FikraPevu
JF-Expert Member
- Jan 2, 2010
- 304
- 236
GRACE Machidya, mkazi wa Kijiji cha Malolo katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, anahangaika kutafuta usafiri wa bodaboda ili impeleke katika zahanati ya Al Jazeera iliyoko Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo katika Mkoa wa Iringa, umbali wa takriban kilometa 25 kutoka kijijini hapo, kumwahisha mwanaye wa miaka miwili aliye mgonjwa.
Mwanaye huyo ana homa kali na pia anaharisha na msaada ambao alitarajia kuupata katika zahanati ya Kijiji cha Malolo hapo baada ya kukuta imefungwa kwa siku ya tatu sasa kutokana na ofisa afya kusafiri.
“Ningejua ningekwenda tu moja kwa moja, kwa sababu tumezowea kutibiwa nje ya kijiji, zahanati gani kila siku imefungwa hakuna huduma?” anasema kwa masikitiko.
Lakini anaieleza FikraPevu | JamiiForums' News Site kwamba, hata kama zahanati hiyo ingekuwa wazi, huenda mwanaye asingeweza kupata huduma kwa sababu hata dawa za malaria tu, ugonjwa unaoua watoto wengi nchini Tanzania, ni shida kupatikana.
Hawezi kutumia usafiri wa gari kwa sababu huduma hiyo haipo, hivyo njia pekee ni kutafuta bodaboda ambayo ataikodi kwa Shs. 10,000 ili imfikishe huko zahanati.
"Hii ni mara ya pili nakuja hapa, mara ya kwanza nilikuja wiki tatu zilizopita, zahanati ilikuwa imefungwa ambapo niliambiwa ofisa afya alikuwa amefuata dawa wilayani, mjini Mpwapwa, sikupata huduma nikalazimika kwenda Ruaha Mbuyuni. Leo nimeambiwa kwamba amepeleka ripoti ya utendaji huko Halmashauri,” anasema.
Hata hivyo, anasema ni gharama kubwa kwenda Ruaha, kwani si kila mtu atakayekuwa na uwezo wa kukodi bodaboda kwa Shs. 20,000 kwa maana ya kwenda na kurudi, achilia mbali uhakika na usalama wa usafiri huo ulivyo, hasa unapokuwa na mgonjwa mahtuti.
Ikiwa mpakani kabisa mwa mikoa ya Dodoma, Iringa na Morogoro, zahanati hiyo ya Malolo ndiyo pekee kwa wananchi wa kijiji hicho chenye wakazi 2,600 kutoka katika vitongoji sita, na iko umbali wa kilometa 155 kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, ambapo siyo tu usafiri hakuna kutoka hapo, bali njia yenyewe imejaa makorongo pamoja na mawe yakiambatana na milima.
FikraPevu ilishuhudia zahanati hiyo ikiwa imefungwa, ambapo baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Malolo walisema, hiyo ilikuwa siku ya tatu tangu ofisa afya, Elias Mlwande, aliposafiri.
“Hapa ni kawaida, wakati mwingine inaweza kufungwa hadi wiki mbili, tumeshazowea kwenda kutibiwa huko Morogoro na Iringa ambako ni karibu na kuna usafiri na huduma za uhakika kuliko hapa kijijini au kwenda Mpwapwa,” anasema Julius Mapalilo, mkazi wa kijiji hicho.
Mapalilo anasema, wakati mwingine hulazimika kuvuka mto kwenda Kijiji cha Malolo ya wilayani Kilosa ama kwenda zahanati ya Al Jazeera Ruaha Mbuyuni au Hospitali ya Misheni ya Mtandika wilayani Kilolo mkoani Iringa.
“Siyo ajabu, tunakwenda pia Hospitali ya Misheni Ilula au Hospitali ya Mtakatifu Kizito ya Mikumi, ambayo ni ya misheni pia. Huko kuna huduma nzuri na usafiri ni wa uhakika,” anaongeza Mapalilo.
Uchunguzi wa FikraPevu umebaini pia kwamba, ni vigumu kufanya kazi katika kijiji hicho kutokana na changamoto ya miundombinu, hususan usafiri, licha ya kwamba kama kuna mgonjwa mahututi gari la wagonjwa linaweza kuitwa kutoka Mpwapwa.
Hakuna maduka ya dawa ya binafsi kijijini hapo na mtu pekee anayehudumu kwenye zahanati ni ofisa afya, ambaye kwa sasa ni Bwana Mlwande.
Bosco Paulo Mwaluga, Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ambaye pia ndiye mtendaji wa Kijiji cha Malolo, anasema zahanati hiyo haina mtumishi mwingine zaidi ya ofisa afya.
"Tunajua kwamba mazingira ni magumu ya kufanyia kazi. Licha ya miundombinu ya mawasiliano ukiwemo usafiri, lakini pia kuna uhaba mkubwa wa dawa," anasema Mwaluga, ambaye anathibitisha kwamba ofisa afya huyo ana siku ya tatu tangu alipoondoka kwenda Halmashauri Mpwapwa kupeleka ripoti ya kila mwezi.
Mwaluga anasema, amekuwa akipokea taarifa ya bwana mganga kila anapotuma orodha ya dawa na vifaa tiba vinavyohitajika kutoka ofisi ya afya ya wilaya, lakini mara nyingi dawa hizo huchelewa na wakati mwingine si zote zinazoombwa ambazo hupelekwa.
"Hili ni tatizo sugu hasa kwa watoto ambao, kwa mujibu wa ripoti ya ofisa afya, ndio wanaongoza kwenye orodha ya wagonjwa,” anasema ofisa mtendaji huyo.
Anaeleza kwamba, kutokana na uhaba wa watumishi wa afya, zahanati hiyo hufungwa hata kwa wiki mbili ikitokea bwana mganga anahudhuria mafunzo au hata akipatwa na dharura binafsi.
Kusoma zaidi, tembelea => Dodoma: Zahanati hufungwa hadi wiki mbili kila wakati mganga anaposafiri