Elimu bora inahitaji ushiriki wa wazazi na walezi

DolphinT

JF-Expert Member
Mar 9, 2016
1,308
1,828
Katika makala zilizotangulia niliweka bayana kuwa ili tuweze kupata elimu bora tunahitaji mambo gani; kwa ufupi tu nilianisisha suala la mazingira bora ya kujifunza na kufundishia, vifaa vya kujifunza na kufundishia waalimu bora, ushiriki wazazi na walezi pamoja na suala zima la stahiki na maslahi ya walimu.

Katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu serikali imekuja na mkakati wa elimu bila malipo kwa shule za umma kama ilivyainishwa katika waraka wa elimu namba tatu wa mwaka 2016. Ambao pamoja na mambo mengine umeondoa baadhi ya michango iliyokua ikitolewa na wazazi kusaidia upatikanaji wa elimu kwa kundi kubwa la watanzania ambao bila mpango huo wangekosa nafasi ya kupata elimu.

Licha ya waraka kueleza wajibu na majukumu ya kila eneo kwa maana ya walimu, viongozi, serikali na wazazi; changamoto bado inabakia kwa wazazi na walezi.

Jukumu la kuhakikisha mwanafunzi anapata elimu na sio kuhudhuria shule tu ni la jamii nzima na sio la mwalimu pekee. Wajibu wa mzazi au mlezi sio tu kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakula, anapata sare za shule dafttari na kalamu pekee. Mzazi ana nafasi kubwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba mwanafunzi au mwanae anahudhuria shule na anajifunza pia anakua na nidhamu ili aweze kufanya vizuri katika masomo yake na kupata maarifa stahiki pindi anopohitimu

Wazazi wengi wana shauku kubwa ya kuona watoto wao wanafanya vizuri katika masomo yao, lakini hawako tayari kufuatilia maendeleo yao shuleni pamoja na mienendo yao kinidhamu wakiwa shuleni na hata nyumbani. Jukumu hilo wameachiwa walimu peke yao. Na walimu wanapojaribu kuwanyoosha kinidhamu jamii inawanyoshea kidole na kuwalaumu.

Kutokana na ugumu wa maisha wazazi wamekua hawana muda wa kukagua daftari za watoto wao, kutembelea shuleni na kufanya mashauriano na walimu, kukaa na watoto na kuwashauri kuhusu maendeleo shuleni na changamoto wanazokumbana nazo na namna ya kuzitatua ili waweze kufikia malengo yao katika elimu na maisha.

Wanafunzi wanapofanya vizuri katika masomo yao hupongezwa sana na wazazi pamoja na serikali, lakini wanapofanya vibaya wazazi na jamii kwa ujumla huwanyooshea kidole walimu kuwa wameshindwa kutimiza na kushindwa kujiuliza je wao walikua wapi na je Je wametimiza wajibu wao kama wazazi na walezi?

Alipata kuandika mwalimu Nyerere kuwa "it takes a village to raise a child" kwa tafsiri isiyo rasmi ni jukumu la jamii au kijiji kumkuza mtoto. Hii inamaanisha kuwa ikiwa jamii itaungana kwa pamoja kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu bora ni dhahiri kwamba hakutakua na malalamiko kama tunayoyaona sasa, kuwa wanafunzi wanafanya vibaya na pia hawana nidhamu kwa walimu na wazazi.

Linapokuja suala la ushiriki wa Jamii katika kutoa elimu iliyo bora wazazi na walezi wanapaswa kuwa sehemu ya vikao vya maamuzi kuhusu maendeleo ya watoto wao katika shule za umma kama inavyokua katika shule binafsi na zile za taasisi zisizo za kiserikali mathalani za kidini. Wazazi lazima watambue kwamba serikali haiwezi kubeba majukumu yote kwa mwamvuli wa elimu bure na wazazi wabweteke na kukaa kimya tu wakisubiri watoto wao wapate elimu itakayoleta mabadiliko katika maisha yao binafsi na jamii imnayowazunguka

Wazazi wasiwe wapiga filimbi kuwalaumu walimu tu na kuzuia adhabu zinazotolewa na walimu kwa wanafunzi; Lazima wayaelewe mazingira wanayofanyia kazi walimu na aina ya wanafunzi walio nao. Wazazi wanaposhindwa kutoa ushirikiano kuhusu suala zima la maendeleo ya wanafunzi walimu nao hukata tamaa na kuamua kuacha liende kwani hawana ambacho wanakipoteza Jambo ambalo kiuhalisia linaumiza mwalimu kushindwa kumsaidia mwanafunzi kufikia malengo yake.

Wanasiasa, watunga sera na watu wenye ushawishi katika jamii lazima walielewe hili na wawe mstari wa mbele kushirikiana na wadau wa elimu kuhakikisha kuwa wazazi wanashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakua na nidhamu , kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kitaaluma, kukaa na wanafunzi na kuwapa ushauri na miongozo kulingana na malengo yao kitaaluma na sio kuliacha jukumu hili kwa walimu ambao wameshaulika na kazi yao haithaminiwi katika jamii ya leo.

Fedha za zinazotumika katika elimu bure zinatokana na makusanyo ya kodi kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo wananchi wenyewe. Kimsingi ni fedha nyingi sana. Utumikaji huu wa fedha ni uwekezaji, na uwekezaji usiokuwa na malengo ya kupata faida hauna maana hata kidogo. Lazima wananchi tuone kwamba fedha zetu zinazokwenda kugharimia elimu ya vijana wetu zinaleta faida kwetu na kwa taifa letu.

Mamlaka ya kudhibiti ubora wa elimu lazima ihakikishe pamoja na mambo mengine inawajengea uwezo wakuu wa shule na walimu wakuu pamoja na walimu katika suala zima la kuashirikisha wazazi kuhusu maendeleo ya wanafunzi katika shule za umma.

Tukiwaachia jukumu hili walimu na serikali tunakua tumepoteza mwelekeo. Tuwajibike kama wazazi kuhakikisha vijana wetu wanakua nguvu kazi madhubuti kwa ajili ya maendeleo ya taifa hili. Vinginevyo shule zetu zitakua vituo vya kulelea watoto kwa miaka kumi na mmoja na baadae watoto hao wasiwe na mchango wowote kwa maendeleo ya nchi yetu.

Tutajenga taifa la watu wasiokuwa na uwezo wa kuchangia maendeleo mara baada ya kuhitimu masomo yao, watakuwa ni walalamikaji kwa wazazi na serikali yao pamoja na kuwa mtaji kwa wanasiasa wenye uchu na tamaa ya madaraka. Wakati ni sasa kila mmoja atimize wajibu wake katika kuhakikisha kwamba vijana wetu wanapata elimu bora. Wazazi watambue elimu bure ni gharama; Gharama yake ni muda na kujitoa kuhakikisha kuwa wanafuatilia nidhamu ya watoto wao na maendeleo ya shule kwa ujumla wake. Washirikiane na walimu kwa karibu na sio kuwanyooshea kidole na kuwaachia majukumu yao.

Serikali kupitia mamlaka husika inalo jukumu la kuhakikisha kuwa fedha za umma licha ya kusimamiwa vyema katika matumizi yake ambayo ni kuhakikisha kuwa watu wote wanapata elimu, inalo jukumu la kuhakikisha kuwa uwekezaji huu una tija kwa siku za baadae. Shule zetu za umma ziwe viwanda vya kuzalisha nguvu kazi itakayo kuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha kuwa nchi ya Tanzania inapiga hatua kimaendeleo kwa kuwatumia watu wake. Vinginevyo tutahesabu hasara baada ya miaka muda fulani tutakapojitathmini na kulinganisha fedha tulizotumia na watu tuliozalisha je wana mchango gani kwa maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.

Makala hii niliandika katika gazeti la kila siku pamoja na ukurasa wa facebook.
 
Back
Top Bottom