Dk Slaa Aleta Kizaazaa!

Pdidy

JF-Expert Member
Nov 22, 2007
50,955
22,127
Habari zaidi!
Dk. Slaa azua kizaazaa
John Mhala, Arusha
Daily News; SUNDAY,July 13, 2008 @06:01


Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo ya Karatu, Dennis Shayo amemwomba Jaji Kiongozi kuingilia ugomvi aliosema upo kati yake na Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Wilbroad Slaa.

Kwa mujibu wa hakimu huyo ambaye amepewa uhamisho kwenda Mahakama ya chini wilayani humu, amelalamika kuwa Mbunge huyo anamchafua katika majukwaa ya siasa kwa madai mbalimbali.

Shayo alimwambia Jaji Kiongozi aliyekuwa ziarani Karatu wiki hii kuwa Dk. Slaa anamwongelea hadi bungeni Dodoma akisema kuwa hamtaki hakimu wa jimbo lake, kitendo alichosema ni cha kumharibia jina lake wakati yeye anatenda haki.

"Mimi najua kuwa ananionea wivu kutokana na akili zangu za kutafuta mali, kwa kweli nina baa na usafiri ila sijapata kutokana na rushwa mahakamani, bali nachukua mikopo kama mahakimu tunavyoruhusiwa," alisema Shayo.

Alidai kwamba Mbunge huyo amekuwa akimsumbua kwa ajili ya kutaka apendelee kesi anavyotaka lakini hakutoa mfano wa kesi hizo. Akijibu malalamiko hayo Jaji Kiongozi alisema mtumishi wa Mahakama asichukuliwe hatua za kuhamishwa na kupelekwa sehemu zingine bila kupewa nafasi ya kujieleza.

Hata hivyo alisema kuwa matatizo mengine mahakimu wanajisababishia wenyewe kutokana na kuendesha biashara kama za baa na daladala. Akizungumza na gazeti hili kutoka Dodoma Dk. Slaa, alikiri kutomtaka hakimu huyo katika jimbo lake. "Nasema hivi siyo namsingizia, bali nina ushahidi kamili na anayetaka nitampa, ili ahakikishe mwenyewe siyo majungu ni ukweli mtupu," alisema Dk. Slaa.

"Ili kuhakikisha hili hakimu huyu anamiliki baa tatu za kifahari. Hizi fedha anatoa wapi? Nina ushahidi baa hizi zinatumika kupokea rushwa … ni lazima niseme," alisisitiza Dk. Slaa. Wakati huohuo, baadhi ya walinzi wanafanya kazi za ukarani wa Mahakama mkoani Arusha bila kupata mafunzo yoyote, Jaji Kiongozi Salim Massati ameelezwa.

Jaji huyo ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi mkoani humu wiki hii aliambiwa kwamba ucheleweshaji wa utoaji hukumu katika Mahakama nyingi nchini hasa za Mwanzo, unatokana na ukosefu wa makarani na kusababisha walinzi wa Mahakama kufanyishwa kazi hizo.

Walinzi wa Mahakama wilayani Ngorongoro walimweleza Jaji Massati kuwa wanafanya kazi za ziada za ukarani, wakati wao ni walinzi lakini wanalipwa mishahara isiyoendana na kazi hizo. Kutokana na hali hiyo waliomba kupatiwa elimu maalumu waweze kufanya kazi za ukarani kwa kiwango cha kuridhisha na ufahamu.
 
Back
Top Bottom