Dr. Rashid Idris wa Tanesco naye ana "Vijisenti" alikoficha Chenge!

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,820
287,887
Anamiliki akaunti Uingereza
Hoseah adaiwa kuvujisha taarifa

Na Saed Kubenea
Mwanahalisi

MTEULE na swahiba wa Rais Jakaya Kikwete amehusishwa na kashfa ya ununuzi wa rada inayochunguzwa na makachero wa Uingereza.

Ni Dk. Idris Rashid, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umme nchini (TANESCO) ambaye wakati wa mchakato wa ununuzi wa rada alikuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT).

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Uchunguzi wa Makosa ya Jinai – Serious Fraud Office (SFO) la Uingereza, Dk. Rashid ni mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi katika ununuzi wa rada iliyogharimu kiasi cha Sh. 40 bilioni.

SFO inachunguza ununuzi wa rada uliofanywa na serikali ya Tanzania kutoka kampuni ya BAE System-PLC ya nchini Uingereza.

Shirika hilo linadai kuwa bei ya rada ilikuwa kubwa kuliko thamani yake na kwamba BAE itakuwa ililipa mawakala kiasi kikubwa cha fedha “kulainisha” baadhi ya viongozi wa serikali ili wakubali bei hiyo.

Dk. Rashid aliteuliwa na Rais Kikwete Novemba 2006 kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO. Mwaka mmoja baadaye, Dk. Rashid aliandika barua ya kujiuzulu lakini rais alimkatalia kujiuzulu.

Uamuzi wa Dk. Rashid kujiuzulu ulitokana na kile alichoita kuamrishwa na Edward Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu, kurudisha umeme aliokuwa ameamua ukatwe, katika kiwanda cha Tanga Cement, jambo ambalo Dk. Rashid alilichukulia kuwa “uingiliaji katika kazi na udhalilishaji.”

Hata hivyo, siku mbili baada ya Dk. Rashid kuandika barua ya kujiuzulu, taarifa kutoka serikalini zilisema, Rais Kikwete aliingilia kati na kukataa barua ya Dk. Rashid ya kujiuzulu.

Badala yake, rais alisema yeyote anayetumia umeme bila kulipa ni mwizi wa umeme, hata kama mtumiaji ni ikulu au jeshi. Alisema anayetumia nishati hiyo sharti alipe na kama hakulipa, aswagwe mahakamani.

Taarifa za kuaminika zinasema Dk. Rashid anamiliki kampuni yenye akaunti nchini Uingereza na kwamba kampuni yake ilimegewa Paundi 600,000 za Uingereza (sawa na Sh. 1.32 bilioni) kutoka akaunti ya kampuni ya Andrew Chenge ambaye tayari anachunguzwa na SFO.

Taarifa za kampuni ya Siemens Plessey System (SPS) zinasema, Dk. Rashid anatajwa kuwa mratibu mkuu wa “taarifa zote kutoka serikalini na BoT.” SPS ndio walihusika kufanya majadiliano ya awali ya ununuzi wa rada hiyo kwa niaba ya Serikali, chini ya ofisa wake aliyetajwa kuwa ni Jonathan Joseph Horne.

MwanaHALISI imeona dokezo la Horne lililoeleza majukumu ya Dk. Rashid ambalo lilisomeka kwa Kiingereza, “Dk. Rashid will from now on act as coordinating point for collecting all documents (etc) from all parties in the Government of Tanzania and Bank of Tanzania.”

Mwaka 1992 hadi 1998, Dk Rashid alikuwa Gavana wa BoT. Ni wakati huo alipewa jukumu la kuwa “kiungo muhimu kwa wadau wote ndani ya serikali na BoT,” kama maelezo ya Kiingereza hapo juu yanavyoelekeza.

Akaunti ya Chenge inayochunguzwa iko katika tawi la benki ya Barclays, katika kisiwa cha Jersey wakati ile ya Dk. Rashid, imo Royal Bank of Scotland International katika kisiwa hichohicho.

Kampuni ya Chenge imefahamika kuwa ni Fronton Investment Ltd na ile ya Dk. Rashid imetajwa kuwa ni Langley Investment Ltd. Uhamishaji wa fedha umerekodiwa kufanyika 20 Septemba 1999.

SFO inadai kuwa BAE System-PLC, kampuni ya Uingereza inayotengeneza vifaa vya kijeshi, ilitoa asilimia 30 ya bei ya mauzo kwa wakala wake kwa shabaha ya, miongoni mwake, kuhonga maofisa wa serikali nchini.

Hadi kukamilika kwa mradi huo, Tanzania ilikuwa inatumia mfanyabiashara raia wa Tanzania mwenye asili ya Kiasia, Shailesh Pragji Vithlani badala ya SPS walioanzisha mchakato.

Ingawa mchakato wa ununuzi wa rada ulianza mwaka 1992, kufuatana na rekodi za SFO, mkataba ulikamilika mwaka 1999. Wakati huo Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

MwanaHALISI limefahamishwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Edward Hoseah alisaliti serikali kwa kuvujisha taarifa kwa Chenge na Dk. Rashid.

Imefahamika kwamba taarifa za SFO kutaka kuwahoji Chenge na Rashid kwa pamoja zilivujishwa na Hoseah na kuwezesha watuhumiwa kukutana kuandaa majibu kwa tuhuma. Hiyo ilikuwa baada ya mawasiliano kati ya SFO na mwanasheria Mkuu wa serikali Johnson Mwanyika ya 31 Machi mwaka huu.

Ni mkakati huo wa Chenge na Dk. Rashid unaodaiwa kuzaa maelezo kwa makachero wa SFO kuwa fedha ambazo Dk. Rashid alipokea kutoka kwa Chenge zilikuwa “mkopo wa kuendeleza biashara yake ya samani (fenicha).”

Mawasiliano kati ya SFO na Mwanyika kuhusu kuwahoji Dk. Rashid na Chenge, yalionyesha pia kuwa yatahusisha mahojiano na Shailesh Pragji Vithlani, Tanil Kurmar Chandulal Somaiya, BAE System ya London, Michael Peter Rouse, Sir Richard Harry Evans, Michael John Turner na Julia Aldridge.

Chenge alihojiwa na SFO mapema mwaka huu baada ya akaunti yake iliyoko Jersey kukutwa na fedha nyingi. Kufuatia upekuzi ofisini na nyumbani kwake na kuchukua nyaraka kadhaa, Chenge alilazimika kujiuzulu nafasi ya Waziri wa Miundombinu ili kupisha uchunguzi.

Taarifa nyingine zimesema hadi 13 Septemba 2006, akaunti ya Chenge ya kampuni ya Franton Investment Ltd, inayomilikiwa na Chenge na mkewe, ilikuwa na paundi za Uingereza 804,000 (sawa na Sh. 1.7 bilioni).

Kwa mazingira ya sasa, ama Dk. Rashid, ambaye alikuwa gavana wa BoT, afuate nyayo za Chenge na kujiuzulu au asubiri uamuzi wa rais ambao hauwezi kuwa tofauti na ule aliochukua dhidi ya Daudi Ballali.
 
Last edited by a moderator:
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom