Elections 2010 Dr. Slaa shujaa!

Uncle Rukus

JF-Expert Member
Jun 16, 2010
2,415
398
HOTUBA YA MWENYEKITI WA KAMATI YA TAIFA YA BARAZA LA VIJANA WA CHADEMA
(BAVICHA) JOHN MNYIKA AKIFUNGUA MKUTANO WA WAWAKILISHI WA WANAVYUO VIKUU VYA
MKOA WA DAR ES SALAAM KATIKA VIWANJA VYA MAKAO MAKUU YA CHAMA KINONDONI JUMAPILI
TAREHE 25 JULAI 2010

Vijana wenzangu wanavyuo;
Wageni waalikwa na wanahabari;
Ni mara yangu ya kwanza leo kuhutubia vijana wenzangu toka Kamati Kuu ya chama
katika kikao chake cha tarehe 25 mpaka 26 Aprili 2010 iliponiteua kuongoza
Kamati ya taifa ya BAVICHA katika kipindi hiki mpaka uchaguzi wa vijana
utapofanyika baada ya uchaguzi mkuu.

Nimeupokea wajibu huu kwa moyo mkunjufu kwa kuwa umenikumbusha kipindi
nilichokuwa Mkurugenzi wa Vijana na hakika ni jukumu muhimu kwa chama hiki cha
kizazi kipya wakati huu ambapo ubunifu, uwingi na uthubutu wa vijana unahitajika
kuwezesha mabadiliko katika taifa letu.

Awali ya yote naomba tusimame kwa dakika moja ya ukimya kuwakumbuka mashujaa
waliomwaga damu yao na kutangulia mbele ya haki wakiwa katika wajibu wa kulinda
na kutetea ardhi ya nchi yetu na watu wake.

Nashukuru tumekutana leo tarehe 25 Julai ambayo ni siku ya mashujaa nchini
kujadili matendo ya kishujaa yaliyofanywa na yanayokusudiwa kufanywa katika
taifa letu.


Tunakutana leo kwa sababu ya tendo la kishujaa la mtanzania mwenzetu Dr Wilbroad
Slaa kukubali ombi la kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tendo
hili la kishujaa la kuachia jimbo la uchaguzi ambalo alikuwa ana uhakika wa
kuletetea na badala yake kugombea nafasi ya urais ambayo baadhi ya watu
wametafsiri kama ni ‘kuuawa ama kujiua’ kisiasa.


Kama vile mashujaa walivyokubali kupoteza maisha yao kulilinda na kulitetea
taifa, ndivyo ambayo Dr Slaa ni shujaa wa demokrasia na maendeleo kwa kufanya
tendo ambalo linaweza kutafsiriwa kuwa ni kutishia maisha yake ya kisiasa
hususani katika bunge kwa kuamua kugombea nafasi ya Urais kutokana na kuweka
mbele maslahi ya taifa kwanza.

Mashujaa wa aina hii huwa hawafi kwa kuwa fikra zao hukumbukwa milele, uamuzi wa
Dr Slaa kujitokeza kugombea wakati huu utaandika historia mpya kwa taifa la
Tanzania. Uamuzi huu wa kishujaa ni sehemu ya kutekeleza kwa vitendo misingi ya
CHADEMA ambayo inaweza kueleweka vizuri zaidi kupitia bendera anayoipeperusha.
Bendera ya CHADEMA ina rangi nne; nyekundu, nyeupe, bluu bahari na nyeusi.
CHADEMA ikiwa ni chama kinachothamini mashujaa wa nchi hii imeweka rangi
nyekundu katika bendera yake ambaye imefafanuliwa vizuri katika katiba na kanuni
za chama kwamba ni ishara uzalendo na upendo kwa taifa.

Leo tarehe 25 Julai wakati sisi tukiwa hapa kwenye mkutano huu viongozi wa
kiserikali wako kwenye viwanja vya mnazi mmoja wakifanya maadhimisho ya kinafiki
ya kuwakumbuka mashujaa kwa maneno huku kwa vitendo wakiwa wamewasahau na
kusahau misingi waliyoisimamia.

Tunu za taifa hili zilizoko kwenye ngao ya taifa ni “Uhuru na Umoja”, hata hivyo
tunavyozungumza hivi sasa uhuru huu umetoweka kwa nchi kuwa tegemezi na
rasilimali kwa sehemu kubwa kuuzwa kwa bei ya kutupwa kwa wageni huku sehemu
kubwa ya watanzania ikiwa hainufaiki na matunda ya uhuru kutokana na kufungwa na
kongwa za umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi. Tanzania imegeuzwa chanzo cha
malighafi ghafi, soko la bidhaa duni toka nje chini ya soko holela na watawala
kukiunga misingi ya uongozi.

Kwa upande mwingine misingi ya umoja inazidi kutetereshwa kutokana na kupuuzwa
kwa utawala wa sheria, kumea kwa ubaguzi na kupanuka kwa matabaka katika jamii
kwenye sekta mbalimbali iwe ni afya, elimu na hata mifumo ya haki hali ambayo ni
tishio kwa ustawi na usalama wa nchi yetu. Hali hii inahitaji mashujaa
kujitokeza kutanguliza mbele uzalendo na upendo kwa taifa ili kulikomboa taifa
kwa kuleta mabadiliko ya kweli ya uongozi na mfumo mzima wa utawala.

Dr Slaa ametimiza wajibu huo kwa kusimamia ukweli, uwazi, uadilifu na amani kama
rangi nyeupe katika bendera ya CHADEMA inavyowakilisha hususani kupitia kazi
yake bungeni, katika jamii na jimboni Karatu katika kipindi cha utumishi wake.
Hata hivyo baadhi ya mambo hayajaweza kutekelezwa na serikali iliyopo madarakani
kutokana na dola chini ya CCM kutekwa na mafisadi na kuwa na mfumo legelege wa
uongozi uliofilisika kidira na kimaadili.

Umefika wakati sasa wa Shujaa huyu kuinuliwa kupewa wajibu mkuu zaidi katika
nchi yetu wa kuwa Rais wa Tanzania aweze kuunda serikali na kusimamia
utekelezaji ili kurudisha nchi kwa wananchi.



Ndio maana tunaunga mkono uamuzi wa
Kamati kuu ya chama iliyoketi tarehe 20 Julai kumwomba kugombea urais ili ajaze
fomu na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama tarehe 12 Agosti 2010.
Na kabla ya kuanza kuutekeleza wajibu huo akiwa ikulu, uchaguzi ambao kampeni
zake zinaanza rasmi tarehe 20 Agosti mpaka 30 Oktoba kabla ya kupiga kura tarehe
31 Oktoba ulipaswa kuwa na mgombea wa uwezo wa Dr Slaa ili uwe sehemu ya
mchakato wa kuiwajibisha serikali wakati wote wa kampeni.


Dr Slaa akiwa mgombea
urais uchaguzi utakuwa ni mchakato wa pekee wa kusambaa kwa elimu ya uraia kwa
umma, kuunganisha watanzania bila kujali itikadi katika kuleta mabadiliko,
kuibua uozo uliopo na kutoa sera mbadala zenye kuleta tumaini jipya la
watanzania kupitia chama na uongozi mbadala. Mchango huu wa kishujaa kwa taifa
utapanda mbegu ya mabadiliko ya kisiasa na kuliondoa taifa kutoka kwenye lindi
la mazoea ya ufisadi kwa kuhamasisha utamaduni wa uwajibikaji.

Katika kampeni hizo kama sehemu ya dhamira ya pamoja ya kuondoa ukiritimba na
hodhi ya chama kimoja kwenye vyombo vya maamuzi Dr Slaa kuwa mgombea urais kwa
uzoefu na makini atazunguka nchi nzima kuwanadi wagombea udiwani na ubunge na
kuwaongeza nguvu ili tuweze kuwa na wakina Dr Slaa wengi zaidi wazee kwa vijana
katika halmashauri na bungeni.

Viongozi hawa mbadala wataweza kujenga taifa lenye kutoa fursa na kutumia vizuri
rasilimali za taifa iwe ni mali asili, kodi, utaalamu na vipaji vya watanzania
katika kuwezesha maendeleo ya mwanachi kwa ujumla na taifa kwa ujumla kupitia
chama mbadala. CHADEMA ikiwa ni chama mbadala kinatambua umuhimu wa kutumia
vyema rasilimali katika sera zake na misingi yake, hivyo Dr Slaa atapeperusha
bendera ya chama rangi ya bluu bahari ikiwa inawakilisha haki na rasilimali za
taifa hususani maji.

Maneno yoyote ya kupingana mwelekeo huu wenye kutanguliza taifa kwanza iwe ni
kwa nia njema inayosukumwa na hofu ya ombwe la Dr Slaa bungeni au mashaka ya
pengo lake Karatu ama dhamira mbaya ya wapambe wa Kikwete za kuhadaa nafsi za
watanzania yanapaswa yapingwe kwa matendo ya wote wenye kuitakia mema nchi yetu
kwa kumuunga mkono Dr Slaa kwa hali na mali.

Ndio maana napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza vijana wenzangu wasomi wa vyuo
vikuu mlioona mbali kabla hata ya kamati kuu kukaa tarehe 20 Julai kwa kutumia
ubunifu na uthubutu wa kuweka saini (petition) ya kumwomba kugombea. Naamini
kamati kuu ilizingatia kuwa demokrasia ni utawala wa watu kwa ajili ya watu na
kukubaliana na wito wenu na wa makundi mengine katika jamii wakiwemo wanachama
wa CHADEMA wa kumuomba kugombea.



Tanzania bila CCM inawezakana kila mtu akitimiza wajibu; hivyo nashukuru kwamba
baada ya kufanikisha hatua ya kwanza leo mmeomba kukutana nasi kwa hatua ya pili
ya kujadiliana namna ya kufanikisha ushindi.


Hivyo ukiondoa hotuba hii ya ufunguzi leo hakutakuwa na mada za viongozi badala
yake tutasikiliza kutoka kwenu mawazo yenu na namna ambavyo mmejipanga kumuunga
mkono Dr Slaa katika azma ya kuleta mabadiliko tunayoyataka.
Karibuni katika viwanja vya ofisi ya chama chenye fikra za kuamini katika
falsafa ya “Nguvu ya Umma” ambayo inakilishwa na rangi nyeusi katika bendera
yetu ambayo ni ishara ya utu wetu: kwamba umma ndio wenye mamlaka juu ya
viongozi; umma ndio wenye wajibu wa kuamua hatma ya maisha yao na ya taifa; na
umma ndio unaopaswa kunufaika na rasilimali za nchi yetu.


Ni falsafa hii hii ndio tutakayotumia kuwezesha ushindi wa Dr Slaa na ushindi wa
wabunge na madiwani mbadala kwa vijana kuwa mstari wa mbele kugombea ama kuunga
mkono wagombea ikiwemo kutafuta na kulinda kura kwa kupitia pia falsafa ya
Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA) kwamba: Vijana; Nguvu ya Mabadiliko.
Serikali yenye woga wa mabadiliko inayotawala kwa hujuma imetoa waraka na
kuziingilia ratiba za vyuo husasani vya umma na kufanya vifunguliwe baada ya
uchaguzi kwa hoja kanyaboya na hivyo kukwamisha baadhi yenu kupata haki ya
msingi ya kikatiba ya raia ya kupiga kura pamoja na kuwa mlishajiandikisha
tayari.



Aidha ratiba hii ina dalili zote za kukwepa mshikamano wa wasomi wakati
wa uchaguzi kwa kila mtu kuwa likizo katika hali inayoweza kutafsiriwa kuwa ni
mpango wa ‘wagawe uwatawale’.
Hata hivyo, ni wakati wa vijana kuwaambia watawala kuwa ‘hatudanganyiki wala
hatugawanyiki’, uamuzi wenu wa kukukutana wawakilishi wa wanavyuo mbalimbali
kabla ya kutawanyika ili kuunganisha nguvu ya pamoja umefanyika katika wakati
muafaka.

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba dhima ya wasomi na kama wajibu wa mtu
aliyepewa chakula aweze kupata nguvu ya kwenda kuleta chakula kwa ajili ya
wengine katika kijiji chenye njaa; mtu kama huyo asiporudi ni msaliti.
Ni wajibu huu ndio unaopaswa kuwasukuma maeneo yoyote ambayo mtakuwa muifuatilie
fursa yenu ya kupiga kura na kufanya hivyo, lakini mnawajibu mkubwa zaidi wa
kutafuta kura nyingine nyingi zaidi kwa kuwaelimisha watanzania wengine na
kuongoza harakati za mabadiliko ya kweli.

Katika kushinda uchaguzi vipo vipaumbele vinne ambavyo naomba nivitaje kwa
kadiri ya umuhimu wake kama sehemu ya kuibua majadiliano yetu siku ya leo; mosi,
mgombea; pili, ajenda; tatu, oganizesheni na nne; rasilimali.

Kwa upande wa Urais mgombea tayari tunaye ambaye anasubiri tu kuthibishwa na
mkutano mkuu baada ya michakato kukamilika; wa upande wa ubunge na udiwani pia
katika maeneo mbalimbali ya nchi wapo wagombea wamejitokeza ingawa milango bado
iko wazi kwa kuwa tarehe ya mwisho ya uchukuaji na urudishaji fomu ndani ya
chama ni tarehe 9 Agosti kabla ya uteuzi wa kiserikali Agosti 19. Kwa bahati
njema pia sehemu kubwa ya wagombea ni vijana wenzetu na wazee wenye kutaka
mabadiliko. Hivyo mnawajibu wa kwenda kuwaunga mkono wagombea katika maeneo
ambayo mnakwenda.

Kipaumbele cha pili ni ajenda za kisiasa ambazo katika uchaguzi huwekwa katika
ilani. Tayari kamati kuu ya chama imepokea rasimu ya ilani na mchakato wa
kuiboresha unaendelea kwa kuzingatia mawazo na maoni mbalimbali unaendelea mpaka
itakapopitishwa na Mkutano Mkuu wa chama Agosti 12 mwaka huu. Hivyo, nyinyi kama
vijana wasomi wa kada za mbalimbali mna wajibu wa kushauri hoja za kuwekwa
kwenye ilani katika sekta mbalimbali ambazo mmezisomea na mnaendelea kuzisomea
kwa kuzingatia pia hali halisi ya taifa na watanzania kwa sasa.


Majadiliano ya
leo yatawezesha kuanza kupokea maoni yenu si tu ya kuchambua hali ilivyo chini
ya uongozi wa CCM bali pia kupendekeza CHADEMA ifanyeje pindi ikiingia katika
uongozi ama ni Tanzania ya namna gani mngependa ijengwe na chama mbadala. Pamoja
na kuwa CHADEMA inazo sera zake na mwaka 2005 ilikuwa na ilani ambayo mnaweza
kuirejea kupitia www.chadema.or.tzbado tunaamini kwamba chama cha siasa kina
wajibu wa kuwasikiliza wananchi badala ya kujifungia na kuandaa ilani
zisizosingatia hali halisi ya taifa.
Kipaumbele cha tatu ni oganizesheni ya kampeni ikiwemo mikakati mbalimbali ya
kujipenyeza katika jamii kwa kutumia mbinu na timu mbalimbali. Hivyo, natarajia
kikosi hiki kitasambaa katika maeneo mbalimbali na kutumia ubunifu, nguvu,
uwingi na uthubutu wa vijana kufanya kampeni za kipekee kama ambavyo
mtabadilishana mawazo katika mkutano wa leo. Tanzania bila CCM inawezekana kila
mmoja akitimiza wajibu.

Kipaumbele cha nne ni rasilimali, izingatiwe kwamba tayari CCM imeshaanza na
imejipanga kutumia nyenzo ikiwemo za dola/serikali na fedha nyingi zikiwemo za
ufisadi na ubadhirifu katika kulazimisha ushindi kwa ushahidi wa nyaraka ambazo
binafsi ninazo mpaka sasa ambazo zitatolewa katika wakati muafaka.


Ni wajibu
wetu kushirikiana kuwaumbua kila mahali mipango yao ya kiharamia lakini ni
wajibu wetu pia kutumia mbinu mbadala na rasilimali mbadala za kukabiliana na
hali hiyo.


Rasilimali mbadala kwa kutumia nguvu ya umma ni pamoja na vijana
wasomi kama nyinyi kujitolea utaalamu wenu, muda wenu, vipaji vyenu na nguvu
yenu kuwezesha maandalizi, kampeni na ulinzi wa kura. Haya ni kati ya mambo
ambayo ni muhimu mkayatafakari katika mkutano wa leo.

Historia ya duniani inaonyesha kwamba mchango wa vijana na wanafunzi ni wa
muhimu sana katika kuanguka kwa tawala za kidikteta, za kibaguzi na za kifisadi.
Historia kama hii inapaswa kuandikwa nchini mwetu kwa njia za kidemokrasia
kupitia uchaguzi ili kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli.

Tuyafanye hayo tukitambua kwa pamoja kwamba mabadiliko ya kweli katika taifa
letu hayawezi kuletwa na mafisadi wale wale, wa chama kile kile, chenye uoza ule
ule, wakiendeleza yale yale kwa Ari, Nguvu na Kasi (ANGUKA) zaidi. Kwa falsafa
ya chukua chako mapema(ccm), ya chama cha mafisadi(ccm); Tanzania yenye neema
haiwezekani. Tuunganishe nguvu kurudisha nchi kwa wananchi; Tanzania bila CCM
inawezekana kupitia chama mbadala na uongozi bora.
Natangaza kwamba mkutano huu umefunguliwa rasmi na tuko tayari kuwasikiliza;
Vijana, Nguvu ya Mabadiliko.
 
Hakika Dr Thlaa ni shujaa haswa ingawa nionavyo mimi atatumika kupangisha chati chama chake kisha atajitahidi kunyemelea majimbo yaliyoboronga katika uchaguzi ili awanie ubunge kisha mambo yakaendelea.
 
Kweli shujaa tatizo ni hawa anaowaita wanavyuo ndo kwanza wanadanganywa kwa Tshirts za njano na kijani na lunch wanasahau matatizo walonayo!
 
Back
Top Bottom