Dr. Slaa bado alia na CCM | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dr. Slaa bado alia na CCM

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Dec 15, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Dec 15, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,587
  Likes Received: 82,209
  Trophy Points: 280
  Dr. Slaa bado alia na CCM

  2008-12-15 12:59:27
  Na Joseph Mwendapole

  Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, amesema ana ushahidi wa vimemo vilivyokuwa vikiandikwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

  Amesema \'vimemo\' hivyo vilikuwa vikiandikwa na aliyekuwa mmoja wa waliokuwa maofisa waandamizi wa chama hicho (jina tunalo) kwenda kwa aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daud Ballali.

  Dk. Slaa, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alisema CCM haiwezi kujiosha kuwa haihusiki na kampuni ya Kagoda kwani ndiyo ilikuwa ikiitumia kuomba fedha hizo.

  Dk. Slaa alimweleza Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kuacha kupiga bla blaa na badala yake azungumze vitu ambavyo ana ushahidi navyo kama ambavyo Chadema wanafanya.

  ``Makamba aache kuzungumza porojo zake, awe na ushahidi kama sisi ambao tunazungumza tukiwa na uthibitisho. Huu si wakati wa blablaa,`` alisema Dk. Slaa.

  Kuhusu madai ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ya CCM, John Chiligati, kuwa chama chao hakihusiki na Kagoda, Dk. Slaa alisema hawezikupoteza muda kujibizana na mtu anayezungumzia propaganda.

  Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita, Chiligati alisema kuwa CCM haina uhusiano wowote na kampuni ya Kagoda inayodaiwa kujichotea fedha za EPA Sh. bilioni 40 kutoka BoT na kufafanua kuwa kama kuna mwanachama wake aliyehusika aandamwe yeye binafsi badala ya chama hicho kwa kuwa hakikumtuma katika uhalifu huo.

  ``Sisi tunatakwimu za namna fedha zilizochotwa na zilienda wapi...hata cheki namba tunazo hao, lazima wajitetee kwa kuwa hakuna mhalifu anayeweza kukiri kosa mahakamani,`` alisema Dk. Slaa, ambaye ndiye aliyeibua tuhuma za ufisadi na hata kuwataja kwa majina baadhi ya vigogo kuwa wanajihusisha na vitendo vya ufisadi katika Uwanja wa Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam Septemba 15, mwaka huu.

  Aidha, alisema si mara ya kwanza kwa viongozi wa CCM kukana tuhuma kwani waliwahi kukanusha kuwa hakuna wizi katika EPA.

  ``Kingunge Ngombale-Mwiru, alishawahi kukanusha kuwa hakuna wizi uliotokea katika EPA, Waziri Seif Khatib pia, sasa unatarajia Chiligati naye aseme nini?`` alihoji.

  Wakati huo huo, Dk. Slaa ameunga mkono kauli ya Jaji Kiongozi mstaafu, Amiri Manento, kuwa kesi za wizi wa mabilioni kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika BoT zinaweza kuwa kiini macho endapo Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hatapeleka ushahidi madhubuti mahakamani.

  Alisema kama aliyekuwa Gavana wa BoT hakuhojiwa na ushahidi wake kupelekwa mahakamani, serikali inaweza kushindwa kesi zote ilizopeleka mahakamani.

  Alisema yeye na Watanzania wengine hawajaridhika na idadi ndogo ya washtakiwa ambao wameshafikishwa mahakamani wakidaiwa kuhusika na ukwapuaji wa fedha za EPA.

  Alisema ni kawaida ya serikali kupeleka kesi mahakamani bila kuwa na ushahidi wa kutosha kwa kuwa mafaili mengi hupelekwa yakiwa matupu.

  ``aji Manento anachosema anakijua, ni mwanasheria, ana uzoefu wa kutosha na kama kasema hivyo basi ujue hajaridhika na taratibu zinazoendelea hivyo ameungana na kilio chetu kuwa EPA isije ikawa kiini macho,`` alisema.

  Dk. Slaa alisema lazima serikali ieleze ni nani wamiliki wa kampuni ya Kagoda na wafikishwe mahakamani kuungana na wengine 20 ambao kesi zao zimeshafunguliwa.

  Alisema mpaka sasa kuna dalili za serikali kushindwa katika kesi ilizopeleka mahakamani kwa kuwa shahidi muhimu kwenye kesi hizo (Ballali) hakuhojiwa.

  ``Balali alikuwa shahidi muhimu sana na serikali lazima itupe maelezo ya kina kwanini hawakumhoji mpaka akafa...kama hakuna ushahidi wa Balali kinachofanyika sasa ni kiini macho tu,`` alisema.

  Alisema kitakachotokea ni kwamba kesi nyingi zitafutwa kwa kuwa hakutakuwa na ushahidi wa kutosheleza kuwatia hatiani watuhumiwa.

  Jumatano iliyopita, Jaji Manento alisema kuwa Jeshi la Polisi ambalo ndilo linafanya kazi ya upelelezi kwa kushirikiana na ofisi ya DPP wanapaswa kujizatiti kwenye ushahidi ili kinachofanyika sasa kisije kikaonekana kuwa ni kiini macho.

  Alisema bila kupeleka ushahidi wa kutosha washitakiwa wote wanaweza kuachiwa huru na machoni mwa jamii ikaonekana kama mchezo wa kuigiza.

  SOURCE: Nipashe
   
Loading...