TandaleOne
JF-Expert Member
- Sep 4, 2010
- 1,644
- 709
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) katika mgogoro wa Libya, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete leo amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya nje wa Italy Dk. Mario Giro, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya mazungumzo maalum.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo, Msaidizi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Suleyman Mwenda alisema, Dk. Kikwete amekuwa na mahusiano ya kirafiki ya muda mrefu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italy Dk. Mario Giro, Hivyo Naibu Waziri huyo amefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya kumjulia hali kama rafiki yake wa muda mrefu.
"Pamoja na kuja kumsalimia kama rafiki wa siku nyingi, lakini lengo hasa la Naibu waziri huyo ni kutaka maelezo juu ya suala la Libya'' alisema Mwenda na kuongeza "Kama mnavyofahamu kuwa Dk. Kikwete ameteuliwa na Jumuiya ya Afrika (AU) kuwa mwakilishi katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Libya.
Alisema, Italy inalipa umuhimu wa kipekee suala la Libya kutokana na kwamba ni nchi jirani hivyo inayo maslahi mapana na ya karibu juu ya suala la amani ya Libya, Dk. Giro ameiwakilisha nchi yake katika kujua hatua ya usuluhishi na hatma ya mgogoro wa Libya.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo aliambatana na Balozi wa Italy hapa nchini, Luigi Scotto pamoja na Dk. Raffaele De Lutio, Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa wa Italy.