El Maamry amtolea uvivu Maximo

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,790
288,047
El Maamry amtolea uvivu Maximo
na Khadija Kalili
Tanzania Daima

MJUMBE wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Said Hamad El Maamry, amewaunga mkono mashabiki waliomzomea Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbrazil Marcio Maximo.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Radio One cha jijini Dar es Salaam hivi karibuni, El Maamry alisema kuwa, zomea zomea ile haikuwa kumchukia kocha huyo, bali kufikisha ujumbe mzito.

Alisema, kikubwa ambacho Maximo anatakiwa kufanya, ni kukuna kichwa, kupata jawabu la nini afanye ili kuwaridhisha mashabiki hao waweze kumshangilia kama ilivyokuwa awali badala ya kumzomea.

“Mbona wakati timu inafanya vizuri katika kampeni za kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika walimshangilia hata kumbeba? Sasa iweje wamzomee akiwa na Kilimanjaro Stars? Kuna jambo hapa,” alisema.

Alisema siku zote, muungwana hupenda kunyooshewa kidole ili kukosolewa, na kwa vile anaamini kocha huyo ni muungwana, anatakiwa kuwauliza au kujiuliza ni kipi wanachokipigia kelele.

“Napenda kumwambia Maximo, akubali kushauriwa na kukosolewa, na kwamba akifanya hivyo bila shaka timu yake itakuwa nzuri,” alisema El Maamry.

Alisema yeye mwenyewe yuko tayari kumpa Maximo ushauri iwapo atahitaji, kwani alihudhuria mechi hizo na pia anao uzoefu wa muda mrefu katika soka.

El Maamry alisema, amebaini kuwa Maximo anachemka katika kupanga vikosi vyake, kwani amekuwa akiwaacha wachezaji wenye uwezo na kuegemea zaidi kwa chipukizi wasio na uzoefu, hivyo timu kufanya vibaya.

“Si kwamba mimi ninapinga chipukizi wasicheze, isipokuwa jambo la muhimu ni kukubali kupokea ushauri na kuufanyia kazi, juu ya kuita wachezaji wazoefu,” alisema El Maamry.
 
Back
Top Bottom