Dk. Mesaki: Ufahamu unavyokua duniani uchawi hufichika zaidi


Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined
Feb 4, 2009
Messages
42,418
Likes
38,602
Points
280
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined Feb 4, 2009
42,418 38,602 280
Septemba 24, mwaka 2008 tuliwaletea makala ya mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Simeon Mesaki, aliyetunukiwa shahada yake ya uzamivu kutokana na utafiti wake kuhusu uchawi na mauaji ya kishirikina katika Tanzania. Sehemu hii nyingine ya utafiti wake anaelezea matukio zaidi yaliyomgusa yeye binafsi, matokeo ya utafiti huo na wasifu wake, kama Mwandishi Wetu, ARISTARIKO KONGA, anavyonukuu utafiti huo.
“Tukio jingine tofauti lililohusishwa na tatizo la ushirikina lilijitokeza tena, likimhusu dada yangu mwingine, aliyekuwa akiishi Dar es Salaam, na ambaye alikuwa akifanya kazi katika mradi mmoja uliokuwa ukifadhiliwa na watu wa nje. Dada yngu huyo (nitamwita Wasiwasi), alikuwa na umri wa miaka 26, alikuwa hajaolewa na wala hakuwa amejaaliwa watoto.
Alikuwa akiishi pamoja na dada yetu mkubwa, ambaye alikuwa na umri wa miaka 42, ambaye alikuwa akifanya kazi kama mpishi katika taasisi mmoja ya elimu. Dada yetu huyo mkubwa pia alikuwa hajaolewa lakini alikuwa ana watoto wanne.
Wakati mmoja, mapema Januari 1992, Wasiwasi aliamua kwenda kuishi na kaka yangu, ambaye alikuwa akiishi katikati ya Dar es Salaam, kwenye nyumba iliyokuwa na ukubwa wa vyumba vitatu, na ambayo ilikodishwa na mwajiri wake. Kaka yangu alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya dawa. Hakuwa ameoa na wala hakuwa na watoto.
Wasiwasi alipokuwa amekwenda kuishi huko alipewa chumba chake cha kuishi, na ilikuwa fursa nzuri kuwa aliweza kumpikia kaka yangu na ndugu yetu mwingine, ambaye wakati mwingine alikuwa akija kuishi kwenye nyumba hiyo.
Siku mmoja usiku umeme ulikatika ghafla na Wasiwasi akalikimbia jengo hilo kwenda nje. Hatimaye tulimkuta akiwa amelazwa hospitalini, ambako aligundulika kuwa alikuwa amepatwa na wazimu.
Baada ya kukaa siku moja hospitalini, alirejea tena kwenda kuishi na dada yake. Wakati akiishi huko usiku mmoja aliondoka kitandani, akatoka nje ya nyumba na kulala chini ya mti. Baada ya kuulizwa kuhusu tukio hilo, alieleza kuwa chumba ambamo walikuwa wakilala kilikuwa kinakaliwa na mashetani, na kueleza zaidi kwamba dada yake na hata kaka zake aliokuwa akiishi nao kabla walikuwa wakitenda maovu ili kumdhuru.
Mimi niliitwa na kisha nikaweza kumshawishi ili aje kuishi nyumbani kwangu, ambako aliishi chumba kimoja na mabinti zangu wawili. Aliishi hapo kwa juma moja, na baada ya hapo akatuambia tujihoji miongoni mwetu, kama ni kweli tulikuwa hatuli njama za kufanya mambo mabaya dhidi yake.
Tulimjibu kuwa tusingeweza kumdhuru dada yetu wenyewe na kushauri kuwa tumpeleke hospitali. Lakini alirejea kwenye makazi ya dada yangu na mambo yakazidi kuwa mabaya kwa kuwa alikataa kula na hata kwenda hospitali yeye mwenyewe.
Baadaye nilimpeleka kwa nguvu kwenda hospitali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Madaktari walimpa dawa za kupunguza maumivu, wakitarajia zaidi kumpeleka hospitali ya rufaa baadaye. Punde tu, watu kadhaa wakawa wanakuja kwangu kunisihi ili niweze kumtafuta mganga wa kienyeji ili amtibu dada yangu. Walitoa hoja kuwa, ugonjwa wake usingeweza kutibika katika hospitali, bali kwa tiba za kienyeji.
Niliwaambia kwamba kwa jinsi nilivyofahamu tatizo lake lilikuwa ni msongo wa mawazo na mfadhaiko. Niliwaambia kuwa dada yangu alikuwa na tatizo la kupata mchumba na kwa kuwa hakuwa na mume, watoto wala nyumba yake, basi asingeweza kusimama mwenyewe kimaisha.
Siku iliyofuatia alianguka ghafla na baada ya miito mingi kutoka kwa wenye kutakia heri, nilikwenda kwa mganga wa kienyeji. Mganga alinishauri niende nikanunue dawa za kigeni zenye mahadhi ya Kiarabu na Kiislam, ambazo zilikuwa zikipatikana kwenye duka pekee katika Soko la Kariakoo la Dar es Salaam. Mganga alizitwanga dawa zile na akazichanganya na dawa nyingine zisizokuwa za kawaida na kisha akauweka mchanganyiko ule kwenye chungu kidogo, na akaanza kuuchoma mchanganyiko huo kwa moto wa mkaa, ili dada yangu aweze kuuvuta moshi wake.
Baada ya kitendo hiki cha kupunga pepo, hali yake iligeuka kuwa nzuri kiasi chake na akarejea kufanya kazi wiki iliyofuatia. Lakini baada ya kurejea kazini siku mmoja, hali yake ilibadilika ghafla na mganga akatoa uamuzi kuwa tatizo lililokuwa likimsumbua lilikuwa kazini kwake, kwamba kulikuwa na mtu ofisini kwake ambaye alikuwa akimroga. Alisema kuwa alikuwa hapendwi kutokana na uchapakazi wake mzuri na wafanyakazi wenzake walikuwa wanataka kumwekea vikwazo ili asiendelee na kazi.
Mganga alieleza kuwa jini lilikuwa limetumwa ili kumdhuru na kwamba ingechukua muda mrefu kumwondoa na kadhia hiyo. Mganga alishauri tumpeleke ili akatibiwe kwenye makazi ya baba yake, ambaye pia alikuwa ni mganga akiishi maili 300 Kaskazini Mashariki ya Dar es Salaam. Tangu wakati huo, yaani Januari 1993 (wakati wa utafiti), alikuwa akiendelea kupata matibabu. Muda mfupi tangu kumpeleka huko nilipata barua kuwa alikuwa akiendelea vizuri akipata nguvu chini ya matibabu ya mganga huyo wa kienyeji.

Kisa kingine kilichohusu hisia za kichawi kililetwa kwangu nikiwa ofisini kwangu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyakazi ofisini hapo chuoni walimwona njiwa ambaye alikuwa amevalishwa hirizi, ikiwa imefungwa kwenye bawa mojawapo. Walihofia kuwa kulikuwa na jambo la kishetani lilikuwa njiani kutendeka. Na kwa kuwa walikuwa wakijua kuwa nilikuwa nikifanya utafiti kuhusu ushirikina, walimleta ndege yule kwangu. Kwa kuwa sikuwa nashawishika kuhusu uchawi, niliifungua hirizi ile kutoka kwenye bawa na kumchukua njiwa yule hadi nyumbani. Nilimnunua njiwa mwingine ili wawe wawili. Niliwanyonyoa manyoya yao ili kuwazuia wasitoroke, lakini baada ya wiki chache, kadri manyoya yalivyokua, walitoweka.
Kuhusu ile hirizi, ilikuwa ina maandishi ya Kiarabu, ambayo nilimpelekea mtaalam wa Koran, ambaye alisema kuwa ujumbe uliokuwa kwenye hirizi hiyo ulikuwa umelenga kumtisha mtu mmoja kwa jina Abdallah. Niliitunza karatasi yenye ujumbe huo ukiwa na maandishi ya Kiarabu.
Tukio jingine linahusu usiku mmoja wakati nilipoombwa kumpeleka mgonjwa kwa mganga wa kienyeji takribani maili 10 kutoka nyumbani kwangu. Ilipofika muda wa saba usiku wa manane majirani zangu katika Kijiji cha Changanyikeni waliniamsha wakaniomba nitoe msaada wa usafiri kwa ajili ya binti mdogo, ambaye alikuwa ameanguka maliwatoni. Walihisi binti huyo alikuwa ameshambuliwa na jini. Ndugu wa binti huyo waliniomba niwapeleke Temeke , maili 10 upande mwingine wa Jiji, ambako wangeweza kumpata mganga wa kienyeji ili wamtibu. Wakati niliposisitiza kuwa ilikuwa ni muhimu tumpeleke zahati ya Chuo iliyokuwa karibu (nikidai kuwa sikuwa na mafuta ya kutosha kwenye gari), ndugu walikubali kwa shingo upande kwa kuwa hawakuwa na njia nyingine ya kumsafirisha binti yule.
Alilazwa katika zahanati ile na kisha sisi tukaruhusiwa kwenda nyumbani. Siku iliyofuatia nilipigwa butwaa kugundua kuwa binti yule alifariki dunia muda mfupi tu tangu sisi tuondoke kwenye zahanati alfajiri ile. Ndugu walidai kuwa kama ningekuwa nimempeleka kwa mganga wa kienyeji usiku ule, angeweza kuokolewa na shetani huyo aliyemteketeza binti yao. Nililaumiwa kutokana na tukio hili kutokana na kushuku kwangu. Ili kuthibitisha kuwa kifo cha binti yule ilikuwa ni matokeo ya shambulio la jini, ndugu walisema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa ukiharibika kwa haraka sana, kiasi kwamba walikuwa wakilazimika kumzika upesi kuliko ilivyokuwa kawaida.
Jambo linalopaswa kusemwa hapa ni kwamba mwili wa marehemu haukupelekwa kwa ajili ya uchunguzi ili kujua chanzo halisi cha kifo cha binti yule.
Kulikuwa na matukio ambayo yalinigusa binafsi katika juhudi zangu za kuangalia dhana ya uchawi katika Tanzania. Nilijiuliza mwenyewe, hivi ni kweli mambo haya yanatokea? Ni ya uhakika kwa kiasi gani? Kwa mtazamo wangu hayakuwa ya kweli. Nikiwa nimekuzwa kama muumini wa Kanisa la Sabato (SDA) ilifikia hatua nikashangazwa na kanisa ambalo ndilo lilikuwa chaguo la baba yangu, lakini sikuzilea hisia za kishirikina.
Tatizo kubwa linalojitokeza hapa ni maana ya mifumo. Nikiwa mmoja wa watu katika jamii fulani, jamii ambayo kuna wanaoamini na wasioamini uchawi, ni lazima nipambane na mifumo inayofanya kazi sambamba.
Kuna maelezo ambayo hutolewa na serikali. Kama kuna ugonjwa utaratibu wa kimatibabu hudai kufuata mafanikio ya sayansi ya kisasa. Lakini katika mazingira ya nchi zinazoendelea, matatibu ya kienyeji hushawishi watu zaidi kwa kuwa yako karibu na watu na ni rahisi kuyamudu.
Utaratibu wa kikoloni na hata baada ya ukoloni unatoa mambo kadhaa. Dini za Kiislamu na Kikristo hutoa tafsiri tofauti kuhusu suala hilo. Chukua mfano Kanisa la Pentekoste ambalo huvuta hisia za watu kwa kuhubiri mazuri na mabaya. Wachungaji wake huhubiri kuwapo kwa kipindi cha baadaye ya neema na raha.
Katika Uislamu masharifu wengi wanaheshimika kuwa ni vizazi vya Mtume. Wanaaminika kuwa wana nguvu zaidi ya zile za watu wa kawaida. Kwenye ukanda wa mwambao, nadharia ya dini na umiliki wa majini vinaunganishwa na utamaduni wa Kiarabu au Kiislamu. Watu wengine wanaamini kuwa masheikh wana uwezo wa kuyadhibiti yote haya kwa kutumia aya za Korani. Kwamba wanaweza kuwalaani watu kwa kutumia jina la Khalubadiri. Huu ni uganga wa kitabu, unaohofiwa na wengi.
Tangu wakati wa ukoloni, jamii za Tanzania zilishuhudia kumomonyoka kwa mifumo yao ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kidini. Hata hivyo, uchawi umeonekana kuwa unavumilia mabadiliko na unadumu. Kwa hakika, kujihusisha na uchawi na mambo mengine yanayofanana nao, vimezidi kustawi licha ya vikwazo vingi kutoka dini za Kiislam, Kikristo na hata serikali.
Imani katika ushirikina na matukio yanayoendelea kujitokeza yameenea mno katika jamii ya Tanzania, kiasi kwamba yanakuwa kizuizi kwenye mambo mengi ya kimaisha. Yanarudisha maendeleo nyuma na ni kitovu cha ugomvi baina ya jadi na ujenzi wa Ujamaa uliokuwa ukifanywa na serikali.
Uchawi mwingine unajitokeza katika viwanja vya soka. Kama ilivyo katika nchi nyingi katika Afrika, Tanzania (hasa upande wa soka) kuna imani kubwa kwa mambo kama ndumba au juju. Maelfu kwa maelfu ya wapenzi wa soka na viongozi wanategemea zaidi waganguzi wa uchawi ili kuweza kushinda mechi muhimu na klabu hutumia pesa nyingi kufanya maandalizi hayo.
Kama inavyotarajiwa kutoka serikali zote zinazowajibika, dola katika Tanzania inapenda kuona uchawi unatokomezwa au angalau kudhibiti madhara yake makubwa. Hali hiyo ni hivyo kutokana na malengo ya dola na matamanio kwa ajili ya maisha ya kisasa ambayo yamekatishwa tamaa. Dola na wasomi wa sheria wapo kwenye maumivu makubwa ili kutafuta majibu na suluhu. Lakini inaonekana kuwa kadri mambo yanavyoonekana kufahamika zaidi duniani ndivyo ambavyo uchawi unavyozidi kutokufahamika zaidi na zaidi.
Kuna vyanzo vingi vya tatizo hili, lakini hakuna majibu rahisi. Mpaka sasa dola imeshindwa kudhibiti tatizo hilo kama ilivyotaka. Kwa jumla juhudi za serikali kutaka kudhibiti mauaji ya kishirikina yanafanya hali kuwa mbaya zaidi. Mtu angetarajiwa kuwa masuala ya kishirikina yangeshughulikiwa na mawakala wanaohusika na utamaduni katika nchi hii. Kuna rekodi kuwa tangu uhuru sekta ya utamaduni haijawahi kuchukuliwa kwa umakini wake.”

Dk. Simeon Mesaki alizaliwa mwaka 1947. Ameoa na ni Mtanzania. Ni mkazi wa eneo la Changanyikeni, Kata ya Kawe, Wilaya ya Kinondoni, Dares salaam
Alipata shahada yake ya kwanza mwaka 1971 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na akapata shahada ya uzamili (M.A.) katika chuo hicho mwaka 1975. Mwaka 1993 alipata shahada yake ya uzamivu ( Ph. D.) katika Chuo Kikuu cha Minnesota, nchini Marekani.
Uzoefu wake wa kazi ni pamoja na kushika wadhifa wa Ofisa Utawala wa Wilaya ya Kisarawe kuanzia Aprili 1971 hadi Juni 10, 1973.
Mwaka 1986 hadi 1988 alikuwa mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Minnesota-Fall kabla ya kuwa mhitimu mchunguzi (mtafiti) katika Taasisi ya Smithsonian, Washington kati ya Septemba 1988 na Novemba 10, 1988.

Oktoba 1991 hadi Februari alikuwa ni mhadhiri mgeni wa Chuo Kikuu cha Hull, Uingereza, kabla ya kuwa mwanazuoni wa Chuo cha Mtakatifu Olaf College, cha Northfield, Minnesota, kati ya Februari mosi hadi Mei 20, 1993.

Dk Simeon Mesaki amekuwa akifundisha elimu-jamii (sosiolojia) na elimu ya binadamu (anthropolojia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya Julai 11, 1973 na Novemba 3, 2007.

SORCE: RAIA MWEMA.
 
Sipo

Sipo

JF-Expert Member
Joined
Jul 25, 2008
Messages
2,146
Likes
41
Points
0
Sipo

Sipo

JF-Expert Member
Joined Jul 25, 2008
2,146 41 0
Raia Mwema ya lini hii Mkuu Buji?
Nataka nikalitafute gazeti lenyewe niweke kumbukumbu home bana
Namkumbuka vizuri Dr. Mesaki ni kati ya walimu wachache wazuri waliowahi kupita pale department ya Sociology and Anthropology.
 
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined
Feb 4, 2009
Messages
42,418
Likes
38,602
Points
280
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined Feb 4, 2009
42,418 38,602 280
Raia Mwema ya lini hii Mkuu Buji?
Nataka nikalitafute gazeti lenyewe niweke kumbukumbu home bana
Namkumbuka vizuri Dr. Mesaki ni kati ya walimu wachache wazuri waliowahi kupita pale department ya Sociology and Anthropology.
Disemba 17 - 23, 2008
KWENYE MTANDAO HIYO ARTICLE INAPATIKANA HAPA:-
http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=28
 
Sipo

Sipo

JF-Expert Member
Joined
Jul 25, 2008
Messages
2,146
Likes
41
Points
0
Sipo

Sipo

JF-Expert Member
Joined Jul 25, 2008
2,146 41 0
Dr. Mesaki na wenzake wana kikundi chao uko Changanyikeni kinaitwa JITU i.e Jirani Tulindane. Ni kikundi cha usalama ni kama sungusungu vile
Ni mtu mzuri kwakweli ukiwa na tatizo ni rahisi sana kwake kukusaidia kwa wale aliowafundisha watakuwa shahidi wa haya maneno yangu
 
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined
Feb 4, 2009
Messages
42,418
Likes
38,602
Points
280
Bujibuji

Bujibuji

JF-Expert Member
Joined Feb 4, 2009
42,418 38,602 280
Basi kumbe ni bonge la mtu.
Nasikia miongoni mwa mambo aliyoyafanya kwenye tafiti zake ni pamoja na kwenda kuzimu.
Anasema miongoni mwa milango mingi ya kuingilia kuzimu uko pale kariakoo shimoni.
Napenda sana nionane nae, nahisi nina mengi ya kumuuliza na kujifunza kutoka kwake.
 
Sipo

Sipo

JF-Expert Member
Joined
Jul 25, 2008
Messages
2,146
Likes
41
Points
0
Sipo

Sipo

JF-Expert Member
Joined Jul 25, 2008
2,146 41 0
Basi kumbe ni bonge la mtu.
Nasikia miongoni mwa mambo aliyoyafanya kwenye tafiti zake ni pamoja na kwenda kuzimu.
Anasema miongoni mwa milango mingi ya kuingilia kuzimu uko pale kariakoo shimoni.
Napenda sana nionane nae, nahisi nina mengi ya kumuuliza na kujifunza kutoka kwake.
Peace Kinoma yule Mzee
Anasema alishapanda ungo na kutaliii sehemu mbalimbali wakati anafanya hiyo PhD yake
Lakini zaidi ukikwama kimasomo hata kikazi ni mtu mwenye ushauri mzuri tu.
Kamsalimie kwake bana upate info zaidi
 

Forum statistics

Threads 1,238,942
Members 476,277
Posts 29,337,464