Dk. Shein Amaliza Mzozo Kati ya Wanakijiji wa Chwaka na Marumbi

Jicho la Tai

JF-Expert Member
Oct 10, 2012
1,449
574
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amefanya mazungumzo na wananchi wa kijiji cha Chwaka na kuwapongeza kwa kufungua ukurasa mpya wa maelewano na kumaliza mzozo uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 kati yao na wanakijiji wa Marumbi.

Akizungumza na wanakijiji hao waliojaa katika viwanja vilivyopo pembezoni mwa skuli ya Chwaka Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusibni Unguja, wakiwa na hamu na furaha ya kumsikiliza kiongozi huyo kama walivyomuomba na yeye kutimiza ahadi yake ya kwenda kijiji hapo aliyoitoa Agosti 15 alipozungumza na wanakijiji wa Marumbi, kwa lengo la kutafuta Sulhu kufuatia mzozo wa bahari kati ya Marumbi na Chwaka.

Katika maelezo yake Dk. Shein aliwataka wananchi hao watambue kuwa wao ni ndugu wa damu hivyo hakuna haja ya kugombana na hasa ikizingatiwa chanzo cha ugomvi huo ni bahari ambayo bahari hiyo imeumbwa na MwenyeziMungu na ni ya Mungu hivyo wao wanatakiwa waitumie ipasavyo.

Dk. Shein aliwaeleza wananchi hao jinsi alivyofarajika na kufurahishwa na risala yao waliyoelezea azma yao ya kufukia chuki, hasama na ugomvi kati yao na wanakijiji wa Marumbi ambao ni ndugu zao wa damu.

Dk. Shein aliwakata wananchi hao wa Chwaka kutambua kuwa kijiji hicho kina historia kubwa ya maendeleo pamoja na historia ya watu wake ambao ni wachapa kazi mahiri hasa katika sekta ya uvuvi na wanajulikana Afrika Mashariki yote.
“Leo kwangu ni siku ya furaha baada ya kusikia risala yenu iliyoandikwa ikaandikika na iliyosomwa ikasomeka… Sulhu ni jambo muhimu kwani hata Mtume wetu Muhammad (S.A.W), alifanya Sulhu iliyoitwa kwa jina la Sulhu ya Hudaibiya”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein aliwapongeza wananchi hao wa Chwaka kwa kuwa na hamu ya maendeleo na kukubaliana na ombi lao la kuiomba Serikali kuimarisha uvuvi wa bahari kuu, na kuwaeleza kuwa hilo ndio lengo kuu la Serikali hivi sasa kwa kushirikiana na wawekezaji na mchakato wake ndio unaendelea na si muda mrefu utakamilika.

Alisema kuwa tayari Serikali imeshatuma ujumbe kwenda nchi mbali mbali duniani zikiwemo China na Shelisheli kwa lengo la kupanua wigo juu ya sekta hiyo ya uvuvi hasa wa bahari kuu. “Bahari kuu haijaguswa na ndio maana zinakuja meli kutoka nje zinakuja kuwaiba samaki wetu”,alisisitiza Dk. Shein.

Pia, Dk. Shein alieleza kuwa nchi hii ni ya demokrasia na kila mmoja ana uhuru wa kuwa na chama chake hivyo hakuna haja ya kubaguana na kutambua kuwa siasa sio ugomvi na kuwataka viongozi wote wa Chwaka kuwatumikia wananchi wote bila ya kuwabagua kwani wote wanahaki ya kupata huduma za Serikali.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kuziheshimu na kuzifuata sheria na taratibu za nchi zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1984 na kusisitiza kuwa hakuna nchi hata moja duniani inayotunga sheria yenye kuwakandamiza wananchi wake.

Kutokana na hatua hiyo aliwataka wale wote wanaodai kuwa Sheria ya Uvuvi iliyopo hivi sasa ina mapungufu watambue kuwa kuna taratibu nyingi za kuondoa mapungufu hayo huku akisisitiza kuwa Baraza la Wawakilsihi haliwezi kutunga Sheria kandamizi.

Alisema kuwa Zanzibar haipo peke yake hivyo ni lazima ifuate sheria na taratibu za Kimataifa na kusisitiza kuwa Sheria zimetungwa kwenda na wakati na ikibainika kuwa kuna kipengele kimepitwa na wakati ama sheria yenyewe basi inaweza kubadilishwa. Dk. Shein aliwataka wananchi na wanakijiji wa Chwaka kutunza mazingira ya bahari.

Sambamba na hayo, aliwaeleza azma ya Serikali ya kuamua kuviwezesha vikundi vya ushirika kupitia mfuko maalum wa kujitegemea ambao utakapozinduliwa wananchi wote watapewa taarifa kwani tayari umeshaanza kukushanya fedha kwa madhumini hayo.

Kwa upande wa tatizo ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika kijiji hicho, Dk. Shein aliwaahidi wananchi hao kuwa ataungana na viongozi wengine kutoa mchango wake wa mabomba akiwemo Balozi Seif Idd na kueleza kuwa serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo muhimu pamoja na kutatua changamoto nyengine.

Nae Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja ambae pia, ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Abdalla Mwinyi Khamis aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Chwaka kwa juhudi zao hizo na kuwataka watambue kuwa ustahamilivu na uvumilivu sio udhaifu.

Mapema wakisoma risala yao, wananchi hao walieleza kuwa watu wa Marumbi ni ndugu zao wa damu kwa hivyo suala la shari na kumwaga damu kwa masuala ya bahari hawatoyapa nafasi tena na litabaki kuwa historia.“Sisi watu wa Chwaka tunakupongeza kwa umahiri wako wa udokta wa kutibu donda hili la miaka mingi kwetu, hili sasa sio ‘issue’ tena kwa sababu wasuluhishaji wako walituunganisha pamoja na ndugu zetu wa Marumbi”, walisema wananchi hao.

Aidha, waliiomba serikali kuwawezesha kuvua katika bahari kuu na kusisitiza kuwa Zanzibar ina rasilimali za kutosha kuanzia Kizimkazi Mashariki na Kaskazini Mashariki mpaka Msuka kisiwani Pemba ambako wapo samaki wengi ambao hawajavuliwa.

Wananchi hao walitoa shukurani kwa Dk. Shein pamoja na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwashukuru viongozi wote walioshiriki katika kuleta Sulhu ya mzozo wa Chwaka na Marumbi. “….. na hii leo baada ya miaka 33 historia imejirea, kwa wewe Mheshimiwa Ali Mohamed Shein kuja kwetu moja kwa moja kuzungumza na watu wa Chwaka, hili ni somo kubwa sana kwetu juu ya upendo wako, sisi watu wa Chwaka tunasema MwenyeziMungu akupe umri wenye mafanikio”, walieleza wananchi.

Sambamba na hayo, wananchi hao walizieleza changamoto mbali mbali zinazowakabili katika upande wa sekta ya elimu, maji safi na salama, rasilimali za mawasiliano ya simu, nyumba kongwe, utawala bora na nyenginezo ambapo miongoni mwa viongozi waliohudhuria katika mkutano huo akiwemo Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban aliahidi kuzifanyia kazi.
 
Back
Top Bottom