Ab-Titchaz
JF-Expert Member
- Jan 30, 2008
- 14,631
- 4,225
Dk.Slaa aandaa Mawaziri
WAKATI Chama cha Wananchi (CUF) kikitamba kunyakua zaidi ya majimbo 47 Tanzania Bara, mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, ameanza kujiandaa kuunda serikali mpya, Raia Mwema limebaini.
Habari za ndani ya Chadema zilizothibitishwa na Dk. Slaa mwenyewe, zinaeleza kwamba tayari wataalamu wa chama hicho wamekwishakufanya utafiti wa muundo wa serikali mpya itakayokuwa na baraza la mawaziri 15 na manaibu wao watano.
Akizungumza na Raia Mwema kwa simu akiwa njiani kwenda Singida jana Jumanne, Dk. Slaa alithibitisha kujiandaa kuunda serikali ndogo aliyosema itakuwa yenye ufanisi kinyume na sasa kwa kuwa sasa fedha nyingi zinapotea katika shughuli za utawala badala ya kwenda kwenye maendeleo na huduma za jamii.
"Ni kweli najiandaa kuunda serikali yenye mawaziri wachache. Hakuna idara itakayovunjwa, lakini hatuhitaji kurundika wanasiasa katika serikali yetu, badala yake watendaji katika idara za serikali na taasisi zake watapewa mamlaka ya kutosha kufanya kazi na kutakuwa na mfumo bora na makini wa uwajibikaji," alisema Dk. Slaa.
Mgombea huyo wa urais ambaye amekuwa akipanda chati kwa kasi na kuwatishia wagombea wenzake akiwamo mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema makatibu wakuu na wakurugenzi katika wizara husika ndio watatumika zaidi katika utendaji wa kila siku.
Uchunguzi wa Raia Mwema umebaini wizara husika kuwa ni pamoja na wizara ya sheria ambayo mwanasheria mkuu wa serikali ndiye atakuwa naibu wa wizara hiyo huku wizara ya elimu ndiyo pekee itakayokuwa na manaibu wawili; mmoja anayeshughulikia elimu ya juu na mwingine elimu ya msingi, sekondari na vyuo na ufundi.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Chadema ameliambia Raia Mwema kwamba, sababu kubwa ya kuwapo manaibu wawili wa elimu ni kutokana na matarajio na malengo makubwa katika sekta ya elimu ili kutekeleza ahadi za Dk. Slaa katika kutoa elimu bure na hivyo ni lazima kuwapo wasimamizi makini katika kusimamia sera za chama hicho katika sekta ya elimu.
Wizara nyingine ni wizara ya kilimo, mazingira na maendeleo vijijini; wizara ya viwanda, biashara na utalii ambayo nayo itakuwa na naibu mmoja; wizara ya ulinzi; wizara fedha na mipango itakayokuwa na naibu mmoja; wizara ya mambo ya ndani; wizara ya utamaduni, habari na michezo; wizara ya mawasiliano, sayansi na teknolojia na wizara ya serikali za mitaa na maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa habari hizo wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa imeunganishwa na wizara ya ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuwa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa maelezo kwamba hakuna umuhimu wa kuwa na wizara mbili zenye kutumia gharama kubwa za kodi ya Watanzania bila sababu ya msingi.
Mtaalamu mmoja aliyeshiriki kufanya utafiti wa uundaji wa baraza hilo jipya la Dk. Slaa, amesema wataunda wizara mpya ya nishati na raslimali za taifa ikiwa na malengo ya kuhakikisha uvunaji na utumiaji wa rasilimali za taifa unafanywa kwa umakini zaidi na kwa maslahi ya Watanzania walio wengi.
Wizara nyingine kwa mujibu wa taarifa hizo ni ya afya na wizara mpya ya kazi na mafao ya uzeeni itakayosimamia maslahi ya wafanyakazi pamoja na wastaafu kuepuka malalamiko yanayojitokeza sasa kuhusiana na haki za wastaafu na wazee kutokana na mfumo mbovu wa utendaji serikalini.
Wizara ya mwisho imefahamika kuwa ni wizara ya wizara ya ujenzi na uchukuzi ambayo itasimamia masuala yanayohusu mpango mpya wa serikali ya Dk. Slaa katika sekta ya ujenzi na uchukuzi kwa nia ya kuwawezesha zaidi Watanzania wa chini.
Akizungumzia kwa undani kuhusu jinsi serikali ya sasa inavyotumia vibaya rasilimali za Taifa, Dk. Slaa alisema Serikali inatumia zaidi ya asilimia 75 ya mapato yake kwa ajili ya matumizi ya kiutawala na sehemu ndogo inayobaki ndiyo hutumika kwenye matumizi ya maendeleo na huduma za jamii.
"Hii Serikali ya Kikwete ndiyo Serikali ghali kuliko zote katika nchi hii. Mfano mdogo tu utaona zinatumika Sh bilioni 506 kwa ajili ya kulipana posho, fedha ambazo zinaweza kulipa mishahara ya walimu 109. Kiwango hicho cha posho ni zaidi ya asilimia 59 ya mishahara wakati kiwango cha kimataifa ni asilimia 25.
"Tanzania ni nchi masikini sana duniani, lakini wakati mataifa makubwa yanabana matumizi sisi tunatumia fedha nyingi kwenye kulipana posho na gharama nyingine za anasa," anasema msomi mmoja ndani ya serikali ambaye kwa sasa yuko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, sehemu ya Mlimani.
SOURCE: RAIA MWEMA