#COVID19 Dunia inakabiliana vipi na janga la UKIMWI huku kukiwa na janga jingine kali zaidi la COVID-19?

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,000
1,019
1638318534432.png

Na Pili Mwinyi

Ugonjwa wa UKIMWI bado unaendelea kuwa tatizo kubwa ambalo linaathiri afya ya mamilioni ya watu duniani. Ingawa dunia imepiga hatua kubwa katika miongo ya hivi karibuni, lakini malengo muhimu ya mwaka 2020 duniani bado hayajatimizwa.

Dunia ikiwa inaadhimisha siku ya UKIMWI, kila ifikapo tarehe 1 Disemba, ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni "Komesha ukosefu wa usawa, komesha UKIMWI, komesha janga la virusi", wadau na watetezi mbalimbali wa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wamekuwa mbioni kuhakikisha makali ya ugonjwa huu yanapungua kama sio kwisha kabisa. Hata hivyo juhudi hizi zinakwama na bado watu wengi wamebakiwa na maswali yanayohitaji kujibiwa hasa wakati huu tunapokabiliwa na changamoto kubwa kabisa ya janga la virusi vya Corona.

Mwezi Februari, mwaka 2020 juhudi za dunia nzima katika kukabiliana na mambo mbalimbali zilikatizwa na dunia ikaanza kukabiliana na hatari iliyopo mbele yake yaani “Janga la COVID-19”. Kufikia Machi 2020, ikawa dhahiri kwamba huu si ugonjwa wa kawaida. Hivyo hata magonjwa yaliyopo awali ukiwemo UKIMWI, yakaelekezewa mgongo na nguvu zote kuelekezwa kwenye gonjwa hili thakili la virusi vya Corona.

Janga la COVID-19 likawa kizingiti kikubwa cha kukwamisha mapambano dhidi ya Ukimwi kwani wagonjwa wengi walijikuta wakianza kukosa huduma mbalimbali muhimu na kufanya maisha yao kuwa na changamoto kubwa.

Hivi sasa, watu wanaoishi na UKIMWI wapo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa COVID-19, kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo magonjwa nyemelezi. Janga la COVID-19 limekuwa likivuruga jamii na mifumo ya afya duniani, kwani linatokea wimbi moja baada ya jingine la maambukizi, ambayo yamekuwa na athari za moja kwa moja kwa mamilioni ya watu hasa wanaoishi na virusi vya VVU. Na sasa kuna aina mpya ya virusi hivi iitwayo Omicron iliyoibuka hivi karibuni nchini Afrika Kusini, ambayo wataalamu wanasema dalili zake ni kali zaidi, hivyo wagonjwa na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi wameingia kwenye hatari kubwa kuliko hapo awali.

Wakati huohuo majukwaa ya UKIMWI yanayoanzishwa badala yake yamekuwa yakisaidia kutoa rasilimali muhimu za kupambana na COVID-19, ikiwemo mifumo ya kimkakati ya habari, mifumo ya usimamizi wa ugavi, uwezo wa kupima kwenye maabara, vifaa vya utoaji wa huduma za kliniki, watumishi wa afya waliofunzwa, na programu za kufikia jamii.

Hivyo kila ifikapo Disemba 1, viongozi na watu wa kawaida huwa wanakumbushana juu ya madhila ya janga hili pamoja na kukabiliana na hali ya kutokuwepo kwa usawa katika kupambana na UKIMWI, vilevile kufikia watu ambao hadi sasa bado hawajapatiwa huduma za lazima za UKIMWI.

Waathirika wengi wa UKIMWI katika Afrika wamekuwa na uwoga wa kwenda hospitali wakihofia kuambikizwa COVID-19. Kwa mfano nchini Kenya, Janga la COVID-19 limeleta changamoto kwenye huduma za upimaji virusi vya UKIMWI, kutokana na idadi ndogo ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi kwenda hospitali. Na huduma zenyewe za upimaji pia zimekwama.

Lakini hali hiyo haionekani nchini Kenya tu bali ipo hata katika nchi za Afrika Mashariki kwani fedha zilizokuwa zikitolewa na mashirika ya kimataifa ya ununuzi wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI, ARVs zimeelekezwa kwenye janga la Corona.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO na Shirika La Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa UNAIDS, athari za matatizo ya kutotoa dawa kwa wagonjwa wa UKIMWI kwa muda wa miezi sita zinaweza kuharibu kabisa mafanikio ambayo yamepatikana katika kuzuia vifo vya UKIMWI.

Kwenye ripoti yake iliyotoa Julai 14 mwaka huu UNAIDS, limesema katika mwaka 2020, kuna watu takriban milioni 37.7 walioambukizwa virusi vya UKIMWI kote duniani, milioni 1.5 kati yao ni maambukizi mapya, na watu takriban laki 6.8 walikufa kutokana na UKIMWI katika mwaka 2020. Hivyo dalili zote zinaonesha kuwa nguvu sawa zinahitaji kuelekezwa kwenye Ukimwi na kwenye Corona na sio kushughulikia janga moja na kusahau jingine.
 
1 Reactions
Reply
Back
Top Bottom