari, chaki, majaladio nk.

(b) Ukarabati wa miundombinu ya shule. 30% ya Tshs 6,000/=, ambayo ni sawa na Tshs 1,800/=. Ukatabati utahusisha majengo, mfumo wa maji, umeme, samani n.k.

(c) Uendeshaji mitihani endelezi, 20% ya Tshs 6,000/=, ambayo ni sawa na Tshs 1,200/=, eneo hili litahusisha uchapaji, urudufishaji wa mitihani, na shajala kwa ajili ya utoaji ripoti za uendeshaji na matokeoa ya mitihani kwa wazazi na ngazi nyingine zinazohusika.

(d) Uendeshaji wa michezo 10% ya Tshs 6,000/=, ambayo ni sawa na Tshs 600/=, eneo hili litahusu ununuzi wa vifaa vya michezo katika ngazi za shule, Kata, Halmashauri, Mkoa, Kanda hadi Taifa.

(e) Utawala 10% ya Tshs 6,000/=, ambayo ni sawa na Tshs 600/=, eneo hili litahusu ununuzi wa shajala kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi za waalimu wakuu, waalimu na maandalio ya masomo.

Nauliza maswali yafuatayo kutokana na hoja hiyo
1. Je, kwa ujumla Ruzuku hiyo inatosheleza mahitaji ?
2. Je, Tshs 1,200/=, iliyotengwa kwa ajili ya mitihani ambayo kwa mwezi ni sawa na Tshs 120/=, inawezesha waalimu kuchapa mitihani, kupiga photocopy mitihani, kununua shajala za kuandikia ripoti nk. ?
3. Kutokana na hali hiyo, je bado tuna sababu ya kuendelea kutoa kauli kuwa tunatoa elimu bure kwa sasa ?

Nawasilisha
 
Back
Top Bottom