Dk. Shein: Waislamu imetosha; Asema uvumilivu wa Serikali umefika kikomo | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dk. Shein: Waislamu imetosha; Asema uvumilivu wa Serikali umefika kikomo

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by nngu007, Oct 27, 2012.

 1. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #1
  Oct 27, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  JUMAMOSI, OCTOBA 27, 2012 09:59 NA WAANDISHI WETU, Z'BAR NA MIKOANI


  *Asema uvumilivu wa Serikali umefika kikomo
  *Dk. Bilal naye akunjua makucha, ataka utulivu

  RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ustahimilivu na uvumilivu wa Serikali, umefikia kikomo kwa watu wote, wanaofanya vitendo vya vurugu na kwamba kuanzia sasa, itamshughulikia ipasavyo mtu yeyote atakayevunja sheria. Dk. Shein aliyasema hayo jana, wakati akihutubia Baraza la Idd el Hajj mjini Unguja.
  Alisema, ustahimilivu na utulivu sio udhaifu, ni heshima kubwa ya kutii amri ya Mungu na kusisitiza hatua ya Serikali kuvumilia vitendo vya uvunjifu wa amani, sasa basi.

  "Serikali haitakuwa na msalie mtume dhidi ya wahalifu wote, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi…nasema sasa imetosha," alisema Dk. Shein.

  Alisema Serikali itafanya kila linalowezekana, ili kuhakikisha watu wanaohatarisha usalama na amani, wanashughulikiwa.

  Alisema Serikali itatumia sheria na taratibu zilizopo, ili kuvishughulikia vitendo vya uvunjifu wa amani, vitakavyofanywa au kuchochewa na kikundi chochote na kusisitiza kuwa, hakuna hata mtu mmoja alie juu ya sheria, bali kila mtu anapaswa kufuata sheria.

  Alisema mpaka sasa, hatua za kisheria tayari zimeshaanza kuchukuliwa na tayari viongozi wanane wa Jumuiya ya UAMSHO, wamepelekwa mahakamani.

  Alisema wakati huo huo, Jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama, vitaendelea na doria katika mitaa mbalimbali, ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani.

  Alisema fujo zilizotokea Oktoba 17, mwaka huu, zilizopelekea kuchomwa kwa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Masikani, kuvunjwa maduka, kuporwa kwa mali za watu na kuharibu miundombinu ya barabara na uharibifu mwingine, havikubaliki.

  Alisema vurugu hizo, zilipelekea kuuawa kwa askari wa polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), mwenye namba F2105, Koplo Said Abdulrahman.

  "Jeshi letu la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama, viko imara kuvidhibiti vitendo vya fujo na vurugu… napenda kukuhakikishieni wananchi nyote kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti, dhidi ya watakaotishia amani ya nchi yetu," alisema Dk. Shein.

  Kutokana na hali hiyo, aliwasihi wananchi wote kuimarisha umoja na mshikamano, ambao ndio msingi mkubwa wa amani na utulivu.

  Kuhusu kuwasaidia wakulima, Dk. Shein alisema, Serikali itajitahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zinazowakabili.

  Alitoa wito kwa wakulima na wananchi, kutumia mvua za vuli pale zitakaponyesha, kwa ajili ya upandaji wa miti ya misitu, biashara na matunda.

  Alisema Zanzibar imepiga hatua ya kuigwa, katika maendeleo kwenye nyanja za uchumi na ustawi wa jamii, tangu Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964. Pia alieleza kuwa, ripoti ya mapitio ya Dira 2020, iliyotolewa hivi karibuni, inaonesha kwamba yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana.

  Mapema asubuhi, Dk. Shein aliungana na waumini wengine wa dini ya Kiislamu, katika sala ya Idd el Hajj, iliyosaliwa katika Msikiti Mushawar, Mwembeshauri.

  Dk. BILAL

  Katika hatua nyingine, Watanzania wametakiwa kuacha mara moja tabia za kujiingiza katika migogoro ya kidini, ambayo inaweza kuvunja amani.

  Kauli hiyo, ilitolewa jana wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, wakati wa sherehe za Eid El Hajj, zilizofanyika kitaifa wilayani hapa.

  Mbali na kushiriki sherehe hizo, Dk. Bilal alishiriki kuweka jiwe la msingi na uzinduzi wa mfuko wa kuchangia fedha za ujenzi wa Shule ya Msingi ya awali na Sekondari ya Vuchama Mosque Islamic Center.

  Alisema Watanzania, hawana budi kushiriki shughuli za maendeleo na kuacha kabisa tabia ya migongano ya kidini, inayoendelea nchini.

  "Siku za hivi karibuni, kumezuka tabia mbovu za baadhi ya waumini wa Kiislamu, kuzusha migogoro isiyo na faida, kama vile kugombea uongozi misikitini.

  "Wengine wanagombania kuhodhi mali za misikiti, hili ni jambo ambalo halikubaliki kabisa, kwani linaleta sura mbaya katika jamii yetu na kusababisha uvunjifu wa amani," alisema Dk. Bilal.

  Dk. Bilal alisema, zipo taasisi za kidini nchini, zimekuwa mstari wa mbele kusaidia Serikali, kutoa huduma za kijamii, hususan elimu kupitia shule zinazoendeshwa na taasisi hizo.

  Alisema kuanzishwa kwa shule hizo, kumewezesha watoto wengi kujengewa uwezo mkubwa wa kupata elimu, kufundishwa maadili na utamaduni wa Kitanzania.

  Harambee ya ujenzi wa shule ya msingi ya awali na sekondari, iliweza kuchangiwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Sh milioni 5, Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya alichangia Sh milioni moja na Mbunge wa Mwanga, Professa Jumanne Maghembe, alichangia Sh milioni moja.


  Taarifa hii, imeandaliwa na Safina Sarwatt, Upendo Mosha (Mwanga) na Rajab Mkasaba (Zanzibar).

   
 2. nngu007

  nngu007 JF-Expert Member

  #2
  Oct 27, 2012
  Joined: Aug 2, 2010
  Messages: 15,871
  Likes Received: 56
  Trophy Points: 145
  Pesa, Pesa zinatoka kwapi? VIONGOZI matajiri Waumini ni Walala hoi Wahitaji MSAADA wa Kiuchumi na kimazingira
   
 3. U

  Ubungo JF-Expert Member

  #3
  Oct 27, 2012
  Joined: Apr 7, 2012
  Messages: 1,239
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Kauli zenye matumaini, tunasubiri utekelezaji.
   
Loading...