Dk Ngowi: Kuwavutia wawekezaji ni kuingia kaburini | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Dk Ngowi: Kuwavutia wawekezaji ni kuingia kaburini

Discussion in 'Biashara, Uchumi na Ujasiriamali' started by MziziMkavu, Jun 23, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 23, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,612
  Trophy Points: 280
  Fredy Azzah
  JUNI 12 mwaka huu, Kamati ya Viongozi wa Dini ya masuala ya Uchumi na Haki za Binadamu (ISCJIC), ilitoa ripoti yake kuhusu uchumi wa nchi na kuonyesha Serikali inapoteza Sh1.7 trilioni kutokana na kukwepa kodi, misamaha ya kodi na mali na fedha za umma kutoroshwa nje ya nchi.


  Ni wazi kwamba bajeti ya Serikali iliyosomwa Juni 14, mwaka huu ilitarajiwa kujibu baadhi ya mambo yaliyoainishwa katika ripoti hiyo iliyopewa jina la ‘The one billion dollar question: how can Tanzania Stop losing so much tax revenue’.


  Kinyume chake, bajeti hiyo bado imeacha maswali mengi na mjadala mkubwa kuhusu uwezo wa Serikali kukusanya kodi pia kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikitengewa fedha, lakini imekuwa haitekelezeki.


  Kutokana na udhaifu huo wa Serikali kukusanya kodi, ndiyo maana watu wanajiuliza ni vipi Serikali itaweza kutekeleza miradi iliyojipangia mwaka ujao wa fedha (2012/13).


  Kamati ya viongozi wa dini, ilitoa ripoti ya utafiti ambayo ilionyesha Serikali inapoteza Sh1.7 trilioni kila mwaka kutokana na misamaha ya kodi, wakwepa kodi na fedha na mali ghafi za nchi kutoroshwa.


  Baadhi ya mambo ambayo Serikali inatarajia kutekeleza katika mwaka ujao wa fedha ni upatikanaji wa uhakika wa umeme, na Sh498.9 zimetengwa kwa ajili hiyo.


  Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye thamani ya dola 1,225.3 milioni za Marekani.


  Katika upande wa miundombinu ya reli ya kati, ukarabati wa injini na mabehewa ya treni, miradi ya barabara, usafiri wa anga na majini, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika, Serikali imetenga Sh1,382.9 bilioni.


  Miradi ya maji imetengewa Sh568.8 bilioni, kilimo na umwagiliaji Sh192.2 bilioni, katika upande wa maendeleo ya viwanda, Serikali imetenga Sh128.4 bilioni.


  Ni ukweli kuwa, licha ya kiasi hiki cha fedha kuonekana kidogo, bado hakuna uhakika kwamba fedha hizi zitapatikana zote na kupelekwa katika maeneo au miradi iliyokusudiwa.


  Pamoja na hali hiyo, Serikali bado imeendelea kupandisha kodi kwenye vitu kama, Soda, Bia na Sigara, huku ikiendelea kutoa misamaha kwenye sekta ya madini, na nyingine ambazo hazimnufaishi mwananchi moja kwa moja.


  Mbali na hayo Serikali inaikingia kifua hoja yake ya misamaha ya kodi katika sekta hizo kwa maelezo ya kuvutia wawekezaji.


  Hali hii ndiyo inanikumbusha kauli ya mtaalamu wa uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Dk Prosper Ngowi, aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa ripoti ya viongozi wa dini.


  Dk Ngowi anasema, suala la nchi za Afrika Mashariki kuendelea kushindana katika kutoa vivutio vya uwekezaji, ni kushindana katika mbio za kuwahi kuingia kaburini.


  Kwa maneno yake anahoji: “Kwanini umvutie mtu kuja kuchimba madini ya dhahabu wakati watu wengi duniani kote wanayatafuta usiku na mchana.


  Moja ya njia za kuwavutia wawekezaji ni pamoja ni pamoja na misamaha ya kodi
  Anasema, madini hayo yalikuwa na soko sana duniani haswa wakati wa mtikisiko wa uchumi duniani na hata sasa thamani yake inazidi kupanda.


  Dk Ngowi anasema ni vyema Serikali ingetoza kodi hizo na kuboresha miundombinu ya barabara, reli, maji na umeme kwa kuwa maeneo hayo yanatazamwa na wawekezaji.


  Kabla ya ripoti hii, kuna tafiti nyingine nyingi tu zimefanyika, zikionyesha ni kwa kiasi gani Serikali inapoteza mapato mengi kutokana na misamaha ya kodi na ukusanyaji mbovu wa mapato na kusababisha wafanyabiashara kukwepa kodi.


  Lakini mwenyekiti wa kamati hiyo Askofu wa Jimbo la Katoliki la Tabora, Paul Ruzoka, anasema katika utafiti huo walibaini moja ya mambo yanayochangia upotevu wa fedha za Serikali ni kuwapo kwa Sera mbovu za Serikali na uzembe katika makusanyo ya kodi.


  “Ipo haja ya kuwa na mipango mizuri ya kukusanya kodi, ili kudhibiti kampuni zinazotoa fedha na pia kubana kama siyo kuondoa kabisa misamaha ya kodi,” anasema Askofu Ruzoka.


  Mwenyekiti huyo wa kamati anafafanua kwamba ni vyema Serikali ikatazama njia nyingine ya kuvutia wawekezaji badala ya kuweka misamaha ya kodi jambo ambalo linawaumiza wananchi.


  Utafiti huo umebainisha kwamba makadirio ya chini, kila mwaka Serikali inapoteza kati ya dola 847 milioni za Marekani na dola 1.29 bilioni za Marekani (Sh1.35 trilioni naSh 2.05 trilioni).


  Ili kuweka uwiano wa takwimu, ripoti hiyo inasema inachukualia kiwango cha kati ambacho kimekuwa kikipotea kwamba kimekuwa kikifikia dola 1.07 bilioni za marekani sawa na Sh1.7 trilioni.


  Ripoti hiyo inasema licha ya baadhi ya watu kukwepa kodi kama ilivyozoeleka, baadhi ya kampuni ambazo zina ofisi katika nchi zaidi ya moja, zimekuwa zikitoa taarifa za uongo kuhusu shughuli za ununuzi ikiwa ni moja ya mbinu za kukwepa kodi.


  Ikinukuu takwimu ambazo chanzo chake ni Benki ya Dunia (WB) katika ukanda wa Afrika Mashariki, inasema kampuni za Tanzania zinaongoza kwa kutoa taarifa za uongo.


  "Asilimia 69 ya kampuni zilizopo nchini zinatoa taarifa sahihi, Uganda ni asilimia 77 na Kenya asilimia 86.


  Ni aibu, licha ya kuwa na kampuni chache bado zinakwepa kodi kwa kiasi kikubwa kiliko wenzetu Kenya ambako kuna kampuni nyingi kuliko sisi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.


  Ni hatua gani zimechukuliwa na Serikali katika kuhakikisha inadhibiti tatizo hili?


  Ripoti hiyo inasema, pia kampuni 400 zinalipa kodi kwa asilimia 70 huku wafanyabiashara wadogo wakilipa kodi kwa asilimia 30.


  Ripoti hiyo inabainisha kwamba kodi zinazolipwa na kampuni ya madini ni ulaghai mtupu.
  Utafiti huo ulishirikisha vyanzo 167, vikiwamo vya Serikali, na mashirika ya kimataifa na kuweka wazi kwamba asilimia 65.4 ya kodi inayolipwa na kampuni za madini, inatokana na makato ya kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi wake (PAYE).


  Wataalamu wa uchumi wanabainisha kwamba kutokana na hali hiyo inaonyesha kwamba Serikali siyo makini kwa kuwa bajeti ya mwaka 2012/13, inaonyesha wawekezaji hao wanaendelea kupata misamaha ya kodi misamaha ya vitu wanavyoingiza nchini vikiwamo magari na vifaa vingine.


  Kwa hali hii ni dhairi kabisa, Serikali haina mpango wa kutatua matatizo ya msingi ya wananchi wake.


  Tunaelezwa kuwa, katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/12, matumizi ya maendeleo yalikuwa Sh2,657.2 bilioni, tofauti na Sh4,924.6. bilioni zilizotarajiwa kutumika.


  Ni wazi kuwa, hali hii imesababaisha miradi kuendelea kusimama na kusababisha wananchi waendelee kuwa katika wakati mgumu kiuchumi licha ya bajeti hiyo kupewa jina la ‘bajeti ya wananchi’.


  Wote ni mashahidi wa wizi wa pembejeo za kilimo, ufujaji wa fedha kwenye halimashauri zetu na wizara husika, lakini watuhumiwa wa pembejeo hizo hawajachukuliwa hatua kali za kisheria mbali ya kupelekwa mahakamani tu.


  Ni vigumu Serikali kutekeleza mpango wa Kilimo Kwanza kama ilivyokusudia licha ya sekta ya kilimo kutengewa Sh192.2 bilioni. Katika sekta ya kilimo kuna mianya mikubwa ya upotevu wa fedha kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali kutokuwa na maadili katika matumizi ya fedha za umma.
  http://www.mwananchi.co.tz/makala/31-uchumi/24089-dk-ngowi-kuwavutia-wawekezaji-ni-kuingia-kaburini
   
Loading...