Dr. Shoo hapa Kasema Kweli! Vijisherehe hivi

kaisa079

Member
Nov 16, 2007
20
0
MOJA ya mambo ambayo hatuwezi kulaumiwa kwamba tuna uhaba nayo bila shaka ni sherehe. Sisi kama Taifa tunazo sherehe chungu nzima.

Zipo zile sherehe ambazo zimepangwa katika kalenda ya kila mwaka. Hizo achana nazo. Kuna sherehe nyingine nyingi kote nchini ambazo kila siku utazisikia katika vyombo vya habari.

Sherehe hizo ni za kukata utepe. Utasikia kiongozi anakwenda kukata utepe wa uzinduzi wa chekechea, shule mpya ya tarafa au kata, zahanati ya kijiji, n.k. Ili mradi kila siku tupo katika mbio za uzinduzi, uwekaji mawe ya msingi, n.k.

Na katika jitihada za kutaka kuonekana kwamba tuna shughuli nzito wakati wa maandalizi ya sherehe ya ukataji utepe, kila mmoja katika asasi zinazotakiwa kutoa huduma kwa umma anakuwa 'bize'. Ofisi zinakuwa tupu. Maofisa wanahangaika huku na kule kutafuta vifaa mbalimbali ili mkubwa anapofika, aone kwamba wale ni wachapakazi kweli.

Shughuli za uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi na makandokando yake yote huvutia sana, kwa sababu zinaonesha kwamba kuna utekelezaji wa jambo fulani unafanyika au walau kuna dalili za kutekelezwa kwa ahadi hii au ile iliyotolewa na viongozi katika nyakati tofauti.

Lakini swali kubwa na la msingi la kujiuliza, ni kwamba mbona sisi ni wepesi wa kutangaza sherehe za ukataji utepe na uwekaji wa mawe ya msingi kuliko tulivyo tayari kusimamia matumizi bora ya hayo majengo yanayozinduliwa au kujengwa?

Moja ya matatizo makubwa katika nchi yetu na hili huhitaji kusimuliwa na ye yote, ni kwamba tu watelekezaji wakubwa wa majengo na miundombinu. Ni wepesi sana kushereheka, lakini ni wazito sana kutunza yale yanayotufanya tushereheke.

Ugonjwa wa utelekezaji ni mkubwa mno na hasara yake kwa Taifa hili ni kubwa mno haimithiliki. Chukua Barabara ya Shekilango ambayo sina uhakika kama imekabidhiwa tayari kwa Serikali. Wakati ujenzi ungali ukiendelea tayari dalili zote za kuharibika kwa barabara hiyo zimekwishajionesha waziwazi.

Barabara imejaa mchanga jambo ambalo ni wazi litaiharibu hata kabla haijamaliza mwaka. Aidha magari yanayopitishwa katika barabara hiyo ni zaidi ya tani 10 yanayoruhusiwa na hakuna anayejali. Kuna tatizo gani wakati shughuli ya vigelegele na nderemo imekwisha?

Tembelea Mtaa wa Yombo uliopo Temeke na utajionea dhahiri ni kwa kiasi gani sisi ni mabingwa kwa kutothamini kabisa mali yetu wenyewe. Barabara hiyo inayoutengeneza mtaa wa Yombo kwa miaka mingi, ilikuwa imeharibika ingawa kwa hakika ubovu wenyewe ulikuwa ni ugonjwa wa utelekezaji kwa sababu ni mchanga ulijaa juu ya lami.

Lakini baada ya Manispaa ya Temeke kuamua kuikarabati na kurashia tena lami upya, kilichofuatia ni kuachiwa mchanga ujae tena barabarani na matokeo yake hayako mbali. Muda si mrefu tutakuwa tena na Yombo ile ya zamani yaani mchanga uliojikita juu ya lami.

Tunatumia mabilioni ya fedha katika ujenzi wa majengo na miundombinu ambayo hatutaki kabisa kuitunza na tunaachia na kila kitu kinasambaratika mbele ya macho yetu, kiasi kwamba tunakuja kulazimika kujenga upya kwa gharama kubwa sana.

Viongozi wetu wa Manispaa ya Kinondoni hawawezi kusema, kwamba hawaioni barabara ya Kinondoni inayoanzia katika kona ya makao makuu ya benki ya Stanbic.

Kwamba barabara hiyo imejaa mchanga kiasi cha kupunguza upana wake unaoweza kutumiwa na magari si jambo jipya. Hali hiyo imekuwa hivyo kwa miaka sasa na inaelekea hakuna kiongozi anayeona umuhimu wa kuingilia kati na kuinusuru barabara hiyo kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Inasikitisha, kuona kwamba ugonjwa huu wa kutojali si tu kwamba umewaingia na kuwamaliza viongozi wetu, bali na sisi wenyewe pia tumeukubali na hatuoni kero kuishi katika mazingira ya ovyo.

Inakuwaje kituo cha mabasi cha Mwenge kiwe katika hali ya ovyo kiasi hicho wakati tunajua kwamba kuna fedha zimeingizwa chungu nzima na zinakusanywa kila uchao kwa malaki na pengine hata mamilioni ya fedha, lakini taratibu kinaachiwa kumong’onyoka hadi tutalazimika kufikia Uchaguzi Mkuu mwingine kuanza tena mradi wa ujenzi wa kituo cha Mwenge?

Mtindo wa utelekezaji wa mali ya umma ni hatari sana kwa maendeleo ya Taifa letu. Ni utelekezaji huo ndio unaotusababishia maisha yetu kuwa ya ovyo.

Soko la Kariakoo halifanyiwi matengenezo hadi Makamu wa Rais au Rais mwenyewe aamue kufanya ziara. Kwamba Meneja Mkuu na wenzake wa Kariakoo walikuwa hawajui kwamba shimoni kuna mazingira ya ovyo sana hadi afike kiongozi wa juu wa nchi ndipo aambiwe, tena na wafanyabiashara, kwamba hali ni mbaya?

Sitaki kuamini na kwa hakika itakuwa ni vigumu kuamini, kwamba viongozi wa asasi zetu hawaoni uharibifu huu mkubwa wa mali za umma unaotokana na wao kukimbilia sherehe za uzinduzi, ukataji utepe, uwekaji wa mawe ya msingi n.k. Badala ya kuhakikisha kwamba kunakuwapo na utunzaji na matumizi mazuri ya mali ili ziweze kutumiwa kwa muda mrefu zaidi na kuepusha gharama inayotokana na uharibifu wa muda mrefu.

Unapotaka kutambua kiwango chetu cha kutokujali, jiulize ni kwa nini barabara inaachiwa kuwa na mashimo ambayo hatimaye hugeuka kuwa mahandaki na tamati ni kutokuwapo kabisa kwa barabara.

Nini hasa kilichozuia kuwa na utaratibu wa kukarabati barabara kwa mfano kiasi cha ile ya Coca Cola, Mwenge, kuwa haipitiki kabisa na ikiwa ilikuwa imejengwa na kuzinduliwa kwa mbwembwe kwa kiwango cha lami? Nani aliwaambia viongozi wetu pamoja na wahandisi wasimamizi wa barabara, kwamba barabara ikishatiwa lami basi haihitaji tena kuangaliwa kwa makini kwa sababu lami haimong’onyoki?

Tabia yetu ya kukimbilia sherehe na kusahau kabisa, tena kwa makusudi, umuhimu wa ukarabati na usimamizi wa karibu katika matumizi ya miundombinu na majengo mengine yote ya umma, unatugharimu fedha nyingi ambazo tungeliweza kuzitumia katika shughuli mpya za maendeleo.

Huhitaji kuwa mchumi kutambua kwamba gharama za kusafisha barabara kwa kuondoa mchanga unaopunguza upana wake ni ndogo mno kulinganisha na gharama za kujenga barabara kunakotokana na utamaduni wa ovyo wa kutojali.

Mifano niliyoitoa katika makala hii ni ya Dar es Salaam. Lakini ukweli ni kwamba utamaduni wa utelekezaji wa miundo mbinu ni wa nchi nzima. Kuna tabia ya kutojali ambayo imejengeka miongoni mwetu na hatutaki kuzinduka na kutambua kwamba sote tunaathirika vibaya.

Moja ya mambo ambayo ni lazima kuyaangalia kwa jicho jipya ni hili la kufanya ukarabati wa kudumu katika miundo mbinu yetu kama njia ya kuhakikisha, kwamba tunajiepusha na gharama za kujenga upya.

Kama hatuzinduki na kuanza kuachana na tabia hii ambayo inatuvurugia mambo yetu, tutaendelea kuwa ni watu wa kujenga upya kila wakati jambo ambalo linatugharimu sana.

Hizi hadithi tunazokutana nazo kila kona ya nchi, kwamba jengo hili liliwahi kuwa na maji, umeme na wakati mwingine hata lifti na kwamba wakati unaambiwa hivyo vitu hivyo havipo tena, ni za kusikitisha.

Unaingia katika jengo la zaidi ya ghorofa nne ambalo kisheria linatakiwa kuwa na lifti, lakini hiyo lifti haipo na huna wa kumuuliza kwa sababu kila mmoja anasema hajui kulikoni. Lakini ukweli ni kwamba lifti ile haikukarabatiwa kama inavyotakiwa, yaani ilitelekezwa na matokeo yake ni kwamba watu wanalazimika kutwanga mguu hadi ghorofa ya saba na zaidi.

Ni wazi kwamba hatuwezi kupiga hatua ya maana kimaendeleo, kama wananchi wataendelea kukaa kimya wakati wakiona waziwazi kwamba miundombinu inaachiwa kuharibika.

Viongozi wasiojali kusimamia au wanaoshindwa kusimamia mali ya umma wanastahili kukataliwa na wananchi. Kwa walioingia madarakani kwa kura wananchi wanatakiwa kuwakataa kwa kura na wale walioteuliwa na viongozi wa juu basi wawajibishwe na hao waliowateua.

Wateuzi wana jukumu la kuwa wakali kwa waliowapatia nafasi za utendaji, kwa sababu wasipofanya hivyo wananchi watawawajibisha kupitia sanduku la kura. Hiyo ndiyo silaha ya umma na itatumiwa wakati utakapofika
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom