Dk Salim ataka mseto Zanzibar,awasifu Maalim Seif, Rais Karume | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dk Salim ataka mseto Zanzibar,awasifu Maalim Seif, Rais Karume

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Pdidy, Nov 21, 2009.

 1. Pdidy

  Pdidy JF-Expert Member

  #1
  Nov 21, 2009
  Joined: Nov 22, 2007
  Messages: 33,277
  Likes Received: 5,638
  Trophy Points: 280
  Dk Salim ataka mseto Zanzibar,awasifu Maalim Seif, Rais Karume

  Na Hawra Shamte

  MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM na Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim amesema dawa ya kudumu ya matatizo ya Zanzibar ni kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa au ya mseto.


  Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni, Dk Salim alishauri serikali hiyo iundwe baada ya uchaguzi mkuu ujao ili kuepusha machafuko yanayoweza kutokea kutokana na tofauti za kisiasa.


  Dk Salim ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (AU), alisema katika mazingira ya siasa za Zanzibar, ni vigumu chama kimoja kukizidi sana chama kingine katika kura, hivyo njia pekee ya kuondokana na tofauti za kiitikadi ni kwa chama kitakachoshinda kuwa tayari kuunda Serikali ya Mseto.


  Baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM uliofanyika kijijini Butiama, mkoani Mara, Machi mwaka jana, CCM kimsingi ilikubali kuanzishwa kwa Serikali ya Mseto, lakini mvutano kati ya chama hicho na CUF ulijitokeza kwa swali kwamba, lini mseto uanze.


  CCM walitaka mseto uanze baada ya Uchaguzi Mkuu mwakani, lakini CUF wakataka uanze sasa. Wakati mvutano huo ukiendelea kulijitokeza hoja ndani ya CCM kwamba yatafutwe maoni ya Wazanzibari wote kuhusu suala hilo, kwa sababu Zanzibar si ya CCM wala CUF pekee.


  “Tofauti ya kura itakuwa ni asilimia moja au mbili, hivyo ni wazi kuwa njia pekee ya kuongoza katika mazingira kama hayo ni kuunda Serikali ya Mseto au Serikali ya Umoja wa kitaifa,” alieleza Dk Salim.


  Alisema hata kama katika uchaguzi mkuu ujao ikishinda CUF, kama haikuunda Serikali ya Mseto itakuwa ni kulihamisha tatizo lililokuwepo; ambalo lilisababisha CCM kulaumiwa, badala yake lawama itapelekwa kwa CUF.


  Kwa mujibu wa Dk Salim, maridhiano yaliyofikiwa kati ya Rais wa Zanzibar, Abeid Karume wa Serikali ya CCM na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ni hatua muhimu katika kujenga Zanzibar yenye amani na utulivu.


  Alisema kwa jinsi hali ya kisiasa Zanzibar ilivyo, jitihada za makusudi zinatakiwa kufanyika kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa salama na amani.


  “Inapofikia wananchi wakawa hawajali, hawaogopi chochote kitakachotokea na sehemu moja kuhisi kama imebaguliwa, imetengwa katika kupata fursa mbalimbali za kijamii kiuchumi na kisiasa; huweza kufanya chochote.


  Na jinsi hali ilivyo, kama haitadhibitiwa mapema; bila shaka uchaguzi mkuu ujao utakuwa na vurugu kubwa na huenda damu ikamwagika,” alisema Dk Salim na kuongeza:


  “Hatua iliyochukuliwa hivi karibuni ya kufikia maridhiano ni nzuri na binafsi natumai kuwa waliyoyazungumza Rais Karume na Maalim Seif ni mambo yenye maslahi kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla”.


  Alisema pamoja na maafikiano hayo yaliyofikiwa na viongozi wa CUF na wa SMZ, lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayo jukumu la kuhakikisha amani ya kweli inafikiwa visiwani humo.


  Alisema huu si wakati wa kuendeleza na kuendekeza chuki. “Siasa za Zanzibar zimetawaliwa na chuki, lakini wakati umefika kwa Wazanzibari wenyewe kuona kuwa chuki hazitawasaidia kujenga nchi yao na pia zina athari kubwa si kwao tu, bali kwa Tanzania na kwa Afrika kwa ujumla,” alisisitiza.


  Aidha Dk Salim alisema kuwa Rais Karume na CCM kwa ujumla wanapaswa kuiona hatua hii ya maridhiano kama ufunguo wa amani Zanzibar na hali hii ikitumiwa vyema yaweza kunusurisha yale yaliyowahi kutokea Zimbabwe na Kenya na hata yale yanayoendelea kutokea nchini Sudan.


  Alisema Sudan mathalani tatizo lake na Darfur limekuwa kubwa sana na sasa wapo watu wanaofikiria kujitenga:


  “Tatizo kubwa la Sudan ni kwamba wananchi walioko pembezoni, wanahisi kama wametengwa… na maslahi yote na maendeleo yote yanatokea katika eneo moja tu la Sudan… tatizo hilo ni kubwa, watu wanapofikiria kujitenga si ishara nzuri kwa amani, siyo tu ya Sudan bali ya Afrika nzima.”


  Novemba 5, mwaka huu Rais Karume alikutana na Maalim Seif, Ikulu ya Zanzibar katika kikao cha faragha ambacho baada ya kukamilika, Seif alifanya mkutano wa hadhara wa wanachama wa chama chake na kuwaeleza kuwa wanamtambua rasmi Karume kwa kuwa hatua hiyo inafungua milango ya makubwa zaidi, ambayo hata hivyo hakuyataja.


  Hatua ya viongozi hao imetanguliwa na kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa alipozungumza na wananchi miezi michache iliyopita kuwa suala la ufumbuzi wa migongano ya kisiasa Zanzibar halijamshinda Rais Karume mpaka yeye aingilie kati.


  Hata hivyo, wakati hayo yakijiri hali imekuwa tete katika vyama vya CCM na CUF.


  Baadhi ya makada wa CCM na hususan wahafidhina ndani ya chama hicho wakianza kuratibu mikakati ya kupinga suala hilo huku wana-CUF wakiitazama hatua ya kiongozi wao kumtambua Karume kwa hadhari kubwa. Baadhi wakiamini hiyo ni ‘janja’ ya CCM kuweka utulivu wa nchi hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.


  Tayari viongozi mbalimbali wa kitaifa wa vyama hivyo wameunga mkono uamuzi wa CUF kumtambua Karume. Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Kingunge Ngombale-Mwiru ambaye alishiriki kwenye timu ya mazungumzo ya muafaka ambayo hayakuzaa matunda.


  Suala la utatuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar lilizungumzwa na Rais Kikwete katika hotuba yake ya kuzindua Bunge Desemba 30, 2005, akisema mgogoro wa Zanzibar una msononesha na kuahidi kuufanyia kazi.
   
Loading...