Dk Slaa apewa onyo kali

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa pamoja na viongozi wenzake wameonywa vikali kutojibu lolote kuhusiana na ujumbe mfupi (SMS) wa simu, ulioeleza mpango wa kumuua Zitto Kabwe.

Onyo hilo limetolewa na mshauri wa chama hicho, Mabere Nyaucho Marando ambaye ameliambia gazeti hili katika mahojiano maalum kuwa amewashauri, Dk.Slaa na viongozi wengine wa ngazi za juu kuchukua tahadhari kubwa kuhusu ujumbe huo uliosambaa kama moto unaotaja mpango wa mauaji ya Zitto.

“Nimewashauri kwamba huu ni mpango wa taasisi moja ambayo haikitakii mema Chadema. Wameandaa huu ujumbe kwa lengo la kukisambaratisha chama ili kisifike mwaka 2015 kikiwa na nguvu,” alisema Marando.
Aliongeza kuwa amewaambia viongozi wa Chadema kwamba wasithubutu kumfukuza Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini katika chama kwa kuwa mbinu zinazotumika kufanikisha mpango wa kukisambaratisha chama, hilo la mbunge huyo nalo limo.

“Unaweza kujua kuwa huu ni mpango wa chombo maalum chenye nia mbaya na chama kwa manufaa ya chama fulani. Kwa kuusoma ujumbe wenyewe, mtu mwenye akili timamu kama kweli mpango huo ulikuwepo, asingeweza kuandika ulivyoandikwa tena kwa kutaja kuwa auawe na majina ya watu yakatajwa,” alisema Marando ambaye ni wakili na mtaalamu wa mambo ya Usalama wa Taifa kutokana na kufanya kazi katika idara hiyo kabla ya kufukuzwa kazi miaka ya 1980.

Alisema amewakumbusha viongozi wa Chadema jinsi Chama Cha NCCR-Mageuzi alichokuwa akikiongoza kwa mafanikio makubwa kilivyosambaratishwa kwa kupandikizwa migogoro isiyokuwa na kichwa wala miguu ambapo kiligawanyika makundi mawili.

“Nimewaonya na nimewaambia na nawaambia wanachama wote na wapenda demokrasia kuwa, waliotengeneza ujumbe ule wamekusudia Chadema kisambaratike na kisifike mwaka 2015 kutokana na mafanikio yaliooneshwa baada ya uchaguzi mkuu na kuvuna wabunge wengi,” alisema Marando.

Ushauri wa Marando umeonekana kuzingatiwa kwa kuwa hakuna kiongozi yeyote wa Chadema ambaye yupo tayari kuzungumzia ujumbe huo wa maneno kwa njia ya simu.

Wakati hayo yakifanyika, bundi bado ameking’ang’ania chama hicho kwani habari zaidi zinasema Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana mwishoni mwa wiki iliyopita, imemteua Profesa Mwesiga Baregu kuongoza kamati maalum ya watu wanne ya kuleta amani ndani ya chama.

Profesa Baregu alipoulizwa kwa njia ya simu alikiri kuteuliwa kuongoza kamati hiyo. “Ndiyo, pamoja na mambo mengine, tumepewa jukumu la kuhakikisha amani na utulivu vinakuwepo ndani ya chama,” alisema Baregu.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Shida Salum ambaye ni mama yake Zitto, Kitila Mkumbo ambaye ni katibu na mjumbe mmoja aliyejulikana kwa jina moja tu la Shilungushela.
Wiki iliyopita ulisambazwa ujumbe kupitia simu za mkononi ukieleza mpango wa kumuua Zitto huku kukitajwa majina ya viongozi wa Chadema na gazeti hili lilifanikiwa kuuona.
Zitto, ambaye alikuwa akihudhuria mkutano wa kichama mjini Bagamoyo, aliugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam ambako madaktari walisema alikuwa na tatizo la kula chakula kichafu (contaminated food).

Madaktari hao walisema alikuwa akisumbuliwa na ‘Gastro enteritis’ ambayo Kiswahili tunaweza kusema ni mchafuko wa tumbo japokuwa Zitto alikuwa na imani kuwa alikuwa amekula sumu iliyokuwa kwenye chakula.
 
Back
Top Bottom