Dr. Charles Mulokozi atiwa mbaroni kwa kutoa Vibali vya kusafirisha Tumbili 62 kwenda Albania

dubu

JF-Expert Member
Oct 18, 2011
3,500
3,481
Dk Charles Mulokozi, mkurugenzi wa wanyamapori ametiwa mbaroni na polisi kwa kutoa vibali vya kusafirisha Tumbili 62 kwenda Albania

Kikosi kazi maalumu cha kuchunguza makosa makubwa ya kihalifu kimewatia mbaroni vigogo wawili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, wakihusishwa na utoaji wa kibali cha kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Albania.

Maofisa hao ni Mkurugenzi wa Idara ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Dk Charles Mulokozi na ofisa mfawidhi wa kituo cha uwindaji wa kitalii, utalii wa picha na Sites cha jijini Arusha, Nyangabo Musika.

Kikosi hicho kinaundwa na wachunguzi kutoka Polisi, Idara ya Uhamiaji, Usalama wa Taifa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kikosi cha kupambana na ujangili nchini na Takukuru.

Wakati Dk Mulokozi anakamatwa, tayari alikuwa amesimamishwa kazi kwa agizo la Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe kwa kutoa kibali wakati Serikali ilishazuia.

Vyanzo mbalimbali vimesema jana kuwa Dk Mulokozi alikamatwa mwishoni mwa wiki na jana alisafirishwa chini ya ulinzi kwenda kituo cha polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

“Hivi tunavyozungumza, Dk Mulokozi yuko njiani anapelekwa Kia chini ya ulinzi mkali wa polisi.Nyangabo yeye tayari yuko mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama pale Kia,” kilidokeza chanzo chetu cha uhakika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alipoulizwa jana hakukanusha wala kukiri kuwa na taarifa za kukamatwa vigogo hao, lakini alisema atakuwa na mamlaka ya kuliongelea wakiingia mkoani kwake.

“Bado sijapewa hizo taarifa, lakini hata kama ningezijua nisingeweza kuzungumzia tukio la kukamatwa kwao lililofanyika mkoa mwingine. Nikikabidhiwa ndiyo naweza kusema chochote,” alisema Kamanda huyo.

Hata hivyo, Waziri Maghembe alithibitisha kukamatwa kwa vigogo hao, akisema katika tukio hilo yeyote aliyetia mkono wake lazima akamatwe na kushitakiwa.

“Ni kweli Dk Mulokozi amekamatwa na siyo yeye tu kuna ofisa mwingine pale ofisi yetu ya Arusha naye tumemkamata. Hatuna mchezo katika suala hili,” alisisitiza.

Profesa Maghembe alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa raia wa Uholanzi waliokamatwa na polisi hawakuwa na vibali halali vya kufanya biashara ya kusafirisha wanyama hai kwenda nje ya nchi kama baadhi ya watu wanavyodai.

“Hawa Waholanzi walikuwa na tourist visa (waliingia kama watalii). Halafu Watanzania waelewe mtu hawezi kupata kibali cha kusafirisha mnyama hai kabla ya kumkamata, kuhesabiwa, akakaguliwa na kupata vibali stahiki,” alisisitiza.

Raia hao wa kigeni ambao ni ndugu wa familia moja, Artem Alik Vardanyian (52) ni mkurugenzi wa mgahawa huko Uholanzi na Eduard Alik Vardanyian (44), meneja wa hoteli huko huko Uholanzi.

Hata hivyo, vyanzo vingine vimedai kuwa pamoja na kuwapo kwa vibali hivyo, lakini hapakuwapo na “release order” inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kama sheria inavyoelekeza.

Chanzo hicho kilidai wanyama hao walikuwa wasafirishwe kwa kutumia ndege ya mizigo ya kukodi ambayo ilitokea Afrika Kusini na ilikuwa iwapeleke wanyama hao Albania kupitia Nairobi nchini Kenya na Nigeria.

“Hao marubani wa hiyo ndege waliitwa pale Polisi (Kia), wakaandikisha maelezo yao kuwa walikuja kuchukua wanyama hao na wakaambiwa wao waondoke tu hakuna mnyama anaondoka,” alidokeza ofisa mmoja katika uwanja wa Kia.
 
Back
Top Bottom