Dk. Sheni apangua uzushi ni kuhusu Maendeleo Pemba iko nyumba kimaendeleo zaidi ya Zanzibar | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dk. Sheni apangua uzushi ni kuhusu Maendeleo Pemba iko nyumba kimaendeleo zaidi ya Zanzibar

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Nov 5, 2011.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Nov 5, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145

  THURSDAY, 03 NOVEMBER 2011 19:03 NEWSROOM

  [​IMG]

  * Ni kuhusu maendeleo Pemba

  * Asema hajavunjiwa heshima

  * Atoboa siri juu ya bei ya mikate

  HATIMAYE Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, amevunja ukimya na kupangua uzushi uliokuwa ukitolewa dhidi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ). Miongoni mwa uzushi huo, ni madai kuwa Pemba iko nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na Unguja, amejivunjia hadhi na kuwa sawa na waziri asiye na wizara maalumu kwa kukubali kuapishwa kwenye Baraza la Mawaziri, na Zanzibar haijashiriki kwenye muswada wa mchakato wa kupata katiba mpya. Dk. Sheni alivunja ukimya jana alipozungumza na wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, Ikulu, mjini Zanzibar.


  Baada ya kutoa taarifa ya kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Dk. Sheni alijibu maswali yote aliyoulizwa katika mkutano huo, uliodumu kwa takriban saa tano bila kupumzika.


  Alisema madai kuwa Pemba iko nyuma kimaendeleo hayana ukweli, kwani katika baadhi ya mambo iko mbele kuliko Unguja na kwamba, tangu kufanyika kwa Mapinduzi mwaka 1964, programu zote za maendeleo zilizotekelezwa Unguja zimetekelezwa pia Pemba.

  Dk. Sheni alitoa mfano wa sekta ya afya, ambayo huduma zake ni bora zaidi Pemba kuliko Unguja, kwa kuwa mtu akiwa Pemba hawezi kutembea zaidi ya kilomita 3.5 bila kupata huduma tofauti na Unguja ambako wastani ni kilomita hadi tano.


  "Natoa nafasi kama kuna mtu anapinga kuhusu hili asimame na kuni-challenge (kunipinga)," alisema na kutoa nafasi kwa waandishi wenye kupingana na hoja hiyo kumpinga hadharani. Hakuna aliyepinga.


  Akizungumzia kuapishwa kwake kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri, Dk. Sheni alisema kitendo hicho hakina madhara na hakijamvunjia heshima kama baadhi ya watu wanavyotaka ionekane.


  "Sijavunjiwa heshima wala hadhi kwa kuapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri," alisema na kufafanua kuwa, hata wakati wa kuapa alianza kwa kusema: "Nikiwa Rais wa Zanzibar…"


  Alisema hata kwenye vikao vya baraza la mawaziri sehemu anayokaa imeandikwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, hivyo kuapa kwake hakumuondolei hadhi, badala yake kunamsaidia kwa kuwa yanapozungumzwa mambo ya Zanzibar anakuwepo na kutoa mchango wake.


  Dk. Sheni alisema kuapa kuingia kwenye baraza la mawaziri kunatokana na mahitaji ya kikatiba, na hata mtangulizi wake Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume aliapa mara mbili. Alisema anashangazwa chokochoko zinatoka wapi kuhusu suala hilo.


  Alisema alichelewa kuapa kwa sababu ya mwingiliano wa kazi, ambapo kuapishwa kwake kulitegemea kazi zake, Jaji Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


  Dk. Sheni alisema kuapishwa kwake kuwa mjumbe wa baraza la mawaziri hakujamshusha cheo au kumfanya awe sawa na waziri na kwamba, kinachoenezwa kinyume cha mahitaji ya katiba ni porojo za mitaani.


  Kuhusu muswada wa katiba mpya, alisema SMZ ilishirikishwa na ilishiriki kikamilifu katika muswada huo unaotarajiwa kufikishwa bungeni hivi karibuni.


  Rais Dk. Sheni alisema alikutana na Rais Jakaya Kikwete na baada ya kujadiliana alimueleza angependa hadi ifikapo mwaka 2014, wakati wa sherehe za miaka 50 ya Muungano, katiba mpya iwe imepatikana.


  "Huu ni muswada wetu wote, marais tulikutana, mabaraza ya mawaziri yalikutana, wanasheria walikutana na sasa unafuata utaratibu mwingine wa kupelekwa bungeni. Huu ni katika kuweka mchakato wa namna gani ya kupata katiba mpya na si wa mabadiliko ya katiba yenyewe," alifafanua na kukanusha kuwa hautakiwi Zanzibar.


  Aliongeza: "Kwamba Zanzibar watu hawataki, tusiwalishe watu maneno, waacheni Wazanzibari wenyewe waseme… utafika mahali wananchi wataongea na kuamua."


  Dk. Sheni alisema kwa sasa Zanzibar imefika mahali ambapo watu hawapaswi kulaumiana na kupiga kelele kwenye majukwaa ya siasa, bali ni wakati wa kujenga nchi na kama kuna kasoro zitolewe kwa misingi ya kuleta maendeleo.


  Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja SMZ imepata mafanikio na kukumbana na baadhi ya changamoto, ambazo nyingine zinatokana na utashi wa wafanyabiashara wenyewe bila kuzingatia hali halisi.


  Dk. Sheni alitoboa siri kuwa siku moja akiwa kwenye mkutano wa Baraza la Pamoja la Biashara Zanzibar, saa sita usiku kwenye hoteli ya Bwawani, alipata taarifa kuwa mikate inataka kupandishwa bei.


  Alisema kwa kuwa alikuwa na wafanyabiashara hao kwenye mkutano, aliwahoji ni kwa nini wanataka kupandisha bei, ambapo walimjibu ni kutokana na shilingi kushuka thamani kulinganisha na dola ya Marekani.


  "Walinishangaza kwa kuwa walitaka kupandisha bei kwa asilimia 100 wakati shilingi haijashuka thamani kwa kiasi hicho, nikawaambia waache kuwafikisha wananchi huko na kuwafanya waichukie serikali yao," alisema.


  Alitaja baadhi ya mafanikio katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake kuwa, nyongeza mbalimbali za mishahara kwa watumishi wa umma na wote watapata sh. 100,000 za nauli wakati wa likizo.


  Mengine ni kuboresha utendaji kazi na kuondokana na ulegelege, kuimarisha kilimo kuelekea cha kisasa, kusimamia na kuhakikisha bei ya karafuu inapanda huku kilimo hicho kikiimarishwa, kuimarisha uvuvi, kutoa mikopo kwa makundi mbalimbali, nafasi za mafunzo kwa wajasiriamali, kuimarisha miradi ya maji, barabara na shule.


  Alisema katika mipango ya baadaye, Hospitali ya Mnazi Mmoja itapandishwa hadhi kuwa ya rufani, ili kupunguza kama si kufuta kabisa gharama za kupeleka watu kutibiwa nje ya nchi.


  Dk. Sheni alisema huduma za kitalii zitaboreshwa maradufu, kujengwa kwa hoteli za kitalii za hadhi ya nyota tano, kununuliwa meli kubwa mpya kwa ajili ya abiria na mizigo na kuimarisha huduma ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.


  LAST UPDATED ( THURSDAY, 03 NOVEMBER 2011 19:22 )
   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Nov 5, 2011
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 58
  Trophy Points: 145
  Ok Pemba na Zanzibar...; wazanzibari mnasemaje??
   
 3. G

  George Smiley JF-Expert Member

  #3
  Nov 5, 2011
  Joined: Oct 24, 2011
  Messages: 470
  Likes Received: 29
  Trophy Points: 45
  Kinda reminds me of press conference ya Mkapa na waandishi

  akawashushua weeeee mpaka

  Hongera shein kwa kuweka facts mbele badala ya uzushi
   
 4. Mkubwa ndevu

  Mkubwa ndevu JF-Expert Member

  #4
  Nov 5, 2011
  Joined: Feb 17, 2011
  Messages: 755
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 45
  Hongera dr wa ukweli.
   
Loading...