Don't Jugde a book by its cover. Read and learn

EINSTEIN112

JF-Expert Member
Oct 26, 2018
21,713
35,518
Ndio kwanza alikuwa ametoka kuhamia hapo hivi karibuni. Hakuwa akiwajua majirani zake.

Ilikuwa ni sehemu yenye nyumba nne zinazofanana. Wengi huziita kota.

Nyumba hizo zilikuwa ni za vyumba vitatu, sebule na vyoo viwili vya ndani. Nyumba mbili walikuwa wakiishi wanaume mabachela na nyingine moja ilikuwa ikiishi familia. Yeye alihamia kwenye hiyo nyingine.

Siku ya pili tu baada ya kuhamia hapo, alionekana akiwa nje ya Nyumba aliyohamia akihangaika kukoleza moto wa jiko la mkaa.

Alikuwa akitumia baadhi ya mbinu kuwasha moto kwani hakuwa na mafuta ya taa. Baada ya muda kidogo alifanikiwa kukoleza moto na kupika chakula chake.

Kwakuwa alikuwa yuko peke yake na ameboreka, akaamua kuanza kufanya usafi wa nje ya nyumba aliyohamia kwani ilikuwa chafu mno kutokana na kutokukaliwa kwa muda mrefu.

Akajifunga kitenge chake na kuanza kukwetua nyasi na kufagia eneo la kuzunguka nyumba aliyohamia. Baada ya muda mchache eneo la nyumba likaonekana ni safi na la kuvutia.

Kwakuwa bado alikuwa na muda, akajifikiria, "Muda bado ninao Kwanini nisifue nguo zangu chafu na kusafisha makapeti?"

Hivyo, akakusanya kapeti, vyombo vyake vilivyopigwa na vumbi, nguo chafu na ndoo zote na kutoka nazo nje kwa ajili ya kuzifanyia usafi.

Muda huo maji ndani ya nyumba aliyohamia yakawa yamekatika. Akatizama mbele kidogo na pale alipohamia akaona kuna watu wanachota maji. Hivyo akachukua ndoo zake na kwenda kuchota.

Akifahamua kabisa mikono yake haina nguvu ya kubeba Ndoo ya Lita 20, akamuomba mwanamke mwingine aliyekuwepo pale awe anamtwisha kichwani hata akafanikiwa kujaza jaba lake ambapo maji yalitosha kufanyia usafi vitu vyote alivyovitoa nje.

Muda wote huo akifanya kazi zote hakujua kwamba moja ya wale Mabachela anayeishi nyumba ya jirani na yake alikuwa akimtazama na kumtathimini.

Yule mwanaume alikuwa akishaangaa kuona mwanamke mrembo, anayeishi mwenyewe akipika kwa kutumia jiko la mkaa alilowasha kwa njia ya Nailoni, kukwatua nyasi zilizozunguka nyumba, kufua nguo nyingi, kubeba maji kichwani na kazi nyinginezo nyingi.

Nafsini mwake yule mwanaume akafikiri hivi, "Huyu ndiye Wife Material, hakika huyu ndio mwanamke wa kuoa". Yule mwanaume alitamani sana aongee na yule dada. Kwa siku chache mbele, hakuweza kuongea nae kwakuwa dada alikuwa bize mno na kazi zake.

Lakini baada ya wiki chache alipata nafasi ya kuongea nae.

Ilikuwa ni Jumamosi moja tulivu, majira ya saa kumi jioni, dada alikiwa amekaa pembeni ya mlango wa nyumbani alipohamia akibonyeza bonyeza simu yake.

Yule jirani yake alijisogeza na kumsalimia. Baada ya kutambulishana na kuongea ya hapa na pale, yule mwanaume akataka kwenda kwenye point moja kwa moja aliyokuwa na shauku nayo.

"Nimeshangaa dada mrembo kama wewe umewezaje kufanya kazi zote ulizokuwa unafanya bila msaada wowote ndani ya siku moja; Kupika kwa Mkaa, kusafisha eneo, kuchota maji, kufua nguo zote zile na mapazia kwa mikono yako, naona umefunzwa vizuri sana. Unafaa kuwa mke wa mtu. Wewe ni wife material. Sio kama hawa wanawake wengine ambao wao wanajali zaidi kucha zao ndefu zisiharibike au nywele za bandia walizoweka kichwani, hawawezi kufanya kazi kama unazozifanya wewe...amebahatika mwanaume atakayekuoa wewe."

Yule dada alikuwa ameshaambiwa na wengi sana hayo maneno hapo kabla, hivyo akafikiri kwamba, atumie muda huo kumuelimisha mwanaume yule nini maana ya mke mwema au Wife material.

Kwanza akamkaribisha akae ili amuelezee vizuri. Baada ya Mwanaume kukaa, dada akaanza kumuelezea;

"Kwanza kaka nikukosoe, umenijaji vibaya, ulivyoniona nahangaika kuwasha jiko la mkaa ni kwa sababu jiko langu la gesi mpira wake umeharibika gesi inavuja, hivyo wakati nasubiri kwenda kuubadilisha nikawa naona nitumie jiko la mkaa, sipendi kabisa kutumia mkaa lakini sikuwa na namna. Lakini kwa kuwa nimeshanunua mpira wa gesi hutaniona natumia tena jiko la mkaa. Mara chache mno nitalitumia."

"Oh, kuhusu kusafisha eneo la nje, ninaye dada wa kazi sema kabla sijahamia hapa nilimruhusu aende kwao akasalimie kwanza nyumbani kwao kwani hajaenda kwao muda mrefu sana. Mara atakaporudi ndiye atakayekuwa akifanya usafi."

"Mimi huwa nakuwa bize sana kazini, ni hizi siku chache nimepewa 'off' kazini ndio maana unaniona nipo nipo, hivyo huwa sina hata muda wa kufagia uwanja kila siku."

.....Kuhusu kufua nguo? Navyo ni hivyo hivyo tu, kwamba kwa sababu dada wangu wa kazi hayupo, akiwepo ndiye hunisaidia kufua nguo. Mimi mara chache sana napopata muda ndio hufua.

....Sijasahau kuhusu kubeba maji kichwani, ah! Mbona jambo la kawaida tu, ni kwamba siwezi kubeba ndoo ya maji ya lita 20 mkononi ndio maana nikaomba kutwishwa kichwani. Vinginevyo nachukia mno kazi za aina hiyo.

.....Hata katika Ndoa yangu, hizo kazi nyingine afanye dada wa kazi, mimi labda kama ninao muda nitafua nguo za mume wangu na usafi ndani kwetu, kazi nyingine anaweza kufanya mtu mwingine!

Kwahiyo naweza kukwambia kwamba, mimi siyo yule Wife material au mke mwema unayemfikiria kichwani mwako. Si ndio?"

Yule mwanaume akashangaa kweli mwanamke kuzungumza vile mbele yake. Mwanamke akaona haitoshi akamuongezea somo zaidi...

Angalia kaka;

"Umefanya kosa kubwa sana kumjaji mwanamke kama wife material kwa kuangalia uwezo wake wa kufanya kazi nyingi. Sio wanawake wote wanaofanya kazi hizo za mikono ni wife material...

....Baadhi ya wanawake ambao ni wa huko vijijini kabisa wanafanya kazi kama punda lakini sio wake wema, wanaume zao hawafurahii ndoa. Kwani kaka, wanaume wangapi ambao walienda kuoa vijijini huko walivyowaleta wake zao Mjini wakabadilika na kuwa pasua kichwa?

....Kaka, kinachomfanya mwanamke awe wife material ni mtazamo wake kuhusu ndoa, na hakuna njia yoyote unaweza ukajaji mtazamo wa mtu kwa kukuangalia namna anavyofanya kazi za mikono kwa bidii.
....Mama zetu ndoa zao zinadumu kwa sababu ya mtazamo wao juu ya Ndoa, kwao ndoa ni sehemu ya Heshima, wanao mtazamo mpana sana juu ya Ndoa kwao Ndoa sio uchapakazi pekee bali kukibali kuwa ameolewa na yupo chini ya Mwanaume, amtunzaje mwanaume wake ili amfurahie

....Nyie wanaume wengi mmeoa wanawake ambao sio sahihi kwa sababu ya hako kamsemo kenu ka 'wife material' kisa anapika kila akija kwako, anaosha vyombo, anakufulia nguo na kufanya usafi.

Lakini mnasahau kutazama ni nini mtazamo wa mwanamke kuhusiana na ndoa. Ndoa sio kufua nguo, kupika kwa jiko la mkaa au kukwetua nyasi nje ya nyumba. Ndoa ni zaidi ya hayo mambo. Mke mwema ni ile asili ya nafsi yake ya utambuzi juu ya mtazamo wa Ndoa.

Kaka, unapotaka kuoa tizama sana mtazamo au 'attitude' ya huyo mwanamke kuhusiana na ndoa. Mwanamke mwenye mtazamo mzuri wa ndoa hayo mengine yote anafundishika tu hata kama hayawezi.

Vyote ulivyoniona nikivifanya, mwanamke mwenye mtazamo mzuri na ndoa yake anaweza akafanya au asifanye lakini bado akawa mke bora. Lakini ukimpata mwanamke kisa anafanya kazi za mikono kwa bidii huku 'attitude' yake ni mbovu nakuhakikishia hutaifurahia hiyo ndoa yako.

Utapata mwanamke anaefanya vyote hivyo lakini mwenye mdomo mbovu anayetukana hovyo, ambaye hana utii na hakujali vilevile.

Kwanini usifikirie wife material ni mtu ambaye mnaweza mkakaa pamoja mkaandika business plan, mwanamke ambaye atasimamia biashara ambayo utamuamini nayo. Kwanini mke mwema asiwe yule ambaye atakuombea wewe na familia kiujumla mpaka mbingu ifunguke??

Nimemaliza kaka, huo ndio mtazamo wangu kuhusu Mke mwema.

Baada ya dada kumueleza hayo, akavuta pochi yake, akatoa 'business card' yake na kumpa yule kaka.

Business Card ilisomeka hivi "Mrs. Batuli Mihayo" - Meneja Uwekezaji, Mihayo Investment Co. Ltd!

Mwanaume akaaga na kuondoka huku akiwa amepata mtazamo mpya juu ya nini haswa ya Wife material...kwamba asitazame uchapaji kazi pekee, bali 'attitude' ya mtu katika suala zima la ndoa.

By: Tweve Hezron
FB_IMG_1560878157412.jpeg
 
Back
Top Bottom