Dr. Slaa: Jk hana nia ya kuunda Katiba Mpya | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dr. Slaa: Jk hana nia ya kuunda Katiba Mpya

Discussion in 'KATIBA Mpya' started by Rutashubanyuma, Jan 2, 2011.

 1. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #1
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Slaa: JK anamiliki Dowans
  • Asema hana nia ya kuunda Katiba mpya

  na Mwandishi wetu


  [​IMG] KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willbrod Slaa amesema kuwa Rais Jakaya Kikwete ni dikteta.
  Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Dk. Slaa, alisema kitendo cha Rais Kikwete, kutangaza kuwa ameunda tume ya kuanzisha mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya na atateua kiongozi na wajumbe kinaashiria kuendeleza udikteta wa uongozi.
  Alibainisha kinachotakiwa kuanzishwa hivi sasa ni Constitutional Assembly au Baraza la Katiba (Bunge la Katiba) ambalo ndilo litakalokuwa na wajibu wa kuratibu kura za maoni ya wananchi juu ya uundwaji wa Katiba mpya.
  Alisema kitendo cha Rais Kikwete, kutangaza kuunda tume ni kiini macho na kinadhihirisha hana nia ya kutaka kuundwa kwa Katiba mpya.
  "Huyu Rais wetu haonyeshi kama yuko 'serious' katika uundaji wa Katiba mpya, anataka kuweka viraka ili aendelee kututawala kidikteta!" alisema.
  Aliongeza kuwa kwa kawaida Baraza la Katiba ambalo hapa nchini halipo ndilo lenye jukumu hilo na linatakiwa lifanye mchakato huo kwa kuishirikisha serikali, Bunge, wadau na wananchi.
  Alisema hakubaliani na tume ya kuratibu mchakato huo, kwani inaweza kufanya kazi kwa utashi wa aliyewateua na hata Bunge pia linaweza likatumbukia kwenye mtego wa kupitisha kitu kisichokuwa matakwa ya wananchi kwa sababu ya wingi wa wabunge wa chama kimoja.
  Alisema katika nchi zote zilizoandika upya Katiba au kutengeneza zilipitia njia ya 'National Constitutional Congress au Convention' (Constitutional Assembly) ambapo ilikubaliwa kati ya serikali, Bunge, wadau mbalimbali na wananchi katika majukwaa yao.
  "Constitutional Congress ni chombo kitakachoratibu maoni ya wananchi na wadau mbalimbali na siyo mtu aliyeteuliwa na Rais ambaye anafanya kazi kwa ajili ya kumfurahisha jambo ambalo ni kuendelea kuweka viraka" alisema.
  Alisema baada ya chombo hicho kuundwa, maoni ya wadau, wananchi mbalimbali hukusanywa kwa njia itakayokubalika.
  Dk. Slaa alisema kuwa 'Constitutional Congress hukaa tena kupitia maoni yote kipengele kwa kipengele na kukubaliana na siyo Rais Kikwete na tume atakayounda jambo ambalo liliwahi kutokea huko nyuma.
  Alisema inawezekana Rais Kikwete, hafahamu au kwa makusudi amepuuza kilio cha wananchi ndiyo maana ameunda tume inayowajibika kwa maslahi yake.
  Alisema kuwa Katiba siyo mali ya Rais wala ya serikali iliyoko madarakani, bali ni mali ya wananchi.
  Dk. Slaa alisema wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa wanahitaji chombo chao ambacho kinaweza kuwekewa utaratibu na Bunge, baada ya kupitishwa na Azimio la Bunge, lakini siyo mtu au watu wa tume wanaochaguliwa na Rais.
  "Tume hiyo haikubaliki kabisa tunachotaka tunajua hakitakubalika kwa maana hakuna serikali duniani itakayounda tume ya kujinyonga yenyewe, mabadiliko makubwa kwa vyovyote, hayakupendwa na serikali iliyoko madarakani" alisema.
  Alisema ana imani kuwa tume hiyo haiwezi kuleta Katiba mpya hivyo kutoa nafasi kwa Rais Kikwete kuendelea kuongoza katika sura ya kidikteta kwa kupitia Katiba ya sasa iliyopitwa na wakati.
  Dk. Slaa alisema kuwa inashangaza katika hili ambapo hata Zanzibar wamepiga hatua kwani waliweza kuruhusu kukusanya maoni ya uundaji wa serikali ya kitaifa na si kuundwa kwa tume.
  Alisema Katiba mpya haiwezi kamwe kupatikana kwa njia ya tume hiyo (Constitutional Review Commission) kwani zilishawahi kutokea tume za aina hiyo na hakuna kilichofanyika.
  Alibainisha kuwa jambo hilo halina tofauti na tume zilizowahi kuundwa na Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi pamoja na ile ya Benjamin Mkapa ambapo matokeo yalikuwa ni kuweka viraka kwenye Katiba tuliyonayo hivi sasa.
  "Uzoefu wa Tume za Mwinyi na Mkapa ni kuwa maoni yalikusanywa kwa upendeleo, hojaji zilipelekwa kwenye matawi ya CCM, halmashauri za wilaya vyombo ambavyo vyote ni vya CCM, hatimaye serikali ikatoa mapendekezo ya vifungu vya kurekebishwa na vingine kuachwa, alisema na kuongeza: "hatua hii inawezekana kwa kuwa tume ni ya Rais, na Rais kama alivyosema mwenyewe ndiye atakayepeleka marebisho kwa vyombo husika (Bunge) ambalo karibu lote ni la CCM bado wana wabunge wengi pamoja na kuwa wapinzani wameongezeka sana" alifafanua.
  Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema ameshangazwa na kitendo cha Rais Kikwete kushindwa kufafanua kuhusu suala la kulipwa kwa Kampuni ya Dowans sh bilioni 185 na Shirika la UmemeTanzania (TANESCO).
  Alisema fidia hiyo iliyoamriwa na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya biashara (ICC) hivi karibuni kuwa TANESCO inapaswa iwalipe Dowans fedha hizo baada ya kuvunja mkataba wa kununua umeme.
  Alisema kimsingi uvunjwaji wa mkataba huo na sakata zima ni uzembe ambao unapaswa uwekwe wazi na watu wachukuliwe hatua lakini Rais Kikwete haonyeshi kushtushwa na jambo hilo.
  Alisema kutokana na majibu ya kiongozi huyo inaonyesha kuwa naye ni sehemu ya kampuni ya Dowans.
  Alisema Rais anaonyesha udikteta kwa kuamua kulibeba shirika la umeme nchini (TANESCO) huku wananchi ambao ni walalahoi wakiendelea kunyongwa na upandaji wa gharama hizo.
  "Hasemi kuwa kitendo cha kulipa kampuni hiyo kimesababishwa na uzembe wao wenyewe kwa kuleta mitambo ya Richmond iliyozaa Dowans huku yeye akiwa sehemu ya kampuni hizo ameamua kuficha uovu wao" alieleza.
  Alisema wataendelea kuhamasisha maandamano pamoja na kupinga gharama kwa kuwa vyama vya upinzani havikusajiliwa kwa Rais bali vimekuwepo kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha vinakataa uozo unaofanywa na serikali.
  Dk. Slaa alisema Rais Kikwete amesahau hali ngumu inayowakumba wananchi imetokana na maamuzi mabovu yaliyoanzishwa na wanasiasa wenzake kwa kukubali kufanya mchakato wa IPTL.
  "Eti Rais Kikwete anasema upandaji wa umeme ni suala la kibiashara na wanasiasa wasilizungumzie kisiasa inawezekana hana uchungu na Watanzania wanaoshindwa kununua umeme kwa ajili ya kuendeleza biashara zao" alisema.
  Alisema vyama vya upinzani vina haki ya kujadili masuala mbalimbali na siyo kama anavyodai kufanya hivyo ni kuendeleza malumbano na ikiwa hataki vyama vifanye hivyo basi hana budi kuvifuta.
  Wakati huo huo Chama cha Wananchi (CUF), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete, kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa juu ya kupata Katiba mpya itakayokuwa na maslahi ya Watanzania wote.
  Naibu Katibu Mkuu wa CUF, bara, Julius Mtatiro, alisema kuwa kitendo cha Rais Kikwete, kukubali kuundwa kwa Katiba mpya kuendane na vitendo hasa kuiunda upya na sio kuifanyia marekebisho kama ilivyokuwa awali.
  Alisema Tanzania imefanya marekebisho mara 14 lakini bado kumekuwa na malalamiko hali inayoweza kuleta machafuko nchini na kuipa nchi doa.
  Alisema ni kipindi kizuri kwa Rais Kikwete kuiga mfano wa Rais wa Zanzibar wa awamu ya sita Amani Karume kwa kuridhia maridhiano yaliyoleta sura mpya ya Zanzibar.
  Alisema suala la Katiba mpya limekuja wakati muafaka, kabla ya kutokea kwa misukosuko inayoweza kuchafua hali ya utulivu na amani ya nchi hatua itakayofanya kupoteza sifa hasa pindi amalizapo muda wake mwaka 2015.
  Hata hivyo chama hicho kilimtahadharisha Rais Kikwete kuhakikisha anatembea katika kauli zake hasa kwa kuunda tume makini itakayokuwa huru na isiyokuwa na upendeleo au agenda ya kuibeba CCM, hasa kwa kufanya maamuzi ya upande mmoja.
  Aidha katika hotuba yake Rais Kikwete aliahidi kuunda Tume Maalum ya Katiba (Constitutional Review Commission), itakayoratibu mchakato kwa kushirikisha wananchi wote ili waweze kutoa maoni yao juu ya yale wanayotaka yaingizwe katika Katiba mpya.
   
 2. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #2
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Dr. Slaa yupo sahihi kabisa kwa asilimia mia moja....................kipimo cha katiba mpya ni Mkutano wa Kikatiba......i.e constitutional Assembly..........................Haya ya JK ni kiini macho ambacho safari hii tunasema hatudanganyiki kabisa..................
   
 3. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #3
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Hili la Katiba litazamwe kwa makini

  [​IMG]

  [​IMG] JUZI Rais Jakaya Kikwete, katika hotuba yake ya kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 alizungumza mambo mengi lakini kubwa zaidi ni serikali kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya Tanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipigiwa kelele haiendani na wakati.
  Wadau mbalimbali kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipaza sauti zao kutaka Katiba ifumuliwe na kuundwa nyingine huku wakiweka bayana baadhi ya vipengele ambavyo vinaonekana kutokukidhi matakwa ya hivi sasa.
  Rais Kikwete, alisema ameamua kuunda Tume Maalum ya Katiba, ambayo itaongozwa na mwanasheria aliyebobea, itakayokuwa na wajumbe wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii hapa nchini kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
  Kwa mujibu wa Rais Kikwete, jukumu la msingi la tume hiyo litakuwa ni kuongoza na kuratibu mchakato utakaowashirikisha wananchi wote bila kubagua, vyama vya siasa, wanasiasa, wafanyabiashara, asasi za kiraia, mashirika ya dini, wanataaluma na makundi mbalimbali ya watu wa nchi yetu kote nchini, katika kutoa maoni yao juu ya wayatakayo kuhusu Katiba ya nchi.
  Tunapenda kuchukua fursa hii, kumpongeza Rais Kikwete, kwa kuona haja ya uwepo wa Katiba mpya licha ya baadhi ya watendaji wa serikali yake akiwemo Mwanasheria Mkuu, Fredrick Werema, kuweka bayana kuwa hakuna haja ya kuwa na Katiba mpya bali iliyopo ifanyiwe marekebisho
  Pamoja na kumpongeza Rais Kikwete, kwa hatua hiyo lakini tayari baadhi ya wadau wameshajitokeza kupinga utaratibu alioutangaza Rais Kikwete wa kushughulikia mchakato huo kwa madai kuwa timu ya waratibu wa zoezi hilo watokane na baraza la Katiba ambalo halitakuwa likiegemea upande wowote.
  Hoja za wadau hao ni kuwa uteuzi huo wa rais unaweza ukawa na ushawishi kwa wajumbe kuchukua maoni fulani kulingana na matakwa ya aliyewateua (Rais) na hata pale yatakapofikishwa bungeni kwa ajili ya maamuzi ambako idadi wa wabunge wa chama tawala ni wengi wanaweza kupitisha jambo ambalo si hitaji la Watanzania.
  Ipo mifano mingi ambayo tume kadhaa ziliundwa na Rais Mstaafu Alli Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa ambazo mwisho wake ziliishia kuweka viraka kwenye katiba na hata mambo mengine ya umuhimu zaidi yalitupwa kapuni.
  Mwaka 1991, iliundwa tume iliyokuwa chini ya uenyekiti wa marehemu Jaji Mkuu mshastafu Francis Nyalali, ambayo ilikusanya maoni namna ya Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi na hatimaye ikatoa mapendekezo ya kubadili Katiba ili iendane ya mfumo huo kwani iliyokuwapo ilikuwa ni ya chama kimoja tena ya kurithi kutoka katika serikali ya kikoloni.
  Katika juhudi za kupata Katiba mpya Mwaka 1991, Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya siasa na kupendekeza kuwepo kwa Katiba mpya na si kurithi Katiba ya chama kimoja ambayo mhimili wake ulikuwa tofauti.
  Hoja hizo hazikupewa majibu na vyama vingi vya siasa viliingizwa ndani ya Katiba ya mwaka 1977, kupitia mabadiliko ya Nane ya mwaka 1992, yaliyotungiwa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya 1992.
  Mwaka 1998 Kamati ya "White Paper" ilipoundwa chini ya Jaji wa Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Jaji Robert Kisanga, ambayo pia ilipendekeza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya.
  Tunajua Rais Kikwete, ana nia ya dhati ya kuundwa kwa Katiba mpya lakini ni vema jambo hili likafanyika kwa umakini mkubwa ili kuepusha nchi kuingia katika malumbano ambayo mwisho wake hautakuwa mzuri.
  Tungependa mchakato huu ufanywe kwa taratibu zitakazokubaliwa na pande zote badala ya kufanyika kwa hila au upendeleo kwa misingi ya itikadi za vyama au maeneo fulani.
  Tunakubaliana na Rais Kikwete kuwa jambo muhimu ni kujenga Tanzania moja yenye ushirikiano, lakini jambo hilo halitoweza kufanikiwa iwapo kasoro au maoni yanayotolewa na wadau hayatoweza kufanyiwa ipasavyo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
  Katiba ni muhimu kwa Watanzania wote, hivyo si muhimu kwa chama tawala au kile cha upinzani kujigamba au kufanya hila ili kionekane chenyewe ndicho chenye haki ya kudai au kuzima madai hayo kwa masilahi ya chama au kundi la watu fulani.
  Zanzibar waliweza kufanya mabadiliko ya Katiba yao ili kuridhia serikali ya Mseto baina ya vyama vya CCM na CUF hivyo ni vema utulivu ulioonyeshwa visiwani humo uendelee hata kwa mchakato huu wa sasa.
  Tanzania ni moja kila mtu ana mchango wake hivyo hakuna sababu ya kugombea fito, hakuna mtu aliyezaliwa ili amtawale mwingine au mwingine awe mnyonge dhidi ya mtawala.
  Tuliamua kuwachagua watawala ili waweze kutuongoza kwa maslahi yetu na wala si kwa ajili ya kuweka mbele maslahi ya chama, mtu binafsi au kundi la watu fulani.
   
 4. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #4
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Kikwete kujinasa kwa katiba mpya?
  [​IMG]

  Ansbert Ngurumo

  [​IMG] KAULI ya Rais Jakaya Kikwete kukubali kuundwa kwa katiba mpya ni ya kiungwana; na uthibitisho kwamba CHADEMA waliposusa hotuba yake Bungeni, aliguswa. Na sasa amejua hawezi kushindana na nguvu ya umma.
  Lakini kauli yake inapaswa kutazamwa kwa uangalifu mkubwa; kwani imeonyesha sura halisi ya serikali anayoiongoza. Na imempa mtihani mkubwa na kumuweka katika mtego ambapo akikaa vibaya utamnasa yeye mwenyewe.
  Yeye ndiye aliyemteua Celina Kombani kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Hata kabla hajakaa ofisini kusoma mafaili, Kombani alionyesha udhaifu mkubwa na upeo mdogo katika suala nyeti kamahili. Akabeza hoja ya mabadiliko ya katiba.
  Kauli ya Rais Kikwete ina maana moja kwa Kombani. Ana uwezo mdogo sana kwa kazi aliyopewa. Ni waziri asiye na upeo wa kuongoza Wizara ya Katiba na Sheria. Kauli ya rais wake, imemshushua yeye.
  Maana yake ni kwamba waziri haaminiki hata kwa rais mwenyewe aliyemteua. Angekuwa muungwana, Celina Kombani angejiuzulu.
  Na kama akikataa kujiuzulu, Rais Kikwete mwenyewe anapaswa kumwondoa katika wizara hiyo. Kama wote watashindwa kuchukua hatua, basi, rais na waziri wake watakuwa wameonyesha udhaifu mkubwa kwa mara nyingine.
  Lakini Rais Kikwete ana mtego wa pili. Ndiye alimteua Jaji Frederick Werema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Katika hali isiyotarajiwa, Jaji Werema amejikuta akifanya kazi ya siasa badala ya kazi ya sheria. Naye akabeza hoja ya katiba mpya; akasema kinachohitajika ni viraka katika katiba ya zamani.
  Huyu ndiye mshauri mkuu wa rais katika masuala makubwa ya kikatiba na kisheria. Kauli ya rais kukubali katiba mpya ina maana kwamba Jaji Werema alikurupuka. Ama hakusoma alama za nyakati na mahitaji ya taifa; au hakujua hata mchezo wenyewe wa siasa aliotaka kuucheza kulinda uhafidhina wa chama tawala na serikali iliyo madarakani.
  Kwa kiongozi, mwanasheria ambaye amefikia hadhi ya kuitwa jaji na akapewa dhamana kubwa kama aliyonayo; Jaji Werema amekatisha tamaa wananchi waliokuwa na imani naye, hasa wale waliokwishachoka kuona ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ikishindwa kutumika kulinda maslahi ya nchi, inalinda ya wachache wenye vyeo na nguvu, kama ilivyotokea huko nyuma.
  Je, naye anajiona shujaa baada ya kushushuliwa na rais? Kwa nini naye asifanye kile tunachomshauri Kombaniâ€" kujiuzulu? Na kama hataki, rais anaona tatizo gani kumpa kazi nyingine inayolingana na uwezo na upeo wake?
  Lakini kuna mtego mwingine ambao unaweza kumnasa rais katika hoja hii. Amesema kwamba atateua mwanasheria aliyebobea kusimamia na kuongoza tume ya kuangalia upya (kurekebisha) katiba.
  Watanzania wenye akili timamu wanaamini kwamba mwanasheria huyo atakuwa na viwango vilivyo juu ya hivi alivyoonyesha Jaji Werema; na wala hatakuwa Werema.
  Maana sote ni mashahidi kwamba inawezekana ana uwezo katika masuala kadhaa ya kisheria, lakini katika hili, Jaji Werema hajabobea. Rais asifanye kosa kumpa kazi hiyo. Ataichakachua!
  Kama kweli Rais Kikwete ametoa kauli yake kwa nia njema na kama anaamini kwamba historia ya Tanzania inapaswa kuandikwa upya baada ya miaka 50 ya uhuru, na kama anataka kukumbukwa kwa urithi mwema wa katiba mpya; aunde tume inayoongozwa na watu ambao hawajipendekezi kwa serikali. Iwe chini ya watu huru, wasioogopa kupendekeza yasiyopendwa na wakubwa; wasiotafutwa kuonekana na "kurushiwa makombo."
  Maana wanasiasa wetu, hasa hawa wa viwango wa Kikwete, hawaaminiki katika mambo nyeti kama haya. Wana kawaida ya kutanguliza maslahi ya vyama vyao, watu wao na serikali wanayoiongoza. Wana tabia ya kuishi ndani ya kapu na kuogopa mawazo mapya, na maamuzi magumu.
  Na tume za marais si jambo la kujivinia sana hapa kwetu. Zimeundwa nyingi huko nyuma. Ripoti zake na mapendekezo yake, vimepuuzwa.
  Rais Ali Hassan Mwinyi aliunda Tume ya Nyalali kuhoji wananchi kama wanataka mfumo wa vyama vingi au kimoja. Ikahoji wana CCM. Wakakataa mfumo wa vyama vingi. Hata wasio wana CCM waliokuwapo wakati ule, si wote walikuwa tayari kwa vyama vingi.
  Wakati serikali inajiandaa kutekeleza hujuma yake ya kukataa vyama vingi kwa kutii mapendekezo ya wananchi, Baba wa Taifa akaingilia kati, akailazimisha ikubaliane na wachache. Kwa kuwa serikali ililazimishwa, ndiyo maana hadi leo inaendelea kufanya hujuma mchana na usiku dhidi ya wanaoipinga na kuikosoa.
  Leo, katika mazingira ambayo Baba wa Taifa hayupo kumshinikiza Kikwete, nani anaamini kwamba matakwa ya wakati ndiyo yatakayozingatiwa?
  Mazingira kama hayo yalitokea mara mbili wakati Rais Benjamin Mkapa alipounda Tume ya Warioba kuchunguza mianya ya rushwa, na Tume ya Jaji Kisanga kuhoji wananchi juu ya suala hili la katiba kwa mfumo wa White Paper.
  Ni nani miongoni mwetu anayeweza kusema pasipo shaka kwamba serikali ya Mkapa ilifanikiwa kupiga vita rushwa? Ni mara ngapi tumemsikia Jaji Warioba akinung'unika pembeni na waziwazi kuhusu kupuuzwa kwa mapendekezo yake?
  Hata baada ya Jaji Kisanga kuwasilisha maoni ya tume yake na kupendekeza mfumo wa serikali tatu kama hitaji la wakati, Rais Mkapa alimshambulia na kumshuhua hadharani. Kisa alitoa mapendekezo ambayo serikali haikuyataka.
  Katika jeuri hii ya ulevi wa madaraka na kushindwa kusoma alama za nyakati, ni kwa nini tusitilie shaka hata nia ya sasa ya rais kuunda tume ya marekebisho ya katiba?
  Na kinachoanza kutia shaka ni kauli ya rais mwenyewe. Amesema: "Baada ya makubaliano kufikiwa, taifa letu litapata katiba mpya, itaamuliwa lini ianze kutumika, pasiwepo kutukanana, kudharauliana, kushutumiana, kubezana, kuzomeana wala kushinikizana. Washiriki waongozwe na hoja badala ya jazba."
  Kwa msomaji wa kawaida, kwa juu juu, rais ametamka maneno mazuri tu. Ni kauli ya kawaida. Lakini kwa mtu anayejua kusoma na kutafsiri msingi na nia ya kauli, ataona kuna kitu kimefinyangwa kwenye kauli hii.
  Kwanza, hakuna haja ya kuhofia kutukanana. Kwa nini watu waungwana watukanane wakati wanashirikiana vema kwa nia ile ile? Na kwa kawaida, watu (hata wasio waungwana kabisa) huwa hawaamki na kutukanana tu. Yapo mazingira yanayochokoza watu hao kutukana. Haya ndiyo rais anapaswa kuhakikisha kwamba hayatakuwapo.
  Lakini hoja nzito kama hii haiwezi kujengwa bila msuguano wa hisia, na hoja kinzani. Maana makubaliano hayafikiwi kirahisi hivi hivi, hasa katika jamii iliyogubikwa na uhafidhina wa watawala.
  Kama serikali au chombo chochote kitathubutu kufanya ghiliba za kutumia tume hii kuhujumu mchakato wa katiba mpya, kushutumiana, kudharauliana, kubezana, kuzomeana na kushinikizana kutajitokeza.
  Lakini hata katika mazingira ya kawaida ya ushindani wa kisiasa, linapojadiliwa jambo zito kama hili, hoja haziwezi kujengwa kama vile watu wako katika nyumba ya ibada. Msuguano utakaojitokeza ni zao la lazima la mchakato wenyewe.
  Kwa hiyo, rais anafanya makosa kutisha watu wasijadiliane, wasitofautiane, na wasitumie staili mbalimbali za kujadiliana kupata watakacho.
  Maana kama serikali yake yenyewe haina kauli moja (rejea ya Kombani, Werema na Rais Kikwete) itakuwaje mchakato unaohusisha wadau wengi zaidi, kutoka mazingira tofauti, uanze na kuhitimishwa bila mikwaruzo? Kama mikwaruzo haitakuwapo, itapatikana wapi furaha ya "makubaliano" anayozungumzia?
  Lakini Rais Kikwete atakuwa muungwana kweli kama atatazama na kusoma kwa umakini rasimu zilizo tayari na ambazo zimekuwa zinapigiwa debe kwa miaka kadhaa sasa. Zimeandaliwa na wanaharakati na wanasheria waliobobea, wanaotazama zaidi maslahi ya taifa kuliko chama, wasioomba upendeleo au kazi serikalini.
  Asiwe wa kwanza kubeza wengine. Wawaulize CUF na CHADEMA. Watamuonyesha pa kuanzia. Maana hata mjadala huu hajaukubali kwa dhati, bali ameshinikizwa na nguvu ya hoja na matakwa ya wakati. Na CHADEMA waliposusia hotuba yake Bungeni, hiki ndicho walikuwa wanatafuta. Sasa kama amekubaliana nao, asiwabeze, awaunge mkono, mchakato uanze.
   
 5. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #5
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Hili la Katiba JK amenena, Watanzania wanasubiri Katiba mpya
  [​IMG]

  Bakari Kimwanga

  [​IMG] WAKATI Watanzania tumeingia katika mwaka mpya 2011 ambao umeonyesha huenda ukawa na historia ya pekee hasa baada ya kilio cha miaka mingi cha kudai katiba walau kuanza kupatiwa ufumbuzi na huenda ikawa nuru ya kuijenga Tanzania mpya.
  Nimefarijika na kauli ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika salamu zake za kuuaga mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011, hasa kuikubali hoja ya wananchi ambao wamekuwa wakidai kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania itakatayokidhi mahitaji ya Watanzania na makundi yote.
  Rais Kikwete, pamoja na kuzungumzia masuala mbalimbali, aliahidi kuwa ataunda Tume ya Marekebisho ya Katiba (Constitutional Review Commission), itakayoratibu mchakato kwa kushirikisha wananchi wote ili waweze kutoa maoni yao juu ya yale wanayotaka yaingizwe katika Katiba mpya ya Tanzania.
  Tume hiyo itaongozwa na mwanasheria aliyebobea ambaye hakumtaja jina, ambayo hata wajumbe wake watakuwa wanaowakilisha makundi mbalimbali katika jamii kutoka pande mbili za Muungano, ili kuihuisha Katiba yetu, hatimaye iweze kuendana na taifa lenye umri wa nusu karne.
  Lakini kubwa mara baada ya kukusanya maoni itatoa mapendekezo yake yatakayofikishwa kwenye vyombo stahiki vya Kikatiba kwa kufanyiwa maamuzi na hapo ndipo mara nyingi wanaharakati wanaodai Katiba wamekuwa wakibeza Mapendekezo yanayotolewa na tume hizo kutozingatiwa na hatimaye kubezwa na watawala.
  Mwaka 1991, iliundwa tume iliyokuwa chini ya uenyekiti wa marehemu Jaji Mkuu Mstaafu Francis Nyalali, ambayo ilikusanya maoni ya namna Tanzania ingeingia katika mfumo wa vyama vingi na hatimaye ikatoa mapendekezo ya kubadili Katiba ili iendane ya mfumo huo kwani iliyokuwapo ilikuwa ni ya chama kimoja tena ya kurithi kutoka katika serikali ya kikoloni.
  Katika juhudi za kupata Katiba mpya mwaka 1991, Tume ya Jaji Nyalali ilipendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa utawala wa vyama vingi vya siasa na kupendekeza kuwepo kwa Katiba mpya na si kurithi Katiba ya chama kimoja ambayo mhimili wake ulikuwa tofauti.
  Hoja hizo hazikupewa majibu na vyama vingi vya siasa viliingizwa ndani ya Katiba ya mwaka 1977, kupitia mabadiliko ya Nane ya mwaka 1992, yaliyotungiwa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya 1992.
  Mwaka 1998 Kamati ya "White Paper" ilipoundwa chini ya Jaji wa Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Robert Kisanga, pia ilipendekeza umuhimu wa kuwa na Katiba mpya.
  Lakini kamati hiyo ilipowasilisha ripoti yake ilikemewa eti imevuka mipaka yake kwa sababu ilikuwa kamati na siyo tume na rais mstaafu wa awamu ya pili Benjamin William Mkapa hata kufikia kudhihaki kuwa ni sawa na debe tupu ambalo haliachi kutika.
  Hakika hii ilikuwa ni fedheha; kumbe zinapoundwa tume za kuratibu maoni ya wananchi ya kuhitaji Katiba mpya kunakuwa na hadidu za rejea sasa ni vema mara baada ya kuundwa tume na Rais Kikwete, ni vema Watanzania wakaelezwa wazi hizo hadidu za rejea ili kuondoa mkanganyiko miongoni mwa Watanzania.
  Mmoja wa wanaharakati na ambaye ni Mhadhiri wa Kitivo cha sheria, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Chris Maina, alipozungumza na Tanzania Daima Jumapili, alifafanua kwa kina baadhi ya maeneo yenye utata katika Katiba iliyopo.
  Profesa Maina alisema Tanzania ni Jamhuri ya Muungano wa nchi mbili, serikali mbili na katiba mbili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na Katiba ya Zanzibar ya 1984, alisema kwamba hivi sasa kuna kero nyingi za Muungano.
  Pia alitoa mfano wa sehemu inayohusu Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo wanaoweza kushtakiana ni Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano tu (Sehemu ya Saba ya Sura ya Tano ya Katiba â€" Ibara ya 125 hadi 128) na kuangaliza kuwa Katiba ya nchi haitakiwi iwe hivyo.
  Na hivi karibu tuliweza kumsikia na hata kumshudia Mbunge wa Ubungo, John Mnyika(CHADEMA), ambaye aliwasilisha taarifa ya hoja binafsi bungeni katika mkutano wake wa Februari, mwaka huu, ili liweke utaratibu wa kuanzishwa, kuratibiwa na kusimamiwa kwa mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia matakwa ya umma.
  Mnyika alisema ameona ni vema kuwasilisha hoja hiyo mapema kuliko alivyokuwa amepanga awali, baada ya kuona dalili za suala hilo 'kupelekwa katika njia zenye kasoro' ambazo ziliwahi kutumika huko nyuma na matokeo yake kupuuzwa.
  Ziko sababu kadhaa ambazo nimeona umuhimu wa kulipeleka suala hilo bungeni sasa, ili lichukue mkondo wa Bunge, kwanza Katiba ni sheria, tofauti yake na sheria nyingine yenyewe ni sheria mama na ni vema hata hii kamati atakayounda Rais Kikwete, ikasubiri maelekezo ya Bunge kwanza ili kupata njia sahihi.
  Ibara ya 63 (2) na (3) zinaeleza kuwa Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria pia ibara ya 98 (1) si sheria tu, bunge lina mamlaka ya kufanya mabadiliko ya Katiba...hivyo kuna haja ya mjadala huu kuchukua mkondo bungeni, ndiyo uende serikalini, kisha urudi bungeni.
  Lakini pia ikumbukwe kuwa Katiba ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa, viongozi na waongozwaji au serikali na wananchi.
  Pamoja na Rais Kikwete, kukiri kuwa yapo mabadiliko mengi yaliyotokea katika nyanja mbalimbali za maisha ya taifa la Tanzania, hivyo na kuwataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yenye mtazamo wa hali ya juu ili kuwa na Katiba itakayokidhi mahitaji ya sasa na kipindi kijacho, ambayo italipeleka taifa letu miaka 50 ijayo kwa salama, amani, umoja na kuwapo maendeleo makubwa zaidi ni vema tukapata maelekezo ya Bunge letu ndio tukaja na mkakati wa kurudi kwa wananchi au vinginevyo ni kuiteka nyara hoja hii na kuifumbata kibindoni.
  Ninampongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kufanya maamuzi haya kwa muda muafaka, kabla ya misukosuko ya madai ya Katiba mpya haijachafua hali ya utulivu na amani ya nchi yetu, lakini pia ni kipindi kizuri kwake cha kuliacha jina lake katika kumbukumbu nzuri ya historia ya nchi hii mara amalizapo muda wake 2015.
  Tunayo mifano ambayo iko hai hasa kupitia kwa Rais wa Awamu ya Sita wa Zanzibar Amani Karume, kwa kuridhia maafikiano yaliyoleta sura mpya ya amani Zanzibar ambayo mchakato wake kwanza ulianza katika Baraza la Wawakilishi na wananchi wakaamua kwa kupewa maelekezo na chombo hicho.
  Huku Rais Kikwete, akitangaza azma hiyo na Chama cha Wananchi (CUF) kiliwasilisha rasimu ya katiba mpya yenye kurasa 88 sura 36 ibara zaidi ya 130 ambayo nayo kimsingi Serikali haitakiwi kubezwa hata kidogo ili kumaliza utata wa jambo hili.
  Hakika kama hili litafanikiwa na utekelezaji wake kufanikiwa Rais Jakaya Kikwete, atakuwa amekonga nyoyo za Watanzania wengi hasa kwa kuimarika kwa demokrasia ya kweli ambayo itashamiri sawasawa.
  Ila kama kutakuwa na uzito wa kutekeleza ahadi yake ni vema akang'amua hasa kwa kusoma kitabu cha hayati Shabaan Robert, kiitwacho Kusadikika, pamoja na maonyo yote kuhusu dunia ya kufikirika ila serikali bora inatakiwa kujua serikali hutawala nyoyo za watu na siyo viwiliwili vya watu hasa kwa kuongeza askari na kununua bunduki ili kuwakabili raia wake.
  Kwa hili la Katiba Rais Kikwete, amenena na ameacha shauku kubwa kuisubiri kwa hamu ili kuweza kuijenga Tanzania ambayo inatimiza Jubilei ya miaka 50, ikiweka historia hasa kwa nchi za jirani zetu na mataifa ya mbali kuendelea kuwa mfano wa kuigwa hasa kwa kupata Katiba mpya.
   
 6. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #6
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  [​IMG]
  Katiba mali ya wananchi si watawala
  [​IMG]

  Christopher Nyenyembe

  [​IMG] WANANCHI wanataka katiba mpya, hawataki katiba yenye viraka viraka vilivyobandikwa na watawala wachache tangu Tanganyika ilipopata Uhuru wake mwaka 1961, pale Watanganyika walipojiondoa kwenye mikono ya wakoloni wa Kiingereza.
  Umuhimu wa katiba mpya ni wa kimahitaji na umefika wakati ambao suala hilo linapaswa kuwa la kitaifa zaidi kuliko jinsi mgawanyiko wa kiitikadi na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanavyokuwa bubu kulizungumzia suala hili au kutaka kulipa zaidi nguvu ya kichama kuliko utaifa.
  Pengine kuna mambo kadhaa ya kujifunza na haitakuwa rahisi kama tunahitaji kujifunza kutokana na machafuko ambayo wenzetu wa nchi jirani yamejitokeza tu kwa sababu ya tofauti za watawala lakini kinyume chake wananchi wa kawaida ndio wanaokuja kuumia.
  Nadhani umefika wakati ambao vyombo vya habari, wanaharakati wa haki za binadamu,viongozi wa madhehebu ya dini, wanasiasa, nchi marafiki na wahisani ambao wanaitakia mema Tanzaniawakubali,washawishi na waone kuwa umefika wakati muafaka wa kuwa na katiba mpya itakayoweza kukidhi matarajio ya watanzania wote.
  Niliwahi kuandika na hatupaswi kuchoka kuandika kuhusu suala hili la katiba kuwa iwe isiwe, kikombe hiki cha katiba mpya serikali isijidanganye ijue kuwa kikombe hiki hakiepukiki, katiba ni ya wananchi na sio ya watawala wachache wanaodhani kuwa kwa kupuuza kwao jambo hili wanaweza kuwa salama.
  Usalama wa viongozi na dhamana kubwa waliyopewa na wananchi wa kuliongoza na kulisimamia taifa hili lisiweze kwenda mrama ni pamoja na uwezo wao wa kufungua akili na masikio yao, kujua na kutambua kwa haraka kuwa sasa wakati umefika mchakato wa kuwa na katiba mpya haupaswi kupuuzwa hata kidogo.
  Nashukuru rais Kikwete, amesoma alama za nyakati kuwa taifa linahitaji katiba mpya na juzi wakati akitoa salama za mwaka mpya alisema ameamua kuunda tume ya watalaamu ambao watasaidia kukusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya na baadae watayapeleka kwenye vyombo husika kwa utekelezaji zaidi.
  Pamoja na dalili ndogo za wazi zinazojionyesha kuwa wapo baadhi ya viongozi ambao kwa uwezo wao mkubwa wa kujua na kupambanua mambo wangeweza kumwambia wazi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa umefika muda wa kuruhusu rasmi mjadala wa kitaifa kuhusu katiba lakini wanamuogopa.
  Pengine kwa mawazo yao wanamuogopa, Rais kwa vile ndiye aliyewateua kushika madaraka hayo waliyonayo au wanamuogopa rais kwa kujua inawezekana wakamuudhi katika kuutoa ushauri huo na kama hatakubaliana nao wanaweza kujikaanga na kuhatarisha vyeo walivyopewa kwa muda mfupi uliopita.
  Lakini inawezekana pia katika hilo hata Rais mwenyewe hajui kama kuna watu muhimu kwake ambao wanamuogopa na hawapo tayari kumpa ushauri mzito kama huu wa katiba kwa ajili ya manufaa ya taifa hili na pengine kuwa na kinga madhubuti ya kujiepusha na machafuko ya kisiasa kadri miaka inavyozidi kusogea.
  Tukiachia mawazo ya washauri wachache wanaopaswa kumjuza rais juu ya jambo hilo, wapo viongozi wa dini, wanaharakati na nchi marafiki wanaosikia kwa karibu matamanio haya ya wananchi ya kuhitaji katiba madhubuti ya nchi na kuondokana na ile ya urithi kutoka kwa wakoloni ambayo tunaweza kusema kuwa imepitwa na wakati, haifai (Ime-Expire).
  Watanzania wanajijua fika kuwa walikuwa koloni la mwingireza na bado ni wanachama wa jumuiya ya madola hilo haliepukiki labda kwa namna nyingine ya kuikana historia ya utumwa na kutawaliwa na taifa hilo ambalo hakuna anayeona umuhimu wa kuwa na sura ya utumwa mamboleo na kujikana kwa akili zetu kutaka kitu ambacho ni chetu.
  Zipo njia nyingi za kuishawishi serikali iliyopo madarakani kuona umuhimu huo na ni wazi na dhahiri ya kweli kuwa kuwepo kwa katiba mpya kutaruhusu na kurejesha undugu na upendo mkubwa walionao Watanzania katika kujijenga nchi yao kwa kuwa kitakachoweza kuwaongoza sasa ni mawazo na maamuzi yao waliyoweza kuridhia kwa moyo mkunjufu bila shaka kuwa wanaonewa.
  Katiba mpya ndio itakayokuwa msingi wa zama hizi mpya za kufufua maadili ya kitaifa yaliyopotea,kupoteza sura ya uzalendo na kutaka kujenga ukuta imara katika jamii nzima bila shaka wala hofu kuwa Tanzania yenye kuhitaji demokrasia halisi inawezekana na bila katiba mpya lazima watawala waliopo wataiongoza nchi hii kwa hofu na mashaka.
  Mbali ya kuwataja washauri kadhaa ambao pengine kwa hulka zao wanaogopa kumweleza ukweli Rais kuhusu hilo lazima tukiri wazi kuwa hata rais mwenyewe kwa nafsi yake,uelewa na ujasiri mkubwa alionao wa kuliongoza taifa hili kwa masikio yake amesikia kuwa sasa Watanzania wanahitaji mchakato wa haraka wa kuwa na katiba mpya.
  Hatuwezi kusema eti rais hasikii haya yanayopiganiwa sasa, anajua kabisa kila kinachosemwa na Watanzania zaidi ya milioni 5 waliompa haki ya kuliongoza Taifa hili aliposhinda kwenye uchaguzi mkuu mwaka jana, ni ushahidi tosha na anajua kuwa nchi hii ina watu wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 40 ambao kwa wingi huo kuna swali la kujiuliza.
  Kwa namna hali ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita huku, taa na kurunzi za wanasiasa zikielekezwa mwaka 2015 na kwa namna hiyo hiyo ya idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza katika uchaguzi huo ipo haja rais akafanya maamuzi sahihi ya kuitengeneza vizuri katiba mpya ili kuwapa kile roho inapenda Watanzania wengi.
  Sio siri naweza kusema usalama na amani ya Wazanzibari iliyofanywa na Rais mstaafu,Amani Karume imeweza kumrejeshea heshima kubwa kuliko jambo lolote kwa kipindi cha miaka 10 aliyoiongoza Zanzibari hivyo kwa rais wetu wa Tanzania,Jakaya Kikwete anapaswa kuliona hili la katiba mpya kuwa ndio silaha pekee iliyobaki ya kumletea heshima kubwa mara atakapomaliza kipindi chake hiki cha mwisho.
  Afadhali aachane na ahadi zote alizozitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu mwaka jana kwa kuwa yapo mambo yasiyoweza kutekelezaka na machache yatatekelezeka lakini hili la katiba mpya ni mzigo ambao serikali ya awamu ya nne ya Rais Kikwete haiwezi kulikwepa.
  Na kwa kutambua hivyo kuwa katiba ndio msahafu mkubwa katika maisha ya hapa duniani ,inayowaongoza watu kuishi kwa haki,uhuru na amani hapo inapaswa kujulikana wazi kuwa katiba ni mali ya umma na sio mali ya watawala wachache,wao watapita lakini umma hauwezi kupita.
  Kwa kuitakia nia njema nchi hii na watu wake,maadam kwa pamoja tumeridhia uwepo wa mfumo wa vyama vingi vya siasa lazima sasa tukubali pia kuiridhia katiba ya umoja wa kitaifa,hicho ndio kilio cha wengi kwa kuwa dalili za mwanzo za watu kutofautiana zimeanza kujionyesha kwa sababu ya itikadi ya vyama vyao,tusifike huko,Katiba mpya haikwepeki.
   
 7. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #7
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Werema tueleze Watanzania ni kina nani?
  [​IMG]

  Innocent Nganyagwa

  [​IMG] KUNA hatari kuwa kwa jinsi linavyoendelea, suala la madai ya mabadiliko, au kuandikwa kwa katiba mpya, kunaweza kutufanya Watanzania wote tuonekane kama mazuzu.
  Hii ni kwa sababu ushauri unaotolewa unaanza kutuchanganya kiasi kwamba upo uwezekano wa watu kukubaliana na ushauri wa kipumbavu.
  Mwalimu Julius Nyerere alishatuonya kuwa akitokea mtu, akakuona una kipande cha almasi, akakuongopea kuwa hiyo ni chupa tu na kisha akakupa kipande chake cha chupa akikuaminisha kuwa hiyo ndiyo almasi halisi, na wewe ukaondoka ukishanglia kama zuzu, haya ndiyo yanayoelekea kutokea katika mjadala kuhusu katiba nchini.
  Wapo watu ambao wanatoa mawazo na ushauri ambao kwa akili za kawaida haupaswi kutolewa na watu wa aina hiyo.
  Kuna watu ambao bila shaka watakubaliana nao hata kama ushauri wanaoutoa si mzuri.
  Wiki hii Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema naye amekuja na mpya!
  Kwanza anadai kuwa aliyoyasema wakati wa sherehe za kuapishwa kwa Jaji Mkuu Jumatatu iliyopita ni maoni na mawazo yake binafsi na hayahusiani na wadhifa wake. Sijui kama hili linawezekana.
  Ni dhahiri kuwa waandishi waliomfuata kumuuliza kuhusiana na mjadala unaonedelea wa katiba mpya, hawakumfuata kama Werema, walimfuata kama Mwanasheria Mkuu.
  Hivyo, anaposema kuwa alichokisema kinawakiisha mtu binafsi, ajue kuwa hayupo sahihi kwani waandishi hawakumfuata mtu binafsi.
  Lakini katika maoni yake anashangazwa kuwa hoja kuhusu katiba imeshikiwa bango na watu wengine wakati Watanzania wenyewe wamenyamaza kimya.
  Kwa mujibu wa Jaji Werema, madai kuhusiana na katiba yanapaswa kutolewa na Watanzania na mpaka sasa yeye hajawasikia hao wakitoa hoja hizo.
  Anashangazwa kuwa wanaozungumzia katiba ni watu wa Dar es Salaam tu, na kuona sehemu nyingine za nchi wamekuwa kimya.
  Kwa maana nyingine, Jaji Werema anatueleza kuwa waliotoa hoja hiyo hadi hivi sasa, ambao wengi ni wakazi wa Dar es Salaam, si Watanzania.
  Anasubiri kuona sauti ya Watanzania ikipazwa kutoka vijijini ambako wanaishi.
  Suala lililoniacha kinywa wazi ni kwa nini Jaji Werema anawaona wanaotoa hoja kuhusiana na katiba mpya hadi hizi sasa si Watanzania?
  Katika hili Mwanasheria Mkuu anapaswa kutupa darasa la nguvu akituelewesha ni kwa nini hawa waliozungumza kuhusu katika mpya mpaka hivi sasa si Watanzania.
  Pia Jaji Werema anapaswa kutueleza hao ambao yeye anaamini kuwa ni Watanzania ni watu wa aina gani?
  La ajabu, alikiri kuwa ni haki na wajibu kwa wanasiasa kutoka vyama mbalimbali vya siasa kulizungumzia hili la katiba.
  Hakuona tatizo katika hilo. Sasa sijui kwa tafsiri yake Watanzania ni wanasiasa au vipi?
  Kwa bahati mbaya sana, wanasiasa (pamoja na viongozi wa dini na wanaharakati) ambao wamelishikia bango suala la katiba, wengi wao wapo Dar es Salaam, ambako Jaji Werema anakuona kamamahali ambako hakuna Watanzania.
  Kibaya zaidi ni kuwa hata hao Watanzania watakapoamua kupaza sauti na kudai katiba mpya, Jaji Werema tayari ameshatoa jibu; kwamba ofisi yake haioni umuhimu wa kuandikwa kwa katiba mpya hivi sasa.
  Ameshatoa mawazo yake kuwa kinachoweza kufanyika ni kuifanyia marekebisho katiba iliyopo.
  Kwa kuonyesha kuwa hana mzaha katika hili, ametoa mifano ya India na Marekani, akisema kila moja ya nchi hizo zimeshafanya mabadiliko ya katiba zao kwa mara 50.
  Lakini nataka nimkumbushe Jaji Werema, kwa maana nina uhakika anafahamu, kuwa katiba ambayo Marekani imeifanyia marekebisho mara 50, ni katiba ambayo ilitungwa na wamarekani kwa umoja wao kama taifa.
  Kuifananisha katiba ya Marekani na ya Tanzania ni hatari sana. Ni hatari kwa sababu watanzania, kama taifa, hawajapata fursa ya kushiriki katika utungaji wa katiba yao.
  Katiba tuliyonayo leo hii, ni kazi ya kikundi kidogo cha watu ambao walifanya kazi hiyo kwa niaba ya wengine. Tena, wakati kazi hiyo inafanyika, mamilioni ya Watanzania wala hawakuwa na habari kuwa kuna kazi fulani inafanyika inayohusu mustakabali wa maisha yao kama taifa.
  Wamarekani wana haki ya kuifanyia marekebisho katiba yao haya mara 100 kwa sababu wanajua kuwa waliiweka katika misingi ambayo ilikubaliwa na jamii kubwa.
  Hii ya kwetu, ambayo ni kazi ya watu wachache, haiwezi kupita majaribio makubwa kama ambavyo katiba ya Marekani imepitia.
  Tazama sasa tunapata matatizo ambayo yanaonekana kuwa kama makubwa wakati ni ya kawaida tu.
  Kama tungekuwa na msingi mzuri (Katiba) wa kushughulikia matatizo hayo, wala leo hii tusingkuwa na mijadala inayoendelea kuhusiana na katiba na mambo mengine.
  Kama Jaji Werema hajawatambua wanaopaza sauti kudai katiba kuwa ni Watanzania, anapaswa kufahamu kuwa ni wananchi wa Tanzania ambao wana haki ya kujiamulia kanuni na sheria za kuwatawala.
  Kuu katika kanuni na sheria hizo ni katiba. Hivi kuna ubaya gani kuwapa watu hawa haki yao ya kujiandikia katiba yao hata kama iliyopo inatoshereleza mahitaji?
  Mwanasheria Mkuu ameongeza sauti yake kwa kauli ya waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani kuwa ni vema watu wakaja na maoni ya nini kisichofaa katika katiba iliyopo ili kupata msingi wa kitu cha kukijadili.
  Lakini, inaonekana kuwa Jaji Werema anakiuka kauli hiyo kwa yeye mwenyewe kuanza kujadili suala hilo hata kabla hajapokea hayo maoni.
  Mbaya zaidi, tayari anaonekana kuwa na msimamo anaposema kuwa hakuna haja ya kuandika katiba mpya, bali kuifanyia marekebisho iliyopo wakati hajajua wale wanaotaka katiba mpya wana maoni gani!
  Haya ndiyo mambo ya kufanyana mazuzu.
   
 8. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #8
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  Werema anajitia upofu wa Samwel ili iweje?
  [​IMG]

  Abdul Juma

  [​IMG] IPO hadithi ya kuchekesha kidogo inayowahusu marafiki wawili Sauli na Samwel. Vijana hawa walikuwa na mitazamo tofauti kiimani na matamanio ya mali.
  Sauli alikuwa kijana wa imani aliyependa kusali wakati wote. Na kutokana na imani yake Mwenyezi Mungu alikuwa akimpatia kila alichokiomba.
  Lakini hali ilikuwa ni tofauti kwa rafiki yake Samwel ambaye alikuwa kijana mwenye tamaa ya vitu na imani haba kwa Mungu, hivyo maombi yake yalikuwa hayana manufaa.
  Siku moja Samwel alimwendea Sauli na kumwambia waombe kwa Mungu ili awapatie kile wanachokitaka. Na kutokana na Samwel kumwamini rafiki yake huyo kuwa ana bahati ya kusikilizwa na mungu na kupatiwa kila ambacho, alimshauri aongoze sala yao.
  "Sauli ndugu yangu, wewe una bahati maana chochote uombacho mungu anakusikiliza, sasa leo mimi niko tayari tusali pamoja na utakachokiomba nami ni hicho hicho" alisema Samwel.
  Sauli baada kusikia kauli hiyo ya rafiki yake, alimkubalia kuwa wataomba pamoja. Lakini hakujua kumbe mwenziye alikuwa na tamaa ya mali.
  Kwa upande wake Sauli alikuwa amekerwa na maovu mengi aliyokuwa akishuhudia watu wakitenda, na kutokana na imani yake kwa mungu aliona ni bora aombe awe kipofu.
  Ndipo akarudia kumuuliza rafiki yake Samwel kwa mara nyingine kabla ya kuomba ili kujihakikishia kama kweli yuko tayari kwa chochote kitakachoombwa. Mwenzie akijibu 'niko tayari'.
  Hapo Sauli akamwomba Samwel afumbe macho waombe na sala yake ikiwa hii, "Ee mwenyezi mungu, tazama tumechoka kushuhudia maovu haya ya dunia.
  Kuanzia sasa mimi na rafiki yangu Samwel tunaomba utupe upofu, tuachane na kuona dhambi hizi za dunia hii" alihitimisha Sauli na kuanzia wakati huo wakawa hawaoni tena.
  Lakini katika hali ya kushangaza Samwel alipojaribu kufumbua macho yake bila mafanikio, alianza kumshutumu rafiki yake akimtaka aombe tena ili apate kuona kwa vile hakuwa akitaka upofu.
  Kama wewe si mwelewa wa kutambua dhamira za viongozi wetu wa serikali, hadithi hii ya Sauli na Samwel haiwezi kukusaidia. Lakini kwa wale wanaoelewa utapeli wa kisiasa watanielewa.
  Tunamshukuru Mungu kwa kuona mwaka mpya wa 2011. Huu hakika ni mwaka mpya kweli, maana tumetoka kwenye vinyongo na visasi vya uchaguzi mkuu, wananchi wanalia na chakachua iliyofanyika.
  Haki na kura zao wanaona kama ziliporwa na sasa wamejielekeza kukata mzizi wa fitina, wanataka katiba mpya. Hii ndiyo inaonekana kuwa suluhu ya kuwabana wachakachuaji wa kila kitu.
  Kwa majonzi makubwa watawala hawataki kabisa kusikia wimbo huo wa katiba mpya na kila anayejitokeza kuuimba wimbo huo hasemi kama mtawala anatoa maoni yake. Utajiuliza yeye anasimamia nini?
  Viongozi wetu wana hulka na tamaa za Samwel, hawaamini kwenye ukweli kama Sauli. Wako radhi kwa wakati huu kujitia upofu wakiamini kuwa Katiba iliyopo haina tatizo na bila haya wanasema eti iweke viraka tu.
  Hatuwalaumu kwa hilo bali tunawaombea watoke madarakani wakae upande wa upinzani ndipo wataona umhimu wa katiba mpya, kwa sasa hawawezi, watajitia upofu bila kutaka kwa vile ubovu huo ndiyo unawasaidia kuendeleza ufisadi wao.
  Mwanzoni kabisa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuibua hoja hii ya katiba mpya, Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani ndiye alikuwa wa kwanza kujipofusha na kusema wazi haoni umhimu huo kwa sasa.
  Kama kawaida yao kugongana wakati wa kuisemea serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye kimamlaka ndiye mkuu wa baraza la mawaziri, alipingana na Kombani akisema madai ya katiba hayakwepeki kwa sasa.
  Kisha akatoa ahadi ya kumshauri Rais aunde kamati itakayoratibu mchakato huo, ili kuhakikisha wananchi wanapata katiba mpya inayotokana na wao wenyewe badala ya ile ya mwaka 1977 inayoonekana kubeba mtazamo wa uliopitwa na wakati.
  Sasa mitaani kila mmoja anazungumzia hoja hiyo, maoni yameanza kutolewa jinsi gani wananchi washirikishwe. Lakini mapema wiki hii, mwanasheria Mkuu wa serikali naye akajitia upofu kamaKombani.
  Mwanasheria Mkuu, Jaji Fredrick Werema alisema kuwa hakuna haja ya Katiba mpya kwa sasa na badala yake hii iliyopo inaweza kufanyiwa marekebisho na kuwekwa viraka kwa kurekebisha vipengele vyenye kasoro.
  Kauli yake tunaweza kuiita ya serikali kwa vile yeye ndiye mshauri mkuu wa serikali kisheria, lakini pia kama raia ana haki ya kutoa kauli yoyote kama maoni yake imradi asivunje katiba.
  Ila ukweli lazima usemwe kuwa Jaji Werema kajiaibisha yeye mwenyewe, kaiabisha taaluma yake na serikali anayoishauri. Huyu hana tofauti na Samwel aliyekwenda kumshawishi Sauli waombe akijua kuwa watapata mali kumbe hakujua hitaji la rafiki yake.
  Hitaji la Watanzania kwa sasa si kutetea wala kuwaonea huruma mafisadi na ving'ang'anizi wa madaraka. Watu wanataka katiba mpya inayoweka mipata ya kuwabana manyang'au wanaokwapuamali za umma, wanaopeana nyadhifa kwa kuangaliana usoni badala ya ufanisi.
  Hoja inajengwa kwa kujenga hoja, kama huna hoja si lazima usema. Heri kunyamaza watu watakuelewa kuliko kusema ukawachefua na kujitia aibu. Kama mwanasheria mkuu ndiye huyu asiyeona matatizo ya nchi, bora tuanze kulia mapema. Tafakari na uchukue hatua.
   
 9. Rutashubanyuma

  Rutashubanyuma JF-Expert Member

  #9
  Jan 2, 2011
  Joined: Sep 24, 2010
  Messages: 157,748
  Likes Received: 416,097
  Trophy Points: 280
  NEC ni tume ya uchaguzi au ya ushindi wa CCM?
  [​IMG]

  Prudence Karugendo

  [​IMG] MOJA ya vyombo nyeti katika uhai wa usalama wa nchi yetu ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
  Tume hii ndiyo imekabidhiwa jukumu la kutoa kauli ya mwisho ya ni nani anapaswa kuwa mhimili mkuu wa nchi yetu kulingana na matakwa ya wananchi.
  Hii maana yake ni kwamba chombo hiki kinapaswa kutoa kauli inayotafsiri matakwa halali na sahihi ya wananchi na siyo kutoa kauli kulingana na namna kinavyotaka chenyewe.
  Haipaswi pia kutoa kauli kulingana na namna kinavyoona inafaa kwa kutegemea tu uadhimu wa mamlaka kiliyopewa.
  Ila kwa vile mamlaka wakati mwingine hulevya upo uwezekano wa chombo hiki kutoa kauli inayokinzana na matakwa ya wananchi.
  Hivyo kauli yake kuonekana siyo tafsiri sahihi ya matakwa yao kitu kinachoweza kuifanya kauli hiyo ya mwisho ya chombo hicho kuonekana haramu na kusababisha tafrani. Hapo ndipo ulipo unyeti wa NEC.
  Chombo hicho kinapotetereka, iwe kwa kushindwa kuhimili nguvu ya kilevi kilichomo ndani ya mamlaka kinayokabidhiwa ama kwa kutumiwa vibaya na mamlaka iliyo juu yake, serikali, kinyume na kusudio lililokianzisha, ni rahisi chombo hicho kuigeuza nchi kuwa jahanamu.
  Mifano hai tunayo, tujikumbushe ya Zimbabwe, Kenya na yale ambayo yamekuwa yakijirudiarudia kule Zanzibar, kwa kutaja sehemu chache tu.
  Kwa kulizingatia suala hilo la unyeti wa NEC, moja kwa moja ndipo unapojitokeza umuhimu wa chombo hicho kuwa huru tofauti na ilivyo hapa nchini kwetu. Uhuru ninaousema unapaswa ujionyeshe tangu pale chombo hicho kinapoundwa.
  Inabidi uwepo utaratibu huru wa kuwapata wasimamizi wa chombo hicho ambao utakuwa hauwabani na kuwafanya waegemee upande fulani, wanapaswa wawe huru ili wasiweze kuegemea upande wowote.
  Huo ni utaratibu ambao unapaswa uwe tofauti kabisa na huu wa sasa ambao wasimamizi wote, au niseme watumishi wa tume hiyo, ni wateule wa serikali iliyo madarakani. Kitu hicho kinaifanya Tume ya Uchaguzi kuonekana kama idara ya serikali.
  Kwa wale ambao hawamo serikalini ni vigumu kuelewa vigezo vinavyotumika kuwapata watumishi wa Tume ya Uchaguzi kuanzia kwa mwenyekiti wa tume hiyo, wakurugenzi wake na watumishi wa chini yao.
  Kwa uzoefu uliopo ni kwamba uteuzi wowote ni lazima ulenge kwa mtu aliye tayari kuwa mtiifu kwa yule anayemteua au mamlaka husika.
  Ni uzoefu huo unaoweka kila kitu wazi na kuonyesha kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyoteuliwa na serikali iliyo madarakani haiwezi kuwa huru.
  Haiwezi kuwa huru kiasi cha kubariki maamuzi yanayositisha uwepo wa serikali husika ambayo tume inakuwa imeahidi kuwa tiifu kwake na kuilinda kwa namna yoyote iwayo.
  Hapo ndipo tunapofika na kugundua kwamba hatuna tume huru ya uchaguzi.
  Na tunapokosa tume huru ya uchaguzi kinachofuatia ni nini? Ukosekano wa tume huru ya uchaguzi unamaanisha kuiweka demokrasia nyuma ya pazia na kubaki ikiimbwa tu bila yenyewe kuonekana jukwaani.
  Uchaguzi utaandaliwa kama alama ya demokrasia, kura zitapigwa lakini kitakachoamuliwa na wapiga kura hakitawekwa wazi kulingana na matakwa yao ila badala yake NEC itageuza.
  Itafanya hivyo kuonyesha kile kinachowafurahisha walioiunda tume hiyo. Wananchi watakuwa wamehangaika bure, pesa ya kodi zao itakuwa imeharibika bure katika mchakato mzima wa uchaguzi wakati mambo yakilazimishwa kubaki vilevile na Tume ya Uchaguzi isiyo na uhuru wowote wa kutangaza kilicho sahihi.
  Kwa mwonekano huo Tume ya Uchaguzi inabaki kuwa kiinimacho kinachotumika kuhalalisha udikteta wa watawala wasiowaamini wapiga kura, hususan katika sehemu kubwa ya Afrika.
  Bara la Afrika inaonekana demokrasia inafuatwa kwa wananchi kufanya chaguzi ambazo lakini, kwa vyovyote vile, matokeo ni lazima yaonyeshe yanawapendelea watawala walio madarakani ilihali katika hali halisi wapiga kura wanakuwa wameishawachoka na hawawataki.
  Hivyo tutaona kuwa tume za uchaguzi katika sehemu kubwa ya Afrika zinatumika kuifunika demokrasia wakati huohuo zikiwa zimeubeba udikteta wa watawala wasiopenda mabadiliko.
  Kumbe tume hizi za uchaguzi kwa maana nyingine ni kikwazo kwa demokrasia iliyo komavu na pia ni kikwazo katika juhudi zinazofanywa na jamii duni kujikwamua katika ufukara.
  Ni vigumu kuuondoa ufukara ambao jamii husika inakuwa imesababishiwa na utawala mbovu usiopenda kuondoka madarakani kwa njia za kidemokrasia.
  Ili kuondokana na ufakara wa aina hiyo ni lazima kuhakikisha kwanza mfumo mbovu wa utawala unaondoka madarakani.
  Kwahiyo juhudi zozote za kukwamisha mabadiliko hayo zinakuwa zimelenga kuidumaza jamii husika kwa kuzidi kuididimiza kwenye lindi la ufukara.
  Tanzania tunayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi, tangu tume hiyo iundwe ni zaidi ya miaka 15 sasa.
  Naweza kusema kwamba tume hii ni ile ile iliyoundwa tangu wakati huo ikiwa chini ya mwenyekiti wake, Jaji msitaafu Lewis Makame.
  Sina hakika kama wale walio chini yake wapo waliositaafu au kubadilishwa, ila mwenyekiti ni yuleyule ambaye amekuwa kwenye nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 15.
  Sidhani kama katika tume hiyo kuna kitu kustaafu kwa vile watumishi wake wengi ni wale ambao tayari ni wasitaafu. Zaidi ya hapo cha kuwastaafisha pengine ni kifo.
  Cha kufikiria ni kwamba kwa kipindi chote hiki cha zaidi ya miaka 15 bila tume hii kubadilishwa, ambapo imeweza kufanya kazi katika awamu tatu za marais tofauti.
  Bila shaka tume hiyo itakuwa ni ya manufaa kwa serikali zote tatu ilizofanya kazi chini yake. Naweza kusema kwamba tume hiyo imeonyesha uaminifu na utiifu mkubwa kwa serikali na hizo.
  Uaminifu na utiifu huo pengine ndiyo sababu ya serikali kutoona umuhimu wa kuifanyia mabadiliko tume hiyo.
  Lakini wakati tume hiyo ikionekana hivyo upande wa serikali, kwa upande wangu, kama mwananchi mpiga kura, naweza kusema kwamba sijawahi kuona chombo kilichovurunda majukumu yake kama hii kama hiki.
  Ikumbukwe jinsi tume hiyo ilivyovuruga Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 ambao ndio uliokuwa wa kwanza tume hiyo kuusimamia ukiwa unahusisha vyama vingi vya siasa.
  Katika hali ya kushangaza uchaguzi huo ilibidi ufutwe katika majimbo yote ya mkoa wa Dar es salaam kwa madai ya upungufu wa vifaa vya kupigia kura!
  Ilidaiwa kwamba vifaa hivyo havikuweza kufikishwa kwa ukamilifu katika vituo vya kupigia kura kwenye majimbo yote ya mkoa wa Dar es salaam.
  Lakini pamoja na hali kuwa hivyo mkoani Dar es salaam, ambako ndiko yaliko makao makuu ya Tume ya Uchaguzi, hali ilikuwa tofauti kwingineko mikoani.
  Kule wananchi walipiga kura bila matatizo yoyote na hakukuwepo na upungufu wa vifaa!
  Fikiria kituo cha kupigia kura kilichopo mita 50 kutoka makao makuu ya Tume ya Uchaguzi, ambako ndiko kulikohifadhiwa vifaa vyote vya kupigia kura, inapungukiwa na vifaa hivyo na kuwafanya wananchi washindwe kupiga kura.
  Lakini kituo kilichoko kilomita 2000 kutoka hapo eti kinakuwa na vifaa vyote na hivyo kuwawezesha wananchi wa kule kupiga kura bila matatizo yoyote!
  Hayo yalikuwa ni maajabu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania.
  Lakini wakati wananchi wa mkoa wa Dar es salaam wakilishwa madai hayo ya kizembe ya tume hiyo, wao walichokiona ni tofauti.
  Ni kwamba majimbo yote ya mkoa huo yalikuwa yaende kwenye kambi ya upinzani, kwahiyo tume tiifu kwa serikali ikaamua kuokoa jahazi.
  Bila shaka isingeweza kuliweka wazi hilo ndiyo maana yakatolewa madai hayo ya maajabu ya kushindwa kufikisha vifaa vya kupigia kura katika umbali wa mita 50 wakati imefikisha vifaa hivyo katika umbali wa kilomita 2000!
  Uchaguzi uliofuata wa mwaka 2000 nao ulijaa mapungufu ya aina ileile ya makusudi na ya kizembe.
  Lakini hatukuona hatua yoyote ya kuwajibika ili kuwarudishia wananchi imani kuwa yaliyokuwa yanatokea yalikuwa hayaifurahishi hata tume yenyewe.
  Ukaja uchaguzi wa mwaka 2005 kwa mtindo uleule.
  Sasa funga kazi ni huu uchaguzi wa mwaka 2010 maarufu kama uchakachuaji.
  Tumeweza kuona jinsi Tume ya Uchaguzi ilivyoendesha zoezi zima la uchaguzi bila kujitofautisha hata kidogo na serikali ambayo ilikuwa ni mshindani katika uchaguzi huo ambapo tume ya uchaguzi ndiyo ilikuwa mshika kipenga.
  Zoezi zima la uchaguzi limeendeshwa katika hali ya kutatanisha kabisa na kuwafanya wananchi wasiweze kuamini kama kuna kitu kinajitegemea kama Tume ya Uchaguzi.
  Imefikia wakati ikaonekana kama vile Tume ya Uchaguzi inapewa maelekezo mmoja wa washindani na kuyafuata badala ya yenyewe kutoa maelekezo.
  Tuliona jinsi madai mengi yaliyokuwa yanatolewa na vyama vilivyokuwa vinashiriki uchaguzi juu ya CCM kukiuka taratibu na kanuni za uchaguzi.
  Majibu yalivyokuwa yakijibiwa na Tume ya uchaguzi badala ya mshitakiwa, CCM, yalistaajabisha kwa sababu tume ilijigeuza mshitakiwa badala kuwa hakimu wakati CCM ikibaki kuwa msikilizaji!
  Hayo na mengine ndiyo yanayoifanya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania ionekane kama taasisi isiyokuwa huru na hivyo kuibua madai kutoka kwa wadau wa uchaguzi, wapiga kura na vyama vya siasa, ya kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi.
  Hata kama madai hayo hayana maana, tume yenyewe, kama siyo kweli kwamba imepewa jukumu maalumu la kusimamia kitu fulani mbali na uchaguzi huru na wa haki.
  Ingebidi NEC, ijionee aibu kwa kushindwa kazi ikiwa inafanya chini ya kiwango kinachokubalika na hivyo kuamua yenyewe kuachia ngazi.
  Vilevile serikali nayo kama kweli haiitumii tume hiyo kama kichaka cha kuficha mambo fulani isingekubali tume hiyo iendelee na kazi kwa kiwango hiki cha udhaifu.
  Hiyo ni kwa sababu chombo chochote chenye utendaji wa kiwango kilicho chini ya asilimia 50 ni wazi kwamba kimeshindwa kazi.
  Tume ya Taifa ya Uchaguzi, bila aibu, ilitutangazia kwamba watu waliopiga kura katika uchaguzi uliopita ni asilimia 42 ya watu wote waliojiandikisha kupiga kura.
  Huo ndio uwezo wa utendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Huyo rais aliyetangazwa na tume hiyo kuwa kapata asilimia 61 ya kura zilizopigwa atakuwa kachaguliwa na asilimia gani ya Watanzania wanaopaswa kupiga kura?
  Rais huyo anawezaje kujivuna kuwa yeye ni chaguo la kidemokrasia la Watanzania?
  Kwa mwenendo huu si itafikia rais achaguliwe na watu 100 katika watu milioni 40? Swali ni je, NEC ipo ili kuhakikisha watu wanafanya uchaguzi au ipo ili kuhakikisha rais aliye madarakani anashinda hata kwa kura sifuri baada wananchi wote kushindwa kujitokeza kupiga kura?
  Tuachane na hiki kiinimacho, ni lazima tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi ili demokrasia ya kweli isimame mahala pake.
   
 10. Ngambo Ngali

  Ngambo Ngali JF-Expert Member

  #10
  Jan 2, 2011
  Joined: Apr 17, 2009
  Messages: 3,194
  Likes Received: 134
  Trophy Points: 160
  Ruta uko sahihi Kabisa, Hatujaambiwa terms of reference ya hiyo tume ni nini. Je kuna uwezekano wa tume iliyoundwa na Rais ikashindwa kuandika kitu anachokitaka. Angalieni mlolongo mzima unavyokwenda AG ni mshauri mkuu wa Serikali katika masuala ya sheria yeye kasema katiba haitabadilishwa.

  Waziri wa Sheria na Masuala ya kikatiba ni msemaji wa serikali kwenye mambo ya kisera kuhusu katiba na yeye kasema bayana kuwa hakuna katiba mpya.

  Msitegemee kuwa hiyo tume itakuwa na maoni tofauti na watendaji hao wawili wakuu wa serikali kwa wateule wa hiyo tume kwa vyovyote watapendezwa na AG, Waziri, retired public officers ambao wote hawatenda kinyume cha matakwa ya wakubwa.
   
Loading...