DPP wetu kizuizi katika mapambano dhidi ya ufisadi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

DPP wetu kizuizi katika mapambano dhidi ya ufisadi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Apr 29, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Apr 29, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,420
  Likes Received: 81,471
  Trophy Points: 280
  DPP wetu kizuizi mapambano dhidi ya ufisadi

  M. M. Mwanakijiji

  Tanzania Daima~Sauti ya Watu

  MAPAMBANO ya ufisadi nchini sasa hivi yanakwamishwa siyo na Rais Jakaya Kikwete kama wengi wanavyotaka tuamini, bali yanakwazwa na Mwendesha Mashtaka.

  Sina wasiwasi hata kidogo kuwa kama tungekuwa na mwendesha mashtaka mzuri anayejua nguvu alizonazo za kisheria, nina uhakika baadhi ya mambo tunayoendelea kuyaimba kila kukicha, yangeisha na kusahaulika karne moja iliyopita!

  Nguvu za Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kisheria ndiye mwenye nguvu kuliko hata rais, linapokuja suala la kuwashtaki watu.

  Ana nguvu za kuchunguza jambo lolote linalohusu makosa ya kihalifu. Yaani, haihitaji hata kupewa ushahidi anaposikia kuna mtu anatuhumiwa hivi au vile, ana uwezo wa kuanzisha uchunguzu mara moja.

  Sheria inampa DPP uwezo mkubwa wa kuhakikisha kuwa sheria za nchi zetu zinafuatwa, wahalifu wanashughulikiwa na utawala wa sheria unadumishwa.

  Hadi hivi sasa, ninadai kuwa DPP wetu ameshindwa kazi hiyo na matokeo yake badala ya kuongoza, amejikuta anafuata. Nimeshaandika juu ya DPP mara kadhaa sasa, bado ninaamini kuwa yeye ndiye mtu pekee anayestahili kubebeshwa lawama za utawala wa kujichagulia sheria za kufuata!

  Mwaka 2008 Sheria ilipitishwa ambayo iliunda rasmi Idara ya Mwendesha Mashtaka ya Taifa, hivyo kujaribu kutenganisha shughuli za mwendesha mashtaka zilizokuwa zikifanyika chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ikiwa na waendesha mashtaka wengi chini ya Jeshi la Polisi.

  Sheria hiyo ambayo wengi tuliililia, ililenga hasa kuhakikisha shughuli za Mwendesha Mashtaka zinakuwa huru kutoka shughuli nyingine na kuondoa mgongano usio wa lazima kati ya wahusika mbalimbali katika mchakato wa utafutaji na upatikanaji wa haki nchini.

  Kwa mujibu wa sheria hiyo (Ibara 1:2) uwezo wa sheria hiyo unahusu mambo yote ya uendeshaji mashtaka upande wa Tanzania Bara na vilevile kuratibu na kusimamia uchunguzi wa makosa yote ya kihalifu.

  Kwa maneno mengine, linapokuja suala la uchunguzi wa makosa ya uhalifu kwa upande wa Tanzania Bara siyo Mbunge, Rais, Waziri Mkuu ama waziri mwingine yeyote anapewa wajibu huo isipokuwa ofisi hii.

  Sheria hii inasisitiza kuwa linapokuja suala la kusimamia mambo ya uchunguzi wa kihalifu, bosi wa mambo hayo ni Mkurugenzi wa Mashtaka.

  Ibara ya 4:4 ya sheria hiyo inasema wazi kuwa DPP au mtu anayepewa jukumu la kuendesha mashtaka kwa niaba yake anakuwa na kile ambacho kisheria kinaitwa locus stand yaani, anaweza kusimama na kuzungumza kwenye Mahakama yoyote nchini.

  Yaani, hata kama kesi haimhusu moja kwa moja lakini endapo kuna ulazima wa yeye kutoa maoni yake, basi anapewa nafasi hiyo.

  Ibara ya nane ya sheria hiyo inaweka kanuni kubwa tatu za utendaji kazi wa DPP (ofisi hiyo ya mashtaka) kwamba katika utendaji kazi wake kanuni hizi tatu zizingatiwe.

  Kwanza, haja ya kuhakikisha haki inatendeka, pili kuhakikisha hakuna matumizi mabaya ya mchakato wa kupata haki na tatu maslahi ya umma.

  Nguvu kubwa na madaraka yake yanawekwa pasipo utata katika ibara ya nane ambapo tunaambiwa nguvu za ofisi hiyo, sheria inasema ana uwezo wa kuanzisha mashtaka, kuendesha na kudhibiti uendashaji wa mashtaka ya kosa lolote isipokuwa yale ya kijeshi.

  Kwa maneno mengine, DPP anaweza kuanzisha mashtaka juu ya mtu yeyote (pale ambapo kuna makosa anayotuhumiwa), kuyasimamia hadi mwisho wake.

  Aidha, sheria hiyo inaeleza, DPP anao uwezo wa kutoa maagizo kwa polisi au chombo chochote cha uchunguzi kuchunguza taarifa zozote zinadokeza uhalifu na kutoa taarifa mapema.

  Ni hii nguvu ya Ibara ya 9:1(e) ndiyo inayonifanya niamini kabisa kuwa DPP wetu aidha hana ubavu wa kuhakikisha haki inapatikana au amekuwa goigoi katika kutimiza wajibu wake wa kisheria na hivyo kuwa mvunjaji wa kwanza wa sheria zetu.

  Kwa maneno mengine, hakukuwa na sababu ya Rais Kikwete kuunda ‘Timu ya uchunguzi wa EPA' kwani jukumu hilo linaangukia mikononi mwa DPP. Hata ibara ya 11 ambayo yawezekana kutumika katika kesi za EPA inasema wazi kuwa kwenye makosa ambapo watu wamenufaika na mapato ya uhalifu, basi idara hii inapaswa kutimiza wajibu wake.

  Nguvu hizi zinarudiwa tena kwenye ibara ya 16:2 ambapo pasipo utata wowote inasemwa wazi kuwa DPP anaweza kuleta mashtaka pale ambapo kuna tuhuma za uhalifu. Yaani hatakiwi kusubiri wabunge wapige kelele au Rais na Waziri Mkuu amuagize. Hizi ni nguvu alizo nazo.

  Kwanini nimeandika haya tena (nilishawahi kuandika huko nyuma). Sababu kubwa ni kwamba DPP wetu hajatumia madaraka yake ipasavyo na amekuwa akisubiri maelekezo ya wanasiasa ili afanye kazi yake. Kuna mifano mingi michache tu nitairudia hapa.

  Kwa muda mrefu tumekuwa tukitoa taarifa za wazi na nyaraka kuhusu masuala mbalimbali ya uhalifu lakini naamini kwamba, DPP wetu ni mzembe, amechoka na hana ubavu wa kufanya mambo kwa mujibu wa sheria wala kuanzisha uchunguzi wakati ushahidi wote uko wazi.

  Kama Rais Kikwete, asingeunda kile Kikosi Kazi cha Kuchunguza EPA, leo tungekuwa tunaendelea kuombea na kulalamika. Hata hivyo DPP ana uwezo na nguvu kubwa ya kuunda timu ya uchunguzi ule bila kuuliza Ikulu; hakufanya hivyo na hivyo kuthibitisha kutokufaa kwake kuongoza idara hiyo.

  Hadi leo, tunalalamika na kuweka ushahidi wa Mwananchi Gold, Deep Green Finance na wenzao lakini DPP wetu anakaa pembeni na kusubiri Rais aunde tume au Bunge lianzishe uchunguzi.

  Tuhuma za Meremeta

  Tayari kuna ushahidi wa kutosha kuwa uhalifu umefanyika ambao umesababisha upotevu mkubwa wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu kwenda kwenye mifuko ya watu wachache ambao miongoni mwao ni watu waliowahi kushika nafasi kubwa za utawala kwenye vyombo vya usalama na ulinzi. Kwa nini DPP hajaanzisha uchunguzi?

  Tuhuma za Mwananchi Gold, Deep Green Finance, Tangold

  Hizi nazo ni tuhuma nzito ambazo zimeshadokezwa mara nyingi na nyaraka, tarehe, hadi majina ya watuhumiwa yako wazi (wengine wakiendelea kushika nafasi za uongozi hadi leo hii) na jinsi gani kundi hilo liliweza kutumia nafasi zao kuchota mabilioni ya fedha za Watanzania.

  Kwa karibu miaka mitatu sasa nyimbo hizi zimeimbwa na kurudiwa kama kiitikio, DPP wetu yuko wapi? Ndugu zangu jibu ni jepesi.

  Tuhuma za Kagoda Agriculture

  Ingawa hili linaangukia kwenye sakata la EPA lakini tukilichukulia kwa upande wake peke yake naweza kusema pasipo utata wowote kuwa ni mojawapo ya mambo ya kipuuzi na kijinga kukuta utawala wa sheria nchini.

  Ni ya kipuuzi na kijinga kwa sababu tunao uwezo wote wa kulishughulikia na kulimaliza kwa sekunde chache endapo tungekuwa na DPP ambaye hagwai mbele ya watawala.

  Inashangaza kuwa licha ya nguvu zote ambazo DPP anazo hadi leo hii, najiuliza Kagoda ni kina nani? DPP anawajua wahusika na akitaka kuwaletea mashtaka anaweza lakini kwa sababu ya woga au kutokuwa na moyo wa kuthubutu amekaa pembeni na kuwaachia wanasiasa wazungushane kama wanaocheza ukuti ukuti.

  Kwa nini DPP na idara yake wanaendelea kugwaya mbele ya mafisadi wa Kagoda? Jibu ni jepesi.

  Tuhuma za manunuzi mabaya jeshini

  Mojawapo ya idara ambazo zimetajwa kuhusika na ufisadi mkubwa na matumizi mabaya ya fedha za Watanzania ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

  Kwa miaka kadhaa kundi la watu wachache wametumia usiri wa mambo yetu ya kijeshi kufanya ufisadi ambao ukiuandika tunaweza kupigiwa kelele na kina Ghasia.

  Kundi hili ambalo linajulikana limeingiza nchi kwenye mikataba mibovu, kuangiza vifaa vibovu huku wao wenyewe wakimegewa mabilioni ya shilingi ambayo wametumia kuanzisha makampuni yao.

  Makampuni ambayo baadaye yakapewa tenda kwenye mambo mbalimbali ya usalama! DPP wetu anajua haya na ushahidi anaujua upo (kwa kuanzia aangalie ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Serikali!).

  Kwanini hajaanzisha uchunguzi? Kwanini hadi leo wahusika wanakaa pembeni na wengine kuachwa kustaafu kwa furaha huku wengine wakiendelea na biashara zao na wengine wakithubutu hata kugombea nafasi za uongozi kwa tiketi ya chama tawala (kwa wasiojua chama hicho ni CCM)? Jibu ni jepesi.

  Tuhuma za ufisadi ATCL

  Kwa karibu mwaka mzima tumeandika na kudokeza juu ya ufisadi uliokubuhu kule ATCL. Tukadokeza malipo yaliyofanyika na kiasi cha pesa kilichotumiwa.

  Tukaonesha kuwa hata ndege tuliyotaka kujivunia ni mkwechwe; tukadokeza jinsi gani marubani hata wanafunzi (huko makwao), wanaingia kurusha ndege zetu.

  Tukadokeza jinsi kundi la watu wachache kule ATCL wametumia nafasi zao kujibinafsisha magari kwa kuingia mikataba ya ajabu. DPP alifanya nini? Hakuna!

  Leo hii, ati wabunge wanaulizana nini kimetokea, rais anashangaa hali imefikaje hapa na waziri mhusika anaunda tume kuchunguza ili kujua wahusika? Kama huu siyo wazimu wa watu waliosoma ni nini hiki?

  DPP muda wote huu yuko wapi? Sheria inampa nguvu ya kuingilia na kuanzisha uchunguzi wa jambo lolote pale panapodaiwa kutokea uhalifu, kwanini DPP wetu amekaa pembeni kusubiri maelekezo ya wanasiasa wakati ana nguvu zote za kufanya uchunguzi na kuleta mashtaka? Jibu ni jepesi.

  Tuhuma za wanafunzi waliotelekezwa Ukraine

  moja ya vitendo ambavyo vinabakia katika historia kama uonevu mkubwa wa serikali dhidi ya raia wake ni suala la vijana wetu karibu 30 walipotelekezwa kule Ukraine na kuachwa kule kwenye ubaridi wa Jiji la Kiev mbele ya ubalozi wa Uingereza.

  Ninatambua ndani ya moyo wangu kabisa kuwa hakuna wakati ambapo ubabe wa watumishi wachache ulivumiliwa na kuzawadiwa dhidi ya vijana wasio na mtetezi kama wakati ule.

  Nakumbuka idadi ya wabunge niliowaomba wawasimamie vijana hawa. Wabunge wote wa CCM niliozungumza nao waliogopa kwa sababu ya kuonekana wanapingana na serikali!

  Kama nilivyoandika wakati ule, nina shukrani yangu milele kwa wale wote waliojitokeza kusimama na vijana wale kwani kwa mara ya kwanza kikundi cha vijana wasio na lolote waliweza kusimama dhidi ya serikali yao!

  Kati ya mambo yote niliyoyafanya na kuyasimamia hakuna jambo linalonigusa moyoni kama ubabe ule wa Serikali ya Rais Kikwete.

  Siwezi kusahau jibu la mmoja wa watendaji wakubwa aliyenijibu kuwa yuko mezani anakula wakati vijana wetu wamelala nje ya ubalozi wa Uingereza wakililia kitu kimoja, waachwe waendelee na masomo! Sijasahau lile, na sidhani kama niko tayari kuwasamehe!

  Tulionyesha wakati ule na kwa karibu kipindi cha mwaka mzima jinsi gani Bodi ya Mikopo iliwahadaa vijana hawa na kuwachuuza ugenini kwa sababu hawakutaka kuwagawia fedha zao za ada na kushiriki katika ufisadi wa bodi hiyo.

  Tukaweka na nyaraka na hoja zikajengwa za kuonyesha jinsi gani bodi hiyo iliyokuwa chini ya wizara iliyoongozwa na Profesa ilivyokuwa inalipiza kisasi kwa vijana hawa na kuwatelekeza ugenini.

  Leo, watu wale wale tuliowapigia kelele ati wameamka na kutambua kuna matatizo bodi ya mikopo! Kama huku siyo kulala kwa dereva kwenye usukani tukuiteje huku?

  Kwa nini hadi leo DPP hajaagiza uchunguzi wa kufuatilia nini kilitokea au kuwahoji wale vijana waliorudishwa kwa maagizo ya serikali na kwa fedheha ili kujua ni nani alikuwa anahusika na kuona kama kuna mashtaka ya kuletwa mbele ya mahakama kama yakina Mramba na Yona au zaidi? Najua kwanini; jibu ni jepesi;

  Tuhuma dhidi ya Rostam

  Kati ya Watanzania ambao majina yao yanahusishwa na uvunjaji mkubwa wa sheria nchini ni jina la Mbunge wa Igunga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rostam Aziz.

  Huyu anatajwa kwenye mambo mengi na kuhusishwa na baadhi ya kesi ambazo nimezitaja hapo juu. Zaidi ya yote katika suala la Dowans wengi tunafahamu kilichosemwa kwenye Kamati Teule ya Bunge na majibu aliyoyatoa mbele ya waandishi wa habari.

  Lakini, tunafahamu maendeleo ya hivi karibuni ambapo mtu anayeonekana kwenye nyaraka za umiliki za BRELA (Suleiman Al-Adawi), anamtaja Rostam kuwa ni rafiki yake na baadhi ya vyombo vya habari vilikiri kuwa Mbunge huyo anamtambua Al-Adawi na kwamba alihusika katika kumshawishi kuleta mitambo ile ya majenereta.

  Rostam, alikana kuwajua watu wa Dowans! Leo, ushahidi wote unamhusisha na wengine katika kujaribu kuhakikisha majenereta ya Dowans yanauzwa kwa Tanzania kwa fedha zilizotengwa tangu kwenye bajeti ya mwaka jana (Angalia Mpango wa Maendeleo wa 2008/2009).

  Tulipopinga kwa sauti kali ununuzi wa mitambo ya Dowans nguvu kubwa ilitumika kujaribu kutushawishi hadi tulipowalazimisha kusalimu amri.

  Hata hivyo kitu ambacho hakijaangaliwa hadi leo ni jinsi gani kampuni ya Dowans Tanzania LTD ilianzishwa kwa makusudi huko Costa Rica ili hatimaye ipate nafasi ya kujiingiza nchini.

  Uchunguzi huru (ambao nimeuratibu mwenyewe) umeonyesha pasipo shaka kuwa kampuni ya Portek International, ambayo ilitajwa na Salva (wakati akiwa Habari News) kuwa ina hisa kwenye kampuni ya Dowans Tanzania haina hisa hizo! Kampuni hiyo inatajwa kwenye nyaraka za BRELA!

  Kampuni ya Dowans ya Costa Rica, ilianzishwa kwenye eneo huru la biashara (Free Trade Zone) haina ofisi, haina jengo na anuani inayotajwa kwenye nyaraka za BRELA ni anuani ya hilo eneo huru!

  Hata ile Dowans Holdings ambayo tuliambiwa ni ya huko Falme za Kiarabu nayo anuani yake hadi simu ni za Benki ya Canadian Royal Bank! Uchunguzi wa huko nao unaonyesha hakuna kampuni iliyoandikishwa huko.

  Katika maeneo yote hayo, Rostam anahusishwa kwa namna moja au nyingine! Kwanini DPP hadi hivi sasa hajaamua kuanzisha uchunguzi huru wa Dowans na wahusika wake?

  Kwanini DPP baada ya taarifa ya Bunge hakuanzisha uchunguzi dhidi ya Rostam? Kama uchunguzi huru ungefanywa na kuhakikisha haya tunayoyasema kuwa yana ukweli au uongo au ni uzushi au ni "chuki binafsi" au ni "ubaguzi" si Rostam angeondolewa hili wingu la ufisadi ambalo linamzunguka?

  Ninafahamu jibu lao la kitabuni "kama mna ushahidi uwasilisheni kwa vyombo husika"! Jibu hili halina msingi kwangu kwa sababu hata tukiwawekea ushahidi hadi kwenye meza zao hawawezi kufanya lolote?

  Kwani suala la DECI lilikuwaje? Watu wa usalama wa taifa waliliandikia hili kabla hata ya watu wa Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana hawajaandika ile taarifa yao kwa DCI.

  Maofisa wetu wa mitaani wa Usalama wa Taifa waliandika taarifa mapema na kutoa mapendekezo yao lakini hatua hazikuchuliwa! Tena wao waliandika kuanzia 2007!

  Sasa, wanataka tuwatafutie ushahidi, tuwaletee, tuwafafanulie na bado tutoe mapendekezo wakati wote huo wao wanafanya nini? Kula bila kulipa? DPP yuko wapi? Jibu ni jepesi!

  Si lazima mashtaka yote yaendeshwe na ofisi yake. Wengine wanaweza kujibu na kusema mambo haya yote unayaleta dhidi ya DPP mbona ni mengi hivyo? Kwamba, hawezi kufanya kazi hizo zote na kuendesha mashtaka yoyote yeye mwenyewe kwani ni mengi na mazito. Watetezi hao wanaweza kusema kuwa DPP ana majukumu mengi na kesi nyingi za kufuatilia.

  Jibu langu ni kuwa sheria iliyounda ofisi yake inatambua hilo. Ni kwa sababu hiyo sheria hiyo inasema hivi (nitainukuu) "The Director may appoint a person to be a Public Prosecutor from other departments of the Government, Local Government authority or private practice to prosecute a specified case or cases on his behalf".

  Yaani, Mkurugenzi anaweza kumteua mtu yeyote kutoka idara ya serikali kuu, serikali za mitaa au hata sekta binafsi kuendesha mashtaka ya kesi mbalimbali kwa niaba yake.

  Nguvu hii ni ya ajabu na DPP wetu hajaitumia ipasavyo. Leo hii tuna wanasheria wengi ambao wanaweza kutimiza masharti ya kisheria ya kuwa PP. Wapo kwenye vyuo vikuu, kwenye mashirika mbalimbali na idara mbalimbali.

  Na kama akitaka msaada wa kuwatambua ni wazi anaweza kuwasiliana na Chama cha Wanasheria au Mahakama Kuu ambao wamesajiliwa.

  Yaani, katika kuendesha mashtaka DPP halazimiki kutegemea waendesha mashtaka wa serikali tu (chini ya ofisi yake) au wa Polisi bali anaweza kuwaomba hata kina Issa Shivji au watu wengine ambao wanaweza kuendesha mashtaka.

  Hii ina maana gani?

  Ina maana ya kwamba kwa vile tayari ana uwezo wa kuagiza chombo kufanya uchunguzi basi anaweza pia baada ya uchunguzi huo kuteua mtu au jopo la watu kuwa waendesha mashtaka kwa niaba yake na watu hao si lazima wawe watumishi serikalini.

  Ninaamini, wanasheria wetu wanaweza kujitokeza au vyama vya sheria vya makundi mbalinbali vinaweza kujitokeza na kumtaarifu kuwa wanao watumishi ambao wako tayari kuendesha mashtaka kwa niaba ya DPP wakiteuliwa hata kama kwa kujitolea (pro bono) au kwa malipo ya mkataba. Wakifanya hivi tutaona kama DPP atawakatalia au atasema hana waendesha mashtaka wa kutosha.

  Akiamua kufanya hivi ina maana kesi mbalimbali na hasa hizi zinazohusiana na ufisadi zinaweza kuendeshwa kwa haraka na kundi la watu waliobobea katika kazi yao na hivyo kuhakikisha kuwa karibu ya 2010 kesi hizi za ufisadi zote zinakuwa zimemalizwa na Taifa lizungumzie ajenda mpya ya uchaguzi. Lakini siamini DPP wetu atafanya hivyo. Kwanini; kwa sababu jibu ni jepesi.

  Jibu Jepesi

  Ndiyo! Jibu ni jepesi. DPP wetu hana uwezo wa kusimamia utawala wa sheria nchini na kuhakikisha mashtaka yanayostahili na yanayotakiwa yanaletwa dhidi ya mtu yeyote, chombo chochote na wakati wowote ule.

  DPP wetu ni mwoga; anaogopa kuwaletea watu kashkash, anaogopa kuwaudhi wale waliomsaidia kufika alipofika. DPP wetu hana uthubutu wa kufanya kazi yake kwa kuangalia sheria na kwa kutumia nguvu alizopewa na Bunge limempa. Hawezi kuthubutu.
   
 2. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #2
  Apr 29, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Nadhani, watu wakisoma wataelewa wanapomtwisha JK lawama za watu kufikishwa mahakamani wanakosea. Wakumkomalia ni DPP. Huyu jamaa ndiyo kikwazo kikubwa cha mapambano haya kwani kama angekuwa anafanya kazi yake kama alivyoapa na kwa mujibu wa sheria leo hii tusingekuwa tunazungumza mambo mengine ambayo tunazungumza. Aidha afanye kazi yake au aamue kukaa pembeni aingie mtu mwingine mwenye ujasiri wa kufanya kazi hiyo.
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  May 1, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Ni DPP ndiye aliye kiuzizi kikubwa cha vita dhidi ya ufisadi nchini.
   
 4. jmushi1

  jmushi1 JF-Expert Member

  #4
  May 1, 2009
  Joined: Nov 2, 2007
  Messages: 17,552
  Likes Received: 1,898
  Trophy Points: 280
  Lakini kwani DPP huteuliwa na nani?
   
 5. Mlalahoi

  Mlalahoi JF-Expert Member

  #5
  May 1, 2009
  Joined: Aug 31, 2006
  Messages: 2,065
  Likes Received: 381
  Trophy Points: 180
  Mzee Mwanakijiji,JK hawezi kukwepa lawama hata chembe.Hebu tuziorodheshe lawama chache ambazo hawezi kuzikwepa.
  1.Ikiwa mtu mmoja aitwaye Mwanakijiji,ambaye hana mamlaka TAKUKURU,UWT,Polisi na vyombo vingine vya dola umeweza kubaini mapungufu ya mtendaji huyo muhimu wa serikali (DPP),how come JK ambaye pamoja na taasisi hizo ana wasaidizi lukuki ambao iwapo amejisahau wanapaswa kumkumbusha kuwa "HUYU DPP KASHINDWA KAZI" ameendelea kulala usingizi na kumwacha mzembe huyu aendelee kula mshahara wa bure?

  2.JK ndiye aliyemteua DPP.Let's assume kuwa wakati anamteua aliamini (au alijua) kuwa mteuliwa anamudu jukumu hilo.Ina maana hayo unayozungumza JK hayajui?Je bado anaendeleza imani kuwa uwezo uliopelekea kuteuliwa kwa DPP wa sasa haujatetereka?Na kama anajua kwamba ameshindwa kazi kwanini asimtimue?

  3.Japo simtetei DPP,naamini kabisa kuwa UWOGA wake unatokana na FACTS:Kwamba wahusika wakuu wa tuhuma zote hizo ni pamoja na hao waliomweka madarakani (sio kumpendekeza tu bali hata kumteua na kumwapisha).Ujasiri tunaoweza kuutegemea kutoka kwa DPP ni yeye kuwa tayari kuacha kibarua hicho...yaani ukishamweka uchi mzazi wako sharti uhame hapo.DPP akifanya kazi yake kama inavyostahili basi muda si muda urais wa JK utakuwa matatizoni.I'm not suggesting kuwa urais wa JK kuwa matatizoni ni balaa au jambo la kuepukwa (i wish ingekuwa hivyo hata leo hii) ila mie na wewe na watanzania wengi wanafahamu kuwa DPP huyu sio Kenn Starr....na itachukua miaka mingi kwa nchi kama Tanzania kuwa na DPP atakayeshinikiza impeachment ya rais

  However,DPP akiamua LIWALO NA LIWE,anaweza kabisa kufuatilia kesi hizo zote.Na naposema Liwalo na Liwe namaanisha pia kuweka rohoni roho yake rehani while ana uhakika wa asilimia 100 kuwa kibarua chake kitaota majani.Let's remember,kama waliweza kum-sarowiwa Sokoine,watashindwaje kwa DPP?

  Finally,naungana nawe mkono kwa asilimia 100.Ila mie niweke hivi:HATUNA DPP as mtu anayeitwa FELESHI au as Ofisi yenye wajibu wa kuendesha mashtaka kwa niaba ya umma.HATUNA because mtu mwenye wadhifa huo ana-exist kwa vile tu yuko hai na anashikilia cheo hicho (lakini utekelezaji wa majukumu ni sifuri) na HATUNA kwa vile ofisi ya DPP imebaki kuwa jengo tu lakini mithili ya picha ya mbwa ambayo haiwezi kubweka wala kung'ata.Hadi hapo tutakapompata Mzalendo,DPP as a person,cheo or office vitaendendelea kuwa hypothetical tu.Na ili kupata DPP Mzalendo,au ofisi ya DPP yenye kuwajibika kwa mujibu wa matarajio,sharti anayefanya uteuzi wa DPP naye awe Mzalendo!
   
 6. Mwiba

  Mwiba JF-Expert Member

  #6
  May 1, 2009
  Joined: Oct 23, 2007
  Messages: 7,606
  Likes Received: 215
  Trophy Points: 160
  Je ni vipi DPP anaweza kushtakiwa kwa kosa la kuzembea ,na ni nani aliepo juu yake ambae anaweza kumwajibisha DPP ,ikiwa kuna ushahidi wa kuzembea kuzorotesha kubabaisha na hata ikiwezeka kupokea rushwa nzito ,ijulikane tu yeye ni muendesha mashtaka basi hodi za rushwa ni lazima zitakuwa zinapigwa kwenye mlango wake.

  Inawezekana majalada ya kesi anayoyapokea yanakuwa moto sana na hawezi au hana ubavu au kama ilivyosema anakuwa mwoga wa kuyakamata na kuyafanyia kazi.

  Let him go to hell & accounted for his deafness.
   
 7. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #7
  May 1, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,420
  Likes Received: 81,471
  Trophy Points: 280
  Na Rais wa nchi
   
 8. Ndumbayeye

  Ndumbayeye JF-Expert Member

  #8
  May 1, 2009
  Joined: Jan 31, 2009
  Messages: 4,784
  Likes Received: 1,038
  Trophy Points: 280
  ukisikia tume imeundwa jua ni kutuliza kasi ya mashambulizi.
   
 9. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #9
  May 1, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Nguvu pekee aliyonayo Rais kwa DPP ni kumteua tu.. hawezi kumfukuza at will.. kama vile asivyoweza kumfukuza Jaji yoyote japo anamteua. Hivyo, kwa DPP kugwea kufanya anachojua ana uwezo wa kukifanya lawama zote zinamuangukia yeye na siyo Rais.. vinginevyo tutawalamu majaji kwa kutotimiza wajibu wao kwa sababu ya kumuogopa aliyewateua kitu ambacho sijaona kikifanyika na majaji wetu wamekuwa huru kweli (hasa Mahakama za Juu).
   
 10. Scientist

  Scientist JF-Expert Member

  #10
  May 1, 2009
  Joined: Feb 7, 2009
  Messages: 392
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Huenda DPP kwa upeo wake wa kuelewa hajui hili hivyo anaogopa kutia kitumbua chake mchanga.. Pamoja na haya yote, lazima alinde maslahi ya waliomfanya akawa alivyo sasa. Ni lazima awe lizuizi!! Huyu ndiye wa kwanza kulaumiwa wengine wafuate...
   
 11. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #11
  May 1, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Scientist.. kama DPP hajui kuwa Rais hawezi kumtimua at will, basi hafai tena zaidi. Mimi nakuambia tungekuwa na DPP ambaye licha ya kujua uwezo wake anaweza kuthubutu wala tusingekuwa hapa leo hii.
   
 12. WomanOfSubstance

  WomanOfSubstance JF-Expert Member

  #12
  May 1, 2009
  Joined: May 30, 2008
  Messages: 5,465
  Likes Received: 72
  Trophy Points: 0
  Kuteuliwa na Rais ina maana kutenda kadri ya matakwa na utashi wa aliyemteua.
  Je kuna political will katika kushughulikia kero au mambo ambayo tunategemea DPP kuyashughulikia?
  Hata pamoja na kuwa majaji wanayo security of tenure kikatiba, kule kuteuliwa na Mkuu, kunaweka ? katika independence yao.
  Haihitaji miwani kuona tatizo liko wapi na kwanini tusitegemee miujiza sana katika utendaji si wa DPP tu bali hata majaji, PCCB na kwingineko.
   
 13. Scientist

  Scientist JF-Expert Member

  #13
  May 1, 2009
  Joined: Feb 7, 2009
  Messages: 392
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Huo ndio ukweli, HAFAI! Hivi hawa watu huwa wanakumbuka nadhiri ambayo huwa wanaiweka wanapoapishwa??!! Mungu aingilie kati!
   
 14. Steve Dii

  Steve Dii JF-Expert Member

  #14
  May 1, 2009
  Joined: Jun 25, 2007
  Messages: 6,416
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  ...kwa hiyo ni bora wateuliwa kama hawa wawe wanapitishwa na chombo/taasisi fulani hivi baada ya kupendekezwa na Rais, na si kuteuliwa tu.
   
 15. Steve Dii

  Steve Dii JF-Expert Member

  #15
  May 1, 2009
  Joined: Jun 25, 2007
  Messages: 6,416
  Likes Received: 67
  Trophy Points: 145
  ...inatia kinyaa kuona jinsi viongozi wetu wasivyotekeleza viapo vyao.
  ...ni nini haswaa jamani? tamaa, kutokuelewa, dharau, unafiki, uoga, genetics... au sijui nini!!
   
 16. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #16
  May 1, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,360
  Likes Received: 6,377
  Trophy Points: 280
  Duh.. I give up.. Je Majaji wanapaswa kutenda kwa "kadri ya matakwa na utashi wa aliye(wa)mteua (Rais)"?
   
 17. Dilunga

  Dilunga JF-Expert Member

  #17
  May 1, 2009
  Joined: Apr 8, 2009
  Messages: 679
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0
  Tena?
   
 18. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #18
  May 1, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,420
  Likes Received: 81,471
  Trophy Points: 280
  Naam, hiyo itasaidia kuwapa uhuru mkubwa katika utendaji wa kazi zao za kila siku kuliko ilivyo sasa.
   
 19. Madela Wa- Madilu

  Madela Wa- Madilu JF-Expert Member

  #19
  May 1, 2009
  Joined: Mar 24, 2007
  Messages: 3,074
  Likes Received: 35
  Trophy Points: 135
  Iwapo nina sifa zote ikiwa nipamoja na hamu uwezo na NIA ya kufanya kazi, kisha rais kwa kutumia uwezo wake wa kikatiba akaniteua kuwa Jaji au DPP.Rais anastahili kubebeshwa lawama juu ya utendaji wangu mbovu na wenye kuelemea upande wa Mafisadi, Wakati katiba ya nchi haimpi uwezo Rais aliyeniteua kutengua uteuzi wangu??Nikiwa Jaji au DPP sifanyi kazi kama Kiranja wa Wilaya au Mkoa.Mimi ni Jaji, mimi ni DPP nafanya kazi chini ya sheria na kwa mamlaka ya kisheria na si vinginevyo.Simwogopi aliyeniteua, Rais, kwamba anaweza kunimwagia unga wangu pale niamuapo kinyume na mapenzi yake au maamuzi yangu yaingiliapo maslahi yake ya kisiasa. kwa sababu rais hana uwezo wa kikatiba wa kuendesha shughuli zangu za kila siku kwa Remote yake.DPP wetu ni mzembe na ana kila dalili za Kufisadiwa au ni mshiriki katika karamu chafu ya Mafisadi au mwenyewe ni Fisadi.DPP huyu ni lazima tumuwashie moto wake mwenyewe kama DPP juu ya kiti chake cha enzi ili apate joto makalioni na kufungua kanywa lake kufanya kazi tulomtuma.DPP wetu ni mchovu au hajui kama ana Rungu mkononi au ni Puppet wa Mafisadi.
   
 20. WomanOfSubstance

  WomanOfSubstance JF-Expert Member

  #20
  May 1, 2009
  Joined: May 30, 2008
  Messages: 5,465
  Likes Received: 72
  Trophy Points: 0
  Appointing authority matters kama kweli tunataka mabadiliko na siyo business as usual.
  Ndo ukweli wa kinachotendeka.
  Ideal situation ( kutenda kufuatana na viapo na matakwa/matarajio ya kazi) na hali halisi kwa maana kinachotendeka katika uhalisia wake NI VITU VIWILI TOFAUTI.( DE FACTO AND DE JURE)
  Kwani watu wanapoapa "nitafanya kadha kadha kadha.." does it really follow kuwa ni kweli wanatenda kama walivyoapa.
  ( this is my observation. Wengine mnaweza kuwa na mawazo /maoni tofauti)
   
Loading...